Mwanzo Sura ya 2
Sura hii kimsingi inaweka msingi na mfumo wa maisha ya Mtu katika hali ya mwili baada ya ile hali ya kiroho iliyofanywa katika Mwanzo 1:27. Ni katika sura hii ndipo tunapoona Mungu akimfanya mtu katika umbo la mwili na kisha anampa majukumu na mwongozo wa namna ya kuishi katika nchi ambayo Mungu alikuwa amemwekea. Kuna mambo ya msingi sana kiroho yanayodhihirishwa katika sura hii na namna ambavyo yanagusa maisha yetu katika zamani hizi. Karibu tuyatafakari mambo haya pamoja msitari kwa msitari.
Ukamilifu wa Uumbaji
Msitari wa 1-3, kimsingi misitari hii ni mwendelezo wa sura ya kwanza; maana utagundua kuwa inamalizia habari iliyoelezwa katika sura ya kwanza juu ya kazi aliyokuwa akiifanya Mungu ya kuumba mbingu na nchi. Kwenye msitari wa 1 kuna neno moja limetumika na ni vema tukalitazama kwa undani kidogo; nalo ni neno “jeshi”. Msitari huu wa kwanza unasema kuwa mbingu na nchi zilimalizika na jeshi lake lote. Tafsiri za kiingereza zimetaja neno “jeshi” kama “host”, na neno la kiebrania lilotumika hapa ni “tsaba”. Maneno haya yote, la kiingereza na la kiebrania, yana maana ya “kundi kubwa la watu au vitu lililowekwa tayari kwa vita;” ndiyo maana tafsiri ya Kiswahili ikasema “jeshi.” Kwa hiyo tunachojifunza hapa ni kuwa mbingu na nchi zilipokamilika kulikuwa na kundi kubwa sana la vitu vilivyokuwa vimekamilishwa pamoja navyo. Ukichunguza vizuri maneno ya msitari huu na kusoma Biblia utagundua kuwa kulikuwa na jeshi mbinguni na jeshi duniani vilivyokuwa vimekamilishwa.
Lakini hatuoni Mungu akituambia kuhusu vitu vya mbinguni vilivyokuwa vimefanywa ili kutengeneza jeshi la mbinguni lakini tunaona msitari huu ukituambia kuwa kulikuwa na jeshi la mbingu na jeshi la nchi vilivyokuwa vimekamilika. Sura ya kwanza imeeleza vizuri juu ya vitu vya duniani (nchi) ambavyo Mungu aliviumba, na ambavyo kimantiki ndivyo vilivyounda jeshi la nchi. Lakini baada ya Mungu kuumba mbingu hatuoni Biblia ikituambia kuhusu vitu vingine ambavyo aliviweka huko mbinguni; msitari huu wa kwanza unatuambia tu kuwa kulikuwa na jeshi la mbingu ambalo pia lilikuwa limekamilika. Ngoja tuangalie mistari hii ya Biblia jinsi inavyosema:
Isaya 45:12 Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru.
Nehemia 9:6 Ezra
akasema, Wewe ndiwe Bwana, wewe peke yako; wewe
ulifanya mbingu, mbingu za mbingu, pamoja na jeshi lake lote, dunia na vyote
vilivyomo, bahari na vitu vyote vilivyomo, nawe unavihifadhi vitu hivi
vyote; na jeshi la mbinguni lakusujudu wewe. (msisitizo umeongezwa)
Katika kitabu cha Isaya Mungu anasema yeye ndiye aliyeamuru jeshi lote la duniani na la mbinguni, na Ezra katika kitabu cha Nehemia, anatujulisha kuwa Mungu alifanya mbingu pamoja na jeshi lake lote. Kwa hiyo ijapokuwa sura ya kwanza ya kitabu cha Mwanzo haituoneshi ni vitu gani vilivyofanywa kule mbinguni, bado Biblia inatuthibitishia uhalisi wa Mwanzo 2:1 kuwa kulikuwa na jeshi la mbinguni ambalo pia lilikuwa limekamilishwa. Unapoendelea kusoma Biblia utakuta ikitaja Malaika, Maserafi na Makerubi, Wazee Ishirini na Nne, na Wenye Uhai Wanne kuwa ni viumbe walioko mbinguni. Ukijiuliza kuwa viumbe hawa walitoka wapi?; hapo ndipo unapogundua ukweli wa Mwanzo 2:1 kuwa kulikuwa na jeshi la vitu vya mbinguni ambavyo pia Mungu alivifanya pale alipoumba mbingu na nchi. Utaona Mtume Paulo akituambaia kuwa kuna vitu vya mbinguni ambavyo pia vinapiga goti na kusujudu jina la Yesu linapotajwa.
