New
NENO
LA SOMO: MATHAYO 6:10
“Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni”
Bwana
wetu Yesu Kristo asifiwe!!!
Ni
kwa neema yake Yesu Kristo tunapata tena nafasi ya kujifunza maandiko
matakatifu ambayo ni uzima wetu. Leo nataka tujifunze jambo moja la msingi sana
katika ukuaji wetu wa kiroho na katika jitihada zetu za kuhakikisha kuwa
tunatimiza kusudi Mungu alilomwekea kila mmoja wetu. Jambo hili ni juu ya
‘kufahamu kiwango cha matokeo ambayo Mungu anayategemea kutoka kwako.’
Tunaposoma
Biblia inatufunulia wazi kuwa kila mtu ambaye Mungu amempa neema ya kuzaliwa na
kuishi hapa duniani liko kusudi ambalo mtu huyo analibeba na ambalo anapaswa
kulitimiza. Kwa mfano, angalia jinsi Bibilia inavyozungumza juu ya Farao,
inasema:
Warumi
9:17 Kwa maana maandiko yasema juu ya
Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa
kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika
nchi yote.
Kwa
hiyo Farao japokuwa aliwatesa Israeli na kuwang’ang’ania utumwani kumbe alikuwa
amewekwa na Mungu kwa kusudi kwamba Mungu apate kudhihirisha nguvu zake na
kwamba jina lake likatangazwe katika nchi yote. Angalia mtu mwingine anayeitwa Bezaleli,
Biblia inasema hivi
Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa
kabila ya Yuda; nami nimemjaza roho ya
Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa
dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora
miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. (Kutoka 31:1-5)
Hapa tunaona kuwa
Mungu alimwita Bezaleli na kumjaza roho yake ili aweze kubuni kazi za ustadi na
kuw fundi wa ujenzi wa hema. Inawezekana kabisa kuwa Bezaleli alikuwa hata
hajulikani katika kusanyiko, lakini Mungu alikuwa amemwandaa tangu mwanzo kwa
ajili ya ujenzi wa hema na wakati ulipofika ikabidi Musa aelezwe juu ya
aliyebeba upako wa ujenzi wa hema.
Lengo kwanza la
somo hili ni kukufahamisha kuwa kuna kusudi ndani yako na ndani ya kila mtu
aliyeko hapa duniani. Inawezekana usijue ni kusudi gani Mungu amekuitia na
inawezekana hujaanza hata kulitumikia hilo kusudi lakini hiyo haimaanishi kuwa
hakuna kusudi la Mungu ndani yako. Nataka uelewe kuwa gharama ambayo Mungu
anaitumia kuhakikisha kuwa unaishi, unakula, unakuwa na afya njema, unafanya
kazi zako unafanikiwa, na mengine mengi ni gharama kubwa sana ambayo Mungu
hawezi kukubali kuilipa bure kama hakuna sababu ya wewe kuendelea kuwepo
duniani. Ndio maana watu wakimaliza kazi waliyopewa na Bwana hapa duniani,
Mungu anawaondoa. Matendo 13: 36 inasema
Kwa maana Daudi, akiisha
kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, ….
Kwa hiyo kama
bado Mungu ameendelea kukuweka hapa duniani jua kuwa bado kuna shauri (kusudi)
la Mungu ndani yako ambalo bado linadai litimizwe na ni hilo ndilo linalomfanya
Mungu aendelee kukuweka hai.
Sasa lengo
langu katika somo hili sio kukuonyesha namna ya kujua kusudi uliloitiwa,
HAPANA. Lengo la somo hili ni kutuka kukujulisha kuwa katika kuishi kwako hapa
duniani kuna “matokeo” fulani ambayo Mungu anasubiria kuyapata kutoka kwako na
matokeo hayo yanakiwango maalumu kilichowekwa na Mungu. Hebu sasa tuliangalie
jambo hili kwa undani wake.
Wanafunzi wa
Yesu walipoomba wafundishwe kusali, Yesu aliwapa sala maalumu tunayoiita “sala
ya Bwana.” Mathayo
6:9-13. Ukiitafakari kwa undani sala hii unagundua kuwa sala hii
iliandikwa kwa lengo la kuweka “mbinu za
kuomba” ndani ya wanafunzi, na mbinu hizi aliziweka katika mpangilio
maalumu. Yale maneno yanayosema “Basi ninyi salini hivi…” yanatupa kujua kuwa
alikuwa hawapi agenda za kuomba ila alikuwa anawafundisha “namna” ya kuomba.
