OUR DAILY MANA
KASI YA KUZIMU KUWAMEZA WATU
Bwana
wetu Yesu Kristo apewe sifa!
Karibu
tena mpendwa katika Bwana katika safu hii ya kuyachunguza maandiko. Katika somo
lililopita tuliangalia juu ya kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu na tukaona kuwa
ni pale tu unapoamua kumweka Mungu mbele ndipo mambo yako yanapofanikiwa.
Katika somo hili nataka tuangalie kitu kingine muhimu sana katika maisha yetu
ya kiroho. Tunachojifunza leo ni juu ya kasi (speed) ambayo shetani anayo
katika kuwavuta watu kuenda kuzimu.
Ni
wazi utakubaliana nami kuwa kasi ya kuongeza maasi duniani hivi sasa ni kubwa
kuliko miaka ya nyuma na cha ajabu ni kuwa kila siku zinaposogea ndivyo na
maasi mengi yanavyogundulika na kuwavuta watu wengi. 1 Timotheo 4:1 inasema
“Basi Roho anena waziwazi ya
kwamba nyakati za mwisho wengine
watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya
mashetani.” Mtume Paulo anazungumza na Timotheo kwamba siku za mwisho wengine
watajitenga na imani; maana yake ni kuwa watu wengi wataacha kumfuata Mungu na
kuamua kufuata tamaa za dunia na mambo ya mwili ambayo mengi yake ni mafundisho
ya mashetani.
Leo hii ukiangalia na kuchunguza
kwa makini utagundua kuwa asilimia kubwa ya watu kwenye kanisa wamerudi nyuma
kiroho au hata wamepotea kabisa na kuamua kumwacha Mungu. Nimeshuhudia watu
kadhaa ambao walikuwa vizuri sana kwa Mungu; walikuwa waombaji wazuri sana;
walikuwa wahubiri wazuri sana; au hata walikuwa wakitumiwa na Mungu kwa ishara
na miujiza mingi, lakini wameanguka katika dhambi hasa zinaa. Hii ikanifanya
nianze kuchunguza ni nini kinaendelea kwenye ulimwengu wa roho.
Ufunuo
12:12 inasema hivi: “Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka
kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana
wakati mchache tu.” Biblia
inasema shetani alipofukuzwa mbinguni akashuka kwetu (duniani), akiwa na
ghadhabu nyingi huku akijua kuwa ana muda mchache tu. Swali la kujiuliza ni
kuwa shetani ana muda mchache wa kufanya kitu gani? Na ghadhabu yake ni juu ya kitu
gani?
Kitabu cha Isaya 5:13-14 inasema: “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu
sana. Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa
yake, kumefunua kinywa chake bila
kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni
mwao, hushuka na kuingia humo.”
Mungu anazungumza kwa
uchungu akisema kuwa watu wangu wamechukuliwa mateka kwa kukosa maarifa na kwa
sababu hiyo kuzimu kumeongeza tama yake, na kumefunua kinywa chake bila kiasi.
Huu msitari umetafsiriwa hivi kwenye kiingereza:“therefore, sheol has enlarged itself, and opened its mouth beyond
measure.” Hii unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili kwamba kuzimu imeongeza
nafasi yake (au imejipanua), na imefungua kinywa chake kupita kiasi.
Hii ni ajabu sana,
yaani shetani kwa kujua kuwa watu wa Mungu wamekosa maarifa ameamua kuongeza
nafasi ya kuwapokea watu wanaoenda kuzimu na amefunua kinywa cha kuzimu kupita
kiasi ili watu wote wasio na maarifa ya Mungu waingie humo. Hii ndiyo
tunayojifunza kuwa ameshuka kwetu mwenye ghadhabu nyingi akijua kuwa ana muda
mchache. Kasi ya shetani kuwavuta watu kwenye uovu ni kubwa kuliko kasi yetu
tuliyonayo katika kumpinga. Yakobo 4: 7
inasema “mtiini Mungu, mpingeni shetani naye atawakimbia.” Hili neno mtiini
kwenye kiingereza wametumia neno submit
yourselves to God. Maana yake jikabidhi kwa Mungu kisha mpinge shetani naye
atakukimbia.
Kanisa la leo
linamezwa na kuzimu kwenye mambo mengi. Watu wameona wokovu kuwa ni mazoea.
Wameona kuomba kuwa ni jambo la watu Fulani wanaoitwa eti wanamaombi. Watu
maeomua kuutoa muda wao mwingi kufanya mambo ya dunia huku wakimsahau Mungu.
Oooohh nakuambia ndugu hujajua kasi ya shetani kukushambulia ilivyo, maana
laity ungalijua basi ungalikesha katika kumtafuta mungu. Jambo moja la ajabu ni
kuwa “Mtu yeyote asiye mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo ni mateka wa nguvu za
giza. Huo ndio ukweli na haijalishi awe anajijua au hajijui, awe anaamini au
haamini ukweli ndio huo. Unaweza kuwa mateka wa
nguvu za giza na shetani akawa anakutumia katika mipango yake bila wewe kugundua. Aliyesalama ni yule
tu aliyemwaminifu kwa Bwana.”
Huduma za watu
zimepotea, uzinzi umeongezeka katika kanisa, maasi yanazidi kuwa mengi lakini
bado kanisa linaona ni jambo la kawaida tu. Watu wameona kuwa unaenda kwenye
maombi kwa toba kila siku kuwa ni jambo la kawaida. Aisee Mungu atusaidie,
maana shetani anafanya kazi akijua kuwa ana muda mchache lakini sisi tunampinga
kwa uzembe tukufikiri kuwa tuna muda mwingi. Mitego ambayo shetani ameweka ili
kuwaingiza watu kuzimu ni mingi mno lakini bado watu hawashituki. Kweli watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa
maarifa.
AMKA LEO JIFUNGE KIUME MAANA NI WAKATI WA HATARI
YESU PEKEE NI NGOME IMARA
Great,
ReplyDeleteGod bless u man of God.