Wafilipi 2:10 inasema: “ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi.” Kwa hiyo tunaelewa sasa kuwa kuna vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi. Kumbe ni wazi sasa kuwa Jeshi la mbinguni na la duniani vilifanywa vyote katika mwanzo sura ya kwanza, hapo Mungu alipoziumba mbingu na nchi.
Jambo jingine linalojitokeza hapa ni “vitu vya chini ya nchi.” Biblia haituambii kuwa kulikuwa na uumbaji wa vitu vya chini ya nchi. Tunapozungumza chini ya nchi haina maana ya bahari, maana bahari ilifanywa kama moja ya vitu katika nchi. Sasa Paulo anaposema kuna vitu vya chini ya nchi ni vema tukajua vitu hivi ni vitu gani, maana si Mwanzo 1 wala 2 ambayo inataja kusuhusu kuumbwa kwa vitu vya chini ya nchi. Kwa sababu Mwanzo 1:1 inasema “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Wakati Mwanzo 2:1 inasema “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote.” Kwa hiyo hakuna mahali tunapokuta uumbaji wa vitu vya chini ya nchi. Sasa swali ni: “Hivi vitu vilivyoko chini ya nchi vilitoka wapi na ni vitu gani?” maana hatuoni vikitajwa katika eneo lo lote la uumbaji.
2 Petro 2:4 inasema: “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu.” Biblia inasema wapo malaika waliokosa, ambao kutokana na kosa lao Mungu aliwatupa shimoni, akawaweka katika vifungo vya giza hata ije hukumu yao. Ufunuo 12:7-9 inasema:
Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
Oooh kumbe aliyetupwa chini alikuwa joka, aitwaye Ibilisi na Shetani, pamoja na malaika walioasi pamoja naye. Kumbe vile vitu vilivyoko chini ya nchi asili yake ni vitu vilivyoasi mbinguni. Ilikuwa ni moja ya sehemu katika jeshi la mbinguni ambayo ilifanywa na Mungu katika Mwanzo 1:1, ila ni kuasi kwao ndiko kulikosababisha kutupwa kwao chini ya nchi. Baada ya mahali pao pa mbinguni kuondolewa na wao kukosa sehemu katika jeshi la mbinguni, Mungu hakutaka kumweka Shetani na malaika walioasi katika nchi pamoja na mtu wake aliyemfanya hivyo alimtupa chini ya nchi, ambako kwa jina la kibiblia panaitwa kuzimu ili afungwe huko hata hukumu yao ije.
Siku ya Saba na Sabato
Msitari wa pili unatuambia juu ya siku ya saba na kile Mungu alichofanya katika siku hiyo; Biblia inatuambia kuwa siku hiyo Mungu alistarehe, akaibariki. Mungu alipoitazama kazi yote aliyoifanya aliona kuwa imekamilika nayo ni njema, kama jinsi Mwanzo 2:1 inavyosema. Mungu alipojiwekea siku ya saba iwe siku ya kustarehe na kupumzika, alitoa pia maelekezo kwa watu waitii siku hiyo na kustarehe (Kutoka 20:9-10; 23:12; 31:15; 34:21; 35:2; Walawi 23:3; Kumbukumbu la Torati 5:13-14).
Siku ya saba inatajwa kama sabato kwa mara ya kwanza katika kitabu cha Kutoka 16:23. Hatuoni adhimisho la siku hii katika vizazi vyote vinavyojitokeza katika kitabu cha Mwanzo, bali tunalikuta adhimisho hili pindi Mungu anapoanza kuwawekea wana wa Israeli sheria na torati. Sabato iliwekwa kwa torati kama utaratibu wa ibada kati ya waisraeli na Mungu wao, na iliendelea kuwa hivyo hata leo.
Lakini ni vema tukajua kuwa Sabato haikuwekwa iwe ishara ya kanisa bali iwe ishara ya watu kumkumbuka Muumba wao na kumwabudu. Wenzetu Waadventista Wasabato wamechukulia suala la sabato kama kanisa na siku ya saba kama ishara ya ibada. Hii si sahihi; Kumbukumbu la Torati 5:15 inatufundisha kusudi la sabato kuwepo na ina maana gani kwetu sisi. Inasema:
Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.
