… tafuteni, nanyi mtaona … (Mathayo 7:7)
Bwana
wetu Yesu Kristo asifiwe!
Leo
katika darasa letu la maandiko nataka tuangalie juu ya mambo ambayo Biblia
inatuafundisha kuwa tunapaswa kuyatafuta tungali hapa duniani. Pia mwishoni
tutaangalia mambo ambayo Biblia inatuonya tusiyatafute wala kuyahangaikia.
Karibu ushiriki nasi kujifunza siri hii Mungu aliyotufunulia kwa majira haya!
Utangulizi
Katika
kitabu cha Mathayo 7:7 Yesu alituelekeza juu ya vitu
vitatu vya kufanya: kuomba, kutafuta na kubisha. Kila kimoja katika vitu hivi
ni somo tosha na linalojitegemea – ila kwa madhumuni ya somo hili tutaangalia
hiki kipengele cha “tafuteni, nayi mtaona.”
Jambo
la ajabu sana la kujua mapema ni kuwa Yesu alipotuambia “tafuteni, nanyi
mtaona” hakusema tutafute nini! Anachofanya ni kutupa uhakika kabisa kuwa
tukitafuta tutaona lakini hatuambii ni kitu gani hicho ambacho tunapaswa
kukitafuta ili tukione. Lakini jambo moja ambalo tuna uhakika nalo ni kuwa Yesu
hawezi kutoa ahadi hewa! Ikiwa alituambia “tutafute nasi tutaona” basi ni
dhahiri kuwa liko jambo au mambo aliyotaka kutujulisha kuwa yapo na tunauwezo
wa kuyaona endapo tutaamua kuyatafuta. Kwa msingi huo basi ni jukumu la kila
anayeamini katika neno la Kristo kuweka bidiii ya kutaka kujua ni mambo gani
haya ambayo Yesu mwenyewe ametuhakikishia kuwa tukiyatafuta tutayaona. Msingi
wa somo hili ni kutaka kukufunulia baadhi ya mambo ambayo Biblia imetuagiza
tuyatafute na faida zake pale tutakapoyatafuta.
Somo hili ni muhimu kwa sababu tusipojua yale yatupasayo kuyatafuta tukiwa hapa duniani basi tutajikuta tumepoteza muda mwingi kuhangaikia vitu ambavyo mwisho wake itakuwa ni mauti kwetu. Mithali 16:25 inasema “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.” Maana ya msitari huu ni kuwa kuna wakati mwanadamu huwa anafanya vitu akifikiri kuwa yuko sahihi lakini mwishowe vitu hivo humwangamiza.
Labda bado
hujaelewa ninachotaka uone hapa! Hebu sikiliza maneno haya mfalme Sulemani:
Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na
kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili
kutaabika ndani yake. Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama,
mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo. (Muhubiri 1:12-14)
Sulemani
alijaliwa hekima na Mungu, na yeye akaitumia hekima aliyopewa ili atafute kujua
mambo yote yanayotendeka duniani (chini ya mbingu). Baada ya kutafuta yote na
kuyavumbua akaishia kusema kuwa “yote ni ubatili na kujilisha upepo.” Kwa lugha
rahisi ni kuwa aliwekeza nguvu nyingi kutafuta mambo ya dunia hii na mwisho
wake hakupata faida yoyote katika mambo hayo aliyoyagundua. Kwa hiyo kwa muda
wote aliotumia kutafuta ufahamu huo ilikua amepata hasara. Sasa unaweza
ukaelewa ni kwa jinsi gani ilivyo muhimu kwa sisi tuliofikiwa na miisho ya
zamani hizi kujitia bidii katika kutafuta kujua kile ambacho Mungu mwenyewe
amesema tukitafute. Ni muhimu sana kujua Mungu ametuagiza tutafute nini muda
tungalipo duniani ili tusije tukatumie muda wetu kutafuta vitu ambavyo mwishoni
tutagundua kuwa ni “ubatili na kujilisha upepo.” Sasa ungana nami katika
kujifunza mambo haya ambayo Bibilia imetuagiza tuyatafute.
