Wednesday, June 1, 2016

MTUMIKIE MUNGU KWA KADIRI YA NEEMA ULIYOPEWA



Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. (Warumi 12:3)



Bwana Yesu asifiwe!

Katika somo hili tunataka kujifunza zaidi kuhusu aina ya utumishi ambao kila mtu anatakiwa kutumika mbele za Mungu. Ni vyema tukafahamu mapema kabisa kuwa Kristo Yesu alipotoa vipawa vya utumishi kwa watu wake hakuwapa wote huduma moja – bali alitoa huduma tofauti tofauti na kila mtu anapaswa kutumika katika huduma aliyopewa na kwa kiwango Mungu alichomwita. Waefeso 4:7, 11, 12 inatuambia hivi:
Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. …Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.

Maandiko haya yanatufunulia kuwa Kristo alitoa huduma mbalimbali na kila mmoja wetu alipewa hiyo sehemu ya huduma hii ambayo inakamilishwa katika Kristo mmoja kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, na kuhakikisha kuwa kazi ya huduma ya kuujenga mwili wa Kristo inatendeka. Kwa maneno haya tunafahamu kuwa katika wahudumu wa kazi ya Mungu hakuna aliyepewa huduma bora kuliko mwingine bali kila mmoja amepewa sehemu yake tu katika kuujenga mwili wa Kristo ambao ni mmoja. 1 Kor 10:17 inatuambia kuwa “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.”

Kwa hiyo kila mmoja wetu amepewa sehemu tu ule mkate – hakuna aliyepewa mkate mzima. Na kwa kusema hivyo twajua wazi sasa ya kuwa hakuna mtu awezaye kujikamilisha mwenyewe katika huduma ya Kristo pasipo uwepo wa wahudumu/ au watumishi wengine. (Ukisoma 1 Kor 12:1-29 utaona jinsi Mtume Paulo anavyosisitiza kuhusu viungo vyote katika mwili wa Kristo kuheshimiana na kuthaminiana kwa kuwa kila kiungo kinahaja na mwenzake wala hakuna kiungo kiwezacho kujitenga na viungo vingine halafu kikafanikiwa.


Mambo haya ni muhimu sana tukayatafakari kama watumishi wa Mungu aliye hai ndani ya Kristo Yesu. Kila aliyemtumishi wa Mungu yampasa kufahamu kuwa kama yeye ajidhaniavyo kuwa mtu wa Mungu ndivyo na wengine walivyo. 2 Kor 10:7 Mtume Paulo anasisitiza jambo hili akisema:
Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu. Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo na sisi.

Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa changamoto kubwa sana kwa watumishi wa Mungu ni mashindano juu ya nani ni mkubwa kuliko mwingine. Mashindano haya yamepelekea huduma nyingi kusambaratika na hata makanisa kuvunjika. Hivi karibuni nimeshudia huduma ya vijana fulani ikisambaratika na kila mmoja wao kuanzisha huduma yake baada ya mmoja wao kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko mwenzake; hivyo akaanza kupitisha maneno miongoni mwa wafuasi wao akimsema vibaya mwenzake. Jambo hili liliposhindwa kutatuliwa kati yao basi Yule aliyekuwa akieneza maneno ya ubaya wa mwenzake akaamua kujitoa katika huduma ile na kuenda kuanzisha ya kwake.

Nataka nikwambie msomaji wangu kuwa mashindano haya ya watumishi wa Mungu hayakuanza leo. Mitume nao walikumbana na changamoto hiyo hata Yesu alipokua akali pamoja nao. Luka 22:24-26 inasema:
Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.

Haya mashindano ya nani mkubwa na nani mdogo yameleta madhara makubwa sana katika kanisa. Hata ukienda kwenye kambi za maombi utaona watu hawaheshimiani sana kutokana na kulinganisha nani ana upako zaidi kuliko mwenzake. Madhara yake ni kuwa kiburi huinuka miongoni mwa watu na mwishowe Mungu huwashusha hawa wenye kiburi. 1 Petro 5:5 inasema: “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.” Neno la Mungu linasisitiza unyenyekevu na kuhudumiana. Tusipojifunza kunyenyekea na kuhudumiana lazima Mungu atushushe.

