MAMBO MATANO AMBAYO SHETANI HUFANYA ILI KUKUTOA KWENYE MPANGO WA MUNGU
UTANGULIZI
Jambo
la msisitizo kwenye somo hili ni kuwa kila mtu ambaye Mungu amempa
nafasi ya kuwepo kwenye dunia hii anakusudi ambalo Mungu amemleta nalo
na ambalo anapaswa kulitimiza bila kujali amekuja duniani kupitia njia
gani au familia gani, au bila kujali kuwa alichukuliwa mimba hatiani au
la!
Ninasema
hivyo kwa sababu kama Mungu angeona hauna sababu ya kuletwa duniani
asingeruhusu uzaliwe halafu uje tu kuongeza idadi ya watu. Au kama Mungu
anaona kuwa sababu ya kuwepo kwako duniani imeshaisha basi angekuwa
ameshakuondoa. Matendo 13:36 inasema “Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala….” Kwa
hiyo mtu yeyote ambaye amekamilisha kazi aliyoitiwa kama Daudi, Mungu
humwondoa, Hivyo tunapoona bado unaishi tunajua wazi kuwa kuna kazi ya
Mungu ambayo bado inakungoja ndio maana Mungu anaendelea kukutunza.
Huwa
ninatafakari gharama ambazo Mungu anatumia kunitunza kwa siku, halafu
huwa nakosa majibu. Yaani nikifikiria gharama ambayo Mungu anatumia
kuhakikisha kuwa napumua, sipatwi na mabaya, nasafiri salama, nakula,
nasoma nafanikiwa, nafanya kazi zangu bila taabu, na mengine mengi
halafu nikifikiri kama akiniambia nilipie hata senti moja kwa siku kama
nitaweza, nabaki tu kujiambia moyoni mwangu kuwa ni lazima kuna sababu
kwa nini bado sijafa. Na hii sababu ndiyo ninayoiita “kusudi la Mungu
juu ya mtu.”
Ngoja
nikuambie jambo hili mapema kabisa, kuwa: kabla wewe hujazaliwa Mungu
alifanya kusudi la wewe kuwepo halafu ndipo Mungu akaruhusu wewe
uzaliwe. Kabla Adamu hajaumbwa Mungu alitafuta kwanza kusudi na kazi
ambazo Adamu angetakiwa kufanya. Ukisoma Biblia yako utaona Mungu
akimuumba Adamu kwenye Mwanzo sura ya 2, lakini kazi na majukumu ya
Adamu vilitangazwa Mwanzo 1:26-27. Kwa hiyo tunachogundua hapa ni kuwa
kumbe kabla sijawekwa rasmi kwenye ulimwengu huu, Mungu alitangulia
kunifanya kwenye ulimwengu wa Roho na akaweka na kazi nitakayofanya
nikija duniani. Ndio maana anamwambia Yeremia “Kabla sijakuumba katika
tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka
kuwa nabii wa mataifa.” Kwa hiyo Yeremia aliwekwa kuwa nabii hata kabla
hajawekwa tumboni mwa mama yake. Jua na wewe leo kuwa kuna kusudi la
Mungu kukufanya uishi hadi leo, na unatakiwa ulifahamu hilo kusudi ili
uishi kwenye mpango wa Mungu.
Sasa
jambo la kujua ni kuwa shetani naye anajua kuwa kila mtu ambaye Mungu
amemweka duniani ana kusudi la Mungu ambalo mtu huyo anapaswa
kulitimiza. Na kibaya zaidi ni kuwa wakati mwingine shetani anajua zaidi
makusudi ya Mungu juu ya watu hata kuliko watu wenyewe. Sasa kutokana
na shetani kuwa na uwezo wa kujua kuwa Mungu alikuleta kwa kusudi gani,
kazi yake kubwa ni kupambana na wewe ili akutoe kwenye hilo kusudi.
Lengo kubwa la shetani siku zote ni kuhakikisha kuwa anamtenganisha mtu
na Mungu aliye hai, na ili afanikiwe katika lengo hilo silaha yake kubwa
ni kumfanya mtu aache shauri (kusudi) alilopewa na Mungu na kumfanya
atumikie shauri la shetani. Ndicho alichofanya kwa Adamu. Alipotaka
kumtenga Adamu na Mungu wake cha kwanza alichofanya ilikuwa ni kumtoa
Adamu kwenye nafasi aliyowekwa na Mungu na kumfanya akajifiche. Mwanzo 3:9-10 inasema:
Bwana
Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti
yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.