JAMBO
LA KWANZA:
Utafute ufalme wa Mungu na haki yake
Hili
ni jambo la kwanza kabisa ambalo Yesu mwenyewe aliagiza tulitafute. Utashangaa
kugundua kuwa suala hili la kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake ni Yesu
mwenyewe aliyesema kuwa ni la kwanza. Mathayo 6:33 inasema: “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake;
na hayo yote mtazidishiwa.”
Yesu
anatuwekea mpangilio wa vipaumbele vya vitu vya kutafuta tukiwa hapa duniani na
cha kwanza anasema ni kuutafuta ufalme wake na haki yake. Sasa utaniuliza:
ufalme wa Mungu ni nini na unautafutaje? Majibu yapo kwenye Biblia yenyewe
iliyosema tuutafute! Luka 17:20-21 inasema:
Na
alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia,
ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule,
kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.
Kwa mujibu wa
maneno hayo ya Yesu ni kuwa ufalme wa Mungu uko ndani yetu. Lakini sasa swali
la kujiuliza ni kuwa kama ufalme wa Mungu uko ndani yetu ni kwa nini atuambie
tena tuutafute? Hii inatupa kujua kuwa kuna kitu ambacho inabidi tukitafute
ambacho hicho ndicho kinachoashiria uwepo wa ufalme wa Mungu ndani yetu. Mtume
Paulo katika Warumi 14:17 anasema
hivi:
Maana
ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika
Roho Mtakatifu.
Tena katika 1 Kor 4:20 anasema: “Maana ufalme wa
Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.” Mtume Paulo anatupa kujua kuwa
maana ya ufalme wa Mungu ni “haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.”
Kwa hiyo Yesu aliposema ufalme wa Mungu uko ndani yetu alikuwa anamaanisha kuwa
pale tunapokuwa na “haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu” hapo ufalme
wa Mungu unakuwa uko ndani yetu. Sasa mambo haya matatu –haki na amani na
furaha katika Roho Mtakatifu- hayapatika kwa maneno matupu bali kwa nguvu. Ndio
maana sasa utaona ile 1 Kor 4:20
Paulo anasema “ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.” Kumbuka
pia maneno ya Yesu katika Mathayo 11:12 kuwa: “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni
hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.”
Kwa
hiyo ufalme wa Mungu – ambao ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu –
unapatikana nguvu na ni wenye nguvu tu ndio wanaouteka. Sasa hii inaanza kutupa
picha ya kwa nini Yesu amesema tuutafute ufalme wake na haki yake. Utakumbuka
kuwa katika Mathayo 6:33 Yesu alisema tuutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake kisha
mengine tutazidishiwa. Sasa utajiuliza kuwa haya mengine nitazidishiwa kutokea
wapi?
Misitari
inayotangulia kabla ya hiyo Mathayo 6:33 inaonesha Yesu akiwaonya watu
wasijisumbue juu ya wale nini au wanywe nini au wavae nini – kwa sababu hata
mataifa huyasumbukia hayo. Kimsingi harakati zote za mwanadamu katika maisha
yake anahangaika ale nini, avae nini, anywe nini. Sasa ukichunguza kwa makini
utangundua kuwa haya mambo ambayo mwanadamu anayahangaikia lengo lake ni ili
awe na amani na furaha ya maisha. Sasa haki, amani na furaha ni vitu ambavyo
viko vimehakikishwa [guaranteed] kwenye kifurushi [package] ya ufalme wa Mungu
(rejea Warumi 14:17).
