UTANGULIZI
Mpendwa
msomaji wetu, tunapenda kukushukuru kwa moyo wako wa dhati wa kuendelea
kujifunza neno la Mungu kupitia mtandao huu wa Fimbo ya Musa. Napenda
kukutia moyo kuwa kadiri unavyoendelea kufuatilia masomo haya Mungu
atakuwa anafanya vitu visivyo vya kawaida maishani mwako ambavyo hata
watu wengine watakushangaa umewezaje! Tumemwomba Mungu kuwa masomo haya
yawe na “UPAKO” wa kukutoa hatua moja kiroho hadi utukufu wa juu ambao
Mungu amekukusudia. Kama haujapata nafasi ya kusoma masomo yetu
yaliyotangulia tafadhali chukua muda uyasome kwa umakini maana iko
hazina ya pekee ambayo Mungu ameweka ndani ya masomo yote yanayoletwa
kwako kupitia mtandao huu. HALELUYA!
Leo nataka nilete kwako jambo muhimu sana kuhusu maombi ya watakatifu wa Mungu. (Hebu sema “maombi ya watakatifu wa Mungu!”) Jambo hili ni juu ya “Maombi ya Kunena kwa Lugha”.
Kuna
mitazamo tofauti – tofauti miongoni mwa makanisa ya Kikristo juu ya
suala la maombi ya kunena kwa lugha. Wako ambao wanasema hakuna kitu
kama hicho katika maisha ya maombi. Hoja yao inajengwa kwenye msingi
kuwa mtu hawezi kunena kitu asichokifahamu mwenyewe halafu akasema eti
ni Roho Mtakatifu! Wengine wanapinga suala la kunena kwa lugha kwa hoja
kuwa Roho Mtakatifu alipowashukia mitume walinena lugha ambazo watu
waliokuwa wakiwasikiliza walizielewa, (Matendo 2:5-13) sasa kwa nini siku hizi watu wanena kwa lugha lakini wanaowasikiliza hawaelewi?
Sitaki
kutumia somo hili kama njia ya kujibu hoja za watu wanaopinga kunena
kwa lugha, kwa hiyo nitajikita katika kueleza ujumbe wa Roho Mtakatifu
kuhusu maombi ya kunena kwa lugha. Utakapokuwa ukisoma somo hili na
kulifuatilia kwa makini wewe mwenyewe utaona kama kweli kunena kwa lugha
kupo au hakupo.
MSINGI WA KUNENA KWA LUGHA
Kunena
kwa lugha kwa kiingereza ni “speaking in tongues,” maana yake kunena
kwa ndimi tofauti. Kunena kwa lugha kuna misingi yake katika agano la
kale kisha ikaja kuwa dhahiri kwa watu wa agano jipya kupitia ujazo wa
Roho Mtakatifu.
Agano la Kale
Isaya 28:11 inasema:
“La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa lugha nyingine atasema na watu hawa”
Msitari huu kwenye kiingereza unasema hivi; Isaiah 28:11
“For with stammering lips and another tongue, He will speak to this people. (NKJV)”
Nataka tuyaangalie maneno haya “with stammering lips and another tongue” kidogo
halafu ndipo tuendelee mbele. Neno “stammer” kwenye Encarta Dictionary
(2009) limetafsiriwa hivi (nitatoa tafsiri kama ilivyo kwenye kiingereza
kisha nitakueleza maana yake):
|
“ni
hali ya kuongea kwa haraka bila hiari, kwa kurudia-rudia maneno
kunakosabishwa na msukumo mzito wa ndani. (speak with many quick
involuntary hesitations and repetition of consonants or syllables
because of a speech condition or a strong emotion.)”
Kwa
hiyo Isaya alipotoa unabii juu ya kusema kwa midomo ya watu wageni na
kwa lugha nyingine alikuwa anazungumza habari za Mungu kuzungumza na
watu wake kupitia “stammering lips and another tongue.” Mungu aliweka
utaratibu wa kuzungumza na watu wake kupitia njia hii ya kuongea kwa
haraka bila hiari ya anaezungumza na kwa kurudia-rudia maneno kupita
mguso mzito ndani ya mtu huyo (strong emotion).
