Mwandishi: Anderson Leng'oko
ZIADA YA MSAMARIA MWEMA
Utangulizi
Kwa
neema ya Mungu bado tuna vitu tunavijadili kuhusu kufanya ziada, na leo
tunakijadili kisa maarufu cha Msamaria mwema. Karibu ujifunze nasi, na kama
hujasoma sehemu zilizotangulia na ungependa kupata mtiririko mzuri bonyeza
hapa.
Luka
10:30-35
Mtu mmoja alishuka
toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo,
wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.
Kwa nasibu kuhani
mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.
Na Mlawi vivyo hivyo,
alipofika pale akamwona, akapita kando.
Lakini, Msamaria
mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,
akakaribia, akamfunga
jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake,
akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.
Hata siku ya pili
akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na
cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.
Hii ni hadithi ambayo husomwa na inajulikana sana, inaitwa hadithi
ya Msamaria mwema. Katika historia, watu wa Samaria(wasamaria) na watu wa
Yuda(wayahudi), walikuwa hawapendani kabisa na chuki yao ilifikia hadi hatua ya
kutokupeana hata maji ya kunywa.
Yohana
4:7-9
Akaja mwanamke
Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.
Kwa maana wanafunzi
wake wamekwenda mjini kununua chakula.
Basi yule mwanamke
Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni
mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)
Umeona? Kama hizi jamii mbili zilikuwa hata kupeana maji
hazipeani, maana yake ni kwamba kulikuwa hakuna namna Msamaria angeweza kumkuta
myahudi amepigwa njiani akamsaidia; sanasana angeshangilia kama ilivyo kawaida
ya wengi wetu kushangilia pale adui anapopatwa na jambo baya.
Huyu Msamaria alikuwa haishi kwa kufuata historia wala mkumbo.
Yeye alijua kuwa yule mtu aliyepigwa licha ya kuwa alitoka kwenye jamii
iliyokuwa ni ya adui lakini alikuwa ni mwanadamu kama yeye na alihitaji msaada.
Yeye hakujali ule uadui. Katika hali ya kawaida isingekuwa rahisi
kupuuzia uadui uliokuwapo kati ya Samaria na Uyahudi. Lakini Msamaria huyu
aliona kuwa hakikuwa kikwazo cha yeye kumsaidia huyu mtu.
Mambo kadha wa kadha alifanya Msamaria mwema kwa mtu huyu,
Myahudi:
-
Hakujali kupoteza
muda wake, kwa kawaida mtu unaposafiri unakuwa na bajeti umeipanga ya kutumia
muda. Kama ulikuwa umepanga kusafiri kwa siku tatu, utajitahidi usafiri kwa
siku angalau tatu kamili au basi zipungue ziwe mbili, ili uweze kukutana na
familia yako mapema inavyowezekana. Lakini msamaria huyu hakujali kama alikuwa
anapoteza muda wake kwa kuchelewa kufika kule anakokwenda kwa sababu ya
kumsaidia mtu ambaye kiasilia alikuwa wa jamii ya adui zake.
-
Hakuogopa kuvamiwa na
majambazi. Wengi katika haya maisha tunajua kuwa ukipita katika njia inayotisha
unafanya haraka sana kupita hayo maeneo ili usije ukavamiwa. Ile njia ilikuwa
mbaya sana; ukiwaangalia wataalamu wanasema ilikuwa ni njia yenye milimamilima
na ya kutisha, ilikuwa ni njia ambayo haikuwa salama hata kidogo, kwa hivyo
kila mtu aliyepitia hii njia alikuwa katika mwendo wa kukimbia ili angalau
apite haraka bila kuvuta umakini wa majambazi. Lakini msamaria mwema alipofika
hapa akamkuta mtu amepigwa aliondoa hofu na kuamua kufanya tendo la huruma bila
kujali kuwa na yeye alikuwa anahatarisha usalama wake. Jambo hili lingekuwa
rahisi kama mtu huyu angekuwa anamsaidia ndugu yake labda; lakini ikumbukwe
kuwa msamaria huyu hapa alikuwa anapoteza muda wake kama tulivyoona hapo juu na
pia alikuwa anaweka rehani usalama wake na hata uhai wake kwa kumsaidia adui
yake.