Mungu
anapomuuliza Adamu “Uko wapi?” haimaanishi kuwa Mungu alikuwa haoni
kuwa Adamu amejificha ila alikuwa anauliza juu ya nafasi aliyokuwa
amepewa; maana Mungu aliona nafasi haina mtu. Watu wengi leo shetani
amefanikiwa kuwadanganya na kuwatoa kwenye nafasi zao na wengi sana wako
mafichoni. YESU AKUTOE HUKO LEO KWA JINA LA YESU KRISTO ALIYE HAI
NJIA ZA SHETANI KUKUTOA KWENYE KUSUDI LA MUNGU
Ili
shetani aweze kufanikiwa kwenye mpango wake wa kukutenga na Mungu ni
lazima awe na njia au mkakati wa kufanikisha azma hiyo. Sasa ndiyo maana
tunataka tuangalie mambo matano ambayo shetani anashughulika nayo
sawasawa ili kukutoa kwenye mpango wa Mungu.
Waamuzi 16:4-5, 15-16, 18-19
4 Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila. 5 Nao
wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua
asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate
kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja…. 15 Mwanamke
akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami?
Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako
nyingi….16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa…. 18 Delila
alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu
akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana
ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti
wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. 19 Naye
akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile
vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake
zikamtoka…. 21 Wafilisti
wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga
kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.
Ukisoma
hayo maneno kwenye mistari hiyo hapo juu vizuri kuna habari ya
kushangaza sana. Tunamwona Samsoni, mnadhiri wa Mungu, akimpenda
mwanamke wa kifilisti jina lake Delila. Na wafilisti walipoona ya kuwa
Delila amepata nafasi kubwa moyoni mwa Samsoni ikabidi watengeneze
mkakati wa kumtumia ili kuweza kumwangamiza Samsoni. Wakamwambia
“mbembeleze ili upate kujua asili ya nguvu zake nyingi na jinsi
tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa….”
Nia
ya wafilisti iko wazi kabisa – ni kumfunga na kumtesa. Wafilisti
hawakumficha Delila nia yao – walimwambia wazi kabisa na wakamweleza
jukumu lake na mshahara ambao wangemlipa kwa kazi hiyo. Ukisoma maandiko
utagundua kuwa vita ya Samsoni na wafilisti inaanza nyuma kidogo kabla
ya hapo. Na walikuwa wamemwinda kwa style na mbinu nyingi sana bila
mafanikio. Ghafula wakagundua mpango wa ajabu sana wa kumtumia mwanamke;
wakagundua kuwa katika mambo ambayo yanaweza kukusaidia kumwangusha
mwanaume kirahisi ni kwa kumtumia mwanamke. Walijua kuwa Samsoni si mtu
wa kawaida na kwamba hata nguvu za wanajeshi wao haziwezi kumshinda
Samsoni maana alikuwa ameshawapiga mara nyingi tu – alikuwa
ameshapambana na simba akamrarua vibaya sana – alikuwa amewafunga mbweha
mia tatu mikia akawawasha moto akawapitisha kwenye mashamba ya
wafilisti. Kwa hiyo wafilisti walijua wazi kuwa Samsoni hawezi kushikika
kirahisi, kwa hiyo ilibidi watafute “super plan.”
Ghafula
wakagundua kuwa iko nguvu ya ziada ndani ya mwanamke. Swali la msingi
la kujiuliza kawaida ni kuwa katika vitu vyenye nguvu ya kuleta
mabadiliko duniani ni wanawake. Kama unataka mabadiliko ya aina yoyote
ile duniani – yawe mema au mabaya we anza na wanawake tu. Ndani ya
mwanamke Mungu aliweka nguvu ya kuzalisha na kuzidisha yaani “power of
multiplying.” Sasa hiyo waliyopewa inaweza kutumiwa kuzalisha mema au
kuzalisha mabaya. Mungu anataka awatumie wanawake kuzalisha vya kwake na
shetani naye anawawinda wao ili wamsaidie kuongeza uovu duniani. Ndio
maana utakuta timu nyingi sana za maombi zimejaa wanawake lakini pia
utaona kuwa kichocheo kikubwa cha maovu duniani ni wanawake. Ndio maana
vita waliyonayo wanawake kwenye ulimwengu wa roho ni kubwa sana.