Kumbe
tunagundua kuwa vitu ambavyo mwanadamu anajisumbua kuvitafuta kila siku na
anapata shida sana kuvipata anaweza kuvipata kwenye package aliyowekewa na
Mungu kwenye kifurushi kinachoitwa “ufalme wa Mungu.” Kumbe ndio maana Yesu
anatuambia tutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake – akiwa na maana kwamba
pindi tutakapoupata ufalme wa Mungu basi tutakua tumeyapata na mengine yote
tunayoyasumbukia kila siku. Hebu sikiliza haya mazungumzo ya Yesu na Petro:
Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote
tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba
ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu
katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili,
mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au
ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili
ya jina langu, atapokea mara mia, na
kuurithi uzima wa milele. (Mathayo
19:27-29)
Sasa
jambo la kuzingatia hapa ni kuwa huu ufalme wa Mungu unapatikana kwa nguvu na
ni wenye nguvu ndio wanaouteka. Hapa sasa ndipo utakapoelewa ni kwa nini tuna
walokole wengi wanaomwamini Yesu lakini hali zao za maisha sio nzuri. Hiyo ni
suala la kiwango cha nguvu itendayo kazi ndani ya Mtu husika (Waefeso 3:20). Katika sala ya Bwana
moja mbinu ambazo Yesu alitufundisha kuomba ni ile ya kuomba ufalme wa Mungu
uje! Alituwekea hii mbinu kwenye sala ya Bwana ili tutambue kuwa ufalme wa
Mungu (yaani nguvu ya Mungu) isipokua ndani yetu hatuwezi kupata tunayotafuta. Hili
ni jambo la kuzingatia sana kuwa kama nguvu inayozalisha ufalme wa Mungu haiko
ndani yako basi ni ngumu sana kufaidika na Baraka zilizomo katika ufalme wa
Mungu hata kama wewe umeookoka. Ndio maana sasa Paulo katika Waefeso 6:10 anasema “Hatimaye mzidi
kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.”
JAMBO
LA PILI:
Utafute uso wa Bwana
Napenda
ujue tokea mwanzo kuwa tunapozungumzia kuutafuta uso wa Bwana tunazungumzia
kumtafuta Bwana. Mtu anayemtafuta Bwana pia anakua ameutafuta uso wa Bwana –
kwa hiyo utakuta mara kadhaa Biblia inatumia maneno “mtafuteni Bwana” na “utafuteni
uso wa Bwana” kwa kuumaanisha kitu kile kile ambacho msingi wake ni “kutafuta
uwepo wa Mungu kati yetu.”
Napenda
ufahamu mapema kabisa kuwa suala la kuutafuta uso wa Bwana ni agizo ambalo
limetoka kwa Mungu mwenyewe. Zaburi 27:8, Daudi anasema:
Uliposema, Nitafuteni
uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.
Msitari
huu hapo juu unatujilisha kuwa ni Mungu ndiye aliyesema watu wautafute uso
wake, na Daudi anatii agizo hili akisema “Bwana uso wako nitautafuta.” Ukisoma
Biblia yako vizuri utakuta maeneo mengi sana ambayo Mungu anawaita watu wake
wamtafute.
Kwa nini lazima tuutafute uso wa Bwana
Isaya 55:6 inatuambia hivi: “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni,
maadamu yu karibu.” Maneno haya yanatuambia jambo la ajabu sana kuwa Bwana
anapatikana na tena yu karibu. Sasa kama Bwana yu karibu tena anapatikana, ni
kwa nini tumtafute? Biblia inatupa kujua sababu za kwa nini tumtafute Bwana
wake amesema anapatikana!
Sababu ya kwanza: Mungu ana sifa ya kujificha uso wake.
Isaya 45:15 neno la Mungu linasema hivi: “Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee
Mungu wa Israeli, Mwokozi.” Labda wacha nikueleze jambo hili hapa ili tuende
pamoja. Tangu mwanzo Adamu na Eva walimwasi Mungu na kuruhusu dhambi itawale,
Mungu hamwamini mtu tena. Na kwa hiyo amejiweka mbali na wanadamu ili kwamba
kila mtu amtakaye Bwana – amtafute!
