Mwanzo Sura ya 3
Udanganyifu
wa shetani kwa mtu
Sura hii inaanza kwa utambulisho
wa ajabu sana kuliko sura mbili zilizotangulia; wakati sura ya 1 na ya 2
zikianza kwa kuonesha uumbaji wa mbingu na nchi na kukamilika kwake, sura ya 3
yenyewe inaanza kwa kumtambulisha kiumbe mmojawapo kati ya viumbe aliowafanya
Mungu. Kiumbe huyu anaitwa nyoka sawa na jina alilopewa na Adamu kwenye Mwanzo 2:19-20. Sura hii ya 3
inamtambulisha kiumbe huyu kuwa ni kiumbe aliyekuwa “mwerevu” kuliko wanyama
wote wa mwitu aliokuwa amewafanya Bwana Mungu. Kwa hiyo kwa lugha rahisi ni
kuwa nyoka ndiye aliyekuwa amewekwa awe juu ya kundi la wanyama wa mwitu na
ndio maana alipewa akili kuliko wengine wote.
Kinachoshangaza ni uwezo wa huyu
nyoka kuzungumza na mwanamke kwa jinsi ambavyo waliweza kuelewana; hakika hili
linahitaji tulichunguze vizuri zaidi. Kwa faida yako msomaji, msitari wa kwanza
unasema hivi:
Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa
mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema
Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?
Hili neno “alikuwa” lililotumika
kwenye msitari huu, tafsiri ya kiebrania imetumia neno “hayah” ambalo kwa
kiingereza linamaanisha “to become” au “to come into being” ambayo kwa
Kiswahili linamaanisha “kufanyika” katika hali fulani. Kwa hiyo Biblia
inaposema nyoka alikuwa mwerevu, maana yake alifanyika mwerevu kuliko wanyama
wengine wote. Tunataka tuone huku kufanyika alikofanyika kulitoka kwa nani na
ni kwa kusudi gani alipata huu werevu. Kabla hatujaenda mbele sana turudi
kidogo kwenye uumbaji tuone Mungu alipoumba nyoka nini kilifanyika.
Mwanzo 1:24-25 ndiyo inayohusika na siku nyoka alipoumbwa, inasema
hivi:
Mungu akasema, Nchi
na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake;
ikawa hivyo. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa
kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
Nyoka alifanywa
kwenye kundi la wanyama wa mwitu (maana ndivyo Mwanzo 3:1 inavyosema) na Mungu
alipomfanya nyoka katika kundi hili aliona kuwa ni vyema. Swali tunalojiuliza
hapa ni: Je, ule werevu alioutumia nyoka kumdanganya mwanamke alifanywa nao au
kuna kufanywa kwingine kulikotokea baadae ambako hakuhusiani na uumbaji wa
Mungu? Biblia inajibu vizuri sana swali hili.
Matthew 10:16 Yesu anasema hivi: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo
kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara
kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua” (msisitizo umeongezwa). Huu
msitari unatufunulia kuwa nyoka alipofanywa na Mungu alipewa busara na wala sio werevu. Yesu hakusema iweni ‘werevu’ kama nyoka bali alisema iweni
na ‘busara’ kama nyoka. Kwa nini Yesu alitaka tufanane na nyoka kwenye suala la
busara na wala sio werevu? Kwa sababu alijua dhahiri kuwa Mungu alipomfanya
nyoka hakumfanyia werevu bali alimpa busara ili awe juu ya wanyama wengine wa
mwitu kama tulivyotangulia kusema hapo kabla. Ni ile busara aliyofanywa nayo nyoka
ndiyo Mungu aliyoiona kuwa “vyema” pale Mwanzo 1:25; huu werevu ulikuwa na
chanzo kingine ambacho hakika hakuwa Mungu maana Mungu alimfanya nyoka awe na
busara lakini sio werevu.
Neno “mwerevu” lililotumika kumweleza nyoka kwenye Mwanzo 3:1, Biblia za kiingereza
zimetumia neno “subtil” au “cunning” kuelezea sifa hii ya nyoka. Sisi
tungependa tuichambue sifa hii kwa kulitumia neno “cunning” kama lilivyotumika kwenye tafsiri ya New King James
Version. Msitari huu wa Mwanzo 3:1 kwenye tafsiri hii ya NKJV unasomeka hivi:
Now the serpent was more cunning than any beast of the
field which the LORD God had made….
Cambridge Advanced learners
Dictionary (3rd Edition) wana jambo la kutuonesha kuhusu maana ya
neno hili. Wanasema hivi:
Cunning
“describes people who are clever at planning something so that they get what they want, especially by tricking other people, or things
that are cleverly made for a particular purpose” (msisitizo umeongezwa)
Maana yake ni kuwa neno “cunning”
hutumika kuwaelezea watu ambao wako makini sana katika kupanga vitu ili wapate
kile wanachokitaka, hasa hasa kwa kuwalaghai (kuwadanganya) watu wengine.
Hakika hiki ndicho kilichokuwa ndani ya nyoka; hakutumia busara aliyoumbiwa na
Mungu bali alitumia werevu (yaani uwezo wa kupanga vitu ili upate unachokitaka
hasa hasa kwa kuwadanganya watu wengine). Nyoka alifanikiwa kupata alichotaka
kwa kutumia uongo na ulaghai. Swali tunalojiuliza hapa ni: huu werevu aliutoa
wapi?
Tumeona hapo juu kuwa werevu
unaozungumzwa kwenye hii Mwanzo 3:1 ulikuwa ni udanganyifu uliopangiliwa
sawasawa ambao ulikuwa na lengo fulani maalumu nyuma yake. Kama nyoka
alifanikiwa kupata alichotaka kwa kupitia uongo basi ni wazi sasa kuwa nyoka
yule hakuwa nyoka wa kawaida, bali alikuwa nyoka ambaye ni baba wa uongo.
Katika Yohana
8:44 Yesu anasema hivi:
Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi,
na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake.
Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (msisitizo umeongezwa)
Yesu anamtaja Ibilisi kama mwuaji
tangu mwanzo na ambaye hajawahi kusimama katika kweli. Kweli ni neno la Mungu;
Yesu alisema “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli (Yohana 17:17).” Ikiwa kweli ni neno la Mungu, basi Yesu anaposema kuwa Ibilisi
hakusimama katika kweli tangu mwanzo maana yake ni kuwa tangu mwanzo Ibilisi
hakuwahi kusimama sawa na neno la Mungu. Hakika hiki ndicho alichofanya kwenye Mwanzo 3:4-5, maana wakati Mungu alisema
kuwa mkila matunda ya mti mliozuiliwa mtakufa, nyoka yeye akasema kuwa hakika
hamtakufa bali mtakuwa sawa na Mungu.
