Bwana Yesu Kristo Asifiwe!
Lengo la somo hili ni kukupanulia tu ufahamu wa watu
mbalimbali katika Biblia na kukupa kuwajua kwa undani wao. Hii ni muhimu ili
kukusaidia kuelewa namna Biblia inavyopangilia matukio na namna Mungu
alivyokuwa akifanya kazi yake kwa kufuata vizazi.
Leo nataka nimlete kwako mtu mmoja kwenye Biblia ambaye
yawezekana umesoma habari zake lakini hujapata kumfahamu vizuri – YETHRO “Mkwewe
Musa”.
Kutoka 3:1 inasema: “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi
la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza
kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu”.
Msitari huu unataja mtu huyu aitwaye Yethro kwamba
alikuwa ni kuhani wa Midiani lakini
pia alikuwa ni mkwewe Musa. Jina “Yethro”
linajitokeza mara 10 tu kwenye Biblia yote na mara zote hizo ni kwenye Kitabu
cha Kutoka tu (Kutoka 3:1; 4:18; 18:1; 18;2; 18:5; 18:6; 18:9; 18:10; 18:12).
Utaona hapo kuwa ni Mistari tisa (9) niliyoorodhesha lakini jua kwamba katika Kutoka
4:18 jina hili linajitokeza mara 2 kwenye msitari huo na hivyo kukamilisha
idadi ya jina hili kujitokeza mara kumi (10) katika kitabu hiki cha Kutoka.
Lakini unapoifuatilia historia ya mtu huyu kwenye
Biblia utagundua kuwa Yethro halikuwa
jina la mtu bali ni cheo. Kama ningetaka kukueleza kwa kiingereza ningesema
kuwa: “Jethro was not a name of a person
but a title”. Unashangaa! Hivyo ndivyo ilivyo.
Ni kama neno Farao. Watu wengi wanafikiri kuwa Farao lilikuwa jina la mfalme wa Misri – hapana! Farao kilikuwa ni cheo cha mtu mwenye mamlaka ya kifalme juu ya Misri. Kwa hiyo mtu mwenyewe alikuwa na jina lake lakini cheo chake ndicho kiliitwa Farao. Ni kama ambavyo tunatumia neno “Rais” kwenye ulimwengu wa sasa. Neno "Rais" ni cheo na mtu anayekuja kutumikia cheo hicho anakuwa ana jina lake binafsi. Mfano, John Pombe Magufuli ni jina binafsi la Rais wa sasa wa Tanzania. Lakini Rais sio jina la John Pombe Magufuli ila ni cheo chake. Nimetaka kuliweka sawa hili jambo ili kukurahisishia kuelewa habari za Yethro kama Cheo na si kama jina binafsi la mtu.
Maana ya Yethro ni ipi?
Yethro kwa kiebrania ni ‘Yithrow’ ambalo kwa tafsiri ya kiingereza linamaanisha “his excellence” yaani mtukufu. Na kama tulivyoona kwenye Kutoka
3:1, mtu huyu alikuwa ni kuhani wa
midiani. Kwa hiyo Yethro ilikuwa ni cheo kilichoambatana na nafasi yake kama
Kuhani wa midiani. Hivyo kama asingekuwa kuhani wa midiani basi mtu huyu
asingetambulishwa kama Yethro bali angetajwa kwa jina lake binafsi.
Lakini kuwa kuhani tu haitoshi kutueleza undani wa
nafasi aliyokuwa nayo mtu huyu.
Tumesema kuwa maana ya Yithrow ni his excellence –
mtukufu. Sasa katika mazingira ya kawaida neno hili hutumika kuwatambulisha
watu wenye mamlaka ya kifalme si makuhani. Huwa tunaona marais wanaitwa “Mtukufu
Rais” au “Mtukufu Mfalme” n.k. lakini hatuoni neno mtukufu likitumika kuwataja
makuhani. Hii inatupa kufikiri zaidi kuhusu huyu Yethro.
