“…kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa
ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake…” (Hesabu 35:33)
Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe,
Utangulizi
Tunamtukuza Mungu Baba yetu kwa neema aliyotupa kupitia Mwana wake pekee
Yesu Kristo kutupa nguvu za Roho wake Mtakatifu ili tupate kuyatafakari
maandiko pamoja. Leo tunaangalia suala moja muhimu sana katika uhai na ustawi
wa taifa (nchi), nalo ni: Madhara ya umwagaji damu katika nchi. Msitari
tuliouweka hapo juu unatupa mahali pa kuanzia katika kulitafakari suala hili
muhimu. Ili tuende pamoja vizuri katika somo hili, ngoja tuangalie mistari
kadhaa katika Biblia.
Bali nyama pamoja na uhai, yaani,
damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa
kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu
nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga
damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano
wake Mungu alimfanya mwanadamu.
Kisha katika Hesabu 35: 30, 33-33 Mungu akasema:
Mtu awaye yote
atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu
hata akafa… Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia
nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu
iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga. Kwa hiyo msiitie unajisi nchi muiketiyo,
ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi Bwana nakaa kati ya wana wa
Israeli.
Nimekuwekea
mistari hii ya utangulizi ili uone mambo yafuatayo:
- Damu ni uhai wa mtu. Kumwaga damu ya mtu ni sawa na kumwaga uhai wa mtu huyo.
- Damu ikimwagika mahali popote inaanza kudai malipizi (kisasi).
- Gharama ya damu kumwagika ni damu nyingine tena imwagike (atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu).
- Damu ya mtu ikimwagika katika nchi inaitia hiyo nchi unajisi.
Mambo
haya yanatupa kujua kuwa damu ya mtu ina thamani kubwa sana mbele za Mungu, na
Mungu hayuko tayari kuona damu isiyo na hatia ikimwagika. Mwanadamu aliyefanywa
na Mungu, anapaswa kuondolewa na Mungu mwenyewe, sio na mwanadamu mwingine. Damu
ni uhai wa mtu. Uhai huu mtu alipewa na Mungu kupitia pumzi yake. Mwanzo 2:7 inasema: “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia
puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai”. Mtu alifanyika nafsi hai baada ya
pumzi ya Mungu kupulizwa ndani yake. Pumzi ya Mungu ndiyo iliyoamsha uhai wa
kila kitu ndani ya mtu. Hivyo kumwaga damu ya mtu ni kuingilia kazi ya Mungu
aliyoifanya, na kufanya hivyo kuna madhara makubwa sana.
Madhara
yatokanayo na kumwaga damu katika nchi
Biblia
inatuongoza vema kabisa juu ya madhara yanayoweza kuipata nchi kutokana na damu
ya mtu kumwagwa juu yake.
- Nchi kukataa kuwafanikisha wanaoikaa
Dhambi
ya umwagaji damu ilileta laana juu ya Kaini katika ardhi. Ardhi ni kiashiria cha vyanzo vya uzalishaji (means of
production) ambavyo Mungu amemwekea mwanadamu. Damu ya Habili ilipomwagika
katika ardhi, kukatokea uhasama kati ya ardhi na Kaini. Ardhi ikazuiliwa kumpa
Kaini mazao yake. Mazao ya ardhi inamaanisha mafanikio yatokanayo na njia za
uzalishaji (prosperity). Kaini alipomwaga damu akajiingiza kwenye laana ya
kutokufanikiwa katika ardhi.
Damu
ya mtu yeyote inapomwagika juu ya ardhi, ardhi inafunga milango yake ya
mafanikio. Ndio maana maeneo mengi yenye matukio ya umwagaji damu wa aina yoyote
ule duniani, hayana mafanikio makubwa.
- Kuzuiliwa kwa maombi yanayohusu taifa (nchi) mbele za Mungu
Neno
la Mungu katika Isaya 1:15 linasema:
“Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu
nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi,
sitasikia; mikono yenu imejaa damu”.
Kwa sababu ya mikono ya watu kujaa damu, Mungu anajificha kila wakati
watu hao wanapokunjua mikono yao mbele zake na pale wanapoomba maombi yao yeye
hasikilizi. Taifa lolote ambalo damu zisizo na hatia zinamwagika ndani yake
linakosa uhalali wa kusikilizwa mbele za Mungu. Watu wanaweza kuomba maombi
mengi kwa ajili ya nchi, lakini kama kuna hatia ya damu juu ya nchi hiyo, Mungu
hasikilizi.