Mungu aliamuru watu waishike siku ya saba kama sabato ikiwa ni ishara ya kukumbuka kwao kuwa walikuwa watumwa na Mungu akawatoa katika utumwa ule kwa mkono ulionyoshwa na wenye nguvu. Iliwekwa iwe ishara ya ukombozi wao; haikuwekwa iwe ndilo kanisa lao au ndio iwe ibada yao. Ndio maana walipomwasi Mungu hata kama waliendelea kushika sabato Mungu aliwapiga.
Hosea 2:11 Mungu anazungumza juu ya watu waliomkosea anasema: “Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.” Tena katika Amos 5:21 anasema: “Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini.”
Tumekuwekea hii mistari ili kujaribu kukuonesha kuwa suala la sabato halina uhusiano na kanisa fulani au dhehebu fulani. Wenzetu waadventista wamekuwa wakitusema vibaya sisi tulioifanya Jumapili kuwa siku yetu ya ibada. Msingi wao umejengwa kwenye imani kuwa siku ya saba ambayo Mungu alipumzika ilikuwa ni siku ya jumamosi. Wanasahau kuwa sabato wanayoiadhimisha si kwa mujibu wa siku ya saba ambayo Mungu alipumzika bali wanafuata siku ya saba ambayo waisraeli waliiadhimisha pale walipotolewa utumwani na Mungu akaanzisha sabato yao pale alipowashushia Mana wale (Kutoka 16:23).
Si kwamba sisi tulioifanya Jumapili kuwa siku ya sabato kwetu tunakosea au kwamba waliofanya Jumamosi kuwa sabato kwao ndo wako sahihi, ila Biblia inatuelekeza kuwa siku za kuabudu hazitatuhukumu mbele za Mungu. Mtume Paulo anasema hivi:
Warumi 14:5 “Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.” Kisha katika Wakolosai 2:16-17 anasema: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.”(msistizo umeongezwa).
Sasa ni kwa nini sisi tuhukumiane katika sabato, wakati mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo? Biblia iko wazi kabisa katika jambo hili; Yesu mwenyewe alisema Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato (Marko 2:27) (msisitizo umeongezwa). Ndiyo maana sasa Waebrania 4:9 inasema raha ya sabato ipo kwa ajili ya watu wa Mungu. Na ndiyo maana Yesu anajitangaza kuwa ndiye Bwana wa sabato (Mathayo 12:8; Marko 2:28; Luka 6:5); hivyo aliye na Yesu ndani yake anayo sabato ndani yake na wala si kanisani kwake. Chagua mwenyewe kipi bora, uwe na sabato kanisani kwako kila Jumamosi au uwe na Bwana wa sabato uwe nayo sabato kila siku ndani yako. Kwa hiyo ni vizuri kuwa nayo siku moja ya kupumzika katika siku saba kwa ajili ya Bwana lakini siku hiyo haijafungwa katika kalenda za kibinadamu.
VIZAZI
Maneno ya msitari wa 4 yanahitaji kutazamwa kwa umakini zaidi kwa kuwa yanaweka fundisho la tofauti na ile mistari inayotangulia. Msitari huu unaanza kwa kusema “hivyo ndivyo vizazi vya ….” Maneno kama haya yamejitokeza mara kumi katika kitabu hiki cha Mwanzo. Mwanzo sura ya kwanza hadi sura ya pili msitari wa tatu inatufunulia mambo yaliyofanyika hapo mwanzo kabla ya vizazi kuwepo, lakini kuanzia msitari wa nne wa sura ya pili Biblia inaanza kwa kutueleza mambo yaliyofanyika katika vizazi mbalimbali vinavyojitokeza katika kitabu hiki. Labda kwa ajili ya kurahisisha fundisho hili wacha tuvitaje vizazi vyote vya kitabu cha Mwanzo.