Sasa linganisha tafsiri hii na kile ambacho wanaonena kwa lugha hufanya. Utagundua kuwa mambo yafuatayo huwa yanawatokea:
- Hujikuta wanazungumza lugha wasiyoifahamu, sawasawa na Isaya 28:11 kuwa atasema na watu hawa kwa midomo ya watu wageni. Jambo hili la kunena lugha usiyoifahamu limetajwa tena katika agano jipya. Matendo 2:4-5, 7-11 inasema:
“4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. 5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu… 7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? 8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? 9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, 10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, 11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”
Biblia
inatufundisha kuwa mitume wote waliokuwa wamejazwa Roho na wakaanza
kunena kwa lugha walikuwa wagalilaya. Lakini walinena lugha zote za watu
waliokuwa wakiwasikiliza. Jambo la kushangaza ni kuwa Biblia haisemi
kuwa mitume walikuwa wakielewa lugha walizokuwa wakizinena ila inasema
watu waliokuwa wanasikiliza ndio walioelewa kuwa kila mtu lugha yake
imenenwa. Ok labda hujanielewa vizuri!
Nasema
hivi; kulikuwa na mitume kumi na wawili waliokuwa wakiomba, na wote
walikuwa wagalilaya. Kwa hiyo kwa hesabu rahisi tu ni kuwa mitume
walikuwa wanafahamu lugha ya kigalilaya na hiyo ndiyo ambayo
wangetegemewa waitumie kwenye maombi yao. Lakini Biblia inasema
waliposhukiwa na Roho, eneo lile walilokuwepo lilikuwa limetembelewa na
watu wa kila taifa duniani ambao walienda kuadhimisha sikukuu ya
Pentekoste. Walokole wengi wanachanganya hapa wakifikiri kuwa Pentekoste
inamaanisha ujazo wa Roho Mtakatifu; haaaaa hapana kabisa. Pentekoste
ilikuwa ni sikukuu ya kiyahudi ambayo watu wa maeneo yote duniani
walikuwa wanakusanyika Yerusalemu kwa ajili ya kuadhimisha sikukuu hiyo.
Sasa
ni katika siku hii watu wa mataifa yote walipokuwa Yerusalemu ndipo
Roho alipowashukia mitume. Walipojazwa walianza kusema kwa lugha
nyingine za watu waliokuwa wamekusanyika pale Yerusalemu. Lugha hizi
mitume hawakuzifahamu wala kuzielewa lakini watu waliokuwa wakisikiliza
ndio waliofahamu kila mmoja wao kuwa na yeye lugha yake imetajwa.
Watu
wengine husema kuwa kama kweli ni Roho kwa nini lugha hizo hazifanani
wakati mnaomba? Hii ni ajabu sana. Hebu tujiuliza swali; kulikuwa na
mitume kumi na wawili waliokuwa wakinena lakini walinena lugha ya kila
taifa duniani. Je, lugha hizo zilikuwa zinafana? Watu kumi na wawili
waliwezaje kusema lugha zote? 1Kor 14:21 “Imeandikwa
katika torati, Nitasema na watu hawa kwa watu wa lugha nyingine, na kwa
midomo ya wageni, wala hata hivyo hawatanisikia, asema Bwana.”
- Hujikuta wakizungumza kwa haraka bila hiari yao na kwa kurudia-rudia maneno. Tumeona maana ya neno “stammering lips” lilotumika kwenye Biblia ya kiingereza kuwa limaanisha hali ya kuzungumza kwa kurudia-rudia na bila hiari, yaani involuntary hesitations and repetition of words.
Ukifuatialia
vizuri watu wanaonena kwa lugha utakuta kuwa kile kinachoitwa
“stammering lips” huwa kinatokea. Utakuta mtu anazungumza maneno kwa
haraka kama vile kafungiwa mota kwenye ulimi na mara nyingi utaona
anongea kwa kurudia-rudia herufi (repetition) kwenye maombi yale na
wakati mwingine huwa kana kwamba ana kigugumizi Fulani (hesitations).
Wakati mwingi watu wanaonena kwa lugha huonekana kuwa kama vichaa kwa
wale wasiolewa habari hizi na wala sio kosa lao maana Paulo anasema
Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini … (1Kor 14:22)
Katika
moja ya tafiti za kisayansi juu ya uhalisia wa kunena kwa lugha
waligundua kuwa mtu anapokuwa akinena kwa lugha ubongo wake unakuwa
umelala na hivyo hakuna kabisa msukumo wa fikra za kibinadamu juu ya
nini atamke na nini aache. Ni maneno yasiyo ya hiari kama jinsi
inavyoelezwa kwenye Isaya 28:11 juu ya “stammering lips”, Mmoja wa
watafiti, Dr. Andrew Newberg, alisema hivi:
“When
they are actually engaged in this whole very intense spiritual practice
their frontal lobes tend to go down in activity. It is very consistent
with the kind of experience they have, because they say that they’re not
in charge. [They say] it’s the voice of God, it’s the spirit of God
that is moving through them,”
Kwa
hiyo ni dhahiri kuwa Isaya alikuwa anazungumza habari za kunena kwa
lugha pale alipotabiri juu ya Mungu kusema na watu kwa ulimi wa watu
wageni na kwa lugha nyingine. Maana tafsiri ya msitari huo imetuonyesha
kuwa kilichokuwa kinazungumzwa na Isaya ndicho kile kinachotokea watu
wanaponena kwa lugha.