Yeremia 31:22 inasema
“…. Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda
mwanamume.” Hii ni kitu ya ajabu sana maana kitabu cha Mwanzo
kinatuambia kuwa Mungu alipomaliza kazi yake ya uumbaji aliona kila
alichokifanya kuwa ni chema na akapumzika, akafunga kazi ya uumbaji.
Lakini cha ajabu ni kuwa anakuja kumtumia Yeremia kutuambia kuwa kuna
jambo jipya Mungu ameumba tena ya kuwa mwanamke amlinde mwanaume. Kwa
nini Mungu alileta jukumu hili kwa mwanamke?
Mungu
alipokuwa ameweka jukumu la ulinzi chini ya mwanaume, shetani
alifanikiwa kumtumia mwanamke kumwangusha mwanaume. Hivyo Mungu akaamua
ampe mwanamke mwenyewe jukumu hili la kumlinda mwanaume. Hili jukumu
shetani analijua vizuri sana na anajua kuwa ili ampate mwanaume basi
inabidi atumie mwanamke Fulani. Angalia watumishi ambao walikuwa vizuri
kihuduma halafu wakaanguka, utagundua kuwa kuna mwanamke aliyetumiwa
kuleta anguko hilo. Sasa shetani akifanikiwa kumkamata mlinzi (mwanamke)
basi shetani anakuwa amepata nafasi nzuri ya kumwangusha mwanaume.
Hicho ndicho wafilisti walichofanya.
Sasa ile Waamuzi 16:15-16 inasema
“Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo
pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya
nguvu zako nyingi. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila
siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.”
Tunachojifunza
hapa ni kuwa licha ya Delila kuwa na nguvu ya kumshawishi Samsoni,
hakufanikiwa kupata alichokitaka kwa mara moja tu. Ila alikua na moyo na
kufuatilia hadi apate anachokitaka. Biblia inasema Delila alimsumbua
Samsoni kwa maneno yake kila siku hadi roho ya Samsoni ikadhikika hata
kufa.
Jambo la Kwanza
Kukusumbua kwa mashambulizi ya kila namna ambayo yatakukatisha tamaa hadi uachane na Mungu wako
Maandiko
yanatuambia Delila alimsumbua Samsoni kwa maneno yake kila siku hadi
alipokata tamaa na kuamua kutoa siri ya nguvu zake. Jambo ninalojiuliza
hapa ni kuwa hayo maneno aliyokuwa anamwambia yalikuwa maneno ya namna
gani? Zaburi 10:7 inasema “Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu.” Huu
msitari unatuambia kuwa ulini wa mtu unaweza kubeba madhara na uovu.
Hiki ndicho kilichompata Samsoni; ulimini mwa Delila kulikuwa kumejaa
maneno ya uovu na madhara ambavyo vililenga kumwangamiza Samsoni. Na
Biblia inatuambia kuwa yale maneno yalimsumbua Samsoni kiasi ambacho
roho yake ilifika mahali ikachoka.
Yale
maneno ya Delila hayakumpa Samsoni nafasi ya kupumzika. Tafsiri za
kiingereza zinasema kuwa “she gave him no peace” yaani hakumpa nafasi
hata ya kupumzika bali alimsumbua kila siku. Kwa hiyo adui alimzingira
kwa maneno ya kumkosesha amani kila siku hadi alipochoka. Hiki ndicho
shetani hufanya anapotafuta kukutoa kwenye mpango wa Mungu. Atahakikisha
amekusumbua kwa kila aina ya matatizo na mikosi na kushindwa na kila
jambo la kukatisha tamaa hadi uchoke. Atatafuta ni eneo gani la maisha
yako linalokupa furaha kisha atashambulia hilo eneo hadi uone Mungu
amekuacha. Atakachofanya ni kuisumbua roho yako ikose nafasi ya
kumtafuta Mungu. Ndio maana watu wengi wakiwa kwenye matatizo huwa
wanakosa hata hamu ya kuomba au hata kwenda kwenye ibada. Hii si kitu ya
kawaida, shetani anawinda kukukosesha amani ili apate mwanya mzuri wa
kukumalizia.