Sasa katika kuwafundisha namna ya kuomba mbinu ya kwanza ilikuwa ni kumtukuza
Mungu na kutambua ukuu wake na ufalme wake katikati ya wanadamu, kama msitari
wa 9 unavyosema.
Msitari wa 10
unaweka mbinu ya pili kwa kusema “Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni.” Sasa maneno “mapenzi yako yatimizwe” yanatupa kujua kuwa
kuna kusudi (purpose) au shauri la Mungu ambalo limewekwa tayari na inabidi
litimizwe. Sasa ile amesema kuwa “yatimizwe” inatupa kujua kuwa kuna mtu
mwingine hapo kati ambaye anatakiwa kwanza ayajue mapenzi hayo ya Mungu, pili
ahakikishe kuwa yanatimia. Ndipo sasa utakuta Biblia ikizungumza hivi kuhusu
Yesu:
Yohana
6: 38-40 Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye
mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka
ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue
siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila
amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho.
Kwa hiyo Yesu
alijua wazi kwa nini alishuka hapa duniani. Anasema “sikushuka ili niyafanye
mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” Kwa hiyo kiufupi ni kuwa
haikuwa suala ya yeye kuamua kuwa afanye nini hapa duniani, kazi yake ilikuwa
ni kuyafahamu mapenzi ya aliyempeleka na kuyatimiza. Na misitari hiyo hapo juu
inatueleza kuwa aliyafahamu vema mapenzi ya Mungu. Kwa kujua hilo ndiyo maana Waebrania
10:9-10 inanena juu yake ikisema:
ndipo aliposema, Tazama,
nimekuja niyafanye mapenzi yako.
Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu
Kristo mara moja tu.
Sasa ukirudi katika ile
sala ya Bwana utagundua kuwa aliposema “mapenzi yako yatimizwe” aliweka pia na
mahali yanapotakiwa kutimizwa, yaani “hapa
duniani.” Kwa hiyo tunafahamu sasa wazi kuwa kuna mapenzi ya Mungu au
kusudi la Mungu ambalo Mungu anataka limitizwe na mahali yanapotakiwa kutimizwa
ni duniani.
Sasa wacha nikwambie
siri moja kuhusu jambo hili. Mungu ni Roho (Yohana 4:24) na dunia asili yake ni
mwili. Sasa vitu vya rohoni haviwezi
kufanya kazi katika ulimwengu wa mwili isipokuwa vimepata umbo la mwili. Ndiyo
maana haikuwezekana Yesu kuja katika umbo la rohoni bali alitwaa mwili akakaa
kwetu tukauona utukufu wa Mungu. Kwa hiyo sasa Mungu anapotaka kutimiza mapenzi
yake katika ulimwengu wa mwili anatafuta mtu katika dunia ili ampe kusudi hilo.
Ndiyo maana sasa ule msitari wa Mathayo
6:10 unasema “mapenzi yako yatimizwe hapa duniani.”
Sasa huyu mtu aliyeko
duniani ni lazima aelewe kuwa kuwepo kwake duniani kunatokana na heshima ambayo
Mungu amempa na kumchagua ili atimize kusudi la Mungu. Si uamuzi wa huyu mtu
kuishi anavyotaka au kufanya chochote anachotaka. Ndiyo maana hata licha ya
Adamu kuishi hapo kwanza katika dunia ambayo haikuwa na dhambi bado Mungu
alimwekea masharti ya namna ya kuishi na nini cha kufanya. Mtu anapoanza kutaka
kuishi kivyake mbali na kusudi alilowekewa na Bwana hapo ndipo anapoanza
kujitenga na Baraka za Mungu na kujikuta akitumbukia katika dhambi.
Ndipo hapo sasa utakuta Waefeso 5:17
ikitusisitiza ikisema: “Kwa sababu hiyo
msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.” Kwa hiyo
kufahamu nini mapenzi ya Mungu kwako ni jambo la muhimu sana, na Mungu mwenyewe
anatualika tumwombe ili tufahamu mapenzi yake maishani mwetu. Isaya 45:11
inasema:
Bwana, Mtakatifu wa
Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize
habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono
yangu; haya! Niagizeni.