Agano Jipya
Ufunuo
wa utabiri wa Isaya unakuja kuwa dhahiri na halisi katika agano jipya.
Katika Marko 16:17 Yesu mwenyewe ndiye aliyeweka msingi wa kunena kwa
lugha. Anasema:
Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya….
Yesu
anasema wale waaminio watasema kwa lugha mpya. Ahaaa kumbe ni suala la
imani. Ikiwa mtu anaamini kuwa amepewa kipawa hiki na Yesu mwenyewe basi
kwake huyo kipawa hiki kinakuwa dhahiri, na kwa yule asiyeamini yeye
ataona kuwa kunena kwa lugha ni ulevi kama wale watu walivyodhani kuwa
mitume wamelewa asubuhi-asubuhi (Matendo 2: 13).
Ukisoma
kitabu cha Matendo ya mitume utaona kuwa kunena kwa Lugha ni ishara
namba moja ya uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu. Okay hebu tuone
mifano michache hapa.
Matendo 2: 1- 4, mitume waliposhukiwa na Roho Mtakatifu kitu cha kwanza walichopewa ni kunena kwa lugha hata kabla hawajaanza kuhubiri. Matendo 10:44 – 46,
Kornelio na wenzake walipoamini tu wakajazwa Roho Mtakatifu na wakaanza
kunena kwa Lugha hata kabla hawajabatizwa. Kama Yesu alivyosema “… hao
waaminio … watasema kwa lugha mpya.” Matendo 19:6, wale wanaume kumi na
wawili walipobatizwa kwa jina la Yesu na Paulo akaweka mikono juu yao
walipokea Roho Mtakatifu na jambo la kwanza ilikuwa ni kunena kwa lugha.
Kwa hiyo ishara ya nje kabisa ya uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu
ni kunena kwa lugha. Katika 2Kor 14:18, Paulo anasema:
Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote
Kwa
hiyo Paulo alikuwa naye akinena kwa lugha tena zaidi ya watu wengine
wote. Najua kuna mtu mwingine ataniuliza kuwa; mbona Yesu hakuwahi
kunena kwa lugha? Ntakujibu swali hili kwenye sehemu inayofuata.
KAZI YA MAOMBI YA KUNENA KWA LUGHA
Katika
kusoma kwangu maandiko nimegundua kuwa kuna kazi kubwa tatu
zinazofanywa na maombi ya kunena kwa lugha. Endelea kuwa nami hapa kwa
umakini zaidi uone.
Kazi ya Kwanza
Kuleta majibu ya maombi juu ya mambo yaliyoko sirini
Isaya 45:3 inasema
“nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.”
Mungu
anazungumza habari ya kumpa mwanawe hazina za gizani na mali
zilizofichwa mahali pa siri. Swali la kujiuliza hapa ni je, huko gizani
ni wapi na huko sirini kuna nini na ni nani aliyeziweka hizo hazina huko
gizani?
Jambo
la kujua ni kuwa Mungu alipomuumba mtu alimwekea kila kitu anachohitaji
kwa ajili ya maisha yake. Hakuna jambo ambalo mwanadamu analihitaji
ambalo Mungu hakumwekea; ndio maana bustani ya Edeni haikupandwa na
Adamu bali ni Mungu aliyeipanda kisha akamweka Adamu aitunze tu. Mwanzo 3:23-24 inatuonesha
kuwa baada ya Adamu kuasi Mungu alimfukuza atoke kwenye bustani ya
Edeni lakini bustani hakuiondoa bali aliweka makerubi wailinde kwa
upanga wa moto.
