NABII WA BWANA TENA
Utangulizi:
Taifa limetoka katika kufanya tukio la muhimu sana la
uchaguzi, ambapo tumepata rais mpya atakayetuongoza kwa miaka mingine mitano.
Ni jambo jema kupata rais mpya, ingawa watu wametofautiana na kuwepo matukio ya
hapa na pale, kwa mfano kuna taarifa nilisikia magazetini siku moja kuwa kuna
mtu alikata kidole chake alichopakwa wino akisema hakubaliani na matokeo kwani
mgombea wake wa urais aliyemuunga mkono kashindwa. Kanisani pia kumekuwa na
kutofautiana kwa mawazo ambako kumegawa watu. Katika somo hili tutaangalia
baadhi ya mambo ya muhimu ya kuzingatia kama kanisa.
(1Wafalme 22:7-30)
Mfalme Ahabu, alikuwa aende vitani kupigana na mfalme wa
Ashuru ili aichukue Ramoth-Gilead, ambapo aliita manabii zaidi ya mia nne,
ambao kwa pamoja walisema aende tu vitani kwani kila kitu kitakuwa sawa na
atashinda vita. Basi baada ya manabii hao kusema hivyo, aliuliza mfalme
Yehoshafati wa Yuda, akisema
“je, hayupo hapa nabii
wa BWANA tena ili tumwulize yeye?” (msisitizo umeongezwa)
(1fal 22:7)
Ndipo Ahabu akasema yupo nabii mwingine ila
1. Huwa Hanitabirii mema
2. Huwa hatoi unabii wa kufaa
1. Huwa Hanitabirii mema
2. Huwa hatoi unabii wa kufaa
Yule nabii alikuwa akitabiri kabla ya hapo,
lakini alikuwa haneni yale ambayo mfalme alikuwa akiyataka.
Watu wengi wa kanisa hapa nchini hawakuwa
na nia hata ya kuwaza kwamba uchaguzi huu chama tawala kitashinda.
Propaganda zilizokuwa zimewekwa kwenye
vyombo vingi vya habari na magazeti vilikuwa vikiwaaminisha watu kuwa upinzani
mwaka huu una nguvu nyingi sana za kushinda hadi waombaji wakawa hawataki au
hawana ile nguvu ya kuomba kinyume.
Wapendwa wengi walikuwa wamechukuliwa na
upepo wa propaganda hizo katika mawazo yao kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa kuwa
walienda mbele za Mungu wakiwa na vivuli vya majibu kabla Mungu hajatoa majibu
na hata Mungu alipokuwa akijaribu kuwaambia vitu tofauti waliendelea
kung’ang’ania vya kwao.
Ndivyo alivyokuwa mfalme Ahabu, alikuwa
anaenda kumuuliza nabii huku ana majibu ambayo yeye kama yeye anayataka kwanza.
Aina ya manabii kama hawa imekuwapo sana katika kanisa la
leo. Katika suala la uchaguzi uliopita walitokea manabii wengi na wagombea wetu
walikuwa wanawapiga chapuo manabii waliokuwa wanawatabiria mema tu wakashindwa
kuomba mapenzi ya Mungu yatimie.
Kiukweli ni vigumu sana kwa mwombaji pia kukaribisha mapenzi
ya Mungu na kumuombea kwa uaminifu mgombea wa chama ambacho yeye hakipendi na
atajikuta kama asiposimama vizuri akiingiza hisia zake na kuziita ndilo neno la
Bwana.
Ilikuwa ni vigumu sana kwa Ahabu kumkubali Mikaya. Manabii
aina ya Mikaya wapo sana hapa katika kanisa letu la leo. Na watu kama akina
Ahabu pia linao kanisa letu la leo. Lakini mwisho wa siku tunarudi kwenye
kipimo kilekile alichotoa Mungu cha kuwapima manabii wa uongo kama alivyoelekeza
Bwana Akasema
“Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu,
ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine,
nabii yule atakufa. Nawe ukisema
moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena
BWANA? Atakaponena nabii kwa jina la BWANA, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena
BWANA; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope” (Kumb. 18:20-22) (msisitizo umeongezwa).
