Friday, October 13, 2017

ADHABU YA AMANI

Mwandishi: Anderson Leng'oko

Isaya 53:5
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Kitabu cha Isaya kinaitwa kitabu cha agano jipya katika agano la kale. Kitabu hiki kinaongelea sana habari za Yesu katika agano la kale kuliko vitabu vingine vyote vya agano la kale. Kitabu cha Isaya kipo katika kundi la vitabu vya kinabii, kwa hivyo maneno mengi yanayoongelewa humo yanatabiri mambo yatakayotokea hapo baadaye. Hivyo hilo suala linaloongelewa hapo juu lilikuwa ni suala la kinabii ambalo lilikuwa halijatokea wakati kitabu kinaandikwa; bali nabii aliona katika Roho mateso ya Bwana Yesu hivyo akawa anayasema kama tulivyoona hapo juu kwenye huo mstari.

Kwa hivyo kabla hatujaendelea natamani tuelewe hapo kuwa ingawa ni katika agano la kale, huo mstari hapo juu unamuhusu Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai. Yesu alikuwa na mambo mengi aliyoyafanya na yaliyotokea katika maisha yake, na hapo huo mstari unaongelea mateso yake aliyoteswa kwa ajili ya dhambi zetu ili sisi tupate kuokolewa.

 Yesu alijeruhiwa na kuteswa ili sisi tupate amani. Kile alichopitia Biblia inakiita ‘adhabu ya amani yetu.’
Adhabu ni nini basi? Adhabu ni kitu anachopewa mtu, au anachofanyiwa mtu pale anapokuwa amekosea.
Je, Yesu alikuwa amefanya kosa gani? Yesu alikuwa hana kosa; alikuwa amethibitishwa kuwa hakuwa ametenda dhambi, wala kosa lolote lililokuwa linasababisha afe/ahukumiwe kufa.

Yohana 19:4
Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake.


Kwa hivyo Yesu, aliadhibiwa pasipo hatia. Ila hapa nataka nikufahamishe kitu ambacho Yesu aliadhibiwa kwacho; nacho ni amani yetu. Yesu aliona kuwa amani yetu isingekuwepo bila yeye kufa msalabani, ndiyo maana aliamua kufa kwa ajili yetu. Kwa kupigwa kwake, sisi tulihakikishiwa amani; na ukiangalia ndani ya amani, kuna furaha, uzima, kuridhika, na burudiko la kudumu. Hivyo vitu havingepatikana kama Yesu asingekufa msalabani.

Maana yake ni nini katika maisha yetu?
Katika haya maisha, kila kitu chema kinauzwa. Ndizi ni tamu na ina virutubisho, inauzwa; sasa ile bei yake, ndiyo adhabu ya amani inayotakiwa kuchukuliwa na yule anayeitaka hiyo ndizi ili apate ile amani ya kuila. Nyama ya kuku kwa mfano, ina uzuri wa ajabu, na kuila nyama hiyo humpa yule alaye amani kwa sababu ya uzuri wake na ushibishaji wake; na pia nyama ya kuku ina virutubisho vingi na ni nyama nyeupe ambayo wataalamu wanasisitiza sana kuwa ndiyo nyama inayofaa kuliwa. Hivyo kuila hiyo nyama humpa amani sana mlaji. Lakini adhabu ya kuila hiyo nyama ni kulipia pesa, alikuja mtu akawa anauza kuku ofisini kwetu, ambapo kuku mmoja aliyeandaliwa akawa anauzwa shilingi elfu nane. Kwa hiyo kula kuku ni amani, ila ili uipate hiyo amani lazima ulipe kwanza hiyo elfu nane. Huko kulipa hiyo elfu nane ndiyo adhabu ya ile amani ya kula kuku; sijui kama tunaelewana.

Tuje kwenye ile elfu nane yenyewe – ili kupata shilingi elfu nane; mtu anatakiwa kufanya kazi, ngumu tena kama ya kutwa nzima hivi. Kama siyo ya kutwa nzima basi mwenye kukupa hiyo elfu nane atahakikisha unafanya kazi nzito inayokuwezesha kustahili kupewa hiyo elfu nane. Kwa hivyo ile elfu nane, ni amani. Ni amani kwa sababu fedha ni jawabu  la mambo yote; kama unataka kujua kuwa fedha ni amani, basi kosa pesa uone utakavyokosa amani. Maana utashindwa kula na hautaweza kufanya lolote.