Swali
la kujiuliza hapa ni kama Mungu alikuwa ameona kuwa Adamu hana chake
tena pale Edeni kwa nini asingeiondoa na bustani? Jibu lake ni kwamba
kila kitu ambacho Adamu alikuwa anakihitaji kwa ajili ya kuishi vizuri
kilikuwa ndani ya Edeni na kama Mungu angeiondoa Edeni basi ingempasa
Mungu amwondoe na Adamu pia. Sasa kilichofanyika ni kuwa Mungu
alibadilisha utaratibu wa Adamu kuvitumia vitu vilivyokuwa Edeni. Badala
ya ule utaratibu wa mwanzo ambao adamu alikuwa huru muda wowote
kuchukua anachokitaka, sasa ilibidi awe anaomba kwa Mungu halafu Mungu
ndiye anamletea. Ndiyo maana utaona Adamu anafukuzwa Edeni kwenye Mwanzo
sura ya tatu halafu wakaanza kuliitia jina la Bwana kwenye Mwanzo sura
ya Nne (Mwanzo 4:26) Kwa
hiyo ilibidi Adamu aliitie jina la Bwana ili aweze kupata mahitaji
yake. Kwa nini? Kwa sababu hazina zake tayari zilikwisha kuwekwa sirini
na zikawa zinalindwa na kerubi. Mungu aliamua kuziweka gizani na sirini
ili kumzuia shetani asije akamdanganya tena Adamu halafu akapoteza
vyote.
Huu
ndio uhalisia wa maisha ya kiroho. Chochote unachokihitaji kwa ajili ya
maisha Mungu amekuwekea tayari, lakini si kila kitu ambacho ni chako
kiko kweupe. Jua wazi kuwa kuna hazina zako nyingi tu ambazo Mungu
ameziweka gizani na anasubiri uliitie jina la Bwana kama Adamu
alivyofanya ndipo upewe. Ndio maana Isaya 45:11 Mungu anatoa utaratibu wa namna ya kuzifikia hizo hazina za gizani. Anasema:
Bwana, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.
Lile
neno “Niulizeni” kwenye kiingereza limetumika neno “ask me” likiwa na
maana ya “niombeni.” Kwa hiyo kwenye msitari wa tatu Mungu anatuambia
kuwa kuna hazina zetu alizotufichia shetani asije akazigusa halafu
kwenye msitari wa 11 anatuita tumwombe juu ya hizo hazina za gizani na
mali zilizofichwa sirini.
Sasa
jambo la kujiuliza hapa ni kuwa; nawezaje kumwomba Mungu juu ya kitu
kilichofichwa na mi sijui kama kipo? Majibu ya swali hili ndiyo
yanayotuleta kwenye point yetu ya maombi ya kunena kwa lugha. Paulo
anasema hivi: 1Kor 14:2
Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.
He he heee!! This is amazing!
Kumbe
kunena kwa lugha hakulengi kusema na watu, bali ni mazungumzo binafsi
kati ya mtu na Mungu juu ya mambo ya siri katika roho yake. Okay, sasa
hapa tunapata kujua kuwa kuna maombi ya siri na maombi ya wazi. Maombi
ya wazi ni yale mnayotaka kujengana kama kanisa la kristo lakini maombi
ya siri yanafanyika ndani ya roho ya mtu kwa njia ya kunena kwa lugha.
Ndio maana Yesu alisema; Mathayo 6:6
Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Yesu
anasema unaposali ingia kwenye chumba chako cha ndani yaani katika
roho, kisha funga mlango maana yake omba kwa jinsi ambayo wengine
hawatasikia yaani kunena kwa lugha; halafu baba yako aonaye sirini maana
yake aliye na hazina zako za gizani atakujazi. Kwa hiyo maombi ya
kunena kwa lugha peke yake ndiyo yenye uwezo wa kuleta majibu ya mambo
yaliyo sirini na yaliyofichika.
Tumewahi
kuomba na dada mmoja huko Arusha na alikuwa amefungwa kwa mapepo na
kila wakati yalikuwa yanamrudia. Siku moja mtu aliyekuwa akituongoza
kwenye maombi yale akapewa ufunuo kuwa siku hiyo tuombe kwa kunena kwa
lugha tu. Aisee haikuchukua muda yule dada akawa ameshafunguka na akawa
mzima kabisa. Wakati mwingine unaweza kuwa unakemea pepo halafu
likanyamaza kimya kabisa kama vile mtu amekufa. Ukiona hivo we
usihangaike sana, ingia kwenye maombi ya kunena kwa lugha halafu utaona.
Ni
maombi ya kunena kwa lugha ndiyo yanayoweza kukupeleka mpaka kwenye
falme za shetani na ukawashinda. Maana Paulo anasema kuna lugha za
wanadamu na za malaika (1Kor 13:1) Tunaponena kwa lugha tunanena
lugha za ulimwengu wa roho kwa ajili ya vitu vya rohoni. Ndio tunatumia
kunena kwa lugha kwenye maombi na sio kwenye mahubiri. Kama unataka
ufaidi vitu vya rohoni omba upewe kunena kwa lugha…. And its simple….
