Wednesday, December 24, 2014

MWANZO SURA YA 5



Mwanzo Sura ya 5

Sura hii ya 5 ya kitabu hiki cha Mwanzo inaanzisha historia mpya katika ulimwengu wa maisha ya mtu duniani. Utakumbuka kuwa katika tafakari yetu ya sura ya pili ya kitabu hiki cha mwanzo tulikueleza mgawanyo wa kitabu hiki kwa mujibu wa vizazi vilivyotajwa ndani yake. Tulikuambia kuwa kama kitabu hiki kingeandikwa kwa kufuata vizazi vinavyojitokeza ndani yake basi kingekuwa na sura 11. Mambo yote yanayojitokeza katika sura ya 2:4 mpaka mwishoni mwa sura ya 4 yanatajwa kuwa mambo yaliyofanyika katika vizazi vya mbingu na nchi. Sura hii ya tano inaanza kwa kutufunulia aina nyingine ya uzao inayoitwa vizazi vya Adamu. Tunayakuta tena maneno kama haya yasemayo “Hivi ndivyo vizazi vya…” kwenye Mwanzo 6:9, na hii inatupa kujua kuwa wote wanaohusika katika Mwanzo 5:1 hadi Mwanzo 6:8 walikuwa na chanzo chao katika Adamu na kwa namna moja ama nyingine waliathiriwa na uhusiano ambao Adamu alikuwa nao kwa Mungu wake.

Msitari wa 2 una jambo la tofauti kidogo ambalo tunataka tulizungumzie. Biblia inasema hivi: mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa.”  Maneno yaliyokolezwa kwenye msitari huu ndiyo tunayotaka tuyaangalie kwa upana kidogo. Ni wazi kuwa watu wengi tumekuwa tukitumia jina Adamu kwa kumrejelea mwanaume, na mwanamke amekuwa akitajwa kwa jina la Eva ama Hawa. Lakini msitari huu unatuambia kuwa jina “Adamu” ni jina ambalo Mungu aliwapa mwanamume na mwanamke siku ile alipowaumba. Kwa hiyo jina “Adamu” kwa maana nyingine ni kuwa halikuwa na kazi ya kutofautisha jinsia kati ya mwanamume na mwanamke, maana lilikuwa jina lao wote.

Unaposoma Mwanzo 1:27 utakuta Biblia ikisema hivi:

Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.

Sasa kitu cha ajabu sana kwenye msitari huu ni kuwa nafsi mbili – umoja na wingi – zimetumika kumwelezea mtu mmoja. Maana utaona Biblia ikisema:“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake” – hii ni nafsi ya umoja, ikionyesha ya kuwa mtu aliyeumbwa alikuwa mmoja. Maana kama wangekuwa wawili au wengi walioumbwa ingeandikwa kuwa “Mungu akaumba watu kwa mfano wake.” Kwa hiyo uumbaji ulifanyika katika mtu mmoja.

Kisha tunaona Biblia ikisisitiza hili la nafsi ya umoja kwa kuendelea kusema kuwa: “Kwa mfano wa Mungu alimwumba.” Kwa mara nyingine tena Biblia haisemi “kwa mfano wa Mungu aliwaumba” ila inasema “alimwumba” – maana yake ni mmoja. Kwa hiyo mpaka hapo tunaelewa kuwa mtu aliumbwa kama nafsi moja katika umoja.

Lakini ghafula kwenye msitari huo huo Biblia inaleta kitu kingine cha tofauti – sasa inasema “mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Hii sasa inatajwa katika wingi, ya kuwa walipoumbwa walikuwa mwanamume na mwanamke. Kwa hiyo kwa maana nyingine ni kuwa mwanamume na mwanamke waliumbwa wote siku moja lakini wote wawili walikuwa ndani ya mmoja. Ndiyo maana utakumbuka kuwa katika tafakari ya sura ya pili tulikueleza kuwa suala la mwanamke kutwaliwa kutoka kwenye ubavu wa mwanamume lilikuwa ni tendo tu la kumdhihirisha katika umbo la mwili kwa kuwa tayari alikuwa ameshaumbwa pamoja na mwanamume siku ile walipoumbwa kwenye Mwanzo 1:27. Kwa hiyo mtu ni mmoja ila ndani yake walikuwemo mwanamume na mwanamke. Ilikuwa ni mpango wa Mungu mwanaume adhihirike kwanza katika mwili halafu ndo mwanamke afuatie, maana Biblia inatufundisha kuwa mwanamume ni utukufu wa Mungu na mwanamke ni utukufu wa mwanamume. 1 Kor 11:7, inasema:

Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume.