Huyu nyoka
anayejitokeza hapa katika Mwanzo 3:1 hakika alikuwa ni Ibilisi mwenyewe
aliyejiingiza tu katika umbo la nyoka. Shetani hakuwa na njia ya kuwasiliana na
mtu isipokuwa kwa kutumia moja ya vitu ambavyo mtu mwenyewe alikuwa anavifahamu
na amevipa majina yeye mwenyewe tena vimewekwa chini yake. Biblia inatufunulia
wazi kujua kuwa yule nyoka aliyezungumza na Hawa alikuwa ni Ibilisi mwenyewe. Ufunuo 12:7-9 unasema hivi:
“Kulikuwa na vita
mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye
akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao
hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka
akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa
zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,
audanganyaye ulimwengu wote;
akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” (msisitizo
umeongezwa)
Msitari huu wa Ufunuo
unataja kuhusu nyoka wa zamani
ambaye kazi yake ni kuudanganya ulimwengu wote; na jina lake anaitwa Ibilisi na
Shetani. Hili neno ‘nyoka wa zamani’ halijitokezi sehemu nyingine yoyote ya
Biblia isipokuwa katika Ufunuo 12:9
na Ufunuo 20:2. Kwa hiyo matumizi ya
neno hili yanatuashiria kuwa hiyo “zamani” inayotajwa ni ile ambayo Yesu
anaitaja kama “tangu mwanzo”. Hivyo tunajua sasa kuwa nyoka wa zamani
anayetajwa kwenye kitabu cha mwisho cha Biblia ni yule aliyemdanganya Hawa
kwenye kitabu cha mwanzo cha Biblia.
Hivyo basi, yule
nyoka mwerevu aliyezungumza na Hawa alikuwa ni Ibilisi na Shetani ambaye tu
alilitumia umbo la nyoka wa kawaida ili kupata njia ya kumfikia mtu. Kosa la
nyoka mwenye busara (yaani nyoka aliyefanywa na Mungu) kuruhusu atumiwe na
Ibilisi ili kumwangamiza mtu lilipelekea adhabu kali kwa nyoka halisi na uzao
wake wote, kama ambavyo Mungu hamwachi bila adhabu mtu yeyote anayeruhusu
atumiwe na shetani katika kuharibu kusudi la Mungu. Shetani ndiye alikuwa
mwanzilishi wa uasi na dhambi katika uzao wa mtu. Kuna mbinu alizotumia
kulifanikisha hili; acha tuone alivyofanya.
Hatua ya kwanza
ilikuwa ni kulitupia wasiwasi neno la Mungu. Hebu sikia anavyosema: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu … (msisitizo
umeongezwa).” Mungu alikuwa ameshasema na ametoa amri yake bila kuficha kitu,
alikuwa wazi kabisa kuwa “walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya
usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika (Mwanzo
2:17).” Ibilisi alitaka kuharibu kweli ya Mungu kwa kujaribu kujifanya kama
hakusikia vizuri, hivyo akaleta uongo wake kwa njia ya swali ili asigundulike
mapema. Kitu cha ajabu ni kuwa hakujipeleka kwa mwanaume na huu ujanja wake
bali alimwendea mwanamke. Kwa nini alifanya hivi?
Utagundua kuwa Mungu
alipokuwa anatoa agizo la kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya
mwanamke alikuwa bado hajafanywa. Agizo hili lilitolewa katika Mwanzo 2:17 na mwanamke alifanywa rasmi
katika Mwanzo 2:22; kwa hiyo ni wazi
kuwa Hawa alijifunza agizo hili kutoka kwa Adamu, maana hatuoni Mungu
akilirudia tena baada ya Hawa kufanywa. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa Adamu
alikuwa na uelewa mzuri zaidi wa neno la Mungu kuhusu agizo hili kuliko hawa,
na shetani alijua hilo hivyo akachagua kutumia kiungo kilicho dhaifu ili
kupenyeza uasi. Biblia iko wazi kabisa kuhusu hili jambo; Paulo anasema hivi:
“Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa
kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa
Kristo” (msisitizo umeongezwa) (2 Kor 11:3). Soma pia 1 Timotheo 2:14.
Kwa hiyo
aliyedanganywa hakuwa Adamu bali Hawa, na kudanganywa kwake kulitokana na
shetani kujua kuwa Hawa hakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya kile Mungu
alichokuwa ameagiza. Lilikuwa jukumu la Adamu kumlinda mkewe na kumjulisha
kweli ya Mungu jinsi ilivyokuwa. Inawezekana kuwa Adamu alimfundisha sawasawa
ila Hawa ndo akajichanganya au Adamu ndiye hakumfundisha mkewe sawasawa. Maana
utakuta majibu ya Hawa kuhusu kile Mungu alichosema yakitofautiana kabisa na
kile Mungu alichoagiza. Mungu alisema kuwa “msile” lakini hawa anasema
wameambiwa “msile wala msiguse”. Hakuna mahali ambapo Mungu alitoa agizo la
‘msiguse’. Hii ilitokana na ufahamu mdogo aliokuwa nao Hawa juu ya neno la
Mungu. Ni rahisi sana kuingia kwenye mtego wa shetani ikiwa hauna neno la Mungu
la kutosha ndani yako. (Fimbo ya Musa Ministry tunaandika kitabu kuhusu hila za
shetani katika kanisa, ndani yake tunaeleza vizuri zaidi jinsi ambavyo
kutokufahamu neno la Mungu kunavyompa shetani nafasi nzuri ya kukudanganya na
kukushinda; tutawajulisha kikiwa tayari).
Shetani ili apenyeze
uharibifu wake kwenye jamii au kanisa daima anatafuta nani aliye dhaifu ili
amtumie. Akiishapata mtu aliye dhaifu basi ni rahisi sana kuwashambulia walio
imara kwa sababu anakuwa tayari ameingia katikati yao kupitia yule mtu dhaifu.