Utaratibu
wa kabla ya dhambi ilikuwa inampasa Mungu kuja kumtembelea Adamu bustanini kila
siku, lakini baada ya dhambi kuingia utaratibu ukabadilika. Sasa Mungu
anaonekana kwao tu wenye haja ya kumwona, na ndio maana inabidi tumtafute. Ngoja
niseme hivi: sasa hivi Mungu anaonekana [by demand] – yaani kabla hajaonekana
kwako lazima uwe umeonesha haja ya kwamba unamwitaji. Ndio maana Yesu akasema Mtu
akiona kiu, na aje kwangu anywe (Yohana
7:37). Maana yake – asiye na kiu asije kwangu! Lazima uoneshe kiu yako ya
kumwitaji Mungu ndipo Mungu aonekane kwako. Na hiyo kiu sasa ndio inayokusukuma
kumtafuta Mungu. Ukiwa na kiu lazima uende – usije ukafikiri kiu yako tu
inatosha kumfanya Mungu ajifunue kwako. Yesu hakusema “mtu kiona kiu, anyweshwe”
bali alisema “mtu akiona kiu, aje kwangu anywe”. Kwa hiyo ni lazima wewe
unayeona kiu uchukue hatua ya kuenda kwake ili unywe. Usipoenda utabaki kuwa na
kiu yako na utakufa nayo wakati maji yalikuwepo.
Sababu ya Pili: ni ili uweze kuishi na kuwa na uzima ndani yako
Amosi 5:4,6,8 inasema hivi:
Maana Bwana awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi; Mtafuteni
Bwana, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu,
nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli. Mtafuteni yeye
afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na
kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga
juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina lake.
Mungu
anaagiza watu wamtafute ili waishi. Maana yake mtu asiyetaka kuutafuta uso wa
Bwana hana uhai ndani yake – amekufa ijapokuwa bado yuko duniani. Sasa hapa
utaelewa kwa nini Yesu alisema “Yeye aniaminiye
mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi (Yohana 11:25).”
Uhai unaozungumzwa
hapa sio suala la kuishi hapa duniani bali ni uzima wa Mungu katika maisha yako
ya sasa na uzima wa milele katika ulimwengu ujao. Tunapaswa kumtafuta Mungu ili
tuwe na huu uzima ndani yetu. Matendo 17:26-28 inasema hivi:
Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae
juu ya uso wa nchi yote, akiisha
kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili
wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali
na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na
kuwa na uhai wetu.
Mistari
hii inatufundisha kuwa Mungu aliwawekea watu mipaka ya nyakati na makazi ili
wamtafute hata kama ni kwa kupapasa-papasa kwa sababu ndani yake tunaishi,
tunakwenda na kuwa na uhai wetu. Kwa lugha rahisi ni kuwa tusipomtafuta Mungu
tunakuwa tumejinyima haki yetu ya kuishi pamoja na Mungu na kwa hiyo tutaukosa
uhai wetu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.
Sababu ya tatu: Ili Mungu akufanikishe na kukustarehesha
Biblia
inatuambia kuwa kuna mafanikio ya wacha Mungu lakini pia kuna mafanikio ya
wapumbavu. Lakini Mithali 1:32 inatuambia kuwa “kufanikiwa kwao wapumbavu
kutawaangamiza.” Napenda kukusihi uwe makini na aina ya mafanikio unayotafuta,
kwa sababu ukifanikiwa kipumbavu hayo mafanikio yatakuangamiza.
Zaburi 35:27 inatuambia
kuwa Mungu anafurahishwa na amani (mafanikio) ya mtumishi wake. Na katika hilo
Mungu anatamani sana ahusike kwenye mafanikio ya kila mtu aliyeko duniani.
Mungu hataki ufanikiwe bila yeye kuwepo kwa sababu mafanikio yoyote nje ya
Mungu yatakuangamiza. Ndio maana ameweka utaratibu wa watu kumtafuta ili
awafanikishe. Wacha tuangalie mistari michache ya Biblia.
Mithali 8:17-21 “Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Utajiri na
heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia. Matunda yangu hupita
dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule. Natembea
katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate
kuzijaza hazina zao.”
2 Nyakati 14:2-7 Basi,
Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa Bwana, Mungu wake; maana
aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo,
akayakata-kata maashera; akawaamuru
Yuda wamtafute Bwana, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena
akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme
ukastarehe mbele yake. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi
ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu Bwana
amemstarehesha. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia
maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta Bwana, Mungu
wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga,
wakafanikiwa.