Utaona
hata ukienda kwa wapendwa wenzio unaona kama wanakung’ong’a, ukirudi
nyumbani unaona kama familia ni chungu, ukienda kazini unakuta
umefukuzwa kazi au wafanyakazi wenzio hawako pamoja na wewe. Yaani
unakuta kila kitu hakiendi sawa. Ukiona hivyo anza kukaa sawa na Mungu
maana ni dalili ya mashambulizi ya shetani kukutoa kwenye mpango wa
Mungu. Shetani akiona kuwa hawezi kukupata wewe moja kwa moja
atakachofanya ni kushambulia vitu vinavyokupa amani. Utakumbuka habari
za Ayubu na jinsi shetani alivyoshambulia mifugo yake, mashamba yake,
watoto wake na mwisho akampa majipu makali sana. Shetani alikuwa
hatafuti mashamba wala watoto wala afya ya Ayubu, yote hayo yalikuwa
mashambulizi yaliyolenga kumtoa kwenye mpango wa Mungu. Shetani anajua
akikusumbua sana utapoteza network yako kwa Mungu.
Jambo la Pili
Shetani atakuletea usingizi wa kiroho ili iwe rahisi kwake kutimiza mpango wake
Waamuzi 16:18-19 inasema
“Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake,
akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii
tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa
Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake…”
Mathayo 13: 24-25 inasema “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.”
Swali
kujiliza hapa ni kuwa kama Samsoni alikuwa ameshamwambia Delila siri
yake yote kulikuwa na haja gani tena ya kumlaza usingizi? Jibu lake ni
wazi kabisa. Delila alijua wazi kabisa kuwa suala la kumnyoa Samsoni
vishungi vya nguvu zake lisingewezekana kama Samsoni angekuwa macho
maana ni lazima angepigana na wafilisti wasingefanikiwa. Shetani anajua
wazi kuwa hawezi kukutoa kwenye mpango wa Mungu ikiwa rohoni uko macho
maana utapambana naye na utamshinda. Kwa hiyo anatakachofanya ni
kukufanya ulale kiroho ndipo aje kukumaliza. Shetani anajua kuwa akija
wakati uko macho utamwona na utapambana nae, kwa hiyo atakuvia wakati
ambao kiroho umelala.
Shetani
anajua kuwa kanisa ambalo lina waombaji waliomacho hawezi kulishinda
hivo atatafuta daima namna ya kuwalaza usingizi ili aweze kuwashinda.
Katika dunia ya leo shetani amefanikiwa kuwalaza usingizi watu wengi kwa
njia nyingi sana. Kuna watu walikuwa waombaji wazuri lakini walipopata
kazi (ajira) wakawa busy na kazi na wakaacha kabisa kusoma neno la Mungu
na maombi wakasahau kabisa. Ukiwauliza watakuambia kuwa wako busy na
kazi. Lakini hawajui kuwa shetani ametumia kazi zao kuwalaza usingizi
ili wasimtumikie Mungu. Wengine shetani amewalaza usingizi kwa kupitia
teknolojia. Watu wengi wako tayari kuangalia TV hadi macho yakauma
lakini ukiwaambia kusoma Biblia hata sura moja kwa siku watakuambia kuwa
hawana muda. Watu wengi leo wanatumia simu ambazo badala ya kuwasaidia
kumtafuta Mungu zinawasaidia kujitenga na Mungu. Unakuta mtu anamiliki
simu ambayo inauwezo wa facebook, twitter, whats app, na pia ina uwezo
wa kuwa na Biblia. Lakini utakuta ame-install program zingine zote
lakini Biblia hajaweka. Au anayo lakini kila anapokuwa anakuwa anaipita
tu kama haioni. Anakuwa busy na kwingineko kote lakini sio kwenye
maandiko.
Nimezunguka
kwenye makanisa mengi sana hapa nchini na kujionea hali za kiroho za
makanisa hayo jinsi zilivyo. Nasikitika kusema kuwa hali ya kanisa sasa
hivi ni ile iliyoandikwa katika Ufunuo 3:1
Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.