Udhaifu wa Hawa ulimpa shetani nafasi ya kumpoteza hadi Adamu ambaye alikuwa
imara. Vivyo hivyo kwenye makanisa na sehemu za ibada shetani huwa anatafuta ni
nani kati yenu ni dhaifu; akiishampata huyo basi humtumia yeye kuwamaliza
wengine walio imara. Ndiyo maana ni muhimu sana kuimarishana kiroho kwa sababu
udhaifu wa wenzako unaweza kutumiwa na shetani kukupoteza wewe uliye imara.
Usifurahi hata kidogo kuona watu unaofanya nao huduma au watu wa kanisani
wanakutegemea wewe tu kwa mambo yote ya kiroho; hii ni hatari kwako maana
shetani akipata mpenyo kati yao inakuwa kwake ni njia ya kukufikia na wewe
kirahisi zaidi. Kama unaona kuwa Mungu amekupa neema ya kuwa na ufahamu wa neno
la Mungu na mambo ya kiroho zaidi ya wenzako basi jitahidi kuwaimarisha na
wenzako ili nao wawe msaada kwako wakati utakapokuwa umepungukiwa nguvu. Hiki
ndicho Yesu alichomwagiza Petro baada ya kumwombea; alisema:
… Simoni, Simoni,
tazama, Shetani amewataka ninyi apate
kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako
isitindike; nawe utakapoongoka
waimarishe ndugu zako.” (msisitizo umeongezwa) [Luka 22:31-32].
Katika jibu lake kwa
shetani Hawa aliongeza kitu ambacho hakikuwepo kwenye neno la Mungu. Biblia iko
wazi kabisa kuwa kuongeza neno au kupunguza neno kwenye maneno ya Mungu ni kosa
kubwa linalostahili adhabu (Ufunuo
22:18-19). Kwa hiyo si ajabu kuwa adhabu ya mwanamke ilikuwa chungu mno
kuliko ya mwanaume kwa sababu ya kosa la kuongeza kwenye maneno ya Mungu. Ni
vema sana kulishika neno la Mungu kwa usahihi na kama lilivyo bila kuongeza
yako au kupunguza.
Ile kuongeza neno
kwenye maneno ya Mungu kulimpa shetani kujua kuwa Hawa alikuwa ni njia rahisi
ya kupenyeza uovu wake. Hatua ya pili sasa ilikuwa ni kulikataa kabisa neno la
Mungu. Katika msitari wa 4 shetani anasema hivi: “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa.” (msisitizo
umeongezwa) Hii ni ajabu sana, Mungu alikuwa ametangaza na ameweka wazi kabisa
kuwa ikiwa mtu atajiingiza katika kulihalifu agizo la Mungu na kuasi kwa kula
matunda ya mti aliokatazwa hakika atakufa. Shetani anainuka na kulikana
waziwazi hili neno la Mungu na kusema “hakika hamtakufa.”
Ni kazi ya shetani
kulipindua neno la Mungu kwa uongo na kuwapoteza watu wa Mungu. Leo hii
tunasikia imani na makanisa kadhaa yakiibuka na kutoa mafundisho ambayo ni
kinyume kabisa na neno la Mungu. Kwa mfano, Mungu ameagiza wazi kabisa kuwa mtu
yeyote atendaye dhambi ataangamizwa katika jehanamu ya moto, lakini wapo watu
wanaosema kuwa Mungu hawezi kumwumba mtu halafu akamtesa tena kwa moto hata
kama mtu huyo amekosea vipi. Ni shetani yule yule aliyepindua kweli ya Mungu na
kumdanganya Hawa ndiye anaendelea kuwadanganya watu kuwa jehanamu ya moto haipo
ili watu waendelee kutenda dhambi. Ndugu msomaji wetu tunapenda kukufahamisha
kuwa Mungu wetu hushika daima neno lake wala hataacha kuadhibu kwa hasira kali
na ghadhabu wale wote watakaofuata udanganyifu wa Ibilisi na kuicha kweli
halisi ya Mungu.
Kosa la kutaka kuwa kama Mungu
Katika msitari wa 5
shetani anaendeleza hila zake kwa kusema: “Mungu anajua ya kwamba siku
mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Shetani aliamua
kuhalalisha uongo wake kwa kumwambia Hawa kuwa Mungu alikuwa amewazuia wasile
matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya kwa sababu alikuwa hataki wawe kama
yeye [Mungu] wakijua mema na mabaya. Fahari ya nje ndiyo aliyokuwa anataka
kuwaonyesha pale bustanini ili aharibu uhusiano wao na Mungu.
Kwa kujua mema na
mabaya mtu angekuwa kama Mungu, japokuwa asingefikia kiwango cha kuitwa Mungu,
lakini angefanikiwa kuwa kiumbe anayejitegemea na mwenye uwezo wa kufanya
maamuzi yake mwenyewe. Hatua hii ilikuwa na madhara makubwa sana kwa sababu
badala ya mtu kuwa mwakilishi wa Mungu katika sura na mfano wa Mungu sasa
alitaka awe na uwezo wake yeye mwenyewe. Hii ilimuondolea uwezo wa kumpinga
shetani tangu hapo hadi pale Yesu alipokuja kumnyang’anya shetani na
kuturudishia tena uwezo huo kwa gharama kubwa ya damu yake.
Tamaa ya ujuzi wa
mema na mabaya na kutaka kuwa kama Mungu ndivyo vilivyomwondolea mtu uwezo wake
wa ki-Mungu aliokuwa amepewa na muumba wake. Ni kweli angepata kujua mema na
mabaya lakini asingepata nguvu ya kuzuia mabaya ili apate mema tu. Na matokeo
yake alikosa mema akawa mtumwa wa mabaya. Katika Yohana 8:34 Yesu alisema hivi:
“…Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa
dhambi.” Dhambi ya kuasi agizo la Mungu haikuwa na nguvu ya kumpa mtu uwezo wa
kuwa huru tena, bali ilimweka awe mtumwa wa hiyo dhambi daima.
Vivyo hivyo watu wote wanaofanya
dhambi huwa watumwa wa hiyo dhambi. Hata kama mtu alifanya dhambi kwa kujaribu,
dhambi ile huwa haimwachi awe huru tena bali humfanya mtumwa ikimtumikisha
katika tamaa na uasi kila siku. Ni katika damu ya Yesu peke yake na kuamua
kuokoka ndipo mtu huwekwa huru tena mbali na dhambi wala dhambi haina nguvu
tena kwao walio katika Kristo Yesu, kwa kuwa “Mwana akiwaweka huru, mtakuwa
huru kweli kweli (Yohana 8:36).”