Kwa hiyo tunapokuta Mwanzo 5:2 ikisema kuwa mwanamume na mwanamke wote waliitwa “Adamu” siku ile Mungu alipowaumba, sasa tunaelewa kuwa haizungumzii siku walipodhihirishwa katika mwili kama ilivyo kwenye Mwanzo 2:7 na Mwanzo 2:22, bali tunajua kuwa inazungumzia siku walipoumbwa kwenye Mwanzo 1:27. Na kweli kama tulivyoona hapo juu ni kuwa walipoumbwa kwenye Mwanzo 1:27 ijapokuwa walikuwa wawili – mwanamume na mwanamke – lakini walikuwa mmoja, na kwa hiyo jina lao waliitwa “Adamu” wote wawili.


Uzao wa Adamu

Msitari wa 1 wa sura hii ya 5 umeanza kwa kusema “hiki ni kitabu cha vizazi vya Adamu,” lakini utashangaa, pamoja na sisi, kuona kuwa kinapoanza kutaja hivyo vizazi kuanzia msitari wa 3 na kuendelea hatukuti uzao unaomhusu Kaini wala Habili ukitajwa. Utakumbuka tumezitafakari vizuri kidogo habari za Kaini na Habili kwenye Mwanzo sura ya 4, lakini suala la kukuta watu hawa hawatajwi kabisa kwenye “kitabu cha vizazi vya Adamu” linatupa kufikiri kwa undani kidogo zaidi ya tuliposhia kwenye sura ya 4.

Kuhusu Habili kutokutajwa tunaweza tusiwe na maswali mengi sana ya kujiuliza, maana alikwisha kufa, lakini pia Hawa alipomzaa Sethi Biblia inatueleza hivi:

Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua. [Mwanzo 4:25]

Kumbe kuzaliwa kwa Sethi kulikuwa ni mbadala wa Habili ambaye Kaini alimwua. Kwa namna fulani ni kama vile kuja kwa Yesu kulivyokuwa ni mbadala wa Adamu ambaye aliasi, na kama vile kuja kwa Yesu kunavyofuta mambo yote ya Adamu, ndivyo na kuzaliwa kwa Sethi kulivyochukua nafasi yote ya Habili ndani ya vizazi vya Adamu. Kwa hiyo kuhusu Habili kutotajwa kwenye “kitabu cha vizazi vya Adamu” mambo hayo mawili yanaweza kuwa ni miongoni mwa sababu za kutotajwa kwake. [Tunasisitiza kuwa hizi zinaweza kuwa tu ni miongoni mwa sababu, sababu nyingine zaweza kuwepo].

Tunapokuja kwenye suala la kutotajwa kwa Kaini kwenye “kitabu cha vizazi vya Adamu” hapa panahitaji fikra tofauti kidogo. Tuliona kwenye sura ya 4 jinsi Kaini alivyoondoka mbele za uso wa Mungu na kwenda kuanza maisha yake kwenye nchi ya Nodi. Pia tulikueleza jinsi ambavyo uzao wake ulivyoishi na jinsi ambavyo Lameki, mtu wa uzao wa Kaini, alivyoingia kwenye uasi kama wa mtangulizi wake.

