Thursday, September 1, 2016

MWEZI WA TISA KATIKA BIBLIA NA BARAKA ZAKE

USIKOSE kufuatilia mfululizo wa masomo yetu LIVE kupita facebook page ya Vedastus Lukiko. Bonyeza hapa kuangalia.
MWEZI WA TISA KATIKA BIBLIA NA BARAKA ZAKE

Wayahudi hapo zamani walikua wana kalenda mbili: kalenda ya kiraia (kifalme)  na kalenda ya kimungu. Kalenda ya kiraia ilitumika kwa mambo ya kifalme, utawala, hesabu ya siku za kuzaliwa na mikataba. Kalenda ya kimungu ilitumika kwa matukio ya kiroho ambayo Mungu aliwaamuru Israel wayatimize mfano sikuu na majira mengine ya kiroho.

Sasa kwa mujibu wa Biblia mwezi wa Tisa unaitwa mwezi wa “Kisleu”. Huu mwezi kwenye kalenda ya kifalme ni mwezi wa tatu (3) wa mwaka, lakini kwenye kalenda ya kimungu ni mwezi wa tisa (9) wa mwaka. Sisi tutauangalia mwezi huu kwa mujibu wa kalenda ya kimungu maana ndicho kinachotuhusu. Ukiutafsiri mwezi huu wa Kisleu kwenye kalenda ya sasa hivi utakuta unaangukia kati ya mwezi November hadi December (siku 29).