Mwanzo 1:1 - Mwanzo 2:3, twaweza kuiita kama – Mwanzo
Mwanzo 2:4 – Mwanzo 4:26, vizazi
vya mbingu na nchi
Mwanzo 5:1 – Mwanzo 6:8, vizazi
vya Adamu
Mwanzo 6:9 – Mwanzo 9:29, vizazi
vya Nuhu
Mwanzo 10:1 – Mwanzo 11:9, vizazi
vya wana wa Nuhu
Mwanzo 11:10 – Mwanzo 11:26,
vizazi vya Shemu
Mwanzo 11:27 – Mwanzo 25:12,
vizazi vya Tera
Mwanzo 25:13 – Mwanzo 25:18,
vizazi vya Ishmaeli
Mwanzo 25:19 – Mwanzo 35:29,
vizazi vya Isaka
Mwanzo 36:1 – Mwanzo 37:1, vizazi
vya Esau
Mwanzo 37:2 – Mwanzo 50:26,
vizazi vya Yakobo
Kwa hiyo kama kitabu hiki cha Mwanzo kingepangiliwa kwa kufuata vizazi vilivyotajwa katika kitabu hiki, basi kingekuwa na sura kumi na moja kama tulivyozitaja hapo juu. Kama tutakavyoona baadae, kila kizazi katika vizazi hivi vyote kilipita katika nyakati zake na hakifanani na kizazi kingine. Kila kizazi kilitembea na Mungu kwa jinsi yake na uhusiano kati ya Mungu na kila kimoja cha vizazi hivi haukufanana. Endelea nasi katika tafakari hii tupate kuona mambo haya jinsi yalivyo.
Vizazi vya Mbingu na Nchi
Neno vizazi linalojitokeza katika msitari wa 4 hutumika kumaanisha chanzo au msingi wa uzao fulani. Katika msitari huu Biblia inatufunulia kuwa vitu vinavyozungumzwa katika Mwanzo 2:4 hadi Mwanzo 4:26 chanzo chake au msingi wake ulikuwa katika mbingu na nchi. Kwa hiyo tunapokuta huko mbele Biblia ikitaja vizazi vya Adamu au vizazi vya Esau n.k. inamaanisha inazungumzia watu ambao msingi wao ulikuwa katika hao waliotajwa. Sasa hapa Biblia inaanza kutuonesha vitu ambavyo havikuwa na asili yake sehemu nyingine yoyote isipokuwa katika mbingu na nchi ambazo nazo chanzo chake ni Mungu mwenyewe.
Katika msitari huu wa 4 pia tunakuta mabadiliko fulani yakijitokeza juu ya jina la Mungu. Kwenye sura ya kwanza yote tunaona Biblia ikimtaja Mungu kama Mungu tu, ila hapa tunaona jina jipya Mungu akiitwa “Bwana Mungu.” Jina hili kwa kiebrania linatajwa kama “Yhovah Elohiym” ambalo ni ‘Jehova Elohim’ likimaanisha – Mungu wa pekee, asiyebadilika, mwaminifu kwa agano lake (self-exsiting, unvarying God). Madhumuni ya kutumika kwa jina hili jipya la Mungu katika sura hii na sura zinazofuata ilikuwa ni kutaka kumtofautisha Mungu akiwa peke yake na Mungu akiwa katika uhusiano na vitu alivyovifanya. Katika sura ya kwanza ni Mungu akiwa katika nafasi ya pekee kama muumbaji wa vitu vyote, lakini katika sura ya pili na kuendelea ni Mungu akianza kumtumia mtu aliyemfanya katika kuendesha shughuli za duniani.
Msitari wa 5-7 inaendelea kuonesha kazi ya uumbaji wa Mungu katika umbo la mwili baada ya lile umbo la neno lililofanywa na Mungu katika sura ya kwanza. Utakumbuka kuwa Biblia inatujulisha kuwa neno likikaa hivyo hivyo bila kutwaa mwili utukufu wa Mungu kwenye jambo hilo huwa hauonekani. Ni pale tu neno linapotwaa mwili ndipo tunapouona utukufu wa Mungu kwenye jambo husika. Yohana 1:14 inasema
“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Ndiyo, wakati mwingine Mungu huwa anatutangazia mambo ambayo anataka kuyafanya katika maisha yetu, lakini si wote ambao huwa wanapokea sawa na ahadi hiyo ya Mungu. Kwa sababu watu wengi Mungu akiwasemesha kile anachopanga kwa ajili yao huwa hawahaingiki kumtafuta Mungu na kuomba ili jambo hilo waliloambiwa liwe halisi kwao, yaani litwae mwili.