Tunapoisoma Biblia na kuitafakari kwa umakini tunagundua kuwa Mungu huwa hajihusishi na kuandika habari za watu ambao wako nje ya mpango wake kwa urefu sana. Kwa mfano ukisoma habari za Ishmaeli na Isaka, utaona habari za Ishmaeli zikiandikwa kwa ufupi sana halafu zinatoweka. Ukisoma habari za Yakobo na Esau, pia utaona habari za Esau zikitajwa kwa ufupi tu kisha zinatoweka. Na vile vile ukifuatilia habari za Yesu na Adamu, utaona habari za Adamu hazina mwendelezo sana kama habari za Yesu zinazozungumzwa kwenye Biblia yote. Kwa hiyo tunagundua kuwa watu waliotembea nje ya utukufu wa Mungu Biblia iliwasahau kwa haraka sana na habari zao hazikukumbukwa. Hii tunaamini ndiyo ilimpata Kaini hadi kupelekea kusahauliwa kwake kwenye “kitabu cha vizazi vya Adamu.” Hata uzao wake hautajwi kwenye kitabu hiki cha vizazi vya Adamu, lakini uzao wa Sethi unatajwa.

Ndugu mpendwa msomaji wetu, jambo hilo hapo juu halikuwapata watu wa kwenye Biblia tu bali linawapata wengi hata leo. Watu wote wanaoishi nje ya mpango wa Mungu kusahauliwa kwao mbele za Mungu ni rahisi sana na hata wakiomba kitu kwa Mungu hawajibiwi kwa kuwa wako nje ya msitari wa Mungu. Lakini wale walio ndani ya Kristo Yesu, Biblia inasema hawatasahauliwa; Isaya 49:14-16 inasema:

Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.

Mungu ameahidi kutokumsahau mtoto wake, lakini Biblia inasema ni wale tu waliompokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wao ndio wanastahili kuitwa watoto wa Mungu, na hao ndio hawatasahauliwa. Amua kumpokea Yesu leo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako nawe utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu na utapokea uwezo wa kukubadilisha na kukufanya mwana wa Mungu [Yohana 1:12; Matendo 2:38]. Hapo hakika hautasahauliwa kama Kaini na uzao wake walivyosahauliwa, bali utakuwa ukikumbukwa daima mbele za Mungu aliye hai.

Msitari wa 3 wa sura hii ya 5 unaleta kwetu jambo jingine zuri sana; sasa Adamu alizaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi. Maneno ya Biblia yaliyotumika kwenye msitari huu ni ya kuzingatia sana maana yanatufunulia kuwa huyu mtoto aliyezaliwa alikuwa ni kwa sura na mfano wa Adamu. Maneno kama haya hayajitokezi sana kwenye Biblia inapozungumzia aina ya mtoto aliyezaliwa. Kimsingi ukiacha pale Mungu aliposema “tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu (Mwanzo 1:26 -27), hakuna sehemu nyingine kwenye Biblia uzao wa namna hii unapotajwa tena isipokuwa hapa kwa Sethi. Hii haikuwa bahati mbaya; Adamu aliumbwa kwa sura na kwa mfano wa Mungu, kwa hiyo suala la Sethi kuzaliwa kwa sura na mfano wa Adamu maana yake alichukua sifa za Adamu wa kwanza ambaye alikuwa amefanana na Muumba wake. Na ndiyo maana utaona Mwanzo 4:26 ikisema:

Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.

Hapa tunagundua sasa kuwa Sethi alizaliwa kama mteule wa Bwana kwa ajili ya kurudisha uhusiano wa mtu na Mungu wake ambao Adamu aliupoteza. Hii ni kweli maana jina Sethi kwa kiebrania ni “Sheth” ambalo linamaanisha “substitute” yaani “mbadala.” Kwa hiyo licha ya kwamba Sethi alizaliwa kama mbadala wa Habili ambaye Kaini alimwua kama Hawa alivyosema, lakini pia Sethi alikuwa ni mbadala kwenye mambo yaliyohusu uhusiano wa mtu na muumba wake. Ndio maana ni katika uzao wa Sethi ndipo tunakuta ibada ikianzia. Biblia inasema “hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.”