Kwa hiyo ni muhimu sana
kuweka utaritibu wa kumuuliza Mungu kuhusu mapenzi yake katika maisha yako.
Utaratibu huu unakusaidia sana namna unavyopeleka maombi yako mbele za Mungu
ili usije ukaomba kinyume na kusudi la Bwana. 1 Yohana 5:14-15 inatuambia hivi:
Na huu ndio ujasiri
tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu
sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia,
tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.
Kwa hiyo kuna kuomba
kitu sawa na mapenzi ya Mungu lakini pia kuna kuomba kinyume na mapenzi ya
Mungu. Ili maombi yako yasikiwe na Mungu basi ni lazima yabebe mapenzi ya Mungu
ndani yake na si mapenzi ya anayeomba. Ndio maana Yesu alipotaka kuomba msalaba
umwepuke alikumbuka kuwa hayo hayakuwa mapenzi ya Mungu na hivo akaruhusu Mungu
atimize yake.
Sasa ukiishajua mapenzi
ya Mungu kwako kinachofuatia ni kuyatimiza na Mungu ndiye anayeweka kiwango cha
namna ya kuyatimiza. Sasa katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu kuna mambo matatu
nataka tuyaangalie.
1. Mapenzi
ya Mungu yanabebwa katika nyakati maalumu ambazo Mungu mwenyewe ameziamuru
Muhubiri 3:1 inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati
kwa kila kusudi chini ya mbingu.” Kwa hiyo Mungu amepangilia kila jambo kwa
kufuata majira yake na kila kusudi la Mungu chini ya mbingu lina wakati wake wa
kutimizwa. Sasa mtu asipojua majira na nyakati ambazo Mungu ameziamuru juu ya
maisha yake anaweza akapishana sana na Baraka za Mungu. Hii ni kwa sababu muda
(nyakati na majira) ndio unaoamua nini kiachiliwe kwako. Sasa ukidai Mungu
akupe kitu fulani yeye anaangalia kwanza nyakati hizo zimebeba nini cha kwako.
Ndio maana alimwambia Habakuki aingojee njozi hata wakati wake ulioamriwa
utakapotimia.
Habakuki 2:2-3
Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao,
ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana
njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia
mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi
kuja, haitakawia.
Kwa hiyo japokuwa Habakuki alipewa
kuona maono ya jambo alilokuwa analalamikia bado jambo hilo halikutokea hapo
hapo kwa sababu wakati wake ulikuwa bado. Watu wengi (hasa vijana) tunakosea
sana katika uhusiano wetu na Mungu kwa sababu ya kushindwa kuelewa ni muda gani
umebeba kusudi gani.
Unaposhindwa kuelewa kusudi lililopo
kwenye muda fulani basi uwe na hakika kuwa mapenzi ya Mungu yaliyokusudiwa
kwenye muda huo hayatatimia. Ukishindwa kuelewa kwa nini Mungu amekuweka sehemu
fulani kwa muda huo ni ngumu sana kuona fursa za kufanikiwa zilizofichwa kwenye
huo muda. Kitabu cha Waefeso 5:16 kinasema
“mkiukomboa
wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.” Msitari
huu kwenye tafsiri ya kiingereza ya New International Version (NIV) inasema:
“…making
the most of every opportunity,
because the days are evil.”
Kwa hiyo Paulo aliposema
“mkiukomboa wakati” alitaka tuelewe kuwa muda ni fursa. Muda ni fursa ambayo
Mungu amempa kila mtu ili aweze kuleta matokeo fulani. Sasa mtu asipoelewa kwa
nini yupo mahali fulani kwenye muda fulani hawezi kuona fursa ambazo muda huo
unampa na hivyo hakuna matokeo yoyote atakayovuna.
Jambo la kujua ni kuwa
kwenye kila muda Mungu anaokupa hapa duniani kuna kusudi aliloweka ndani ya huo
muda na kuna matokeo anayotarajia kuyaona yakizalishwa na mtu husika kwenye
muda huo, ndio maana Paulo alitaka tuenende kwa hekima pale inapokuja suala la
muda kwa sababu ni fursa ambayo Mungu anakupa ili ulete matokeo fulani.