Msitari wa 5 unatuambia kuwa kila mche na mboga ya kondeni hazikuchipuka kutokana na mvua. Mungu aliziotesha kwa kutumia ukungu uliopanda kutoka katika nchi ukaitia ardhi maji. Jambo tunalojifunza hapa ni kuwa asili ya miche yote ilikuwa ni nchi yenyewe na nchi haikutegemea mvua ili kuzalisha miche kwenye ardhi maana ulikuweko ukungu uliopanda kutoka kwenye nchi ambao ndio ulikuwa na jukumu la kutia maji juu ya ardhi. Kimsingi tunaona mvua ikinyesha kwenye Mwanzo 7:4 baada ya watu kumwasi Mungu (hatusemi mvua ni matokeo ya uasi). Kwa hiyo inawezekana kabisa kuwa katika utaratibu ambao Mungu aliuweka, ardhi haikutakiwa kuitegemea mvua eti ndo ichipushe miche. Kwa sababu utaratibu wa Mungu ilikuwa kwamba kila wakati ukungu ungepanda juu na kutia maji juu ya ardhi na ardhi ingechipusha miche ya kila aina. Lakini baada ya uasi wa mtu utaratibu ulibadilika, tunaona tegemeo la ardhi kuchipusha miche sasa likiwa kwenye mvua wala si ukungu tena.
Mtu kama nafsi hai
Msitari wa 7 una jambo la muhimu zaidi. Tunaona kwenye msitari huu mambo mawili ya muhimu sana yakifanywa na Mungu. Moja ni Mungu anamfanya mtu kutoka katika mavumbi ya ardhi. Pili ni Mungu akimpulizia “pumzi ya uhai” mtu yule naye akawa “nafsi hai”.
Utakumbuka kuwa katika Mwanzo 1:20 Mungu alianza utaratibu wa kuumba viumbe wenye uhai ndani yao, ikiwa ni pamoja na wanyama, samaki na ndege. Sasa hapa tunaona mtu naye akifanywa kuwa “nafsi hai.” Suala la – uhai - halimtofautishi mtu na viumbe wengine aliowafanya Mungu, ila ni jinsi alivyopata huo uhai ndiyo inayompa mtu utofauti na viumbe hai wengine.
Umbo la nje la mtu ni mavumbi ya ardhi, na wenzetu wa-Kiingereza wanatumia neno “dust of the ground” yaani uchafu wa ardhi. Hapa Mungu alitaka kutufundisha kuwa umbo letu la nje halina thamani yoyote na wala hatutakiwi kujivunia umbo hili la nje maana ni uchafu tu. Sehemu yenye maana na ya thamani ya mtu ni utu wake wa ndani ambao umefanywa kwa “pumzi ya Mungu.” Utu huu wa ndani unaitwa “nafsi hai.” Hakuna kiumbe kingine katika viumbe vilivyofanywa na Mungu ambacho kilipewa nafsi isipokuwa Mtu peke yake. Ile pumzi aliyopuliziwa Mtu kwa kiebrania wanatumia neno “nshamah” linalomaanisha – divine inspiration or intellect – uvuvio au utashi wa kimungu. Kwa hiyo mtu alipewa uvuvio na utashi wa kimungu ambao huo ndio uliomfanya awe “nasfi hai.”
Kuna mambo matatu yanayomwelezea mtu alivyo; Mwanzo 1:26 Mungu anatangaza kuwa Mtu amefanywa kwa sura na kwa mfano wa Mungu – Yohana 4:24 inatuambia kuwa “Mungu ni Roho.” Kwa hiyo kwa kuwa mtu alifanywa kwa sura na kwa mfano wa Mungu basi asili yake ni Roho – mtu ni roho. Baada ya hapo Mungu alimfanyia mtu umbo ambalo lingemwezesha kuishi katika dunia na hivyo akamfanyia mwili kama nyumba ya roho ya mtu kuishi. Ili kuwezesha mawasiliano kati ya roho na mwili Mungu alimpa mtu uvuvio na utashi wa kiroho ulioitwa nafsi. Kwa hiyo mtu ni roho anayo nafsi na anaishi katika mwili. Nafsi na roho zilitakiwa kumwezesha mtu kuwasiliana na Mungu wake bila matatizo wala mwili hauna uwezo wowote wa kuwasiliana na Mungu. Mtu aliumbwa kwa mfumo huu ili awe tofauti na viumbe wengine na ili awe mwakilishi na sura ya Mungu duniani.