AMINI TU NAYO YATAKUWA YAKO
Kazi ya Pili
Kukujenga na kukuimarisha kiroho
Maisha
ya mwanadamu mara nyingi yametawaliwa na hofu na mashaka kutokana na
vitu mbalimbali. Mashaka haya huwasibu watu hata kwenye maisha yao ya
kiroho. Watu wengi wana mashaka juu ya kujitambulisha kwao kuwa
wameokoka na wengine hawawezi hata kusema Bwana Yesu asifiwe kwa sababu
ya mashaka waliyonayo. Hii inatokana na ukosefu wa nguvu na ujasiri wa
kiroho. Moja ya tiba ya hofu na mshaka ya kiroho ni kunena kwa lugha.
Kunena kwa lugha huleta ujasiri wa Roho Mtakatifu juu ya mtu kwa ajili
ya ushuhuda wa kristo.
1Kor 14:4 inasema “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake;
bali ahutubuye hulijenga kanisa.” Kwa hiyo mwenye kunena kwa lugha
hujijenga nafsi yake katika mambo ya kiroho. Ndio maana akina Petro
kabla ya kujazwa Roho walikuwa na hofu sana na hawakuweza kuitangaza
injili. Lakini pindi tu walipoanza kunena kwa lugha nafsi zao zikatiwa
nguvu na wakaanza kuwahubiria wale wale waliokuwa wakiwasikiliza.
Nataka
nikupe kiu leo ya kutafuta upako wa kunena kwa lugha kama kweli unataka
kuwa imara katika Bwana. Uoga ulionao juu ya injili utapotea kama upepo
siku utakapoanza kunena kwa lugha. Lakini pia suala la kuijenga nafsi
yako kwa kunena kwa lugha linajumuisha vitu zaidi ya kimoja. Mtu
anayenena kwa lugha kweli kweli hata dhambi haina nafasi ndani yake.
Watu wengi leo wamebomoka kiroho kwa sababu hawaneni kwa lugha.
Kazi ya Tatu
Kuomba katika Roho
Liko
somo lingine ambalo Roho amenipa nifundishe juu ya “tofauti ya kuomba
kwa roho na kuomba kwa hisia.” Haya nitakayokueleza hapa yatakuwa kwa
uchache tu lakini chakula kamili juu ya jambo hili fuatilia masomo haya
utaona.
1Kor 14:14 inasema hivi: “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba,
lakini akili zangu hazina matunda.” Huu ndio ukweli kuhusu kunena kwa
lugha. Paulo anasema kuwa nikiomba kwa kunena kwa lugha hakuna suala la
kuhusika kwa akili yangu bali ni roho yangu ndiyo huomba. Nimetangulia
kukueleza utafiti uliofanywa na wanasayansi ambao wamethibitisha kuwa
mtu akiwa kwenye kunena kwa lugha akili zake zinakuwa hazihusiki kabisa,
na ndicho Paulo anachokisema hapa.
Maombi
katika roho hayahusishi akili za mtu bali roho ya mtu ndiyo huwa katika
kuwasiliana katika ulimwengu wa roho. Unaponena kwa lugha unakuwa una
uhakika kabisa unachoomba ni sawa na mapenzi ya Mungu maana akili zako
hazihusiki. Kuna wakati huwa ninaenda kwenye maombi na agenda zangu
mwenyewe lakini nikiisha kumkaribisha Roho Mtakatifu huwa najikuta
nasahau hadi agenda nilizokuwa nazo.
Wakati
fulani Mungu alinionesha jambo ambalo lilikuwa linakuja mbele yangu na
mimi nikawa sitaki lije. Hivyo nikaanza kuwa na maombi ya kukataa jambo
hilo lisitokee lakini kila nilipokuwa nikienda kwenye maombi nilikuwa
ninakamatwa kunena kwa lugha. Mwishowe jambo lile likatokea. Nilipokuwa
najiuliza kwa nini Mungu aliliruhusu wakati mi sikulitaka, rafiki yangu
mmoja akaniuliza “ulikuwa unanena kwa lugha wakati unaombea jambo hilo?”
Nikajibu, “ndiyo.” Kisha akaniambia “wakati unaponena kwa lugha Roho
hubatilisha mapenzi yako na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatendeke.”
TAFUTA UPAKO WA KUNENA KWA LUGHA WEWEEEEE
Ngoja nihitimishe kwa kukupa kile Paulo alichotuambia tufanye maana naona hapa hapanitoshi.
1Kor 14:5, 39 anasema “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha …. Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha.”
HALELUYAAAA
No comments:
Post a Comment