Msitari wa 4 mpaka wa 20 kwenye sura hii kimsingi inazungumzia tu watu waliozaliwa ndani ya ukoo huu wa Adamu na siku zao za kuishi. Biblia imenyamaza kuhusu maisha yao na jinsi walivyoenenda kwenye mambo yao na Mungu, na kwa kuwa Biblia imekaa kimya na sisi tunabaki kusema tu kama Musa mtumishi wa Mungu alivyosema kuwa:

Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele… [Kumbukumbu la Torati 29:29]

Kwa hiyo hayo ambayo Biblia haikuyanena juu ya watu hawa hatuna haja ya kuyaulizia sana maana Mungu hakutaka yawe yetu, ila yaliyo yetu na watoto wetu alitufunulia wazi wazi. Ndiyo maana Biblia inapofika msitari wa 22 inatulia kidogo na kuanza kutuelezea habari za Henoko kwa undani kidogo tofauti na vile ilivyowaelezea wengine waliotangulia.

Uhusiano wa Henoko na Mungu wake

Henoko alikuwa wa saba kutoka kwa Adamu (maana ndivyo Yuda 1:14 inavyosema kuwa Henoko alikuwa mtu wa saba baada ya Adamu) kwenye uzao wa Baraka uliopita ndani ya Sethi, na kama vile Lameki, aliyekuwa wa saba kutoka Adamu kwenye uzao wa laana uliopita ndani ya Kaini, alivyokuwa na tabia ya tofauti na wenzake, ndivyo na Henoko naye alivyokuwa tofauti na wengine. Katika Lameki tunaona ulimwengu na walio ndani yake wakimwacha Mungu na kuingia katika kuasi, lakini katika Henoko tunaona bidii ya mtu katika kumtafuta na kutembea na Mungu wake.

Maneno ya Mwanzo 5:21-24 yanahitaji tuyatafakari kwa undani kidogo zaidi; mistari hiyo inasema hivi:

Henoko akaishi miaka sitini na mitano, akamzaa Methusela. Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia tatu, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na sitini na mitano. Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa.

Tafsiri ya kiingereza ya New King James Version inaitafsiri mistari hii kwa kusema hivi:

Enoch lived sixty-five years, and begot Methuselah. After he begot Methuselah, Enoch walked with God three hundred years, and begot sons and daughters. So all the days of Enoch were three hundred and sixty-five years. And Enoch walked with God; and he was not for God took him.

Maneno yaliyokolezwa hapo juu yana msisitizo tofauti ambao tunataka tuuzungumzie hapa. Biblia inatoa hesabu ya idadi ya siku zote alizoishi Henoko kuwa ni miaka mia tatu na sitini na mitano (365), lakini inasema katika miaka hiyo Henoko alitembea na Mungu miaka mia tatu (300). Maana yake miaka sitini na mitano (65) Henoko alikuwa akitembea kwenye njia yake mwenyewe. Biblia inaweka wazi kabisa kuwa Henoko alianza kutembea na Mungu baada ya kumzaa Methusela na utakumbuka kuwa Methusela alizaliwa Henoko akiwa na miaka sitini na mitano (65). Kwa hiyo tunachogundua hapa ni kuwa miaka sitini na mitano ya mwanzo ya maisha ya Henoko alikuwa akitembea mwenyewe kwenye njia aliyoijua mwenyewe, maana Biblia haituelezi maisha yake kabla ya kumzaa Methusela yalikuwaje. Lakini kwa kuwa Biblia haikuona umuhimu wa kutueleza maisha yake kwenye hiyo miaka 65 yalikuwaje na sisi hatuhangaiki sana kujiuliza yalikuwaje, tunachotaka uone ni kile Biblia ilichotaka wote tuone na hiki ni kile inachosema “Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia tatu…”

Kitu ambacho tunataka tujifunze pamoja kwenye msitari huu ni ule uwezo wa Henoko kutembea na Mungu miaka 300. Unajua Biblia haisemi kuwa “Henoko akaenda pamoja na Mungu kisha akaanguka katika dhambi kisha akainuka tena!” Biblia inasema Henoko alienda pamoja na Mungu miaka 300, maana yake ni kuwa katika kipindi chote alichoanza kutembea na Mungu akiwa na miaka 65 mpaka anakuja kutwaliwa akiwa na miaka 365 hakuwahi kuachana na Mungu wala kupoteza uwepo wa Mungu maishani mwake. Hii siyo kitu cha kawaida, lazima kuna vitu vya kiroho ambavyo vilikua ndani ya Henoko ambavyo vilimwezesha kutembea na Mungu kipindi hiki chote bila kumkosea. Biblia inatueleza undani wa mambo haya yalivyo… endelea tu kufuatilia pamoja nasi somo hili utaona.