Kitu ambacho ni kigumu kukielewa katika uchaguzi wa mwaka
huu ni yale madai ya ‘manabii walioshindwa kwenye uchaguzi’, nasema hawa ni
manabii walioshindwa kwenye uchaguzi kwa sababu kwa mujibu wa utabiri wao
alitakiwa aliyeshindwa ndiye awe kiongozi wa nchi yetu lakini haikuwa hivyo.
Sasa manabii hawa wamekwenda mbali hadi kufikia hatua ya
kuwashawishi watu kuomba Mungu toba ili alirehemu taifa kwa kumpata rais ambaye
siye chaguo lake.
Inakuwa vigumu sana kumuelewesha mtu asiyeamini kukubaliana
na mtazamo huu kwamba Mungu hakuwa na nguvu za kutosha kumzuia mwanadamu
kulitimiza kusudi lake.
Mgogoro wa suala hili una ngazi nyingi, siyo mgogoro
unaoishia tu kwenye vyama vya siasa, bali pia hadi kanisa lenyewe limekuwa na
kutokuelewana.
Kanisa linaweza kukutana na kutoa uamuzi wa jumla lakini
kumekuwa na kutofautiana sana hasa kwa baadhi ya sisi waumini na waombaji na
msingi mkuu wa tofauti hizi ni kwamba sisi wenyewe tumekuwa na agenda zetu
binafsi ukiachilia mbali kile ambacho hasa Mungu anataka.
Lazima kwanza tujue sifa za manabii wa aina ya Mikaya kama
ifuatavyo;
Manabii hawa ni wachache sana
Angalia uwiano wa manabii zaidi ya mia nne kwa nabii mmoja
aliyesema kweli.
Manabii hawa hawapendwi na wanapuuzwa
Uzuri wa habari ya Mikaya ni kwamba alikuwa siyo tu
anapuuzwa na mfalme bali pia alikuwa anapuuzwa na walokole wenzie, manabii
wenzake. Kwa hiyo hapa tunajifunza kuwa kuna mambo ya kitaifa ambayo yakitokea
kanisa lenyewe halielewani kwa hiyo hali tuliyo nayo sasa si ngeni kibiblia.
Baada ya kuziona sifa
hizo hapo juu, tunajifunza nini na hali iliyopo sasa?
Hakuna namna ambayo unaweza kumshawishi nabii aliyetabiri
kuwa rais magufuli atashinda aombe toba. Hakuna namna.
Mtu ambaye anaamini kuwa rais aliyepo siye, atafute kwa
Mungu kwanza kujua kwanini rais huyo ameruhusiwa kuwa pale juu.
Kwa sababu mawazo ya Mungu si ya mwanadamu, Mungu lazima awe
na agenda yake katika kumuinua rais aliyeko.
Kwa sababu Mungu hawezi kufanya jambo bila kuwaambia
watumishi wake, lazima manabii hawa waliokosa urais wangeambiwa kabla ya
uchaguzi kwamba Mungu anamtaka fulani lakini kutokana na hila za uchaguzi rais fulani
(mwingine) atapita. Jambo hili halikutakiwa kuwa la kushitukiza (surprise) kwa
waombaji.
Mwombaji wa kweli anapewa taarifa kabla suala lolote
halijatokea. Mwombaji akisha kupewa taarifa ataomba na kujiridhisha kuwa kusudi
la Mungu lazima litokee.
Maswali yafuatayo ataulizwa mtu anayeamini kuwa yaliyotokea siyo
mapenzi ya Mungu
1.
Kwanini Mungu aliruhusu mapenzi yake
yasitimizwe?