2 Nyakati 26:3-5 Uzia
alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko
Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa
Yerusalemu. Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote
aliyoyafanya Amazia babaye. Akajitia
nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika
maono ya Mungu; na muda
alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.
Nimekuwekea hii
mistari ili uone jinsi ambavyo kumtafuta Mungu kunasababisha mafanikio ya watu
wa Mungu. Asa aliwaamuru Yuda wote wamtafute Mungu na vile walivyomtafuta,
Mungu akawafanikisha na kuwastarehesha. Tunaliona jambo hili pia kwa Uzia ambae
alianza kumtafuta Mungu akiwa na miaka 16 na muda wote alipomtafuta Bwana Mungu
alimfanikisha. Nataka uelewe kuwa huwezi kuendelea katika njia yako mwenyewe na
kufanikiwa usipomtafuta Mungu na kumweka awe sehemu ya maisha yako.
Ndio maana
Mungu alipokataa kutembea na Israeli kuelekea Kanani – akasema atawapa malaika
aende nao, Musa naye aligoma kuondoka pale walipokuwa. Kutoka 33:15
Musa anamwambia Mungu “Uso wako usipokwenda pamoja
nami, usituchukue kutoka hapa.” Kwa nini Musa alikataa kuondoka kama uso wa
Mungu usingeenda nae? Ni kwa sababu raha ya Israeli na mafanikio yao yote
yalitegemea uwepo wa Mungu kati yao. Angalia Mungu anachojibu kwenye Kutoka 33:14, anasema “uso wangu
utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.” Maana yake uso wa Mungu usingeenda
pamoja nao wasingepata raha huko waendako. Sasa kwa nini wewe unataka
kufanikiwa mwenyewe bila uso wa Mungu kuwa pamoja nawe?
JAMBO
LA TATU
Tafuta kuwa na amani na watu wote
Kuna
watu wanapenda kusema kuwa ‘huwezi kuwafurahisha watu wote duniani.’ Mimi huwa
sikubaliani na msemo huu kwa sababu hii ni kauli ya watu wanaotaka kuhalalisha
kuwa kwao na ugomvi na watu wengine. Biblia inapinga kitu hiki. Waebrania
12:14 inasema: “Tafuteni kwa
bidii kuwa na amani na watu wote.”
Utaona
katika msitari huu kuwa - amani na watu wote ni jambo linalopaswa kutafutwa kwa
bidii. Kwa hiyo hatuwezi kuridhika na kauli kuwa ‘huwezi kuwafurahisha watu
wote.” Biblia haisemi tafuteni kwa bidii kuwafurahisha watu wote bali inasema
tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote. Kwa sababu hiyo sio vema kuwa na
mafarakano na kuishi kwenye kutoelewana na watu wengine. Angalia jinsi mtume
Petro anavyosema juu ya jambo hili katika 1
Petro 3:10-11
Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie
ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende
mema; Atafute amani,
aifuate sana.
Huu
ni ujumbe wa ajabu sana – kwamba kila mtu anayependa maisha na kupenda kuona
siku yake imekaa vizuri basi asinene mabaya bali atende mema na kutafuta amani,
tena hii amani aitafute sana. Sasa utagundua kuwa Wakati Waebrania inatuambia
kuwa tutafute amani kwa bidii, Petro anasisitiza kwa kutuambia kuwa tuitafute
sana.
Kwa
msisitizo huu ambao Biblia imeweka kwenye jambo hili tunapata kuelewa kabisa
kuwa suala la kuwa na amani na watu wote sio suala la kupuuza – sio suala la
kuchukulia kijuu-juu tu. Lazima tulipe uzito wake unaostahili na tuitafute hiyo
amani sana na kwa bidii hadi tuipate.
Madhara ya kutokuwa na amani
Maisha
ya watu wengi yamesimama pasipo kusonga mbele kwa sababu ya kutokuwa na amani. Kukosekana
kwa amani kunaleta uchungu na huzuni ya moyo ambayo madhara yake ni kupunguza
kasi ya mafanikio ya mtu huyo. Isaya 38:15 inasema:
Nitakwenda polepole miaka yangu yote, kwa
sababu ya uchungu wa nafsi yangu.