Kabla hatujanza kuangalia mambo yaliyomwezesha Henoko kutembea na Mungu kipindi chote hicho bila kuachana na uwepo wa Mungu, ngoja tuangalie jambo lingine fupi kidogo. Kitu ambacho tunataka uone kwanza ni kile Biblia inachosema kuwa: “Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa.” Biblia inasema Henoko, baada ya kuwa ametembea na Mungu miaka 300, alitwaliwa na Mungu; maana yake yeye hakufa kama ilivyo kawaida ya watu wote. Kitabu cha Waebrania kina jambo la kutufundisha hapa; Waebrania 11:5 inasema:

Kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.

Waebrania inasema Henoko alihamishwa na Mungu ili asije akaona mauti. Hii inaleta swali moja kubwa sana, nalo ni: Kama Mungu mwenyewe ndiye aliyeagiza mauti juu ya kila mwanadamu kwa sababu ya kosa la Adamu, ilikuwaje Mungu huyo huyo ndiye amhamishe Henoko eti kisa asije akaonja mauti? Maelezo yafuatayo hapa chini yanajibu swali hili.

Biblia inaelezea maisha ya Henoko kuwa alikuwa nabii na aliweza kutabiri kuja kwa masihi katika hukumu juu ya wote watendao maovu. Inawezekana unajiuliza, hiyo imeandikwa wapi kwenye Biblia? Hii hapa; Yuda 1:14-15 inasema hivi:

Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.

Biblia inasema Henoko alitoa maneno ya unabii juu ya watu wote wasiomcha Mungu juu ya hukumu ya Mungu iliyokuwa tayari kuwajilia wote watendao maovu. Tunaamini kuwa unajua kuwa atoaye maneno ya unabii ni nabii; kwa hiyo kama Henoko alitoa maeneno ya unabii basi ujue alikuwa nabii na hivyo yeye alikuwa nabii wa kwanza kwenye Biblia. Au hujui pia kuwa Ibrahimu nae alikuwa nabii; tutakueleza hilo tukifika kwenye sura zinazomhusu Ibrahimu.

Unabii aliotoa Henoko ulikuwa ni juu ya hukumu kwa watu wasiomcha Mungu, na unaelewa wazi kuwa watu wasiomcha Mungu huwa hawapendi kusikia habari za hukumu au habari za kitakachowapata wakati wa mwisho. Inaonekana kuwa Henoko alipotoa unabii wa namna hii watu waovu walianza kuwinda uhai wake wakitaka kumwua, kama ambavyo wakuu wa makuhani na mafarisayo walivyokuwa wakitafuta kumwua Yesu kila waliposikia habari za hukumu yao.Henoko aliishi kwenye nyakati ambazo neno la Mungu lilikua adimu na watu walikuwa wakifanya maovu mengi, hivyo suala la yeye kuwa mcha Mungu miongoni mwa wengi wasioenda katika njia ya Mungu lilihatarisha sana maisha yake – ni wazi sasa mauti ilimwandama kila alikoenda – na hivyo Mungu akaona akimwacha aendelee kuishi pamoja na watu hawa waovu wangeweza kumwua – hivyo akamhamisha (akamtwaa).

Ile Waebrania inathibitisha kuwa uhai wa Henoko ulikuwa mashakani kwa kuwa Waebrania 11:5 inasema:

Kwa imani Henokoalihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.

Maneno yaliyokolezwa yanasema “wala hakuonekana” – swali la kujiuliza hapa ni kuwa: hakuonekana kwa akina nani? Maana kama ni kwa Mungu – yeye ndiye aliyemtwaa. Hii inatupa kujua kuwa walikuwepo watu waliokuwa wakimtafuta Henoko na ilikuwa wakati walipokuwa katika kumtafuta “hakuonekana” kwao. Ndiyo maana utakuta Biblia za kiingereza kwenye ile Mwanzo 5:24 zikitumia neno “and he was not” kumaanisha “akatoweka.” Kutoweka ni kupotea katika mazingira tatanishi ambayo hayakutegemewa – ndiyo, Mungu alimtowesha Henoko katika mazingira ambayo hayakutegemewa ili kuwaduwaza waliokuwa wakiwinda uhai wake.

Sasa ngoja turudi kwenye mambo yaliyomwezesha Henoko kutembea na Mungu miaka yote hiyo 300 bila kupoteza uwepo wa Mungu. Majibu yako kwenye Biblia; Yuda 1:14-15 inasema hivi:

Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.

Kisha Waebrania 11:5 inasema:

Kwa imani Henokoalihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.

Kuna mambo makubwa matatu ambayo tunaona yalimwezesha Henoko kuwa na stamina kubwa kiasi kile ya kutembea na Mungu kwa muda mrefu hivyo. Tutayaangalia hapa kwa ufupi, maana nia ya tafakari hii ni kukufikirisha zaidi kuliko kwenda kwenye undani wa masomo kipekee. (Kwa masomo zaidi fuatilia vitabu vyetu vingine na masomo tuanayoweka kwenye mtandao).

1.      Jambo la kwanza ni IMANI. Waebrania inasema “kwa imani Henoko alihamishwa…” Kumbe Henoko alikuwa mtu aliyeishi kwa imani; hakuishi kama wengine wa kipindi kile walivyoishi – yeye aliishi kwa imani. Utakumbuka kuwa ni “IMANI” ndiyo pia iliyomtofautisha Habili na Kaini kwenye uhusiano wao na Mungu (rejea tafakari yetu ya sura ya 4). Biblia inaweka wazi kabisa kuwa suala la kumpendeza Mungu ni suala la ki-imani na pasipo imani haiwezekani kutembea vizuri na Mungu. Waebrania 11:6 inasema:

Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

Imani inayozungumzwa hapa ni zaidi ya imani ya kusema kuwa Mungu ni Mungu; hii ni imani ya kuchukua hatua kumwendea Mungu na kutafuta kukaa uweponi mwake siku zote huku ukiamini kwamba kwa kumtafuta yeye utapata thawabu. Hii imani inakupa bidii ya kuendelea kumtafuta Mungu kila siku bila kuchoka na bila kuridhika kuwa umefika mwisho. Hiyo ndo imani iliyokuwa ndani ya Henoko ambayo ilimwezesha kutembea na Mungu miaka 300. We jiulize imani yako ikoje kwanza kabla ya kufikiri unamahusiano gani na Mungu wako. Biblia inasema “kila mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kuwa yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Lazima uamini, hivyo ndivyo Biblia inavyoiweka kanuni ya kutembea na Mungu – kuwa lazima aamini. Jifunze zaidi hii imani ya Henoko itakusaidia sana.

2.      Jambo la pili ni MAISHA YA HUDUMA. Biblia imetueleza kuwa Henoko alikuwa ni nabii, hivyo ni wazi kuwa huduma yake kwa Mungu ilikuwa ni unabii. Maisha ya huduma ni muhimu sana katika kukuwezesha kutembea na Mungu. Huduma inamweka mtu katika mwendo wa kumtafuta Mungu kila siku na kujiweka kwenye uwepo wa Bwana kila wakati ili asije akazimisha moto wa madhabahu. Huduma ya mtu ili ikue na kufanikiwa inatakiwa ichochewe kwa maombi na neno la Mungu na utakatifu. Hizi ndizo kuni za huduma, zikikosekana hizo huduma inapoa au kufa kabisa. Ndivyo Mithali 26:20 inavyotuambia kuwa “Moto hufa kwa kukosa kuni…” 