Maisha ya mtu ndani ya Edeni
Baada ya mtu kuumbwa na kukamilishwa, Mungu anamtengenezea mahali pa kuishi na mahali pa kufanya kazi. Msitari wa 8-9 unatujulisha kuwa Edeni ilipandwa na Mungu mwenyewe ikiwa ni ishara ya kutufundisha kuwa kabla mtu hajazaliwa Mungu humwandalia mtu huyo Edeni yake, yaani kusudi lake na ni Mungu ndiye anayemweka mtu kwenye kusudi hilo. Siyo Adamu ambaye alichagua kuishi Edeni, ila ni Mungu ndiye aliyemweka ndani ya bustani hiyo. Mungu anapokupa nafasi ya kuishi kwenye dunia hii fahamu pia kuwa anakuwekea na kusudi ambalo kazi yako ni kuishi ndani ya hilo kusudi na kumtumikia Mungu humo.
Katika bustani ya Edeni Mungu alipanda kila aina ya mti uliostahili kumwezesha Adamu kuishi, lakini kuna miti miwili inayohitaji tuizungumzie kidogo. Kumekuwa na usemi wa siku nyingi kuwa Mungu alimzuia mtu kula matunda ya mti wa katikati ya bustani, na kumekuwa na mkanganyo juu huo mti ulikuwa ni nini? Lakini kwa kusoma kwetu Biblia hatukutani na msitari kama huo kwenye kitabu hiki cha Mwanzo. Tunachokuta ni katika msitari wa 16 -17 Mungu akimzuia mtu asile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, lakini hasemi “usile matunda ya mti wa katikati”.
Tunaambiwa katika msitari wa 9 kuwa palikuwa na mti wa uzima katikati ya bustani na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kwa kuweka mti wa uzima Mungu alitaka kumkumbusha mtu kuwa kuna maisha zaidi ya yale aliyokuwa akiyaishi wakati ule na kwamba kama angefuata maelekezo na masharti ya Mungu angeweza kuyafikia maisha hayo. Hatuoni mtu akizuiliwa kuyala matunda ya mti wa uzima ambao pia ulikuwa katikati ya bustani. Mti wa ujuzi wa mema na mabaya uliwekwa kwa kazi kubwa mbili. Moja ilikuwa ni kumpa mtu jukumu la kufanya la kiibada. Ilimpasa mtu asile matunda ya mti huo ili kuonesha kuwa anamheshimu na kumtii muumba wake. Mungu hakutaka kumwacha mtu awe huru kwa kila jambo ili asije akajiona kuwa sawa na Mungu wake, hivyo alimwekea kitu ambacho kingemfanya anyenyekee na kujiweka chini ya Mungu kwa kutii.
Pili, ilikuwa na kumkumbusha mtu kuwa katika dunia ambayo mtu alikuwa amewekwa kuna mambo ambayo yeye angeyaona kuwa mema lakini kumbe ni uharibifu. Biblia inasema “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti” (Mithali 14:12). Hili ndilo Mungu alilotaka kumtahadharisha mtu wake; kuwa kati ya mambo atakayoyaona kwenye dunia anayowekwa yapo ambayo kwa nje atayaona kuwa mema lakini kumbe mwishoni yamejaa uharibifu na mauti. Ndivyo ilivyo kwetu hata leo; mambo mengi yanayowakosesha watu wengi ni yale ambayo kwa nje yanaonekana kuwa ndiyo mazuri na matamu lakini mwisho wake siku zote imekuwa ni msiba na kilio. Wewe mwenyewe wayajua mambo hayo; hatuna hata haja ya kuyataja hapa.
Msitari wa 10-14 Unaeleza juu ya mito iliyowekwa ili iimwagilie Edeni. Mito hii ilitoka katika mto mmoja kisha ikagawanyika katika vichwa vinne. Biblia inatuonesha uzuri uliokuwa ndani ya mito hiyo na jinsi ilivyobeba dhahabu na vito vya thamani. Kwa hiyo tangu mwanzo Mungu alimwekea mtu wake maisha mazuri na ya thamani. Edeni haikupaswa kuwa kavu kwani mito hiyo ilitakiwa kuimwagilia maji kila wakati. Hii inatufundisha kuwa katika kusudi ambalo Mungu anakuweka ulitumikie huwa anaweka na mito ya kumwagilia kusudi hilo ili lisije likakauka kwa ukame. Kazi yako ni kuitunza bustani yako, yaani kusudi uliloitiwa na Mungu, kama ambavyo Msitari wa 15 unatuambia kuwa ilikuwa ni kazi ya Adamu kuilima bustani na kuitunza.