Hebu ngoja tuuangalie
mfano huu aliotoa Bwana Yesu katika Luka 13:6-9
Akanena mfano huu; Mtu
mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda
akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu,
Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate
kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache
mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye,
vema! La, usipozaa, ndipo uukate.
Hebu chunguza kwa makini
hoja ya huyu mtunzaji wa mtini; anasema ‘miaka mitatu hii naja nikitafuta
matunda nisipate.” Hoja ya juu ya kutaka kuukata mtini huu haikutokana na
kutokuzaa tu bali ilitokana na kutokuzaa ndani ya muda ilitegemewa kuzaa. Ndio
maana nakwambia kuwa kwenye kila muda uliopewa yapo matokeo au matunda ambayo
Mungu anatarajia uyazae. Sasa ni kazi yako kuchunguza kama unazaa au umedumaa.
2. Mapenzi
ya Mungu yanatimizwa kwa kufuata viwango alivyoweka Mungu mwenyewe
Sasa turudi kwenye Mathayo 6:10
inasema “Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni.”
Yesu alikua anatufundisha jambo la ajabu sana katika msitari huu. Anasema
mapenzi ya Mungu yanapaswa kutimizwa hapa duniani kama yanavyotimizwa mbinguni. Hili ni jambo zito kidogo. Ni nini
maana ya kusema “kama yanavyotimizwa mbinguni?”
Maana yake ni kuwa
mbingu zinapoachilia kusudi ndani ya mtu huwa pia zinaachilia na kiwango cha
matokeo yanayotegemewa. Sasa kiwango hicho huwa si kwa mujibu wa anayetimiza
kusudi bali kwa mujibu wa aliyetoa kusudi. Okay!! Wacha niseme hivi ukienda
kwenye kiwanda cha kutengeneza magari utakuta kuna watu wanaofanya kazi ya
designing na wengine wanafanya kazi ya kutengeneza. Sasa yule designer ndiye
mwenye kubeba kusudi (picha ya gari inayotakiwa kutokea) na yule mtengenezaji
ni mtimiza kusudi. Sasa huyu mtengenezaji anatakiwa kutengeneza gari kwa
kufuata mapenzi ya designer na kama akifanya tofauti na hapo kazi inakua
imeharibika.
Sasa Mungu ndiye
designer wa maisha ya kila mtu na ndiye anayebeba kusudi la kila mmoja wetu na
mtu ndiye mtimiza kusudi. Sasa ni kazi ya huyu mtu kujua ni aina gani ya kusudi
lipo moyoni mwa designer (Mungu) ili aweze kulitimiza. Asipofanya hivo kazi
inakua imeharibika.
Kwa hiyo tunatakiwa
kutimiza kusudi la Mungu hapa duniani “kama linavyotimizwa huko mbinguni.”
Maana yake lazima ujiulize mbingu zinataka uzalishe kitu gani? Mungu anataka aone
matunda gani kutoka kwako? Matunda hayo yanatakiwa kuzaliwa katika muda gani?
Haya ni mambo ya msingi sana kuyajua kwa sababu yana nafasi kubwa sana katika
kupima kazi yako hapa duniani.
Angalia Ufunuo 22:12
Yesu anavyosema: “Tazama, naja upesi, na
ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila
mtu kama kazi yake ilivyo.” Kwa hiyo kila mtu ana kazi yake na kila mtu
atalipwa ujira wake kwa kadiri alivyotimiza kazi aliyopewa.
Kwa hiyo kila mtu
ameajiriwa na Mungu kwenye kazi maalumu. Unaweza ukasema kivipi. Hebu angalia
hii Ayubu 14: 1-6, msitari wa 5 na 6 unasema:
Kwa kuwa siku zake
zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake
asiyoweza kuipita; Acha kumwangalia yeye, apate kupumzika, Hata atakapoitimiza siku yake, kama aliyeajiriwa.
Ayubu anamtaka kila mtu
aitimize siku yake kama mtu aliyeajiriwa. Kwa hiyo Mungu ametuajiri katika kazi
inayoitwa kutimiza kusudi ndani ya muda tuliopewa na tunatakiwa kutimiza hilo
kwa kufuata viwango vya matokeo Mungu anayotazamia tuyapate.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment