OUR DAILY MANA
JE,
JINA LAKO LINAJULIKANA MBINGUNI?
Karibu tena ndugu yangu
katika Kristo katika sehemu yetu ya Kujifunza maandiko ili tupate kuukulia
wokovu. Leo nina mada iliyo katika mfumo wa swali. Swali hili nahisi ni muhimu
mno kwa mtu yeyote aliye kwenye safari ya kuelekea mbinguni akajiuliza mapema.
Katika utaratibu wa
duniani, mtu anaweza akaenda sehemu hata kama hafahamiki lakini akajitambulisha
na kuelezea alikotoka na kilichomleta, kisha akapokelewa kama vile alikuwa
anafahamika tangu zamani. Huu ni utaratibu mzuri kwa sababu unakupa uhakika wa
kupokelewa sehemu yoyote unayooenda hata kama wewe mwenyewe unajua kuwa
unakokwenda hawakufahamu. Kwa bahati mbaya sana utaratibu wa mbinguni ni
tofauti kabisa na huu tunaotumia hapa duniani. Utaratibu wa mbinguni unataka
mtu awe anafahamika mbinguni tangu akiwa duniani, ili siku akienda wasipoteze
muda kumjua yeye ni nani?
Kilichonisukuma mpaka
kuleta ujumbe huu kwako kinatoka pale Kutoka
33:17.unasema
“Bwana akamwambia
Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.”
Jambo la ajabu
tunalojifunza kutoka kwenye msitari huu ni kuwa Mungu aliamua kufanya kile
ambacho Musa alikuwa ameomba kwa sababu Mungu alimjua jina lake. Kitu cha
kujiuliza hapa ni kuwa kulikuwa na umuhimu gani wa Mungu kumwambia Musa kuwa nakujua jina lako?
Ni ajabu sana kugundua
kuwa licha ya kuwa Mungu alitembea na Musa tangu kabla ya kutoka Misri lakini
anakuja kumtangazia kuwa anamjua jina lake huku mwishoni kabisa mwa kitabu cha
Kutoka. Ni nini Mungu alitaka tuone hapa?
Katika Mathayo 7:21 Yesu anasema “Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba
yangu aliye mbinguni.” Kwa
lugha nyingine Yesu alikuwa anasema kuwa si kila mtu anayelitaja jina Bwana
anajulikana mbinguni,bali ni yule ambaye anayafanya mapenzi ya Baba yetu aliye
mbinguni. Maana yake unaweza kuwa unafikiri unamtumikia Mungu kumbe
unayatumikia mapenzi yako mwenyewe au mapenzi ya wanadamu.
Katika Luka
13: 25-27 Yesu aliwaambia watu akasema
Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi
mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye
atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na
kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.
Hii inatufunulia kujua kuwa kuna kitu zaidi ya kutumika ambacho
ndicho kinachompa mtu nafasi kwenye ufalme wa Mungu. Kitu hicho ni JINA LAKO
KUJULIKANA MBINGUNI. Ndiyo maana Yesu akasema “Wengi wataniambia siku ile,
Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na
kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia
dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” (Mathayo 7: 22-23)
Haya maneno yanatisha sana, hawa ni watu waliokuwa wakimtumikia
Yesu duniani lakini siku ya mwisho anawaambia dhahiri kuwa hawajulikani
mbinguni. Kwa nini? Matendo 13: 36 inatupa
jibu. Inasema: “Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika
kizazi chake, alilala…
Kumbe ni kulitumikia shauri la Mungu ndiko kunakufanya ujulikane
mbinguni. Unaweza kuwa unatumika kumbe unatumikia shauri la mchungaji wako, au
shauri la wazazi wako, au shauri lako mwenyewe. Jiulize kwanza, utumishi
unaofanya unafanya ili kumridhisha nani? Ukiona kuwa unafanya kwa sababu ya mtu
Fulani ujue jina lako halijulikani mbinguni. Lakini pia kuyafanya mapenzi ya
Mungu kunaambatana na kuacha dhambi na kuamua kuwa mwaminifu kwa Bwana. Ukikosa
uaminifu kwa bwana ujue wazi kuwa jina lako halijulikani mbinguni. Unaweza
kusema kuwa unayafanya mapenzi ya Mungu eti kisa unaona Mungu akionekana katika
utumishi wako. Ooooh my friend its more than that. Mungu anaweza kushuka kwenye
huduma lakini asishuke kwako. Huduma inaweza kufanikiwa kupitia wewe lakini
wewe ukawa huna nafasi mbinguni. Ndiyo maana Paulo akasema “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri
wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa. 1 Kor 9:27
Kumbe
unaweza kuwahubiri wengine halafu wewe ukawa mtu wa kukataliwa, yaani ukawa
hujulikani mbinguni. Oooh nakupa shauri leo uhakikishe jina lako limeandikwa
mbinguni.
HAKIKISHA
UNAJULIKANA MBINGUNI
YESU
ANAKUJA UPESI NA UJIRA MKONONI
No comments:
Post a Comment