Kimsingi msitari wa 15 unaweka msingi wa kufanya kazi katika maisha. Biblia inasema “ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula (2 Thesalonike 3:10).” Jambo hili halijaanzia kwenye Agano Jipya; tunaona hapa kuwa ingawa Adamu alikuwa katika hali isiyo na hatia, bado Mungu hakutaka aishi bila kazi; alimtaka ailime bustani na kuitunza. Ndivyo ilivyo, Mungu hahitaji watu wavivu bali anataka kila mtu ajishughulishe. Biblia inasema hivi:
Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa (Mithali 13:4); Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa (Mithali 19:15).
Kwa hiyo Mungu hakutaka mtu wake awe mvivu hivyo alimpa jukumu la kuilima na kuitunza bustani. Sasa wewe huo uvivu ulionao unautoa wapi; au kama ni mzazi kwa nini unawaacha watoto wako wawe wavivu. Kwa nini hawafanyi kazi hata hizo ndogo; siyo mpango wa kimungu kabisa kuwa na watu wavivu duniani. Licha ya kuwa mtu alikuwa katika hali isiyo na hatia Mungu aliamua kumwekea sheria ndogo za kumfanya amheshimu Mungu na kumtii kama tulivyosema hapo kabla.
Na pia Mungu aliona si vema kumuacha mwanadamu awe hana cha kufanya kabisa. Mwenyewe jaribu kufikiria maisha ambayo asubuhi, jioni na usiku umekaa tu huna cha kufanya, maisha ya namna hiyo kimsingi yanakera na hautajisikia vizuri. Ndiyo maana Mungu kwa kuliona hilo alitaka Adam awe ana kitu cha kufanya. Kama utakwepa kufanya kile ambacho Mungu amekupa kufanya katika bustani yako, basi jua fika kuwa adui shetani atakupa cha kufanya kwani mwili wako haujaumbwa kukaa bila kazi, ndiyo maana wavivu wengi hujikuta wanawasengenya wengine na kuchonganisha watu, ni kwa sababu pale ambapo ilibidi wafanye kazi aliyowapa Mungu wao walizembea na shetani akaingiza cha kwake.
Msitari wa 16-17 Mungu anamzuia mtu kula matunda ya mti mmoja tu kati ya mingi iliyokuwepo pale bustanini. Mungu wetu hapendi kututwika mizigo mizito hivyo aliamua kuipunguza sheria yake kwa Adamu mpaka kiwango cha chini kabisa; akamruhusu ale matunda ya miti yote kasoro mmoja tu. Hebu jiulize kama Mungu angemwambia Adamu asile matunda ya miti mingine yote isipokuwa ale matunda ya mti mmoja tu, unadhani nini kingetokea? Vile vile jiulize kama Yesu angesema dhambi zote watakazotenda wanadamu watasemehewa isipokuwa zinaa, unadhani wangapi wangeingia mbinguni?
Utaratibu wa Mungu wetu ni kutupunguzia sheria kwa kadiri inavyowezekana. Jambo la ajabu ni kuwa mtu anapenda kuacha mazuri mengi aliyoruhusiwa na Mungu na kuamua kufanya yale machache aliyozuiwa na Mungu. Ndicho alichofanya Adamu hapo baadae, akaacha yote aliyopewa na Mungu akakimbilia lile moja tu alilozuiwa na Mungu. Kwa kawaida ya Mungu kila anapotoa maelekezo ya nini kifanyike au kisifanyike huwa anatoa pia matokeo ya kila utakachofanya. Adamu alielezwa madhara ya endapo hatatii maelekezo aliyopewa na Mungu, kama ambavyo Biblia inatuonya sisi wote juu ya hukumu na moto wa jehanamu kwa watu ambao hawakumwamini Yesu Kristo na kuifuata njia ya utakatifu. Lakini kama vile ambavyo Adamu alishindwa sheria hii ndogo sana ndivyo na watu wengi ambavyo watashindwa kuingia mbinguni ingawa neema ya Kristo iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa.
Mwanamke anafanywa
Msitari wa 18-24 inatuanzishia jambo jingine kubwa sana; Mungu hakumuumba Adamu ajitegemee katika kila jambo hivyo alihitaji msaidizi wa kufanana nae. Jinsi huyu msaidizi alivyotafutwa hadi kupatikana ndiyo tunayotaka tuiangalie hapa. Biblia inasema baada ya Mungu kuona kuwa anahitaji kumfanyia Adamu msaidizi, jambo alilofanya lilikuwa ni kufanya wanyama wa msituni na ndege wa angani na kuwaleta kwa Adamu ili aone atawaitaje. Kwa lugha nyingine Mungu alitaka kuona kama kati ya hao Adamu atachagua wa kumsaidia; wote akawapa majina lakini hakuonekana wa kufanana nae aliyefaa kumsaidia. Ndipo Mungu akakumbuka kuwa kuna mtu aitwaye mwanamke ambaye tayari alikuwamo ndani ya Adamu; ndipo akamletea Adamu usingizi akachukua ubavu wake na ule ubavu “akaufanya mwanamke”.
Hii inatufundisha kuwa katika suala la kuoa au kuolewa si kila mtu atakayepita mbele yako ni msaidizi wa kufanana na wewe; hata kama amepitishwa na Mungu. Wengine ni wanyama wa mwitu na ndege wa angani, na Mungu anawapitisha tu mbele yako aone utawaitaje – wewe unakurupuka kusema “Mungu kanionesha huyu ndiye mke/mme wangu”- wewe tulizana kwanza uelewe kama hao wanaopita wamefanywa kutoka ardhini au kutoka ubavuni mwako. Hebu piga picha ya simba alipopitishwa mbele ya Adamu halafu Mungu akawa anategea tu aone Adamu atamwitaje. Hivi kama Adamu angekurupuka na badala ya kumwita simba akamwita mke nini kingetokea kwenye maisha yake; si ingekuwa kuraruriwa tu. Wakati mwingine Mungu anataka kuupima uwezo wako wa kuchanganua mambo na kuwajua watu hivyo anaamua kuwapitisha watu ambao ni simba kwako, ili aone wewe utawaitaje. Usipojua kuwa ni simba wewe utakurupuka kusema ni mke wako matokeo yake ni kuraruriwa tu kila siku. Na watu wengi wanaojifanya wameona maono ya mke au mme wameishia kuwaita simba kuwa ni wake zao au waume zao, na matokeo yake wameraruliwa.
Kama Adamu angeishi kwenye nyakati hizi halafu suala la kumfanyia mke ndo likapitishwa kwa jinsi ile ya kwanza sijui kama angekurupuka kama walokole wa siku hizi wanavyokurupuka. Hebu jifunze kuwa ni Mungu ndiye aliyewapitisha wale wanyama mbele ya Adamu ili apime utashi wa Adamu katika kugundua yanayomfaa na yasiyomfaa. Ni Mungu huyo huyo ndiye pia anaweza kupitisha wadada/wakaka kadhaa mbele yako tena kwa maono na ndoto ili tu apime uwezo wako kama mwana wa Mungu wa kuchanganua kati ya wanyama mwitu na mkeo/mmeo.
Utaona kuwa baada ya Adamu kutegua kitendawili alichotegewa na Mungu, Mungu alirudi kazini akamletea yule ambaye kweli alikuwa wa kufanana nae, na alipomfikisha tu kwa Adamu haikuhitaji utambulisho wa Mungu kuwa huyu ni nani maana Adamu alimjua mapema. Sasa wewe kwa nini unatafuta mchungaji wako ndo akutambulishie mmeo/mkeo. Kaa vizuri na Mungu ili uwe na uwezo wa kumtofautisha mkeo/mmeo na wanyama wa mwitu au ndege wa angani.
Biblia inasisitiza kuwa suala la kuoana linawatenga watu na familia zao za mwanzo na kuwapa nafasi za kuanzisha familia zao wenyewe. Hii ni somo kwa wazazi ambao wanapenda sana kuingilia mambo ya watoto wao wakiishaolewa au kuoa. Biblia inasema wawili hawa watawaacha wazazi wao, maana yake watatengwa na utawala wa wazazi wao ili wakusanye mawazo yao binafsi kwa ajili ya nafasi mpya ambayo Mungu anawapa. Tafadhali wazazi kuweni makini na namna mnavyoingilia mambo ya watoto wenu pindi wanapooa au kuolewa.
Msitari wa mwisho wa sura hii unasema Adamu na mkewe walikuwa uchi wala hawakuona haya. Msitari huu unaonesha uthabiti wa hali isiyo na hatia ambayo watu hawa waliishi hapo mwanzo. Hata hivi leo mtoto mdogo akiachwa uchi, yeye hataona shida yoyote. Ndivyo walivyokuwa Adamu na mkewe; walikuwa kama watoto wachanga wasiojua ubaya wa kuwa uchi na hivyo hawakuona haya.
No comments:
Post a Comment