Utaona kwenye
msitari huo hapo juu jinsi ambavyo suala la kukosa amani lilivyo na madhara
makubwa. Huyu mtu anasema miaka yake yote atakwenda polepole kwa sababu ya
uchungu wa nafsi yake. Kwa hiyo kwenye kila eneo la maisha yake ana [slow down]
kwa sababu tu hana amani, na hii ni kitu anasema itamgharimu miaka yake yote. Huwezi
kuelewa ubaya wa kukosa amani kama bado hujawahi kupita kwenye eneo hilo. Lakini
nataka kukwambia kuwa kwenye eneo lolote lile ambalo hakuna amani mafanikio ya
eneo hilo lazima yana [slow down].
Angalia nchi
zenye vita, angalia familia zenye ugomvi, angalia makanisa yenye migogoro kote
huko utagundua kuwa kama walikua wanakimbia kwa spidi fulani hapo mwanzo, ule
ugomvi ulio kati yao umepunguza kwa kiasi kikubwa sana maendeleo na mafanikio
yao. Ndio maana katika Yeremia 29:7 utaona
Mungu anawaagiza Israeli akisema:
Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji
huo ninyi mtapata amani.
Sasa
utajiuliza ni kwa vipi Mungu awaagize Israeli wautakie amani mji ambao wao ni
mateka. Ni kama vile anawaambia wawaombee wanaowatesa. Lakini utagundua kuwa
hata kama walikuwa utumwani bado walihitaji kufanikiwa na kuendelea kuishi na
hakuna namna ambavyo wangefanikiwa nje miji waliyokuwa wanaishi. Kwa hiyo ili
wao wafanikiwe ilikuwa ni lazima miji wanayokaa ifanikiwe kwanza. Ili wao wawe
na amani ilikuwa ni lazima miji wanayokaa iwe na amani kwanza.
Ninalotaka
uone hapa ni kuwa suala la kutafuta amani na watu wote ni la muhimu sana. Usitunze
kinyongo na watu. Usichochee ugomvi hata kama mliyegombana naye hataki mapatano
bado Biblia inasema sisi wateule wa Mungu tumepewa huduma ya upatanisho kwa
hiyo lazima tuyatafute kwa bidii hayo mapatano.
JAMBO
LA NNE
Tafuta watu sahihi wa kushirikiana nao
Watu
wote duniani ni wa muhimu kwako ila si watu wote duniani wamewekwa kwa ajili
yako. Suala la watu gani unashirikiana nao ni suala la muhimu sana na la kuangalia
kwa makini kwa sababu maandiko yanasema “adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake (Mathayo 10:36).
Nachotaka uelewe
hapa ni kuwa huwezi kuchukua mtu yeyote tu unayemwona na kuamua kushirikiana
nae. Biblia inakataza! Lazima ufuate vigezo vya ki-Biblia juu ya aina ya watu
unaotakiwa kuwa nao, na neno la Mungu linasema hao watu lazima uwatafute. Angalia
Yesu alichowaambia wanafunzi wake wakati anawatuma kwenda vijijini kuhubiri
injili. Mathayo 10:11 anasema:
Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu
mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.
Hebu
cheki hapo! Yesu hawaambii waingie kwenye nyumba yoyote ile bali anawaambia
watatute kwenye mji huo au kijiji hicho mtu aliye mwaminifu ndiye wakae kwake.
Sasa fahamu kuwa Yesu aliwajua watu wote walikuwa na hicho kijiji au mji na
angeweza kuwaelekeza moja kwa moja ni kwa nani waende lakini akawapa vigezo ila
suala la kumpata mtu akawaachia wao wenyewe watafute.
Yusufu
alipomfafanulia Farao ile ndoto alimweleza na nini cha kufanya, kisha akasema: “Basi,
Farao na ajitafutie mtu wa akili na
hekima amweke juu ya nchi ya Misri (Mwanzo 41:33). Utaona hapa kigezo anachoweka Yusufu cha aina ya mtu
atakayebeba maono aliyoyaona Farao ni awe mtu wa akili na hekima. Na Farao
alipoona hicho kigezo akaona hakuna mtu mwingine mwenye sifa katika Misri yote
isipokuwa Yusufu.