Hili
ndilo kanisa la sasa na watu wake jinsi tulivyo. Tumebaki na majina ya
historia za jinsi tulivyokuwa zamani lakini sasa hivi wengi shetani
amewalaza usingizi. Utasikia mtu anasema: enzi zangu banaaa… nilikuwa
mwombaji sana, mwingine anasema nilikuwa nasoma sana neno la Mungu,
mwingine nae anasema nilikuwa mfuatiliaji mzuri sana wa ibada n.k. Swali
ambalo huwa najiuliza ni: huo uwezo umeenda wapi? Kuna watu wengi leo
wanasema kuwa wanasali makanisa ya kiroho lakini wao wenyewe sio watu wa
rohoni. Watu wengi wamelazwa usingizi na shetani.
Bahati
mbaya ni kuwa ukiwa umelala usingizi hujui kinachoendelea juu yako. Na
ndivyo walivyo watu wa leo, wengi wamelala usingizi kiasi kwamba hawajui
hata kile shetani anachofanya kwenye maisha yao. Kutokana na usingizi
waliolala wanajiona kuwa bado wanamtumikia Mungu kumbe shetani
alishawamaliza nguvu zao.
Waefeso 5:14 inasema, “Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”
Jambo la Tatu
Shetani atahakikisha ameharibu chanzo cha nguvu zako za kiroho
Waamuzi 16:19 “…Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.”
Shetani
atahakikisha kuwa ameua asili ya nguvu zako ili afanikiwe kukumaliza
kabisa kiroho. Baada ya kukulaza usingizi wa kiroho kitakachofuata ni
kuua msingi wa nguvu zako; maana akipiga chanzo anakuwa amekugeuza
kutoka kwenye kuwa hai unabaki mkristo aliyekufa kiroho. Chanzo
kikipigwa ndipo unakutana na watu wenye majina ya kuwa hai lakini
wamekufa. Chanzo kikipigwa ndipo unaanza kusikia mtu anasema: “nilikuwa
mwombaji sana” “nilikuwa mtu mzuri sana wa neno la Mungu” n.k.
Ukiona
mtu anaanza kusimulia habari za utumishi wake wa nyuma ambao kwa sasa
hawezi kuufanya ujue kuwa chanzo cha nguvu zake kimepigwa. Shetani
akiisha kukuweka busy na shughuli za dunia na kufanikiwa kukulaza
usingizi, atakachofanya baada ya hapo ni kunyoa vishungi vya nguvu zako
ili usiwe na mtaji tena wa kusimama. Watu wengi leo shetani ameua vyanzo
vyao vya nguvu za kiroho na wamebaki na historia tu kuwa waliwahi
kufika mahali Fulani kiroho. Usiruhusu shetani anyoe chanzo cha nguvu
zako, usiruhusu shetani aharibu mtaji wako wa kiroho. Kama asili yako ni
maombi basi usiruhusu jambo lolote lile likuzuie kuomba; unahitaji
kuchochea chanzo cha nguvu zako kila siku.
Jambo la Nne
Shetani atakuletea mahangaiko na mateso makali ya kimaisha ili uachane kabisa na imani yako kwa Mungu
Waamuzi 16:19 “… Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.”
Baada
ya shetani kuwa amekusumbua kule mwanzo kwa mashambulizi ya kila namna
na kukatisha tamaa, na baada ya kuwa ameshakulaza usingizi na kisha
kuharibu chanzo cha nguvu zako, sasa atakachofanya ni kuleta juu yako
mahangaiko na mateso ambayo yatakufanya usimkumbuke kabisa Mungu wako.
Delila aliamua kumsumbua Samsoni baada ya kuwa amemnyoa vishungi vya
nguvu zake ili kuhakikisha kuwa hakuna nguvu hata kidogo iliyosalia
ndani ya Samsoni ambayo inaweza kumsaidia akainuka tena. Ndicho shetani
anachofanya; akiishavunja chanzo cha nguvu zako ataendelea kuleta
mashambulizi mengine mengi ili ukose kabisa nafasi ya kumrudia Mungu na
ukose kabisa nguvu za kusimama tena kiroho.
Ndio maana 2Petro 2:20 inasema:
Kwa
maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na
Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya
mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.
Hali
yao mwisho inakuwa mbaya kwa sababu shetani akifanikiwa kukunasa kwenye
mtego wake atafanya kila jambo ili kuhakikisha kuwa haurudi tena kwa
Mungu wako.