Mtego wa shetani ulikuwa umesukwa
kiwerevu sana maana msitari wa 6 unasema
“Mwanamke alipoona ya
kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza
macho, nao ni mti wa kutamanika kwa
maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye
akala.” (msisitizo umeongezwa)
Shetani alichagua
kumdanganya mtu kupitia mti ambao ulikuwa una mvuto kwa mambo ya mwili. Ulikuwa
ni mti wa “kupendeza” na “wa kutamanika.” Lakini shetani anasema kuwa mti ule
ulikuwa pia unavutia kwa ajili ya kuwa kama Mungu. 1 Yohana 2:15-16 inasema:
“Msiipende dunia,
wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo
ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani,
tamaa ya mwili, na tamaa ya macho,
na kiburi cha uzima, havitokani na
Baba, bali vyatokana na dunia.”
(msisitizo umeongezwa)
Yohana anasema tamaa
ya mwili, tamaa ya macho, na kiburi cha uzima havitokani na Mungu bali na
dunia. Ndicho kilichowapata Adamu na Hawa, maana waliingiwa na tamaa ya macho,
tamaa ya mwili, na tamaa ya utukufu wa kutaka kuwa kama Mungu (kiburi cha
uzima) ambavyo vyote havikutoka kwa Mungu bali vilitoka katika dunia. Mvuto wa
haya mambo ya dunia ulimshinda mwanamke kiasi ambacho aliamua kufanya tofauti
na Mungu alivyoagiza; alitwaa matunda aliyozuiliwa akala, kisha akampa na
mumewe ambaye naye kwa kusahau nafasi yake kama kichwa cha mkewe alikubali
mkewe amuongoze, naye akaingia katika kuasi.
Shetani hutumia vitu
vya dunia ambavyo vina mvuto kwa macho na kutamanika kwa mwili ili apate nafasi
ya kumwingiza mtu dhambini. Mara nyingi amekuwa akimtumia mwanamke kama mlango
wa kupitia, na hii inatokana na wanawake wengi kupenda vitu vya dunia kuliko
vitu vya Mungu. Ndio maana utaona mambo mengi yenye mvuto katika dunia hii,
kama mavazi, vito vya thamani n.k. huwahusu wanawake. Tamaa ya vitu vya dunia
ilimwingiza Hawa katika kuasi naye akamwingiza mumewe katika dhambi. Ni vizuri
kwa wanawake kuwa makini sana na vitu vya dunia hii hata kama vina mvuto mkubwa
kiasi gani, na ni vizuri pia kwa wanaume kuchunguza kwanza uamuzi unaofanywa na
wake zao kabla hawajaamua kuwafuata. Maana uzembe wa Adamu, kama kichwa cha
mkewe, ulimwingiza katika uasi wa daima.
Matokeo ya uasi
Baada ya kuasi agizo
la Mungu, sasa mtu alikuwa mwenye dhambi katika hali ya uasi. Msitari wa 7
unatuambia kuwa sasa macho yake yalifumbuliwa akajua kuwa yu uchi. Elimu ya
ujuzi wa mema na mabaya aliyoipata kutoka katika ule mti sasa ilimwelekeza
kwamba kuwa uchi ni jambo baya hivyo akatafuta namna ya kusitiri ubaya huo.
Kutokana na ukweli kuwa ujuzi wa mema na mabaya walioupata haukuwa na nguvu za
kuwasaidia kuyashinda mabaya ili wapate mema, sasa mtu alijikuta akitafuta njia
zake mwenyewe za kuuficha ubaya wake ambao hata yeye alikuwa akiuona.
Ndivyo ilivyo siku
zote; mtu yeyote akianguka dhambini huwa anafahamu kuwa nimefanya dhambi ila
kwa sababu ya utumwa wa ile dhambi huwa hakumbuki kumtafuta muumba wake bali huwa
kwanza anatafuta namna ya kuuficha uovu wake ili usijulikane. Bahati mbaya kwa
Adamu na mkewe ilikuwa ni kuwa hapakuwa na mahali pa kujificha mbali ambapo
Mungu asingewaona. Uovu wao uliwapelekea kujificha sasa kwa kutumia majani ya
miti ya bustani ile ile ambayo Mungu aliwapa iwe baraka yao. Sasa waligueza
baraka ya Mungu kuwa laana ya kuficha uovu wao. Bahati mbaya sana ni kuwa hata
njia yao ya kuficha uovu wao haikuwa ya uhakika, maana walishona majani ya
mtini ili kutengeneza nguo. Kwa wale wanaoufahamu mtini wanajua hakika kuwa
majani ya mtini ni membamba na laini sana kiasi kwamba ni rahisi sana
kuharibika. Hii ni kweli kabisa kuwa nguo walizojifanyia ili kuficha uchi wao
hazikuweza kuwasaidia maana utakuta kwenye msitari wa 10 Adamu akikiri kuwa “mimi
ni uchi.”
Msitari wa 8
unatuambia jambo jingine alilofanya Adamu na mkewe baada ya uasi wao;
walimsikia Mungu akitembea bustanini kisha wakaamua kujificha ili Mungu
asiwaone. Walidhani kuwa wanaweza kumficha Mungu uovu walioufanya, kama ambavyo
watu wengi wakishafanya dhambi badala ya kurudi kwa Mungu kwa toba, wanaamua
kwenda kujificha wakidhani kuwa Mungu hawaoni. Biblia inasema hivi:
“Ole wao wanaojitahidi kumficha
Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye?
Nani atujuaye?” (msisitizo umeongezwa) [Isaya 29:15]
Adamu na mkewe walifikiri
wanaweza kumficha Mungu matendo yao ya giza; yawezekana walisema mioyoni mwao
kuwa “tujifiche maana Mungu hakutuona kuwa tu uchi.” Lakini kilichowapata ni
kile kilichonenwa na Nabii Ezekieli kuwa:
“Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misunobari haikuwa
kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo wote uliofanana naye kwa
uzuri. Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea
wivu. Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa
kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake; mimi
nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake.” [Ezekieli 31:8-11] (msisitizo umeongezwa).
Licha ya Adamu
kutafuta kujificha kwenye miti ya bustani ya Mungu, Biblia inasema miti ile ya
bustani haikuweza kumficha. Ezekieli anasema kuwa kabla ya uasi wake, Adamu
alikuwa mzuri mno kiasi kwamba miti yote ya Edeni ilimwonea wivu, lakini kwa
kuwa moyo wake uliinuka kwa urefu na kutaka kuwa kama Mungu, basi Mungu
alimfukuza kwa sababu ya uovu wake (Mwanzo 3:24). Maneno haya
yanatufundisha kuwa hakuna namna ambavyo unaweza kuuficha uovu wako mbali na
Mungu. Hata vitu utakavyotaka vikufiche navyo havitakubali uovu wako bali
vitakufichua.