-
Msamaria mwema huyu pia alitumia
vitu vyake vya safari. Biblia inatuambia kuwa msamaria mwema alizitibu zile
jeraha kwa divai na mafuta. Vitu hivi vilikuwa ni vitu ambavyo msamaria mwema
alikuwa amejibebea kwa ajili ya safari na angependa visiishe. Lakini kwa
ukarimu wake alionao, alitumia vitu hivi kumsafishia myahudi vidonda. Hapa
msamaria alikuwa anatoa vyote alivyo navyo kumsaidia adui. Ni jambo adimu sana
katika maisha ya sasa.
- Msamaria mwema pia alitoa fedha
zake. Alikwenda na mgonjwa huyu hadi mjini, akampangishia hoteli kwa gharama
yake na alimkabidhi huyu mtu kwa muhudumu, akampa na yule mhudumu kiasi cha
pesa, ambapo kama kingepungua aliahidi kurudi na kuongezea. Hapa wapendwa
najaribu kuona ni kwa jinsi gani msamaria mwema huyu alijihakikishia usalama wa
safari yake. Huwezi ukasafiri kwa uoga katika safari kama hiyo kwa sababu kwa
hakika Mungu hawezi kukuacha ukaumizwa safarini ukiwa umetenda matendo
yaliyougusa moyo wa Mungu kwa kiwango kikubwa namna hiyo.
- Hapo kumbuka kuwa yule myahudi
aliyesaidiwa alikuwa ana moyo wa shukrani kwa msamaria huyu. Lazima uwe na
uhakika kuwa myahudi yule atamuombea yule msamaria kwa Mungu wake na kumbariki
usiku na mchana; hii itaongeza kiwango cha mafanikio katika safari ya msamaria
huyu. Na msamaria huyu ndani yake kana kwamba alikuwa hajatosheka na
aliyoyatenda, alikuwa bado anataka kurudi ili kumalizia gharama za yule
aliyemhudumia.
- Msamaria mwema pia alikuwa
mfuatiliaji. Watu wengi wanafanya huduma ya Mungu siku hizi lakini wanasahau
kipengele hiki cha ufuatiliaji. Ukisoma hapo utaona kuwa msamaria mwema
aliahidi kurudi na kujua kuwa kiasi gani kimeongezeka katika kumtunza na
kumtibu yule myahudi. Siku moja nilipokuwa nahudumu kupitia door to door,
(kushuhudia injili nyumba kwa nyumba - mitaani), nilimshuhudia dada mmoja na
baada ya kama wiki moja hivi tulirudi kwake tena tukiwa tunamuangalia
anaendeleaje. Ni kweli kuwa mume wa yule dada tulikuwa mwanzoni hatukumkuta,
bali tulimkuta mkewe, mkewe alikuja kumwambia habari zetu, lakini yeye anasema
alidhani sisi ni kama wainjilisti wengine tu aliowazoea ambao huja mara moja na
wakiondoka hawarudi tena. Lakini sisi alitushangaa sana na akamshukuru Mungu
kwa ajili yetu kwa vile tulivyorudi tena kuona anaendeleaje, tulikuwa tumeonesha
upendo mkubwa sana kwake kwa kufanya vile.
Ufuatiliaji
ni jambo la msingi sana katika huduma, ni vyema kufuatilia watu tunaowaleta kwa
Kristo ili tuhakikishe kwamba mbegu tuliyoipanda inamea. Hayo tuliyoyaona hapo
juu ni mambo ya ziada ambayo kama Msamaria mwema akiulizwa na Mungu “Ulifanya
ziada gani?” basi huyu msamaria mwema atayataja mambo hayo hapo juu. Je na wewe
ukiulizwa leo, Unafanya ziada gani, utajibu kitu gani? Tafakari… Unafanya ziada
gani???
No comments:
Post a Comment