Utangulizi
Mpendwa
msomaji, tunaendelea na mwendelezo wa mafundisho yetu ya somo la Kwa habari ya
zinaa, na sasa tupo sehemu ya sita; sehemu ya sita inaendelea kutoka
tulipoishia kwenye sehemu ya tano. Na kama utakuwa umekosa sehemu
zilizotangulia tafadhali bonyeza hapa ili uweze kupata mtiririko mzuri. Kuna
watu wanaweza kuwa wanapata shida kuhusu mana ya neno zinaa linapotumika katika
somo hili; lakini tunatumia neno zinaa kiujumla; ikumbukwe katika sehemu ya
kwanza tuliweka utangulizi wenye kuelezea maana hii kama ifuatavyo:
ZINAA
NI NINI?
Katika
biblia zinaa inatumiwa kumaanisha tendo la kufanya mapenzi na mtu asiyekuwa
mkeo wala mumeo, ukiwa tayari mwanandoa. Lakini katika somo hili tutatumia neno
la zinaa kumaanisha kufanya mapenzi isivyo halali kwa ujumla, ambapo kuna
wakati neno zinaa litatumika kumaanisha uasherati, yaani kufanya mapenzi kabla
ya ndoa, kuna wakati litatumika kumaanisha pia tendo la kufanya mapenzi na mtu
asiye mumeo wala mkeo wakati wewe umeoa au umeolewa.
Upendo endelevu na upendo usio endelevu
Wapo watu kwa kutokujua wanawapenda wenzi wao kiasi cha
kuwapa kila kitu wanachohitaji. Huu nao ni upendo. Lakini ni upendo usio
endelevu. Si endelevu kwani mwisho wake ni madhara kwetu na kwa tuwapendao; Au
tuliweke hivi, tuchukulie ule upendo unaopelekea watu kuzini nao ni upendo,
lakini tuuite upendo usio endelevu. Kisha
ule upendo ambao ni wa kumfanya mtu atimize makusudi ya Mungu ni upendo endelevu. Upendo usio endelevu
hupelekea matumizi yasiyo endelevu na upendo ulio endelevu hupelekea matumizi
yaliyo endelevu. Ukimpenda mpenzi wako hadi ukaamua kuzini naye kabla ya ndoa
wewe una matumizi yasiyo endelevu na ukimpenda mpenzi wako ukamheshimu na
kumtunzia uhusiano wake na Mungu hadi mkafunga ndoa wewe una matumizi endelevu.
Mwenye matumizi yasiyo endelevu ni yule anayemtumia
mpenzi wake kuzini; kwa sababu anamtumia, na anamfurahisha na kujifurahisha
yeye, ila matumizi yale yanamfanya mwenzi wake asidumu na usitawi wake kiroho
uathirike. Anachoka na kupoteza thamani mbele za Mungu na mbele za mwanadamu
kwani ‘anapata jeraha na kuvunjiwa heshima, wala fedheha yake haitafutika’.
Lakini pia kuzini kusiko na baraka za ndoa ni matumizi
yasiyo endelevu ya mwenzi wako kwani unaua umilele ndani yake, unaangamiza nafsi
yake na kumfanya awe ni mtu ambaye ataishi tu hapa duniani na anakuwa amepoteza
nafasi ya kuingia mbinguni. Sasa unapata picha ya kwanini tunasema kuzini kabla
ya ndoa au nje ya ndoa ni matumizi yasiyo endelevu au upendo usio endelevu.
Hapa tunamaanisha kuwa upendo endelevu ni ule upendo
ambao siyo tu unajali furaha ya mwenzi kwa wakati huu, bali kwa wakati ujao na
milele yote, wakati kinyume na hapo, ndo kwenye upendo usio endelevu, ambao
unajali tu furaha ya wakati huu.
Upendo usio endelevu ni kumpenda mwanafunzi na kumzinisha
na kuharibu masomo yake na kumwacha analia.
Upendo usio endelevu ni kumpenda mtu na kumharibia ndoa
yake na kuzini naye na kusababisha aachike arudishwe kwao wakati wewe
uliyemponza mwenzio ndoa yako iko salama.