Kwa hiyo ili huduma ya Henoko ya unabii idumu ilimpasa yeye kuchochea moto wa huduma kila siku. Katika kuchochea huko uhusiano wake na Mungu ulikuwa ukiimarika siku kwa siku hata haikuwepo nafasi ya dhambi kupenya ndani yake. Tunataka uone hapa umuhimu wa kutafuta kujua huduma yako Mungu aliyokuwekea ndani maana hiyo inayo nguvu ya kukusaidia katika kutunza uhusiano wako na Mungu. Maisha ya huduma yametusaidia sana sisi watu wa Fimbo ya Musa Ministry kujiweka karibu na Mungu na kuzikimbia tamaa za ujanani. Ndugu mpendwa, anza leo kuchochea huduma yako nayo itakusaidia sana kujiweka karibu na Mungu.

3.      Jambo la tatu ni MAISHA YA KUMPENDEZA MUNGU. Biblia inasema wazi kuwa kabla ya kuhamishwa (kutwaliwa) Henoko alishuhudiwa kuwa amemependeza Mungu. kiukweli hauwezi kumpendeza Mungu kama maisha yako siyo matakatifu. Maisha ya utakatifu ndiyo yanamfanya mtu ampendeze Mungu. Suala la kumpendeza Mungu ni jambo linaloanzia moyoni mwa mtu mwenyewe kuweka dhamiri ya kuishi kwa kumpendeza Mungu. Daudi alimpendeza Mungu hata kabla hajaanza huduma [Matendo 13:22]. Kwa hiyo siyo huduma inayokufanya umpendeze Mungu, maana wako wengi tu walio kwenye huduma na bado Mungu hapendezwi nao. Jifunze kumpendeza Mungu kutoka moyoni mwako kwa kuishi maisha mtakatifu, naye Mungu atakupa kibali na neema ya kutembea nae siku zako zote.

Kuzaliwa kwa Nuhu

Baada ya kueleza habari za Henoko, Biblia inaeleza watu wengine waliozaliwa baadae – mara hii tena bila kutaja kwa undani habari zao. Inapofika msitari wa 29 inasema Lameki alimzaa mwana akamwita Jina lake Nuhu akasema: “Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani Bwana.” Kwa lugha rahisi ni kuwa Lameki alikiri kuwa kizazi kile kilikuwa ni kizazi kibaya na kuwa kilikuwa kimelaaniwa na Bwana, lakini alitabiri vema juu ya nafasi ya mtoto aliyemzaa katika kuleta badiliko juu ya uovu uliokuwa umetokea. Jambo tunaloweza kujifunza hapa ni kuwa yale maneno tunayoyatamka pale watoto wetu wanapozaliwa yana nafasi kubwa sana katika kile ambacho kitakuja kutokea kuhusu maisha ya mtoto huyo huko ukubwani. Angalia sana unachokiongea kuhusu mtoto wako, sasa huyu mwingine eti mtoto akishazaliwa, akishasikia tu kuwa mtoto kazaliwa wa kike utasikia anasema “Malaya mwingine huyo kazaliwa,” halafu mototo huyo akikua akifanya kosa utasikia baba anamwambia “Hili litakuwa Malaya kama mama yake,”! Maneno yote unayoyasema kuhusu mwanao yana nguvu na yanaathiri maisha ya mwanao kama tunavyoona kwa Lameki kuhusu Nuhu. Kama tutakavyoona katika sura zitakazofuata kuwa Nuhu ndiye aliyekuwa daraja la kizazi cha zamani na cha leo, maana ndiye aliyetengeneza safina na akaokoa wanyama na familia na ile mvua kubwa. Sura hii ya 5 inamalizika kwa kuonesha uzao wa Nuhu – tutawazungumzia hawa kwenye sura zinazofuata.

Endelea kufuatilia mfululizo huu kwa ajili ya sura ya 6

DOWNLOAD MWANZO SURA YA 5

No comments:

Post a Comment