Mungu kumtafuta mtu wake
Msitari wa 9 wa sura
hii ya 3 unamuonesha Mungu akiwa katika harakati za kumtafuta mtu wake
aliyeanguka dhambini na kuamua kuenda kujificha ili muumba wake asimuone.
Dhambi ya Adamu ilimnyima ujasiri wa kusogea tena uweponi mwa Mungu na kusimama
mbele za muumba wake. Katika hali hiyo Mungu angeweza kumwacha tu Adamu na
mkewe katika dhambi yao au hata kuwaangamiza kabisa. Lakini Mungu
anaudhihirisha upendo wake na wingi wa rehema zake kwa mtu wake; anaenda
kumtafuta huko alikojificha. Kwa sababu ya kujificha kwake Adamu alipoteza
nafasi aliyokuwa amewekwa na Mungu hivyo tunaona sasa swali la kwanza la kitabu
cha Agano la Kale ikiwa ni Mungu akimtafuta mtu wake. Swali la kwanza kabisa la
Biblia ni Mungu akisema “Uko wapi?”
Tangu kuulizwa kwa
hili swali la “uko wapi,” kitabu chote cha Agano la Kale kinajaribu kujibu hili
swali bila mafanikio. Adamu alijaribu kujibu kwa kujitetea lakini katika
harakati za kujitetea kwake akajikuta akiufunua uovu wake; akasema “mimi ni
uchi.” Vitabu vyote vya agano la kale vinaonesha maisha ya mtu akijaribu
kujitetea juu ya mahali alipo lakini hakufanikiwa kumgeukia Mungu na kutembea
nae sawasawa. Tunapofika mwisho wa Agano la Kale tunakuta kitabu cha Malaki
kikionesha jinsi mtu alivyoshindwa kujirudisha kwenye nafasi aliyokuwa amepewa
na Mungu, na kitabu hiki kinaishia na kuonesha jinsi Mungu alivyokuwa
amechoshwa na kujificha kwa mtu wake. Maneno ya mwisho ya Agano la Kale ni
Mungu akisema “… nisije nikaipiga dunia kwa laana.” [Malaki 4:6] Utaratibu wa Mungu kumtafuta mtu wake kwenye Agano la Kale
haukuweza kumtengeneza mtu arudi kwenye nafasi aliyoumbiwa, kila mara mtu
alirudi kwenye uasi na dhambi, hivyo Mungu anamaliza Agano la Kale kwa kutaja
laana.
Tunaanza kitabu cha
Agano Jipya kwa kukuta jambo la tofauti sana. Swali la kwanza linalojitokeza
kwenye Agano Jipya ni watu wakimtafuta Mungu badala ya Mungu kuwatafuta watu
kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale. Utakuta swali la kwanza la Agano Jipya
likisema “Yuko wapi yeye aliyezaliwa
Mfalme wa Wayahudi?” (msisitizo umeongezwa)
Wakati swali la
kwanza la Agano la Kale alikuwa ni Mungu akimtafuta mtu wake kwa kusema “Uko wapi?” swali la kwanza la Agano
Jipya ni watu wakimtafuta Mungu kwa kusema “Yuko wapi?” Kitabu chote cha Agano Jipya kinajaribu kujibu swali
hili la watu kusema “yuko wapi… mfalme wa wayahudi”, na tunakuta mwisho wa
kitabu hiki cha Agano Jipya Yesu akijifunua kwa watu wake na kuwakaribisha
kwake. Utakuta Ufunuo 22:13 Yesu akisema “Mimi
ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.” Halafu katika Ufunuo 22:20 anamalizia kwa kusema “Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana
Yesu”
Hii inatufunulia kuwa
baada ya mtu kumwasi Mungu mpango wa wokovu wake haukuwa ndani ya mwingine
yeyote isipokuwa katika Yesu Kristo. Pia tunagundua kuwa suala la kuokoka na
kuachana na dhambi limo katika uamuzi wa mtu mwenyewe anapoamua kumtafuta na
kumrudia muumba wake. Mungu aliamua kumtafuta Adamu wakati ambao Adamu alikuwa
hajaamua kumrudia muumba wake, na matokeo yake tunaona maisha yote ya Agano la
Kale yakiishia na laana. Lakini Agano Jipya linatufunulia kuwa pindi mtu
anapoamua kumtafuta muumba wake aliko, basi Mungu huwa anajifunua kwake na
mwisho wake ni maisha ya ushindi. Ndugu msomaji wetu tunapenda ujue leo kuwa
suala la kubadili mwenendo wako na kumrudia Mungu liko mikononi mwako na Mungu
alishafanya sehemu yake kwa kumtoa mwana wake pekee ili kila amwaminiye
asipotee bali awe na uzima wa milele (Yohana 3:16). Kama bado unaishi
katika dhambi chukua uamuzi leo wa kumpa Yesu maisha yako ili uanze kuishi tena
kwenye bustani ambayo Mungu alikuwekea.
Lawama za mtu kwa Mungu wake
Baada ya Adamu kukiri
kuwa yu uchi, Mungu, kwenye msitari wa 11 anamuuliza Adamu kuwa umejuaje kwamba
u uchi, je umekula matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Katika kujibu swali
hili Adamu anamrushia Mungu lawama juu ya kosa alilofanya; anasema:
“Huyo mwanamke
uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.”
Ni kama vile Adamu
alikuwa anamwambia Mungu kuwa ‘kama usingenipa huyo mwanamke awe pamoja nami
basi haya yote yasingetokea.’ Mungu hakumuuliza Hawa moja kwa moja swali hili
japokuwa alijua kuwa Hawa ndiye aliyekuwa wa kwanza kula matunda ya mti
waliokatazwa. Hii ilitokana na ukweli kwamba Mungu alikuwa amemweka Adamu ndiye
awe kichwa cha mkewe hivyo alitakiwa ndiye awe wa kwanza kuwajibishwa kwa kila
litakalotendeka kati yao. Adamu akijua hilo, akaamua amrushie Hawa lawama
lakini kwa upande mwingine akamlaumu na Mungu kwa kumpa huyo mke awe pamoja
nae.
