OUR DAILY MANA
UWEZA
WA KUFANYIKA MWANA WA MUNGU
HALELUYA!!
Karibu tena ndugu yangu
katika mfululizo wa masomo haya yenye lengo la kufungua na kupanua ufahamu na
uelewa wetu juu ya neno la Mungu. Katika somo lililopita tuliangalia juu ya
kasi ya shetani kuwapeleka watu kuzimu na tukaona kuwa watu wa Mungu
wanachukuliwa kuwa mateka wa nguvu za giza kwa kukosa maarifa ya neno la Mungu.
Leo nataka tuangalia juu ya nguvu au uweza unaombadilisha mtu na kumfanya mwana
wa Mungu.
Ukisoma Biblia yako
vizuri utagundua kuwa, kabla mtu hajaookoka anakuwa akitumikia mambo ya dunia
na anasa zake na kufanya mambo yanayomchukiza Mungu lakini saa anapookoka na
kujikabidhi kwa Bwana, Mungu huleta badiliko kamili kwenye maisha yake na
kumwingiza katika mfumo mpya wa maisha. Mtume Paulo katika Tito 3:3 anasema:
“Maana hapo zamani
sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku
tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda,
tukichukiza na kuchukiana.”
Maandiko haya yanatuonesha aina ya maisha
ambayo mtu huishi kabla hajampokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake. Paulo anasema
kuwa hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili. Akili inayozungumzwa hapa ni
suala la kumtafuta Mungu na kuishi sawa na mapenzi yake, mtu akiacha kumtafuta
Mungu na kuenda katika njia zake mwenyewe, Biblia inasema huyo ni mjinga na
hana akili. Zaburi 53:1 inasema “Mpumbavu amesema
moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna atendaye
mema.” Kwa hiyo yule asemaye kuwa hakuna
Mungu, na wale watendao uovu na ufisadi na kuchukiza na kuacha kutenda mema,
Zaburi inasema ni wapumbavu. Vile vile Mithali
6:32 insema “Mtu aziniye na mwanamke hana akili
kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.” Kwa hiyo wanzinzi
wote Biblia inasema hawana akili kabisa kwa sababu wanafanya jambo
litakalowaangamiza wenyewe. Cha ajabu zaidi ni kuwa Biblia inawafananisha watu
wa namna hizi (yaani wasio na akili na wapumbavu kama maandiko yasemavyo) na
wanyama wapoteao. Zaburi 49:20 insema “Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama
wapoteao.”
Nimekupitisha kwenye maandiko hayo ili uone kuwa Mungu
anawafananisha watu walio nje YA Kristo, wale watendao maovu, na wanayama
wapoteao. Kwa hiyo suala la kumpa Yesu maisha yako ni suala la muhimu sana kama
kweli unataka kuishi sawa na mpango wa Mungu kwako.
Baada ya kuangalia jambo hilo sasa tuende kwenye kiini
cha somo letu. Lengo la somo hili ni kutaka kuangalia ni kitu gani muhimu sana
kinachomwezesha mtu kuendelea na maisha ya wokovu baada ya kuwa amempokea Yesu
Kristo awe Bwana na Mwokozi wake.
Utakubaliana name kuwa kuna idadi kubwa sana ya watu
ambao waliopookoka walikuwa na kiu sana ya kukua kiroho na kuishi katika
utakatifu lakini wengi wameanguka tena katika dhambi na wengine wameshindwa
kabisa kusimama tena. Mi binafsi ninawafahamu watu kadhaa waliookoka vizuri
sana lakini walishindwa kuendelea na maisha ya kiroho na kurudi katika dhambi. Hii
ikanipa kujiuliza sana juu ya nini kinachohitajika ili mtu aliyeookoka aendelee
kusimama imara katika Kristo. Ndipo neema ya Mungu iliponifunulia kujua kuwa
kuishi katika utakatifu wa kristo ni jambo linalohitaji kitu fulani zaidi ya
kuokoka tu. Na hicho ndicho tunachotaka tujifunze sasa.
Kitabu cha Yohana
1:12 kinasema hivi:
Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto
wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.
Haya
maandiko yanatuambia kuwa wale waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Jambo ninalotaka
uone hapa ni juu ya kile kinachoitwa “UWEZO WA KUFANYIKA”. Haya maneno yametafsiri
kwenye baadhi ya tafsiri ya kiingereza kama “POWER TO BECOME” au “AUTHORITY TO
BECOME”.
Haya
maneno yanatufunulia kuwa suala la watu hawa kuwa wana wa Mungu halikutokana na
wao kumpokea Kristo ila lilitokana na uwezo waliopewa na Mungu wa kufanyika
watoto wa Mungu. Lile neno “kufanyika” linatupa picha ya kuwa uwezo waliopewa
watu hawa ulikuwa na nguvu ya kuwabadilisha kutoka kwenye utu wao wa kwanza na
kuwafanya watoto wa Mungu. Kwa hiyo kumbe sio kwamba kuokoka ndiko kunakomfanya
mtu awe mwana wa Mungu, ila kuokoka ni hatua ya kwanza inayomruhusu Mungu
kukuletea juu yako uwezo wa kubadilishwa ili uwe mwana wa Mungu.