Upendo usio endelevu ni ule unaopelekea wewe kumfarikisha
mtu na Mungu wake kwa kumtumbukiza katika zinaa na uasherati na kupelekea
mwenzako kukosa Baraka za Mungu kwa sababu ya tamaa zako za muda mfupi.
Angalia; na utagundua kuwa watu wengi wanaingia katika
mahusiano wakiwa na upendo usio endelevu.
Chunguza mahusiano yako, jaribu kuondoa kila kitu ambacho
kina ishara ya upendo usio endelevu, na jaribu kuvunja kila mahusiano ambayo
siyo endelevu kama mwenzi wako anakataa na kung’ang’ania tabia zisizo endelevu.
Upendo ulio endelevu ni upendo ambao unajali mafanikio ya
mtu ya mwili na roho.
Upendo ulio endelevu hauegemei na kutegemea furaha za
muda mfupi, ambazo hazina tija ya milele.
Upendo ulio endelevu una heshima, upendo ulio endelevu
una subira, upendo ulio endelevu hautafuti mambo yake wenyewe, upendo ulio
endelevu ndio hasa unaostahili kuitwa upendo na ndio ulioongelewa kwenye
1Wakorintho 13
1Wakorintho
13:1-8a
Nijaposema kwa lugha
za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu
uvumao.
Tena nijapokuwa na
unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi
cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.
Tena nikitoa mali
zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama
sina upendo, hainifaidii kitu.
Upendo huvumilia,
hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;
haukosi kuwa na
adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;
haufurahii udhalimu,
bali hufurahi pamoja na kweli;
huvumilia yote;
huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
Upendo haupungui neno
wakati wo wote;
Huo unaoongelewa hapo juu ndio upendo endelevu, kwa
misingi ya imani lakini pia ukiutumia upendo huu katika kila sehemu, ni aina ya
upendo inayolipa sana.
Tukisema upendo huvumilia, hatutaki mtu anayejifanya
anakupenda na anataka akuoe na anataka azini na wewe leoleo. Huyo atakuwa
amekosa uvumilivu. Tena anakuwa amekosa kuwa na adabu; tena huyo atakuwa
anatafuta mambo yake mwenyewe, tena haoni uchungu kama wewe unaweza kupotea na kuishia
kuzimu, halafu pia anafurahia udhalimu na kuikataa kweli. Sawa dada?
Kama mtu unamwambia kuwa unamwamini Mungu na hujamjua
mwanaume na hutaki mjuane kabla ya ndoa, halafu hakuamini, huyo hakupendi,
kwani upendo huamini yote.
Ndiyo maana watu wengine wanakuwa wanashangaa sana kwamba
mbona mtu fulani ni malaya na tumeshamwambia mumewe amuache lakini tunashangaa
hamuachi, lazima mjue kuwa upendo huamini yote, na yule mwanaume anaamini yote
anayoambiwa na mkewe kwamba yote hayo mnayosema siyo ya kweli.
Kwa hiyo katika somo letu hili, tunauita upendo ulio
endelevu upendo na upendo usio endelevu ni chuki, japo inaonekana kama ni
upendo. Ukimpenda mtu halafu ukamfanyia mambo yasiyo endelevu kama kuzini naye,
basi wewe umemchukia.
Hiyo ndiyo maana halisi ya upendo ndugu; usitumie
neno upendo vibaya, ujichunguze upendo ulio nao kama hautokani na upendo
wa Mungu kwetu, bado siyo upendo. Rudi msalabani ili Yesu akutengeneze na kukupa maana halisi ya upendo, kwani yeye ni Pendo na hakuna maana sahihi ya Upendo inayoweza kupatikana isipokuwa katika Yeye.
Usikose
kufuatilia sehemu zinazofuata za somo hili kwani bado Mungu ana mengi ya kusema
nasi; pia uwasambazie na wengine ili nao waipate kweli hii iwajenge mwili na
roho.
No comments:
Post a Comment