Katika kisa hiki siri
ya uasi wa mtu kwa mara nyingine inafichuliwa. Mtu akifanya dhambi au kosa
fulani, basi kama hatakana kosa hilo au dhambi hiyo, atatafuta mtu wa kumtupia
lawama na ikiwezekana hata kumlaumu Mungu. Tumesikia mara nyingi watu wakifanya
dhambi na kusingizia kuwa shetani alinipitia. Wengine wamekuwa wakisingizia
hali za maisha, na wengine hata kumlaumu Mungu wao kuwa kama angewatetea
wasingeanguka katika uasi huo. Hii haijaanza leo, ilianzia kwa Adamu ambaye
ndiye aliyefungua mlango wa dhambi kuingia.
Baada ya kutoka kwa
Adamu swali lililofuatia lilimhusu Hawa. Mungu alimuuliza ni nini hili
ulilofanya? Hawa hakuulizwa “uko wapi?” kama Adamu alivyoulizwa bali alihojiwa
kuhusu kosa alilokuwa amefanya. Swali la ‘uko wapi?’ lililenga kuonesha kuwa
Adamu alikuwa ametoka kwenye nafasi aliyokuwa amepewa na Mungu. Hawa hakuulizwa
swali hili kwa sababu Hawa alipofanywa na kuletwa kwa Adamu, usitawi wake ndani
ya ile bustani ulitegemea nafasi aliyokuwa nayo Adamu. Hawa hakupewa nafasi ya
peke yake mle bustanini bali alipelekwa kwa Adamu ili awe msaidizi. Msaidizi
hufanya kazi kulingana na nafasi mkuu wake aliyonayo. Nafasi ya Hawa pale Edeni
ilitegemea sana Adamu yuko wapi. Kwa hiyo Mungu alipokuta Adamu yuko nje ya
nafasi haikumsumbua kuuliza Hawa yuko wapi. Kama mme ndo kichwa cha familia
basi nafasi ya mke hutegemea sana mme wake yuko wapi. Ndiyo maana wanawake
wengi wanaoolewa na wanaume walevi au wapenda anasa nao hujikuta wamekuwa hivyo
kwa sababu ya nafasi ya waume zao.
Hawa alipoulizwa ‘ni
nini hili ulilolifanya?’ jibu lake nae halikutofautiana sana na lile la mume
wake; naye aligeuzia lawama kwa nyoka kuwa ndiye aliyenidanganya. Ni kweli kuwa
nyoka alikuwa amemdanganya lakini swali la Mungu halikuuliza kuwa ni nani
aliyekwambia kula, Mungu aliuliza ni nini hili ulilolifanya? Lakini Hawa kwa
kutaka kukwepa kuwajibishwa, akamgeuzia nyoka lawama. Cha ajabu ni kuwa nyoka
hakuulizwa swali lolote na Mungu kama ilivyokuwa kwa wengine, alipogeukiwa yeye
ilikuwa ni kutangaziwa adhabu tu.
Adhabu ya Mungu juu ya uasi
Maneno ya Mungu
katika msitari wa 14 yanatoa adhabu kwa kizazi chote cha nyoka; huyu alikuwa
nyoka wa kawaida aliyeruhusu kutumiwa na shetani. Kwa kuwa yeye ndiye alikuwa
chanzo cha uovu ule kupita, nyoka anashusha hadhi yake na kufanywa awe chini ya
wanyama wote na chini ya hayawani wote wa mwitu. Anapewa adhabu ya kula
mavumbi, mavumbi ambayo katika hayo mtu alifanywa. Kwa namna fulani Mungu
alikuwa anampa nyoka adhabu ambayo ilitakiwa imwangukie mtu; maana mtu ni
mavumbi na kwa hivyo suala la nyoka kupewa adhabu ya kula mavumbi linamaanisha
alikuwa anachukua adhabu fulani ya mtu ambayo angestahili aipate Adamu.
Adhabu anayopewa
nyoka kwenye msitari wa 15 inaashiria kuwa haikumuhusu nyoka wa kawaida tena
ila ilikuwa juu ya Ibilisi shetani ambaye alikuwa amemtumia nyoka kuleta
uharibifu ule. Mungu hakutaka kumwacha shetani bila adhabu kwa kosa la
kumkosesha mtu wake. Adhabu anayotoa kwa shetani ni kuweka uadui kati yake na
mwanamke, na kati ya uzao wake na uzao wa mwanamke. Inahitaji kufikiri vizuri
ili kugundua kitu ambacho Mungu alikuwa anafanya hapa. Uzao wa shetani
unaotajwa hapa ni roho zote za uasi zenye asili yake, na hizi zote zimewekwa
katika uadui mkubwa na uzao wa mwanamke.
Kwa kutaja kuwa uzao
wa mwanamke utamponda shetani kichwa, ni wazi kuwa Mungu alikuwa anatujulisha
kuwa mkombozi atakuja siku moja kutuokoa kutoka katika uangamivu wa shetani
naye atamwangamiza shetani kabisa, yaani “atamponda kichwa.” Mungu alitangulia
kutaja habari za kuja kwa Yesu tangu mwanzo mara tu dhambi ilipofanikiwa
kuingia ulimwenguni. Kazi ya Yesu ilikuwa ni kuja kumponda kichwa shetani,
lakini kabla ya Yesu kumponda kichwa shetani, shetani alipewa kumgonga
kisigino. Yesu mwenyewe alinena kwa habari hii akasema: “Mimi sitasema nanyi
maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu [Yohana 14:30].” Shetani si kitu
mbele za Yesu ndivyo Bwana wetu alivyosema.
Kuna mambo manne
yanayotujulisha kuwa uzao wa mwanamke uliotakiwa kumponda kichwa shetani
alikuwa si mwingine bali Yesu peke yake.
1.
Katika suala la uumbaji wote, tangu mtu mpaka kwa viumbe wengine
wote, uzao hufuata mwanaume na si mwanamke. Lakini hapa Mungu anazungumzia kitu
ambacho kilikuwa kinyume na utaratibu wa kawaida, kuleta uzao kupitia mwanamke.
Ni wazi kabisa kuwa hata kuzaliwa kwa Yesu hakukufuata utaratibu wa kawaida,
maaana bikira asiyemjua mume alipata mimba akazaa mwana.
2.