Naona
hujaelewa sawasawa. Hebu ngoja tujifunze kutoka kwa Yesu. Soma pamoja name kitabu
cha Luka 3:21-22. Biblia inasema hivi:
Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa
mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti
ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.
Nimeamua kukoleza sehemu za maneno haya kwa makusudi ya kukuonesha
kile kilichofanyika pale Yordani. Biblia inasema Yesu alipokwisha kubatizwa
alianza kuomba. Alikuwa anaomba nini? Biblia haituambiii alikuwa anaomba nini,
lakini majibu ya maombi yake yanatupa kujua kuwa alikuwa anaomba juu ya
kuhitaji kwake kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu. Sasa cha ajabu ni kuwa Roho
aliposhuka juu yake tu na Mungu akatangaza hapo hapo kuwa huyu ni mwanangu
mpendwa wangu.
Swali la kujiuliza hapa ni kuwa Mungu alitaka kutuonesha nini? Kwa
nini asinyamaze tu kimya maana tayari kwenye kuzaliwa kwake tulikwisha ambiwa
kuwa ni mwana wa Mungu. Na kwa nini Mungu asitangaze hivyo kabla ya Roho
Mtakatifu kuja juu yake? Ni nini kilichomfanya Mungu asubiri kwanza Roho
Mtakatifu ashuke juu ya Yesu ndipo akatangaza kuwa huyu ni mwanangu?
Maswali haya yanatufungua macho kujua kuwa Mungu alitaka tujue
kuwa ni uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu ndio unaomwezesha kufanyika kuwa mototo
wa Mungu. Mtu anaweza akaokoka lakini asipojazwa Roho Mtakatifu mtu huyo
anakuwa bado hajafanyika mototo wa Mungu. Ndiyo maana Biblia inasema
waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Na Yesu mwenyewe
anatuambia kuwa uwezo huo ni nguvu ya Roho Mtakatifu. Luka 24: 45 Yesu anasema: “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu;
lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Yesu aliwazuia wanafunzi wake wasitoke mjini mpaka wamevikwa uwezo
utokao juu. Jambo la kujiuliza ni kwa nini aliwazuia? Tunachogundua ni kuwa
bila Roho wa Mungu hatuwezi kuishinda dhambi wala hauwezi kumpendeza Mungu. Rumi 8:8 inasema “Wale waufuatao mwili
hawawezi kumpendeza Mungu.” Na Warumi 8:14 inasema “Kwa
kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu”
Kwa hiyo kama mtu haongozwi na Roho wa Mungu huyo hawezi
kumpendeza na Mungu na hawezi kuwa mwana wa Mungu. Sasa hauwezi kuongozwa na
Roho wa Mungu, kama Roho wa Mungu hayuko ndani yako. Ni lazima kwanza Roho aje
juu yako ndipo anaweza kukufanya uwe mwana wa Mungu. Warumi 8: 15 inasema “… bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa
hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.”
Kumbe ni Roho wa Mungu ndiye anayetufanya wana wa Mungu. Kuokoka ni
hatua ya kwanza ya kumruhusu Roho wa Mungu apate nafasi ndani yetu, kisha pindi
tunapovikwa Roho wa Mungu hapo ndipo tunapopewa uwezo wa kufanyika wana wa
Mungu. Katika wagalatia 4:6 Paulo
anasema “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe
mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.”
Ooooh kumbe ni uwezo wa Roho Mtakatifu ndio unaotuwezesha kuwa
wana wa Mungu kweli kweli na kutuwezesha kuishi bila dhambi. Ikiwa hatuna Roho
wa Mungu basi nguvu yetu ya kumshinda shetani inakuwa kidogo sana na baada ya
muda mchache mtu hujikuta ameanguka na kumwasi Mungu. Ili uishi katika wokovu
na kumpendeza Mungu basi ni lazima uombe Roho wa Mungu aje juu yako. Yesu
anatupa mfano mzuri. Yeye alipokwisha tu kubatizwa alianza kumwomba Mungu na
Mungu akamvika Roho Mtakatifu aliyekuja juu yake na kumfanya kuwa mwana wa
Mungu.
Watu wengi leo wanaokoka na kisha kuanguka kwa sababu walipookoka
hawakujazwa Roho Mtakatifu hivo wakakosa nguvu ya kufanyika watoto wa Mungu. Watumishi
wengi hupenda kuwahubiria watu waokoke lakini wakiisha kuokoka husahau
kuwaombea nguvu ya Roho Mtakatifu ili wafanyike kuwa watoto wa Mungu. Katika Matendo 19: 2, 6 Paulo anatuonesha
umuhimu wa watu kumpokea Roho Mtakatifu wanapookoka. Biblia inasema
akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La,
hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia… Na Paulo, alipokwisha
kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa
lugha, na kutabiri.
Kwa hiyo uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu ndio uwezo pekee
unaomfanya mtu huyo kuweza kuishi katika utakatifu na kumpendeza Mungu na kuwa
mwana wa Mungu.
NAKUOMBEA UMPOKEE ROHO MTAKATIFU SASA KWA JINA LA YESU.
YESU NI BWANA
YESU NI BWANA
Natowa asante kwa mafundisho
ReplyDeleteAsante Mutumishi Kwa mafundisho yako,inaeleweka vizuri.
ReplyDelete