OUR DAILY MANA
UTAFUTE
UFALME WA MUNGU KWANZA
Karibu tena mpendwa
katika Bwana katika darasa letu la kujifunza maandiko katika mfululizo huu.
Somo liliopita tuliangalia juu ya kuhakikisha kuwa jina lako linajulikana
mbinguni; na tukaona kuwa unaweza kuwa ni mtumishi hapa duniani lakini jina
lako likawa halijulikani kwa Mungu. Leo tunataka tuangalie walau kwa ufupi juu
ya suala la kuutafuta ufalme wa Mungu kwanza, kabla ya mambo mengine.
Watu wengi hasa kwenye
ulimwengu wa leo wameweka kipaumbele kwenye kutafuta kile wanachokiita
‘MAISHA.’ Utawasikia watu wengi wakisema kuwa ‘ninatafuta maisha.’ Katika suala
hili kunahusisha mambo mengi; wako wanaohangaika kutafuta elimu; wengine
wanatafuta ajira; wengine wanatafuta wapenzi; wengine wanatafuta mambo ya
kibishara; n.k. Katika kutafuta kwao watu wengi wamejikuta wakikosa muda kabisa
wa kuutafuta uso wa Mungu. Na ukipata nafasi ya kuwauliza, jibu lao ni kuwa
muda hautoshi.
Nimejaribu kulichunguza
jambo hili kwa umakini mkubwa nikagundua kuwa, shetani ametengeneza mkakati
mkubwa sana wa kuwatenga watu na Mungu wao kwa kutumia mahitaji ya kila siku ya
maisha. Katika kuchunguza maandiko nikagundua kuwa Biblia haijanyamaza kuhusu
suala hili.
Mathayo
6: 25, 31-33 inasema hivi:
Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au
mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na
mwili zaidi ya mavazi? … Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini?
Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa
mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote
mtazidishiwa.
Haya
maneno yanatuambia kuwa Mungu anajua kila tunachokihitaji, na kwamba haitupasi
kusumbuka kuyatafuta hayo ila tuutafute kwanza ufalme wake na haki yake na hayo
mengine tutazidishiwa. Iko siri ya ajabu sana kwenye maneno haya ambayo
imetupasa kuifua kabla hatujasonga mbele.
Mtume
Paulo anatuambia jambo la ajabu sana kwenye Wafilipi
4:19. Anasema; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya
utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”
Huu msitari unaonesha kuwa uko utajiri wa kutosha ndani ya kristo
na Mungu yuko tayari kuwajaza wale wamtafutao kila wanachokihitaji. Ni ajabu
sana neon hili. Je, inamaana hatupaswi kufanywa kazi? Je, ni nini maana ya
kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake?
Daudi anaanza kutupa majibu ya maswali haya katika Zaburi 27:8. Inasema
hivi: “Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.” Daudi
anatuonesha kuwa Mungu alitoa tangazo kuwa watu wamtafute uso wake, nay eye
Daudi akajiweka tayari ili autafute uso wa bwana. Kwa nini ilikuwa ni muhimu
autafute uso wa Bwana?
Kitabu cha 2 Nyakati 26: 5
inasema: “Akajitia nia amtafute
Mungu katika siku za
Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta
Bwana, Mungu alimfanikisha.
Iko
siri ya ajabu sana kwenye huu msitari. Biblia inasema huyu ndugu alijitia nia
(hebu sema, nia) ili amtafute Mungu. Na alipoanza kumtafuta Bwana, Mungu
akaanza kumfanikisha kwenye mambo aliyokuwa anayafanya. Huyu ndugu Uzia alikuwa
mfalme, na Biblia inatuambia alianza kutawala akiwa na umri wa miaka 16. Hebu
fikiria leo, kijana wa miaka 16 apewe kuingoza nchi atafanyaje? Lakini Uzia
yeye aliamua kumtafuta Bwana kwanza. Kwa nini? Kwa sababu alijua kuwa hakuna
namna nyingine yoyote ambayo angeitumia kuendesha nchi ile akafanikiwa
isipokuwa amemtafuta Mungu kwanza.
Leo
hii watu wengi wanatumia muda mwingi sana kutafuta majibu ya matatizo yao ya
kimaisha kwa sababu wamesahau mahali ilipo chemchemi ya mafanikio yao. Mungu
anashangaa sana jinsi watu wake walivyopotea kwa kuamua kujitafutia wenyewe
majawabu ya maisha yao huku wakiwa wamemsahau yeye. Katia Yeremia 2:13 anasema:
Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi,
niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.
Mungu
anasema watu wake wamejichimbia mabirika yavujayao, yasiyoweza kuweka maji.
Maana yake licha ya kuwa wanahangaika sana kutafuta maisha, bado hawafanikiwi
kwa sababu wamemweka mbali yeye aliye chemchemi ya mafanikio yao. Ndiyo maana
licha ya watu kuamua kufanya kazi mpaka siku za ibada na kumsahau Mungu, bado
mambo yao hayaendi vizuri.
Iko
faida ya kuutafuta uso wa Mungu kwa sababu, pindi unapomtafuta Mungu yeye
anakufanya kufanikiwa. Marko 10: 28-30
inasema hivi:
Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata
wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu
waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili
yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na
mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.
Ukiamua kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake, Mungu
anakufanikisha mara mia na kukupa uzima wa milele kwenye ulimwengu ujao. Biblia
inasema hayo mengine ni ziada tunayozidishiwa pale tunapoweka suala la
kumtafuta Mungu namba moja.
CHAGUA KUMTAFUTA MUNGU KWANZA
YESU YU KARIBU KUJA
No comments:
Post a Comment