Tunajifunza
kuwa suala la watu wa kushirikiana nao ni suala la ki-Mungu kabisa na Mungu
ameliwekea utaratibu. Hii ni pamoja na suala la unaoa au unaoelewa na nani? Huwezi
tu kumkubalia mtu yeyote anayekuja kutaka kukuoa au kuolewa na wewe hata kama
ameokoka. Watu sahihi wanatafutwa katika mkono wa Bwana. Yeye ndiye anayeijua
mioyo ya wanadamu na siri zao hivo hakuna namna utawapata watu sahihi wa
kushirikiana nao bila kumshirikisha Mungu. Yesu mwenyewe kabla hajachagua wale
Thenashara alienda mlimani akakesha huko usiku kucha akimwomba Mungu ndipo
akawachagua wale kumi na wawili.
JAMBO
LA TANO
Utafute unyenyekevu
Suala
la unyenyekevu ni suala muhimu sana katika kutunza mahusiano ya mtu na Mungu
lakini pia kutunza mahusiano kati ya mtu na mtu mwingine. Biblia inasema katika
1 Petro 5:5 kuwa:
Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema.
Usipojifunza
kunyenyekea kiburi kitainuka ndani yako, na pale kiburi kinapoinuka basi uwe na
hakika Mungu lazima atakupinga. Ndio maana Zefania 2:3 anasema
Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi
mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni
unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana.
Kwa
hiyo unyenyekevu una nguvu ya kukuletea neema na pia una nguvu ya kukuficha
siku hasira ya Mungu ikiwaka. Kati ya vitu vilivyomtofautisha mfalme Daudi na
mfalme Sauli machoni pa Mungu ni unyenyekevu wao mbele za Mungu. Sauli
alipokosea alijitetea na kutafuta namna ya kuhalalisha kosa lake lakini Daudi
alipokosea alianguka magotini pa Bwana kuomba rehema. Kiburi kinaleta
kujihesabia haki na kwa mujibu wa maandiko hakuna mtu awezaye kujihesabia haki
maana wote tunahesabiwa haki bure kwa njia ya imani katika Kristo Yesu (Warumi
3:25-27).
JAMBO
LA SITA
Utafute mambo mema
Amosi 5:14-15 anasema hivi:
Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo Bwana, Mungu wa majeshi,
atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana,
Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.
Biblia
inatujulisha kuwa mambo mema yanatafutwa na sisi kama wateule wa Mungu
inatupasa kuyatafuta. Mambo mema ni yale yampendezayo Mungu – yale ambayo yeye
ametuagiza tuyatende. Kila jambo Mungu alituzuia kulifanya basi hilo si jema
kwetu na hatupaswi kulitafuta. Mtume Paulo yeye anasema kuwa “Basi mkiwa
mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu Kristo aliko (Wakolosai 3:1).” Hatupaswi kuhangaika kuyatafuta mambo ya dunia hii kwani hayo
yote yanapita bali tuyatafute yaliyo juu Kristo aliko kwani huko ndiko yaliko
mema yote.
Mwisho
Kwa
vile Biblia ilivyotuwekea mambo tunayopaswa kuyatafuta vile vile imetuwekea
mambo ambayo hatupaswi kuyatafuta wala kuhangaikia. Mambo ya Walawi
19:31 inasema “Msiwaendee
wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi
Bwana, Mungu wenu.” Mungu anatuzuia kuwaendea wachawi wala kuwatafuta kwa
sababu kufanya hivyo ni kutiwa unajisi. Kwa hiyo usiwategemee wachawi wala
waganga – wewe weka tumaini lako kwa Bwana. Yako na mambo mengine ambayo Biblia
inatuzuia kuyatafuta ila kwa leo tutaishia hapo. Tutayaangalia hayo wakati
mwingine Mungu akitupa nafasi.
JIWEKE
TAYARI YESU YU KARIBU KURUDI
No comments:
Post a Comment