Friday, August 22, 2014

BIDII KATIKA KUMTAFUTA MUNGU

BWANA YESU ASIFIWE!

Mhubiri 11:6 
"Asubuhi panda mbegu zako, wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa, kama ni hii au hii, au kama zote zitafaa sawasawa"
Katika mstari huo hapo juu mhubiri anatufundisha kuwa na bidii na kutokukata tamaa akitumia mfano wa mpanzi.

Mhubiri anamsisitiza mkulima kutokusita katika kupanda mbegu, kuendelea kupanda kwa juhudi asubuhi mchana na jioni bila kujali uchovu wala kuangalia dalili ya mvua. Mkono ambao mhubiri anauongelea ni ule mkono ambao unapanda mbegu ambao unaweza kuzuiwa na mpanzi kwa sababu kadhaa anazoziona mwenyewe kuwa ni za msingi. kwa namna nyingine hapa mhubiri anamshauri mkulima kutokukubali sababu yoyote ile ambayo inaweza kumsababishia asipande hizo mbegu.

Ndivyo inavyotakiwa kuwa katika maisha yetu ya kila siku. Tukianzia kwenye upande wa mahitaji ya kila siku, mwanadamu hutakiwa kula kufua na kuoga bila kupunguza, ambapo akiacha kufanya lolote kati ya hayo afya yake huathirika kwa namna moja ama nyingine.

Vivyo hivyo tunatakiwa kutoacha mambo ambayo kwa hayo afya yetu ya kiroho inaimarika hasa suala la maombi. "Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumuomba Mungu siku zote wala wasikate tamaa" Luka 18:1 Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi mfano wa mwanamke aliyekuwa akienda kwa kadhi dhalimu, ambaye kwa kumsumbua yule kadhi, japokuwa yule kadhi alikuwa siyo mcha Mungu, aliamua kumpa haki yake. Kadhi anasema "Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima".

Ndicho kilichotokea, Haleluya, huyu mama nadhani alikuwa amemsoma mhubiri vizuri, asubuhi alipanda mbegu zake, wala jioni hakuuzuia mkono wake, kwa maana yeye hakujua ni zipi ambazo zingefaa sawasawa, kama ni ya asubuhi, ya jioni au zote.

Sasa kwa huyu mama zote zilifaa sawasawa, kwani zile za mwanzoni sio kwamba hazikufaa, bali ndizo zilizotumika kumchosha yule kadhi dhalimu. Ziliendelea kumsumbua na kumnyima usingizi-maana anaposema- "Kwa kuwa mjane huyu ananiudhi," tayari hii ni athari ya mbegu aliyoipanda huyu mama 'mbegu ya kumuendea kadhi daima'. Hapa nina ushuhuda fulani ambao ulinitokea mimi mwenyewe. Nilikuwa nasafiri kutoka Mpwapwa kwenda NARCO-kongwa, mahali ambapo kondakta wa basi aliniambia kuwa nauli yake ilikuwa ni shilingi elfu nne. Mimi nilimuomba yule kondakta anipunguzie kidogo kwani mimi nilikuwa na shilingi elfu tatu tu. Baada ya kumsihi alikubali na kwa bahati mbaya nikampa noti ya shilingi elfu tano. Baada ya kuona nimempa ile noti na nauli inayotakiwa ni shilingi elfu nne, alinirudishia shilingi elfu moja badala ya shilingi elfu mbili kama tulivyokubaliana nimlipe shilingi elfu tatu. Yaani yeye alikuwa amekata ile nauli halali ya shilingi elfu nne.

