Haleluyaaa!!!
Hakika Jina la Yesu ni kuu kupita majina yote na uweza wake ni wa ajabu wala hauelezeki. Mwaka 2014 sasa unaelekea ukingoni na kuupisha mwaka 2015 kushika hatamu za nyakati na majira. Tunamshukuru Mungu, baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, katika uweza wa Roho Mtakatifu, yeye aliyeziamuru nyakati na majira viwepo tangu mwanzo, kwa kutupa neema ya kuishi katika mwaka huu wa 2014. Neno la Bwana linasema:
Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba. [Isaiah 33:6]
Kama mtu wa Mungu Isaya alivyosema, ni kweli nyakati hizi kwetu zimekuwa za kukaa imara, za wokovu tele na hekima na maarifa, na kumcha Bwana ndiyo imekuwa hazina yetu. Mwaka huu sasa unamalizika, na sisi kama wahudumu wa Kristo Yesu kupitia FIMBO YA MUSA MINISTRY tunamshukuru Mungu kwa kazi yote aliyotuwezesha kuifanya kwa mwaka huu. Tumekuwa na semina mbalimbali, tumefanya huduma makanisa mbalimbali, lakini pia tumewafikia watu wengi zaidi kwa njia ya mtandao. Ni neema kubwa ambayo Bwana Yesu ametuheshimu nayo hadi kutufikisha hatua. Ni kweli “mtu akinitumikia Baba atamheshimu [Yohana 12:26].
Tunataka tukushukuru pia wewe ndugu yetu katika Bwana kwa kutupa ushirikiano wako mkubwa sana katika kuiendeleza huduma hii. Tunajua wako watu wanatuombea, na wako watu wanafuatilia masomo yetu kila mara maana mpaka sasa tuna watu zaidi ya 560 kila mwezi wanaofuatilia mafundisho yanawekwa kwenye mtandao huu. Hii ni hatua kubwa sana ambayo Mungu amefanya kwetu. Tunakushukuru sana wewe msomaji wetu kwa kuendelea kufuatilia masomo yanayokuja kwako kupitia mtandao huu.
Mwaka ujao 2015 tunatarajia kufanya mambo mengi zaidi kuliko mwaka huu, kumbuka “Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi.” [Hagai 2:9] Kwa hiyo kwa mujibu wa neno la Bwana hatutakiwi kupungua bali kuzidi na kuongezeka kila siku ili utukufu wa mwisho uwe mkuu kuliko ule wa kwanza. Tunakuomba uzidi kutuombea na kuendelea kufuatilia mambo mbalimbali tutakayoleta kwako kwa ajili ya utukufu wa Bwana.
KWA PAMOJA TUNAKUTAKIA HERI YA KRISMAS NA MWAKA MPYA; 2015 UWE MWAKA WA KUINULIWA KWAKO KWA JINA LA YESU KRISTO ALIYE HAI, UBARIKIWE UINGIAPO NA UTOKAPO, UBARIKIWE MIJINI NA MASHAMBANI.
MUNGU AKUBARIKI, NA WATU WOTE TUSEME “AMINA”
No comments:
Post a Comment