2. Kuna mtu ana nguvu zaidi ya kuzuia mapenzi ya Mungu?
3. Kwanini manabii walioutabiria upinzani hawakujua kabla kwamba hizi hila zingetokea ili wazipinge kwa maombi?
4. Wanawapa nafasi gani manabii waliotabiri kinyume nao?
2. Kuna mtu ana nguvu zaidi ya kuzuia mapenzi ya Mungu?
3. Kwanini manabii walioutabiria upinzani hawakujua kabla kwamba hizi hila zingetokea ili wazipinge kwa maombi?
4. Wanawapa nafasi gani manabii waliotabiri kinyume nao?
Kimsingi manabii waliokosa urais walitakiwa kujua kwa sasa
taifa linahitaji nini. Huu siyo wakati wa kanisa kuuaminisha uma kuwa kuna haki
iliibiwa kwani kanisa halitakiwi kutofautiana na serikali(mamlaka), kama
serikali inatafuta amani na usalama kwa kutafuta kuutuliza uma dhidi ya
wapotoshaji wanaodai kuwa kura ziliibiwa, kwanini mtumishi wa Mungu awe dhidi
ya kazi hiyo njema?
Maneno kama hayo ambayo watumishi wa Mungu wenye hasira ya
kushindwa wanayatoa wanataharakisha uma na yanachochea machafuko. Basi tujue tu
kwamba hatukumlingana Mungu vizuri katika kumuuliza kusudi lake, na tunapokuwa
na uhakika kuhusu kile tunachokiamini, basi siyo kitu cha kukisambaza kwenye
mitandao ya kijamii kuuaminisha uma katika mambo ambayo hatuwezi kuyathibitisha.
Chama tawala kina watu wake ambao pia wanamuabudu Mungu
katika roho na kweli, nao wanaomba, nao wanafunga kwa ajili ya hili taifa,
hivyo anayefikiri kuwa ana maono ya Mungu kweli atumie hekima ili asichochee
mambo ya uvunjifu wa amani.
Sidhani kama ni sahihi kwa mtumishi wa Mungu unapoona kuwa
mapenzi ya Mungu hayajatimizwa (hata kama ni kweli) ukaingia moja kwa moja
kwenye mitandao ya kijamii ambako kila mtu hata asiyekuwa na imani kama wewe
anasoma. Wewe ni kuhani wa siri za Kristo ulipaswa kujadiliana na Mungu wako
kwanza kabla hujasema na jamii.
Ashukuriwe Mungu kuwa taifa hili siyo la kifalme na
haliongozwi kwa torati, ingekuwa hivyo wale watu wote waliotabiri kuwa vyama
vya upinzani vingeshinda wangefungwa au hata kuuawa.
Lakini pia tukumbuke habari ya mfalme Nebukadreza aliyewaita
manabii na wafasiri wa ndoto, waliposhindwa aliamuru wauawe,
Hivyo yule nabii aliyemwambia mgombea kuwa atashinda na
hajashinda, ana kesi ya kujibu kwa huyo mgombea. Lakini nchi hii ikiingia
vitani na kuwa na machafuko, manabii na watumishi wa Mungu tunatakiwa
kuwajibishwa maana sisi ndio tunasimama mbele za Bwana. Wewe nabii ambaye
hukujua kuwa taifa litaibiwa kura(kama ni kweli) basi ama hukusimama kwenye
nafasi yako na wewe ndiye wa kulaumiwa au wewe ni nabii wa uongo.
Vinginevyo ni wakati wa kukaa na Mungu na kumuombea rais
aliyeko madarakani, la sivyo tutakuwa tunapingana na mamlaka iliyoamriwa kama
lisemavyo neno la Mungu.
Na pia tukumbuke kuwa hakuna mtu asemaye jambo nalo likawa
ikiwa BWANA hakuliagiza. Maombolezo 3:37
No comments:
Post a Comment