Sasa tukishaona kuwa pesa ni amani, ile elfu nane, ili uipate unatakiwa ufanye kazi, ile kazi ndiyo inakuwa adhabu ya amani ya kupata pesa! Hii ina maana kuwa hapa duniani, ili upate kitu chochote kizuri ni lazima uteseke; yale mateso yenyewe ndiyo adhabu ya amani yako ya kupata kitu kizuri. Hata amani yenyewe ya moyo au ya nchi, lazima uteseke ili uipate. 

Sisi wenyewe ni mashuhuda wa jinsi babu zetu walivyomwaga damu zao kwa ajili ya kupigania uhuru wa nchi zetu za Afrika; ile amani tuliyoipata na ambayo tunayo hivi sasa ilipatikana kwa tabu, wapo waliopata mateso hadi leo hii sisi tunaishi kwa utulivu na amani hii, na hayo mateso ndiyo ilikuwa adhabu ya amani tuliyonayo sasa; kwa hivyo adhabu ni gharama ambayo mtu anaingia ili kupata kile kitu anachokitamani.

Wanandoa pia wanapata adhabu ya amani ya kuoa. Wanaume wanalipa mahari; hivyo wanapopewa mke wanakuwa wamepewa kitu chema; ambacho ni kitu chenye kuongeza amani katika maisha yao na furaha; lakini adhabu yake ni mahari na matunzo wanayotakiwa kuyatoa kwa hao wake zao.

IJUE HASA AMANI ILIYOLIPIWA NA YESU
Yesu alipata adhabu ili sisi tupate amani. Lakini tunatakiwa kujua ni amani ipi hasa tuliyolipiwa ili tusijetumia zaidi ya kilicholipiwa. Mtu akikulipia maji ya Kilimanjaro ya shilingi elfu moja na mia tano, inabidi uelewe kwamba umelipiwa maji ya elfu moja na mia tano ili usichukue maji ya elfu tatu, kwani ukifanya hivyo, gharama zote zilizozidi itabidi ulipe mwenyewe.

Yesu alipata adhabu ili sisi tuwe huru, tupate mambo ambayo tusingestahili kuyapata kwa nguvu zetu sisi wenyewe; nayo ni pamoja na uzima wa milele na uzima wa hapa duniani. Lakini amani aliyotulipia Yesu ilikuwa na masharti, ambayo ndiyo hasa yanayouwekea mipaka huo ustahili aliotupa Yesu. Mambo kama kuwa na amani katika maisha yetu, furaha na kufanikiwa, ni vitu ambavyo vipo katika yale ambayo Yesu alitulipia pale msalabani.

Alisulubiwa, ili sisi tupone kwani neno linasema kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi tuna haki ya kuwa wazima na ya kutokuugua. Na hiyo haki tunaweza kuidai kutoka kwa Mungu na tukaipata.
Yesu alitupa ushindi dhidi ya nguvu za giza, kwani alimshinda shetani na shetani alishashindwa pale msalabani. Na kama neno lilivyosema kuwa adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, hakuna kitu kingine chochote cha kutukosesha amani kutoka kwa mwovu ibilisi ambacho sisi tunaweza kuumizwa nacho.

Vigezo na masharti
Kama wewe hujampokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na kumtegemea yeye kwa asilimia mia moja, basi amani hiyo haikuhusu. Amani hiyo inamuhusu mtu aliyejikabidhi kwa Bwana Yesu na kumuamini kuwa yeye ni Bwana na mwokozi wa maisha yake siku zote.

Hata hivyo
Bado katika kuwa umempokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako unatakiwa kujua kuwa una uwezo wa kufurahia huduma zote zinazopatikana ndani ya jengo uliloingia – jengo la wokovu, na kama utahitaji huduma yoyote ile iliyo nje ya jengo hilo utatakiwa utoke uende kuichukua inakopatikana na huko uendako unaenda lakini siyo kwa mapenzi ya Mungu.