Tangazo la kupatikana kwa uzao wa mwanamke lilitolewa kabla ya
uzao wa mwanamume kuwepo. Adamu alikuwa sio wa uzao wa mwanamume kwa maana yeye
alikuwa moja katika vitu vya uzao wa mbingu na nchi. Uzao wa mwanaume ulianzia
kwa Kaini na bahati mbaya ulikuwa uzao uliojaa uovu kwa maana Kaini naye
alifanya dhambi ya kuua. Mungu alitangulia kuutaja huu uzao wa mwanamke kwa
sababu haukutakiwa kuhesabiwa kama uzao wa kibinadamu, Yesu alikuja kama Adamu
wa pili japokuwa yeye alijitaja kama mwana wa Adamu. Yesu alikuja katika uzao
wa tofauti ili awaongoze watu katika haki ya Mungu tofauti na uzao wa mwanaume
ambao uliwaongoza watu katika uasi.
3.
Uadui kati ya uzao wa nyoka na uzao wa mwanamke ulitakiwa kuisha
kwa ushindi wa uzao wa mwanamke, yeye angemponda kichwa nyoka. Kichwa ndiyo
sehemu yenye werevu na utashi wote. Suala la Yesu kumponda kichwa shetani
lilimaanisha kukomesha biashara ya shetani kuwadanganya watu na kuwapoteza. Ni
Yesu peke yake aliyeweza kufanya hili, maana uzao wote wa mwanaume ulishindwa kumponda
shetani, hata Musa alifika mahali akakosea. Yesu ndiye Bwana wa vita dhidi ya
shetani na hila zake, yeye anajua namna ya kumponda kichwa.
4.
Mwisho ni kwamba Mungu alitanguliza kuonesha kuwa ushindi huo
ulikuwa na gharama na maumivu. Mtu aliyewahi kugongwa na nyoka ataelewa vizuri
hiki tunachosema hapa, lakini yatosha tu ujue kuwa maumivu ya kugongwa na nyoka
ni makali sana na yaweza kusababisha kifo. Katika kutembea, kisigino huwa ndiyo
sehemu ya kwanza kabisa ya mguu wako kukanyaga chini. Nyoka alitakiwa kumgonga
kisigino yule mzao wa mwanamke. Ni kweli kuwa ni pale tu Yesu alipokanyaga
duniani ndipo alipopata maumivu. Hakuwahi kupata maumivu akiwa mbinguni, lakini
alipokanyaga duniani kama kisigino kitanguliavyo kukanyaga chini ndipo
alipopata maumivu, tena maumivu ya mijeledi na kupigiliwa misumari. Ilikuwa ni
gharama aliyotakiwa kulipa Bwana wetu ili apate ushindi wa kumponda nyoka
kichwa. Ashukuriwe Yesu kwa kuwa alilipa gharama na ushindi tumeupata, sasa
hatuko tena chini ya udanganyifu wa shetani.
Baada ya kutoa adhabu
kwa nyoka, ilikuwa sasa ni zamu ya mwanamke. Adhabu yake ilikuwa na pande
mbili; moja, kuzaa kwake kungekuwa kwa uchungu siku zote; na pili, aliwekwa
chini ya mumewe kwa kila jambo. Siku hizi kumekuwa na jitihada za kila namna
kutaka kupingana na hiki Mungu alichoagiza kama adhabu. Kumekuwa na harakati
zinazoitwa harakati za ukombozi wa mwanamke. Tumesikia kampeni za kutaka haki
sawa kati ya mwanamke na mwanaume na kutaka mwanamke alingane na mwanaume kwa
kila kitu. Hii imepelekea kuharibika kwa maadili katika jamii na msingi wa
jamii (social order) umevurugika. Suala lililoamuriwa na Mungu sasa mwanadamu
anataka ashindane nalo ili ikiwezekana alibadilishe; hakika sisi hatutaki kuwa
sehemu ya upinzani huo juu ya Mungu.
Zamu ya Adamu ilipofika
adhabu yake inatoa fundisho la ajabu kidogo; alikuwa amesikiliza sauti ya mkewe
na kuacha agizo la Mungu sasa alitakiwa kuadhibiwa kwa hilo. Mtu yeyote
anayeacha agizo la Mungu na kufuata sauti za watu lazima awe na adhabu kwa
Mungu. Ardhi ililaaniwa kwa ajili ya Adamu. Ni wazi kuwa adhabu ya laana
ilitakiwa imwangukie Adamu, lakini kwa jinsi Mungu alivyompenda mtu wake
aliipindisha laana ile na kuielekeza kwenye ardhi. Sasa ardhi ilipewa kiburi
juu ya mtu; haikutakiwa imzalie mtu bure kama ilivyokuwa mwanzo. Sasa ilimpasa
Adamu ailime ardhi tena kwa jasho na kwa uchungu ndipo apate mazao yake. Ardhi
hii pia ilipewa kumpokea mtu katika kifo chake, maana sasa neno la Mungu
lilikuwa likitimizwa ya kwamba ‘siku utakapokula mtunda ya mti huo hakika utakufa.’
Kifo sasa lilikuwa ni jambo ambalo Adamu asingeweza kuliepuka. Ni katika hatua
hii Adamu anaamua kumwita mkewe jina la Hawa.
Fumbo la kuvikwa ngozi
Adamu na mkewe
walijaribu kuuficha uchi wao kwa nguo zilizoshonwa kutokana na majani ya mtini.
Mungu alikuwa ameahidi kuja kwa uzao wa mwanamke ambaye angemponda nyoka kichwa
na kukomesha kabisa hila za shetani juu ya mtu. Ujio huu wa mwokozi, Mungu
alianza kuudhihirisha tangu katika kitabu cha Mwanzo na jinsi ambavyo wokovu
huo ungetokea. Mungu aliamua kumchinja mojawapo ya wanyama waliokuwa bustanini
ili awashonee nguo ya ngozi watu wake. Uovu wa Adamu na mkewe haukuweza
kufichwa kwa majani isipokuwa kwanza kwa kumwaga damu.
Hakuna namna ambavyo
ngozi hii ingepatikana isipokuwa kwanza kuna kifo cha mnyama fulani. Ndivyo
alivyokuwa akitangulia kutujulisha Mungu kuwa hakuna namna dhambi zetu
zingeweza kufichwa isipokuwa kuna kifo cha mtu fulani na damu yake imwagike kwa
ajili ya dhambi hizo. Ni wazi kuwa mnyama aliyechinjwa na Mungu pale bustanini
ili akina Adamu wapate nguo hakuwa na hatia iliyomsitahili mauti yale. Lakini
kwa ajili ya upendo wa Mungu kwa mtu, damu isiyo na hatia ilimwagwa ili mtu
apate kuepukana na aibu yake.