- Kuondoa uwepo wa Mungu katika nchi
Hesabu
35:33-34 inasema: “Hivi hamtaitia
unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa
damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi,
kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo
aliyeimwaga. Kwa hiyo msiitie unajisi
nchi muiketiyo, ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi Bwana nakaa
kati ya wana wa Israeli”.
Neno la Mungu hapa linatuonya waziwazi kuwa damu
huitia nchi unajisi. Madhara ya unajisi ni kuwa unamwondoa Mungu asikae mahali
hapo. Kwa hiyo damu ya mtu inapomwagika inatia nchi katika unajisi ambao
unamfanya Mungu ashindwe kukaa pamoja na taifa hilo.
- Kuzalisha chuki na visasi kati ya watu
Damu ikimwagika inadai kisasi. Damu ya Habili
ilimlilia Mungu kutoka katika ardhi (Mwanzo 4:10) ikidai kisasi. Abneri
alipomuua Asaheli ndugu yake Yoabu, Yoabu nae alimuua Abneri kwa ajili ya damu
ya Asaheli (2 Samweli 3:27). Mfalme Yoashi alipomuua Zekaria mwana wa Yehoyada,
watumwa wake mfalme Yoashi nao wakamfanyi fitna mfalme wakamwua kitandani pake ‘kwa
ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada’ (2 Nyakati 24:20-25).
Kwa hiyo nchi inapomwaga damu ya mtu mmoja ni kuwa
inaanza kuzalisha vizazi vyenye chuki na visasi moyoni.
Tanzania na damu
zilizomwagika ndani yake
Nchi ya Tanzania imeshuhudia damu za watu
zikimwagika katika maeneo mbalimbali ya nchi. Watekelezaji wa matukio hayo kwa
sehemu kubwa hawajajulikana. Lakini madhara ya umwagaji damu hizo yanaweza
kuliathiri taifa pasipo kujali kama wahalifu wanajulikana au hawajulikani.
Kadiri matukio haya yanavyoongezeka katika nchi, ndivyo nchi inavyozidi
kujitenga na mfumo wa baraka zake kutoka kwa Mungu. Watu wanaweza kufanikiwa
katika ngazi ya mtu binafsi (individual wise) lakini mafinikio ya ngazi
yakitaifa yanaweza kukosekana kwa sababu ya wingi wa damu zinazodai visasi
katika nchi. Pia taifa linaweza kujikuta linapoteza kabisa umoja na amani yake
kwa sababu ya chuki na visasi mioyoni mwa watu vinavyotokana na madhara ya
umwagaji damu za watu.
Nini kifanyike?
Hesabu 35:33-34 inasema: “Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo
mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala
hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani
yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga’.
Kwa kuangalia maneno yaliyokolezwa hapo juu utaona
kuwa ili kufuta madhara ya umwagaji damu basi lazima damu ya huyo iliyeimwa pia
imwagike. La hasha! Sasa tunayo damu ya Yesu Kristo. Yeye ambaye amekufa na
kufufuka ili aziondoe laana zote. Tukinyenyekea chini ya msalaba wa Yesu kama
taifa na kuuitia damu yake ipate kututakasa basi tunaliokoa taifa letu na
madhara ya damu zilizomwagika ndani yake.
Ili hayo yafanyike, lazima tukubali kama nchi
kutubu na kuomba rehema za Mungu. Maombi ya kitaifa yanathamani sana mbele za
Mungu pale kiongozi mkuu wa taifa anapotambua dhambi yake na ya watu wake na
kuamua kwa dhati kabisa kutafuta rehema za Mungu. Wana wa Israeli walipokua
jangwani wakafanya ndama, wakaiabudu, Mungu alitaka kuwaangamiza. Lakini Musa
kama kiongozi wa taifa lile alisimama mbele za Mungu akaomba rehema kwa ajili
ya watu wake (Kutoka 32:1---).
Tanzania inamhitaji Yesu wakati huu kuliko nyakati
zote ilizowahi kupitia. Toba na kunyenyekea kuanzia kwa Rais wa nchi mpaka kwa
raia wa kawaida kunahitajika sana wakati huu ili kuomba rehema za Bwana Mungu
wetu juu ya nchi yetu.
Mungu irehemu Tanzania,
Jina lako Mungu wa mbinguni litukuzwe daima katika
Kristo Yesu.
Amen.
No comments:
Post a Comment