Jambo la Tano
Shetani akiisha kukukamata atakufanya ulitumikie shauri (kusudi) ambalo hukuitiwa
Waamuzi 16:21 “Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”
Tumejifunza
mwanzoni kuwa kila mtu ambaye Mungu amempa nafasi ya kuishi amempa na
shauri ambalo mtu huyu anapaswa kulitumikia. Lakini shetani akikukamata
na kukuweka chini ya himaya yake atakutoa kwenya kazi ambayo Mungu
alikuitia na kukupeleka kwenye kazi ambayo hukuitiwa kabisa. Samsoni
aliwekwa awe mnadhiri wa Mungu na alipaswa kuwatetea waisraeli dhidi ya
adui zao. Lakini shetani alipofanikiwa kumweka chini ya himaya yake
alimfanya akalitumikie shauri la wafilisti kwa kusaga ngano gerezani.
Leo
hii wapo watumishi wa Mungu wengi sana ambao shetani anawasagisha ngano
gerezani badala ya kumtumikia Mungu. Wapo wachungaji wanaosaga ngano,
wapo waimbaji wanasaga ngano, wapo walimu, mitume, manabii n.k. ambao
wanajidai kuwa wanamtumikia Mungu lakini kimsingi wanasaga ngano kwenye
magereza ya wafilisti. Ikiwa ni mtumishi wa Mungu kweli kweli hebu
angalia sana huduma Mungu aliyokupa usije kuwa unadhani bado unamtumikia
Mungu kumbe macho yako yametobolewa na unasaga ngano kwenye gereza la
wafilisti.
Unaweza
ukafikiri kwamba labda atakuvikwa kuwa mwenye dhambi wa kutupwa, lakini
nataka kukwambia kuwa shetani atakutumikisha kwenye shauri lolote lile
ambalo anajua kuwa litakufanya uunufaishe ufalme wake. Anaweza akakuacha
uendelee kuwa muumuni wa kanisa lako lakini kazi yake ni kuvuruga kazi
ya Mungu mahali hapo isiende mbele. Utaona mtu anakua mchonganishi na
mwenye kuvuruga kila kikundi cha kihuduma kinachoinuka. Kwa vile aliwahi
kuwa mtumishi mzuri basi watu wanamwamini sana kiasi kwamba hawadhani
kama yeye ndiye anayesababisha vurugu. Lakini kila kikundi anachoenda
kinakufa – oooh ujue huyo ni anaesaga ngano kwenye gereza la shetani.
NEEMA YA KUREJESHWA TENA
Muhubiri 3:15 inasema “Yale yaliyoko yamekuwako; na hayo yatakayokuwako yamekwisha kuwako; naye Mungu huyatafuta tena mambo yale yaliyopita.”
Maneno
haya yanatufundisha kuwa licha ya wakati mwingine kuwa tumepoteza uhai
wetu kwa Bwana, Mungu anao uwezo wa kuturejesha tena kwenye mpango wake
maana yeye huyatafuta tena mambo yaliyopita ili atuinue tena. Ijapokuwa
shetani anaweza akawa amekuangusha na kukutoa kwenye mpango wa Mungu
nataka kukwambia kuwa kuna kuinuka tena. Samsoni alitobolewa macho,
akanyolewa nywele zake, akasagishwa ngano gerezani lakini Mungu
alimrejeshea tena ushindi mkubwa. Ayubu 22:29 inasema “Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.”
Waamuzi 16:22 inasema
“Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya
kunyolewa kwake.” Haya maneno yanatuonesha kuwa licha ya kunyolewa
kwake, bado Mungu alikuwa ameacha mzizi wa nywele ndani ya Samsoni.
Haijalishi walikuwa wamemnyoa kipara au aina gani ya kinyozi ila
ninachokijua ni kuwa hawakunyoa hadi mzizi wa nywele. Nataka kukwambia
hivi: ikiwa shetani amekunyoa nywele zako bado liko tumaini kwa Bwana.
Mungu anao uwezo wa kukuinua tena na kukuinulia tena nguvu zako. Bado
Bwana anayo nafasi ya kukusimamisha mbele ya adui zako na kuwaangamiza
mbele yako. Mwisho wa huduma yako bado haujafika, Mungu anazo nguvu za
kukusimamisha tena.
NAKUPA SHAURI MKUMBUKE MUNGU NAYE ATAKUINUA TENA
Nimebarikiwa sanaa na neno
ReplyDelete