Mwandishi: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Mpendwa msomaji hili somo linaendelea na hii ni sehemu ya nne.
Nakusihi pata muda usome sehemu zilizotangulia ili upate mtiririko mzuri wa
mambo yanayozungumziwa humu. Hapa tumefikia mahali pa kuongelea mifano mbalimbali
ya watu kwenye biblia ambao walimgeukia Mungu wakasema naye wakati wa magumu
naye akawatoa katika shida zao. Na lengo ni kuonesha umuhimu wa kuwa na
mahusiano binafsi na Mungu na mara zote kutafuta kuyatengeneza pale
yanapotokea. Kama haujasoma tangu mwanzo na ungependa kusoma sehemu
zilizotangulia bonyeza hapa.
Mfano wa nabii Yona na mji wa Ninawi
Tuhamie kwa nabii Yona, mara baada ya kwenda kwa kujilazimisha
kuuonya mji wa Ninawi. Unaona kabisa kuwa Yona mwenyewe alikuwa anatamani sana
mji wa Ninawi uangamizwe. Yona
4:2-3
Akamwomba Bwana,
akasema, Nakuomba, Ee Bwana; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika
nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana
nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira,
u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya.
Basi, sasa, Ee Bwana,
nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
Lakini kwa yale aliyoyafanya mfalme wa Ninawi, yalimfanya Mungu
aamue kuusamehe mji ule, kisha safari ya Yona ikawa ni ya faida. Kwa sababu
Mungu unadhani angefaidika nini kama angetumia gharama zote zile za kumtuma
Yona halafu akaishia kuuangamiza mji wa Ninawi?
Angalia gharama alizotumia Mungu kumleta Yona Ninawi, aliichafua
bahari ili Yona atupwe majini ashindwe kuendelea na safari yake ya kwenda
Tarshishi, aliwapa hasara wale wenye meli ambao walilazimika kutupa shehena zao
baharini ili meli isizame; na bado Mungu akalazimika kumtuma samaki ammeze Yona
ili ampeleke pwani akamtapike ili akili zimrudie na alirudie kusudi la Bwana.
Yona
1:4-17
Lakini Bwana alituma
upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na
kuvunjika.
Basi wale mabaharia
wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena
iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka
hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.
Basi nahodha
akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu
wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.
Wakasemezana kila mtu
na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu
ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.
Ndipo wakamwambia,
Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi
yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa
kabila gani?
Akawaambia, Mimi ni
Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.
Ndipo watu wale
wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu
wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa
amewajulisha.
Basi wakamwambia,
Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.
Naye akawaambia,
Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni
kwa ajili yangu tufani hii imewapata.
Lakini wale watu
wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari
ilizidi kuwachafukia sana.
Basi wakamlilia
Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai
wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana
wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda.
Basi wakamkamata
Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.
Ndipo wale watu
wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka nadhiri.
Bwana akaweka tayari
samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule
muda wa siku tatu, mchana na usiku.
Hayo yote ni mambo ambayo Mungu aliamua kuingia gharama ili
kuufanya mji wa Ninawi kumgeukia.
Mfalme wa Ninawi hakuwa na mpango wa kuongea na Yona tena baada ya
Yona kufikisha ule ujumbe. Yeye tena angethubutu kwenda kumng’ang’ania Yona
yumkini angekutana na makubwa kuliko yaliyomkuta Sauli kwa Samweli, kwa sababu
tunaona hapa kuwa ni dhahiri Yona alikuwa anatamani sana Ninawi uangamizwe.
Kiukweli mfalme wa Ninawi angetegemea huruma za Yona asingepona,
angekufa papo hapo. Lakini mfalme wa Ninawi aligeukia ukutani, akamlilia Mungu
wake, siye yeye peke yake aliyefanya hivyo, bali na watu wote aliokuwa nao
katika mji ule; hadi wanyama.
Yona
3:4-10
Yona akaanza kuuingia
mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini
Ninawi utaangamizwa.
Basi watu wa Ninawi
wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye
aliye mkubwa hata aliye mdogo.
Habari ikamfikia
mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake,
akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.
Naye akapiga mbiu,
akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake;
kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala
makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;
bali na wafunikwe
nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam,
na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake.
Ni nani ajuaye kwamba
Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?
Mungu akaona matendo
yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya,
ambalo alisema atawatenda; asilitende.
Hiki ni kitu ambacho nilikwambia hapo juu kwamba Sauli
angekifanya, nani ajuaye kuwa Mungu asingeghairi yale mabaya aliyomtajia
kupitia Samweli?
Basi mpendwa, tumuige mfalme wa Ninawi, ambaye hata hakujisumbua
kujua Yona yuko wapi baada ya kuyasikia maneno yake, yeye alijisumbua kujua
Mungu yuko wapi baada ya kusikia yale maneno ya balaa yaliyotamkwa na Yona
alipokuwa ‘amepaniki’ kwa kulazimishwa kufanya kazi ambayo asingependa
kuifanya.
Mtafute Mungu mpendwa, usiwatafute akina Yona ambao kwanza
wanatamani uangamie hata leo; usipate nafasi ya kutubu; usije ukachana mavazi
yao kwa kuwalazimisha wakuombee wakakulaani kama Samweli alivyomlaani Sauli.
Bado unaweza kujidhili mbele za Bwana na akakuhurumia na
akawatumia kina Isaya haohao kukuletea neno la ushindi kama ambavyo Isaya
alimpelekea Hezekia habari za kuongezewa miaka. Haleluya!
Usikose
kuendelea na sehemu zinazofuata kwa ajili ya tafakari zaidi kuhusu habari hizi
za kugeukia ukutani. Unaweza pia kusambaza somo hili na kuwaalika wenzio
wengine walisome.
No comments:
Post a Comment