 Kwa Israeli huu mwezi ulikua na mambo mawili makubwa
  1. Ulikua ni mwezi wa majira ya mvua nyingi na kwa hiyo ulikua ni mwezi wa kulima na kupanda.
  2. Mwezi wa tisa unadhihirishwa kama mwezi wa kuomba, mwezi wa watu kumtafuta Mungu, mwezi ambao Mungu anawaonya watu kuhusu dhambi zao na makosa yao. Ni mwezi ambao watu wanasukumwa kujenga upya uhusiano wao na Mungu.
Nehemia alipata msukumo wa kurudi Yerusalemu kujenga upya ukuta wa mji ndani ya mwezi huu wa Kisleu (yaani mwezi wa 9). Soma Nehemia 1:1-11, msitari wa 1-4 inasema:
Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisleu, mwaka wa ishirini, nilipokuwapo Shushani ngomeni, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu. Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto. Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni.
Tunaona hapo kuwa msukumo wa kuomba toba na kumrudia Mungu, na kujenga uhusiano mpya kati ya mji wa Yerusalemu na Mungu ulikuja ndani ya Nehemia kwenye mwezi wa Tisa. Huo msukumo ulimpa Nehemia kiu ya kuomba na kufunga ili Mungu arudishe tena hadhi ya mji wa Yerusalemu ambao ulikua umebomolewa na kudharauliwa mbele ya mataifa mengine.
Jambo hili pia linajitokeza kwenye kitabu cha Yeremia 36:1-10. Utaona hapa Mungu akiwa anatafuta namna ya kuwarudisha watu wake waliokuwa wameanguka dhambini na anamwagiza Yeremia aandike maneno yote ya unabii ambayo alikua amepewa na awasomee watu ili wasikie na wageuke na kumrudia Mungu. Msitari wa 9-10 unasema:
Basi, ikawa katika mwaka wa tano wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kenda, watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, na watu wote waliokuja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakapiga mbiu ya kufunga mbele za Bwana. Basi, wakati huo Baruku akayasoma maneno ya Yeremia katika nyumba ya Bwana, katika chumba cha Gemaria, mwana wa Shafani, mwandishi, katika ua wa juu, mahali pa kuingilia kwa lango jipya la nyumba ya Bwana, akiyasoma katika masikio ya watu wote.
Watu walitangaza mbiu ya kufunga mbele za Bwana katika mwezi wa tisa na katika siku hiyo maneno ya Bwana yakasomwa masikioni mwao ili waweze kutubu na kumrudia Mungu wao. Toba kama hii pia ilifanyika wakati wa Ezra pale ambapo Israel walifanya dhambi kwa kuoa wanawake wageni tofauti na Mungu alivyokua amewaamuru (Ezra 10:1-9). Msitari wa 9 unasema:
Ndipo wanaume wote wa Yuda na Benyamini wakakusanyika katika muda wa siku tatu; ulikuwa mwezi wa kenda, siku ya ishirini ya mwezi; na watu wote wakaketi katika uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakitetemeka kwa sababu ya neno hilo, na kwa sababu ya mvua kubwa.
Tunaona hapo juu pia roho ya toba iliwaangukia hawa watu kwenye mwezi huu wa 9 na wakafanya agano na Mungu la kuachana na wanawake hao waliowaoa.
Ukisoma kitabu cha Hagai 2:10, 17-18 utakuta tena wito wa watu kumrudia Mungu ukiachiliwa ndani ya mwezi huu wa tisa. Neno la Mungu linasema:
Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa kenda, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema….. Naliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunielekea mimi, asema Bwana. Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kenda, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la Bwana tafakarini haya.
Sasa ukija kwenye agano jipya haukuti huu mwezi wa tisa ukiongelewa kabisa lakini utakuta namba tisa ikiwa ni namba inayoashira muda wa kurejesha uhusiano na Mungu na muda wa kuomba. Tutaangalia mistari michache:
Mathayo 27:45-46 Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? (Yesu alikata roho saa tisa na ukombozi wetu unaopatikana kwa njia ya mauti yake ulianzia hapo)
Matendo 3:1-2        Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. (Hawa ndugu walikua wanaenda kusali saa tisa na Yule kiwete ukombozi wake ulikuja muda huo)
Matendo 10:30-31Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing'arazo, akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.
Nimekuwekea tu hiyo mistari ili kukuonesha kuwa namba tisa sio namba ya kawaida kwenye ulimwengu wa roho. Ni namba inayoashiria muunganiko wa mbingu na watu hasa kwenye suala la uhusiano wao na Mungu. Ni wakati ambao Mungu anawatafuta watu wake lakini pia ni majira ya watu kumrudia Mungu wao.
Nataka nikupe hamasa ya kumtafuta Mungu ndani ya mwezi huu. Sina maana ya kwamba miezi mingine usimtafute Mungu, La hasha! Ninachotaka ni kuwa kama ulikua umerudi nyuma kiroho basi sasa anza upya safari yako na Mungu. Mungu wetu ni wa rehema na kila tunaporudi kwake kwa toba ya kweli yeye hutusamehe na kutukumbatia tena.
Huu ni mwezi wa kulima na kupanda (kwa maana ya kiroho). Kama shamba lako ulilopewa na Bwana ulikua umelitelekeza basi ndugu amka shika jembe rudi shambani mwa Bwana. Huu ni mwezi wa mvua nyingi za Baraka lakini hata mvua ikinyesha vipi kama mtu hajaingia shambani akalima bado atakufa kwa njaa. Usiruhusu hii mvua itakayoachiliwa mwezi huu uwanufaishe wengine halafu wewe ufe kwa njaa. Rudi shambani mwa Bwana ifanye kazi yake nawe utafurahia Baraka za mwezi huu wa tisa. Tengeneza uhusiano wako na Mungu. Huu ni mwezi wa kufunga na kuomba. Mpe Mungu muda wa kutosha katika maisha yako ndani ya mwezi huu. (Devote yourself to worship him and seek his presence in your life).
Rudi Yerusalemu yako ukajenge tena kuta zilizobomoka na malango yaliyotiwa moto. Bwana yuko pamoja nawe endapo utachukua hatua ya imani na kumtafuta Mungu kwa bidii katika mwezi huu wa Tisa. Kumbuka Mithali 8:17 Bwana anasema: “Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.”
MUNGU WETU AKUBARIKI UNAPOSHIRIKI BARAKA ZA MWEZI HUU WA TISA

5 comments:

  1. Mungu mwema asiyemchoyo wa fadhili naomba akanikirimie katika mwezi wa tisa sawasawa na mahitaji yangu ila MAPENZI YAKE YATIMIZWE. AMINA

    ReplyDelete
  2. Amen! Amen!
    Naipitia Leo hakika 2022. Brother Lukiko your blessed

    ReplyDelete
  3. Amen stay blessed servant
    It's my time
    I'll never be the same again

    ReplyDelete