Hapo nilianza kumdai elfu moja yangu (siyo kwa ugomvi-kwa upole sana na unyenyekevu). "Wewe nauli ni shilingi elfu nne, unanipaje elfu tatu?" Alilalama yule kondakta. "Tulikubaliana elfu tatu lakini" Mimi nikawa namjibu. "Wenzio huwa wanasema hivyo huku wana elfu tatu kamili, sasa wewe unasema hivyo alafu una elfu tano bwana!" Nilicheka kimoyomoyo halafu nikaendelea kumdai. Aliniacha na kuendelea kukusanya nauli kwa watu wengine, kwa kuwa alikuwa anazunguka gari zima huku na huku; mbele na nyuma. Kila alipokuwa anafika nilipokuwa nimesimama, nilikuwa namkumbusha deni langu. Baada ya kumkumbusha mara nyingi, aliahidi kunipa kituo kilichofuata. Tulipofika Kongwa stendi ambapo ndipo alipokuwa ameahidi kunipa, sikumuona tena, ila kwa bahati tuliposafiri hadi NARCO ninaposhukia, nikiisha kushuka chini nikamuona na kumuendea tena, nikaendelea kumdai! "Sasa hivi mtu kama wewe unaweza ukakosa nauli hadi ukang'ang'ania elfu moja?" Sikujali maneno hayo ambayo yalikuwa ni baadhi tu ya majibu yake. Niliendelea kusisitiza makubaliano yetu na kuendelea kudai. Huwezi amini, yule jamaa alinipa elfu moja yangu saa ile! Hapa tunajifunza kuwa sio kwamba yule jamaa alikuwa mwema, la, ila alichoshwa na usumbufu niliokuwa namfanyia. Na mimi nikijua siri iliyokuwa katika kumsumbua mtu, niliendelea kudai bila kuchoka nikijua atachoka tu na kunipa na ndivyo ilivyokuwa.

Ni kwa kiasi gani umetumia muda mwingi kulifuatia hilo jambo ambalo linaonekana kutokufanikiwa? Je ni kila asubuhi tu? Basi unatakiwa kulifuatilia na jioni pia. Nilipokuwa nacheza 'gemu' ya mpira wa miguu kwenye kompyuta, moja ya kanuni nilizofundishwa ilikuwa ni kupiga mpira kwa ghafla kinyume na matarajio ya wachezaji wa timu pinzani. Na wewe pia waweza kulifanya hilo ulifanyalo kwa namna bora zaidi na isiyokuwa ya kawaida. Mtu mmoja akasema kuwa namna moja ya kufanya maajabu  katika dunia hii ni kufanya jambo la kawaida kwa namna isiyokuwa ya kawaida. Ili uelewe, tutumie mifano ya baadhi ya mambo tunayokutana nayo kila siku.

Katika maombi, muombaji ambaye anaomba kila siku mara tatu kama Danieli, baada ya mwezi mmoja mtu huyu hatakuwa sawa na anayeomba mara moja kwa siku kila siku. Kwa kanuni tuliyoitumia hapo juu, kuomba likiwa ni suala la kawaida, limefanywa na yule anayeomba mara moja kwa siku kwa namna ya kawaida na hivyo anapokea matokeo ya kawaida ambayo hata hivyo yatakuwa bora kuliko ya mwingine anayeomba mara moja kwa wiki. Lakini mtu huyo hawezi kuwa sawa na yule aombaye mara nyingi yaani mara tatu kwa siku, na nguvu ya Mungu ndani ya mtu huyu lazima iwe ni ya tofauti. Kwa nini? Ni kweli kwamba apandaye haba atavuna haba, endelea kupanda kwa bidii mpendwa. kwani kwa hakika katika Kristo hakuna bidii hata ya sekunde moja ambayo itakwenda bila kuzaa matunda yaliyo makubwa kuliko bidii hiyo!

Pia tulifahamu hili ya kuwa ushindi katika Kristo unamtaka mtumishi wa Mungu atumie bidii na wala asiwe mlegevu, kwani mashindano yoyote, huwataka washindani watumie nguvu zao zote bila kuzembea na yule anayetumia nguvu kuliko wote na akili pia, ndiye anayeshinda. Ni kweli kuwa yapo baadhi ya mashindano ambayo watu ambao ndio wenye juhudi kuliko wote hawashindi, lakini hayo ni mashindano ya udhalimu, lakini katika mashindano ya kumtafuta Mungu, kwa maana Mungu ni wa haki, na shetani yupo kulithibitisha hilo kwamba Mungu ni wa haki, Mungu anahitaji tutumike katika ukamilifu wote ili tuwe washindi wanaostahili kuvikwa taji.

Lazima kumuomba Mungu usiku na mchana, kufunga na kuutafuta uso wa Mungu katika kila jambo unalopitia, nguvu ya Mungu haiji kwa kulala tu na kuamka, bali kwa kuitafuta, kumbuka, ufalme wa Mungu wapatikana kwa nguvu nao wenye nguvu wauteka. Ukitaka kujenga msingi wa utumishi imara lazima na njia yako ya kuufikia utumishi uliotukuka iwe ni imara na halali, hakuna namna ambayo unaweza kuwa na nguvu ya Mungu na kukisogelea kiti chake kwa ujasiri bila kuutafuta uso wake kwa bidii mchana na usiku. 

MUNGU AKUTIE NGUVU!

No comments:

Post a Comment