Ufalme wa Mungu ni package - kifurushi, maisha ya wokovu ni package - kifurushi, kumtumikia Mungu ni kuchagua maisha ambayo ni package - kifurushi. Kifurushi hicho kina mambo yote yanayojitosheleza na mtu aliyechagua hayo maisha anatakiwa kutosheka na maisha yaliyo ndani ya kifurushi hicho na kamwe asitamani kitu kinachopatikana nje ya kifurushi hicho. Kama akitamani kitu kilicho nje ya kifurushi hicho anatakiwa kukumbuka kuwa, ni maisha ya ndani ya kifurushi cha wokovu tu ndiyo yaliyolipiwa kwa gharama za Yesu pale msalabani, huduma nyingine yeyote inayopatikana nje haijalipiwa hivyo ataifuata kwa gharama ya maisha yake- siyo kwa gharama ya maisha ya Yesu tena…
Vitu vilivyo nje vitakuua kama ambavyo ilimgharimu Yesu kufa kwa ajili ya hivi vilivyo ndani.

Amani tuliyolipiwa ni amani inayopatikana ndani ya maisha ya utakatifu
Maisha ya utakatifu ni maisha ambayo ndani yake yana kufuata na kuheshimu utauwa na utakatifu – kutii amri za Mungu. Maisha yoyote yale ambayo hayatii amri za Mungu hata kama yanakupa amani, basi kaa ukijua kuwa amani hiyo haitakuwa ya bure bali utatakiwa kuilipia kwa gharama zako.
Kwa kuvunja amri za Mungu, utakuwa unaishi maisha ambayo hujalipiwa gharama zake na utatakiwa kuzilipia mwenyewe. Pia unapoteza ile haki ya kustahili ulinzi, yaani ile kinga ya kutokuteswa au kutokupigwa inaondoka mara moja (automatically), unapovuka au kukiuka masharti ya kustahili amani aliyotupa Bwana Yesu.

Kwa hivyo unapofanya mambo yaliyo kinyume na amri za Mungu basi unastahili kupata adhabu ya kila amani unayoipata. Ndiyo maana watu tunapatwa na mabaya, kwani tunastahili kupata adhabu ya amani tuliyonayo nje ya Kristo. Watu wengi huwa wanauliza kwamba kama Mungu yupo inakuwaje anaruhusu watu wake wanapatwa na mateso ya aina hiyo wanayopata? Basi jibu ni kwamba watu hao ndio wa kwanza kutafuta amani ambazo hazijalipiwa kwa hivyo ni lazima wazilipie, sasa wakiwa katika kuzilipia, ndiyo maana unaona wengine wanakufa, maana gharama za amani zingine huwa ni mauti, na wengine wananyang’anywa mali na hata wengine kuwa walemavu; kila mtu anapata adhabu inayoendana na amani aliyopata.

Tafuta kuwa na amani iliyolipiwa
Unapotaka kuishi maisha ya amani hapa duniani tafuta kuishi maisha yaliyojaa amani iliyolipiwa na Bwana Yesu pale msalabani. Yesu alitulipia amani ya maisha mema yenye kumtukuza na kumpendeza yeye; na yeye kwa kujua ubaya wa maisha nje yake alikuja duniani ili kutufanya sisi tuishi kwa amani duniani na mbinguni.

Kuishi maisha ya toba
Kama tulivyokwisha ona hapo juu, kuishi maisha ambayo ni ya kuvunja amri za Mungu ni kujipatia amani ambayo haijalipiwa hivyo tunapaswa hata kama hatutaki; kuilipia sisi wenyewe kwa gharama zetu; lakini maisha ya toba hutufanya tusilipe gharama hizo; au kupunguziwa zile adhabu tunazozistahili. Kwa hivyo mtu aliyeokoka akitenda dhambi, bado anaweza kusaidiwa kulipa ile adhabu na Bwana Yesu kama tu, atatubu na kuahidi kuacha dhambi ile. Hivyo wewe unayetenda dhambi, tubu na kugeuka uiache ile dhambi ili ya kale yote yawe yamepita na sasa yageuke kuwa mapya katika maisha yako kwa jina la Yesu.

1Yohana 2:1
Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.




No comments:

Post a Comment