Kamusi kadhaa za Biblia zinaeleza kuwa licha ya kuwa
kuhani, Yethro alikua pia ni mfalme wa Midiani. Kwa asilimia kubwa hii inaleta
maana halisi ya neno Yethro. Sasa ukichukua nafasi yake kama kuhani
ukachanganya na nafasi yake kama mfalme utapata kuelewa ni kwa nini Yethro
alikuwa na hekima ya kumshauri Musa kuhusu masuala ya uongozi kule jangwani.
Angalia jinsi Kutoka
18:13-24 inavyosema:
Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie
hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe
Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili
uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama
kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu
hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua
kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe
Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na
hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi
wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na
awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu
maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia
ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo
utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa
kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa
maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue
watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila
neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi,
nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu
akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda
mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote
aliyokuwa amemwambia.
Hii hekima ya uongozi ambayo Yethro alimpa Musa
inatuthibitishia kuwa lazima mtu huyu alikuwa ni kiongozi mahali fulani. Na
kama tulivyoona hapo juu, mtu huyu anatajwa kuwa alikuwa ndiye mfalme wa Midiani. Na hivyo hekima aliyompa Musa lazima ilitokana na uzoefu aliokuwa
ameupata kwa miaka yote aliyotumika kama mfalme wa midiani. Naamini tunaenda
pamoja!
Jina la mkwewe Musa ni nani?
Kama Yethro sio jina la mtu bali ni cheo, basi ni
vizuri tulijue jina sahihi la huyu mkwewe Musa. Kutoka 2:16-18 inatuambia kuwa
jina la huyu kuhani wa Midiani ambaye Musa alioa mwanawe alikuwa anaitwa Reueli.
Basi kuhani
wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza
birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. Wachungaji wakaja
wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. Walipofika kwa Reueli baba yao,
akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?
Kwa hiyo baba yao akina Sipora alikuwa anaitwa Reueli sio Yethro. Hesabu 10:29 inathibitisha jambo
hili kwa kutuambia kuwa Reueli Mmidiani ndiye alikuwa mkwewe Musa. Reueli kwa kiebrania maana yake ni rafiki wa Mungu (a friend of God). Kwa hiyo
tunaweza kusema kuwa Reueli ndilo lilikuwa jina la baba-mkwe wake Musa na Yethro
kilikuwa cheo chake kama kuhani na mfalme.
Reueli/Yethro ni uzao wa nani?
Kutoka 2: 15 inatueleza
kuwa Musa alipokua anaukimbia uso wa Farao baada ya kumwua yule Mmisri alienda
katika nchi ya Midiani. Kwa hiyo Midiani ilikuwa ni nchi inayojitegemea na
ilikuwa na mfalme na kuhani wake aitwaye Yethro/Reueli. Kwa hiyo ili tuweze
kufuatilia uzao wa Reueli vizuri lazima tuelewe hili taifa la Midiani lilitokea
wapi.
Pana mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wanatheolojia juu
ya alikotokea huyu Reueli. Lakini acha sisi tuangalie kile Biblia inachosema.
Mwanzo 25:1-3 unasema hivi:
Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake
akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua.
Nataka tumuangalie huyo mtoto anayeitwa Midiani kwenye huo uzao wa Ibrahimu.
Baada ya Sara kufa, Ibrahimu alioa mke mwingine aitwaye Ketura na akamzalia
wana. Miongoni mwa wazao wa Ibrahimu waliopatikana kwa Ketura alikuwa ni huyu
aliyeitwa Midiani. Sasa ukifuatilia
Biblia vizuri utaona kuwa huyu Midiani naye alizaa wana na baadaye walikuja
kujulikana kama jamii ya Wamidiani. Hawa Wamidiani ndio waliomnunua Yusufu
mikononi mwa Waishmaeli wakaenda kumuuza kwa Potifa huko Misri (Mwanzo 37:28, 36).
Kwa mpangilio wa matukio ulivyo inaonekana
kuwa Midiani ilikuwa karibu na Misri na ndio maana hawa Wamidiani waliweza
kwenda kumuuza Yusufu huko Misri. Inawezekana ndio sababu pia Musa akakimbilia
huko alipotoka Misri.