Ni sura ya dhahiri
kabisa ambayo Mungu alikuwa anaionesha juu ya kile ambacho kingeleta ukombozi
wa dhambi. Yesu anaitwa mwana-kondoo wa kuchinjwa, alichinjwa na kuuawa kwa
ajili ya deni ambalo yeye hakuwa na hatia nalo wala hakushiriki kulifanya. Kama
vile mnyama yule wa bustanini ambavyo hakuwa na hatia bali alichinjwa kwa ajili
ya Adamu, ndivyo na Yesu naye alivyokufa na kutolewa awe sadaka kwa ajili ya
dhambi zetu.
Ukomo wa maisha ndani ya Edeni
Inasikitisha sana
kuona kwa jinsi gani mtu aliishi muda mfupi kwenye kusudi aliloitiwa na Mungu.
Sasa Adamu alikuwa amepata ujuzi wa mema na mabaya, lakini bila nguvu yoyote ya
kumwezesha kuyapata hayo mema bali akivutwa daima kuyendea mabaya. Mungu
akaliona hili, ya kuwa huyu mtu sasa anajua mema na mabaya lakini hana uwezo wa
kuyashinda mabaya na kuyapata mema. Katika hali hiyo Mungu akasema:
“…Basi, huyu mtu
amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha
mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo
Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo
alitwaliwa.” [Mwanzo 3:22-23]
Mti wa uzima ulikuwa
haujaondolewa katika bustani, na bado Adamu alikuwa na uwezo wa kuufikia
akatwaa matunda yake akala. Hii ingempa kuishi milele, lakini katika hali ya
uovu. Mungu hakutaka hilo litokee hivyo alimfukuza Adamu atoke pale bustanini
aende akailime ardhi ambayo kwa hiyo alitwaliwa. Na pia Adamu, asingeruhusiwa
kutwaa matunda ya mti wa uzima akayala kwani angefanya hivyo neno la Mungu
aliloahidi kama adhabu kwa Adamu la ‘hakika utakufa’ lisingetimia. Na kama
unavyojua moja kati ya sifa kuu za Mungu wetu ni kutogeuka, yeye siyo kigeugeu
na akisema amesema.
Msitari wa mwisho wa
sura hii una fundisho jingine kubwa sana. Mungu alipogundua kuwa Adamu angeweza
kula mtunda ya mti wa uzima akaishi milele kwenye uovu wake, hakuamua kuukata
mti wa uzima, bali alimfukuza Adamu atoke bustanini na akaweka makerubi
wailinde njia ya mti wa uzima. Swali la kujiuliza hapa ni kwa nini Mungu
asingeukata tu mti wa uzima, halafu akamwacha Adamu aendelee kuishi Edeni?
Kitabu cha Ufunuo
kinatueleza mambo kadhaa kuhusu mti wa uzima na sababu kwa nini Mungu
hakuukata. Ufunuo 2:7 inasema:
“Yeye aliye na sikio, na alisikie
neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda
ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya
Mungu.” (msisitizo umeongezwa)
Hapa kitabu cha Ufunuo
kinatuambia kuwa matunda ya mti wa uzima ulio katika bustani ya Mungu
yalitunzwa ili iwe zawadi kwa wale watakaoshinda ya ulimwengu. Bustani ya Edeni
ilikuwa ni mahali pema ambapo Mungu alitaka mtu afurahie ushirika wake na Mungu
hapo. Ikiwa Adamu angebaki katika ile bustani basi uhalisia wa ile bustani na
uthamani wake usingekuwepo tena. Ufunuo 22:2 inatueleza jambo lingine, inasema:
“…Na upande huu na upande huu wa
ule mto, ulikuwapo mti wa uzima,
uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.”
(msisitizo umeongezwa)
Hii ni habari ya mji mpya ambao
Mungu amewaandalia watu wake wale ambao wameushinda ulimwengu na tamaa zake.
Ndani ya huo mji Mungu anaurudisha tena mti wa uzima, ambao majani yake
huwaponya mataifa. Ni wazi kuwa huu mti wa uzima ni Yesu Kristo maana yeye
ndiye atuponyaye. Ikiwa Mungu angeukata mti wa uzima pale Edeni basi hiyo
ingekuwa ni ishara ya kuwa tusingekombolewa kutoka dhambini. Ashukuriwe Mungu
ambaye alituwekea uzima huu tangu kale.
Tumeona kuwa baada ya Adamu
kufukuzwa atoke pale bustanini, njia ya mti wa uzima ilizuiwa ilindwe na
makerubi pamoja na upanga wa moto. Hii haina maana kuwa hatuwezi kuufikia tena
huo mti wa uzima, maana kitabu cha Ufunuo 22:14 kinasema hivi:
“Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima,
na kuingia mjini kwa milango yake.” (msisitizo umeongezwa)
Maneno haya yanatufundisha kuwa
wale waliofua nguo zao, maana yake waliotakaswa kwa damu ya mwana-kondoo Yesu,
wanayo amri ya kuuendea huo mti wa uzima. Maana yake ni kuwa watakatifu wa
Yesu, na wale tunaoishi katika kweli ya Kristo tunayo amri ambayo kwa hiyo
tukiwa tunauendea huo mti wa uzima ule upanga wa moto unatupisha na yule kerubi
anatupigia saluti huku akituelekeza mti wa uzima ulipo. Ni raha iliyoje kupata
kujua fumbo hili kubwa, ya kuwa mti wa uzima ulitunzwa na unalindwa kwa ajili
yetu sisi tulio wake Kristo Yesu. Ndugu msomaji wetu kama hujampa Yesu maisha
yako, chukua uamuzi leo wa kuokoka na kuziacha dhambi zako ili uungane nasi
pamoja na Bwana arusi Yesu Kristo katika safari ya kuuendea mti wa uzima. Maana
tunapokula mtunda ya mti huo tunaishi milele. Yesu alisema:
“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho.” [Yohana 6:54]
Je, unataka kuwa na
uzima wa milele ndani yako? Je, unataka nawe ufufuliwe na Yesu siku ya mwisho?
Njia ni moja tu njoo uule mwili wa Yesu na kuinywa damu yake. Yaani OKOKA LEO.
Mungu akupe neema ya kumpokea Yesu leo.
No comments:
Post a Comment