Lakini nilipokua nikijiuliza ni kitu gani kinapelekea mashindano haya baina ya watu wa Mungu – nikagundua kuwa moja ya sababu ni watumishi kutaka kutumika nje ya kiwango cha neema waliyopewa na Mungu katika huduma husika. Mtume Paulo anasema hivi:
Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Warumi 12:3
Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Waefeso 4:7

Mtume Paulo anawaasa warumi wasinie makuu kuliko impasavyo kila mtu kunia; bali kila mtu anie kwa kiasi sawasawa na kipawa cha imani aliyopewa. Nia ya mtu katika huduma inaweza kumpelekea mtu kutumika nje ya kusudi la Mungu. Unaweza kunia mambo mbalimbali katika maisha yako na hata katika huduma uliyopewa lakini neno la Mungu linakuzuia kunia makuu kuliko kiwango cha neema uliyopewa (Warumi 12:3, 16). Mtu akinia makuu kuliko imani yake au kuliko kiwango cha neema aliyopewa ndipo anapoanza kushindana na watumishi wengine. Kwa sababu kila mtu anapaswa kutumika sawasawa na alivyoitwa na tena kwa kulingana na neema Mungu aliyoweka ndani yake. Sasa wewe unapoamua kushindana na mtumishi mwingine jua kuwa unashindana na neema aliyopewa wala husindani na yeye. Kwa sababu hakuna mtu anayetumika kwa uwezo wake mwenyewe bali kila mtu hutumika kwa kadiri ya kipawa alichopewa. Sasa unaweza kuwa unashindana uwe kama mtu fulani au unashindana ili umzidi mtu fulani – lakini nakwambia utajichosha bure na hicho unachoshindania hutakipata kwa sababu neema aliyopewa huyo mtumishi mwingine sio neema uliyopewa wewe. Hebu soma kwa makini msitari ufuatao; 1 Kor 7:17
Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote.

Mtume Paulo anasema kila mtu na aenende kama Mungu alivyomgawia. Sasa wewe unaposhindana kuwa kama/ au kumzidi mtumishi fulani jua kuwa unashindana na usichokijua kwa sababu yeye aliyemgawia ndiye ajuaye kazi aliyompa huyo mtu na nini anachotakiwa kurudisha mwisho wa kazi yote. Naamini unaifahamu habari ya wale watumwa waliopewa talanta na Bwana wao ili wafanye biashara. Neno la Mungu linasema kila mmoja wa watumwa wale alipewa talanta kwa kadiri ya uwezo wa kuzalisha aliokuwa nao. Mathayo 25:14-15 inasema:
Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.

Kwa hiyo Mungu kabla hajampa mtu kipawa anapima uwezo wa huyo mtu katika kuzalisha. Kumbuka kuwa Mungu hafanyi kazi kwa hasara – hivyo anataka kila mtu anayepewa kazi ya kufanya alete mavuno kamili mwisho wa kazi. Sasa kwenye kile Mungu alichokupa lazima ujue kuwa anakutaka ukifanyie kazi na kuleta matunda. Suala la kuongezewa vipawa sio suala lako kutafuta ni suala la yeye atoaye vipawa kuamua. Kazi yako ni kutumika kwa uaminifu kwenye zamu yako na kutimiza ipasavyo kazi yako.

Unapotumika nje ya neema uliyopewa lazima uumie – kwa sababu utatumia nguvu kubwa sana lakini bila matunda yoyote. Ndio maana unaweza kufunga sana na kuomba ili huduma yako ikue lakini usione majibu. Kwa nini? – Kwa sababu Mungu akiiona nia ya kufunga kwako na kuomba anakuta kusudi lako sio kujenga ufalme wa Mungu ila kusudi lako ni kushindana na mtumishi fulani.
Vijana wengi sana wanapenda kuwaiga watumishi waliofanikiwa katika huduma na kutaka kuwa kama wao. Nataka ujue kuwa sio mbaya kujifunza na kutaka karama zilizo kuwa ila ni mbaya sana kutaka kuwa kama mtumishi fulani alivyo. Huwezi kujua yeye neema aliyopewa inamtaka arudishe matunda kiasi gani kwa Mungu. Sasa wewe unaposhindana naye unajipa tabu bure.

Napenda kukutia moyo kuwa Mungu aliyekupa huduma uliyonayo ni mwaminifu sana na anachotaka kwako ni uaminifu wako katika hiyo neema uliyopewa. Ukifanya vizuri kwenye ngazi uliyopo ni rahisi sana Mungu kuku-promote kwenda ngazi nyingine ila kwa mpango wake yeye wala sio kwa mpango wako wewe. Tumika kwenye neema uliyopewa wala usishandane na mtumishi mwingine. Kumbuka kuwa wote tunajenga mwili mmoja – yaani Kristo.

Soma pia somo letu linalosema: OMBA ILI MUNGU AKUPE KUFAHAMU KIWANGO CHA MATOKEO ANAYOTEGEMEA KUTOKA KWAKO kwa kufuata link hii hapa http://fimboyamusa.blogspot.com/2015/06/omba-ili-mungu-akupe-kufahamu-kiwango.html

Yesu akubariki sana.

No comments:

Post a Comment