Sasa kama Midiani alikuwa ni mzao wa
Ibrahimu, na Yethro alikuwa kuhani na mfalme wa Midiani maana yake ni kuwa mtu
huyu aitwaye Yethro alikuwa ni wa uzao wa Ibrahimu. Ukilitazama jambo hili kwa
jicho la rohoni utagundua kuwa kulikuwa na uhusiano wa kiuzao kati ya Musa na
Yethro na ndio maana Mungu alimwongoza Musa akimbilie huko pale alipotoka
Misri.
Ukitaka kuiona hii kitu kwa ndani zaidi
jiulize Sipora – mkewe Musa- alipata wapi ufunuo wa kumtahiri mtoto pale Bwana
alipotaka kumwua Musa? Kutoka 4:24-25 inasema:
Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa
kulala, Bwana akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na
kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe
u bwana arusi wa damu kwangu mimi.
Sasa Biblia inatuambia kuwa agano la
kutahiri watoto aliliweka Mungu kati yake na Ibrahimu na uzao wote wa Ibrahimu.
Mwanzo 17:10-14 inasema:
Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na
wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. Mtatahiriwa
nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na
ninyi. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi
vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao
wako. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na
agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele. Na mwanamume
mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake;
amelivunja agano langu.
Kwa hiyo suala la kutahiri watoto lilikuwa suala la Mungu
na uzao wa Ibrahimu. Sasa swali la kujiuliza ni kuwa: Kama Sipora hakuwa wa uzao
wa Ibrahimu alipata wapi ufunuo wa kujua kuwa jambo lililofanya Bwana atake kumwua
Musa njiani ilikuwa ni kwa sababu ya kutokumtahiri mtoto wao? Hii
inatufikirisha na kutufanya tuamini kuwa Yethro alikuwa wa uzao wa Ibrahimu
kupitia kwa Midiani mtoto wa Ketura na kwa hiyo alikuwa amewafundisha watoto
wake agano la Mungu na uzao wa Ibrahimu na hii ndiyo ilimpa Sipora kujua
umuhimu wa kumtahiri mtoto.
Nimekueleza haya yote ili upate kujua kuwa Musa
hakukimbilia kwa Midiani kwa bahati mbaya na wala hakukutana na Yethro kwa
nasibu bali Mungu mwenyewe ndiye aliyekuwa anamuongoza.
Mambo ya kujifunza kutoka kwa
Yethro
1. Karibisha wageni na uwe mkarimu kwa watu wote hata kama huwajui maana hujui wamebeba baraka gani ndani yao. - Kutoka 2:20-21
2. Mfuate Mungu wa kweli popote aliko hata kama wewe ulikuwa na Mungu wako mwanzoni. – Kutoka 18:1-12
3. Tumia uzoefu ulionao ili kuwasaidia wengine waweze kuvuka mahali unapoona wamekwama. Kutoka 18:13-24
4. Wajulishe na uwafundishe watoto wako agano lililopo kati yako/yao na Mungu ili wajue namna ya kulisimamia na kulifuatilia. Kutoka 4:24-26
1. Karibisha wageni na uwe mkarimu kwa watu wote hata kama huwajui maana hujui wamebeba baraka gani ndani yao. - Kutoka 2:20-21
2. Mfuate Mungu wa kweli popote aliko hata kama wewe ulikuwa na Mungu wako mwanzoni. – Kutoka 18:1-12
3. Tumia uzoefu ulionao ili kuwasaidia wengine waweze kuvuka mahali unapoona wamekwama. Kutoka 18:13-24
4. Wajulishe na uwafundishe watoto wako agano lililopo kati yako/yao na Mungu ili wajue namna ya kulisimamia na kulifuatilia. Kutoka 4:24-26
Yesu Kristo akubariki sana!
Endelea kufuatilia blog hii ili ujue nani anafuata
katika mfululizo huu!
No comments:
Post a Comment