Tuesday, August 8, 2017

UNAFANYA ZIADA GANI? (SEHEMU YA TATU)




 Mwandishi: Anderson Leng'oko
 
Utangulizi
Yesu ndiye chanzo cha mafundisho ya kanisa; kila neno tujifunzalo lazima liwe na msingi wake katika mafundisho ya Yesu, kwani yeye ndiye hasa aliyetumwa kuja kuishi ili kwa maisha yake tuone ni kwa namna gani tunaweza kumuishia Mungu. Tuangalie kile Yesu alichokisema kuhusu kufanya ziada ili tuendelee kuona ni uelekeo gani hasa kama kanisa tunatakiwa kuwa nao. 
Kama hukusoma sehemu zilizotangulia katika somo hili bonyeza hapa ili upate mtiririko mzuri.


Tutafakari mistari ya Yesu, kwa undani tukahusianishe na somo hili

Mathayo 5:48
Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Yesu anatamani tuwe wakamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Hii inamaanisha kwamba yale yote ambayo Baba yetu wa mbinguni anayafanya kwa wema wake tunatakiwa kumuiga na kuyafanya vilevile; na hayo yanajumuisha aliyoyataja Yesu ya kuwanyeshea mvua waovu na wema na kuwaangazia jua. Na sisi pia tunatakiwa kuwasaidia na kuwahudumia wakosefu sawasawa na waaminifu na kuwapenda wote pasipo kubagua.


Hii ina maana kuwa hatutakuwa na roho za visasi, wivu, uchungu au kutafuta kuwakomesha watu. Kuna wakati huwa nakutana na watu wanaopenda kushindana na kuonekana wao ndio washindi siku zote. Hilo siyo fungu la Mkristo hata siku moja; mimi huwa naamini kwamba Wakristo tu washindi hata kama wengine hawatatuona hivyo, sisi tu washindi tena zaidi ya washindi, hatuhitaji kupigana vita ambayo ilishapiganwa tayari. Kushindana na mwanadamu ni kujishusha na kupigana na mtumwa wako. Kwa mfano, Mungu wa mbinguni hawezi kupoteza muda wake akibishana na mtu kwamba yeye ni mkuu kuliko mwanadamu; kwani ni ukweli ulio dhahiri kwamba yeye ni mkuu kuliko mwanadamu. Sasa sisi Wakristo huyo aliye mkuu kuliko mwanadamu anakaa ndani yetu; na neno linasema siyo sisi tena, bali ni Kristo aliye ndani yetu;

Wagalatia 2:20 Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.

Kwa hivyo Kristo akishakuwa hai ndani yetu, sisi tunakuwa juu kama Kristo alivyo juu na hivyo tunakuwa washindi kama yeye alivyoshinda. Sasa ile akili ya kimungu inahamia kwetu kwa hivyo tunaanza kuwaona wanadamu wengine wote kama Mungu anavyowaona; ndiyo chanzo cha kuwa wakamilifu kama Mungu baba yetu wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Hii ni kwa sababu Kristo, kwa kuwa kwake ndani yetu anaondoa udhaifu wa kiutu katika fikra zetu na kutufanya tuwe na uimara wa kifikra wa kimungu; kisha tunaanza kuwaza kama Baba yetu wa mbinguni anavyowaza kwa sababu tayari tuna ‘mindset’/ akili za Mungu.

Kwa hivyo akitokea binti mrembo, akili yetu itakuwa inamtazama huyo binti kama Mungu anavyomtazama, tunawaza juu yake kama ambavyo Mungu anamuwazia, na wote tuna uhakika kuwa siku zote Mungu huwawazia mema watu wake, kwa hivyo tukiwa na akili za kimungu tunakuwa tunamuwazia mrembo huyu mema likiwemo suala kuu la wokovu wa roho yake. Haleluya!

Kuwaza kama Mungu ndiko kunakotusaidia kufanya mambo magumu kama kuwasamehe adui zetu. Kuwa na upendo wa kimungu ndani yetu ndiko kutatusaidia kuwa wepesi kuwaombea adui zetu, siyo kwa lengo la kuwafanya waishi muda mrefu ili waone baraka za Mungu maishani mwetu, hapana, bali wasamehewe, waishi maisha ya utakatifu na kumuogopa Mungu kama sisi, ili wabarikiwe na kuifikia toba ya kweli.

Tunapata ziada katika upendo kwa kuwapenda wale wanaotuudhi kama tulivyoona; kuwapenda watu hao ni kuwawazia kama tunavyowawazia tunaowapenda; ndiyo maana ya upendo. Maana ya kuwapenda, ndiyo inayonifanya nisikubaliane na watu wanaosema ombea adui yako aishi siku nyingi ili unapobarikiwa ajionee kwa macho; na pia huwa siungi mkono sana ile dhana ya kupalia watu makaa ya moto. Ninachofanya mimi ni kuwaombea wawe kama mimi; au wawe kama Kristo ili waurithi uzima wa milele, maana natamani kufanya vilevile kwa ninaowapenda kweli na kwa wale ambao kwa kunikosea kwao ilibidi niwachukie. Kufanya vinginevyo hakutakuwa kuwapenda bali ni kuwachukia tu; maana kumpalia mtu makaa ya moto kichwani siyo kumpenda. Na wala kumuombea maisha marefu ili aone unavyobarikiwa siyo kumpenda; bali kumuomba Mungu mtu huyo abarikiwe na kuifikia toba ya kweli ndiyo kumpenda.
Stefano alifanya mfano mwema sana wa jinsi ya kuwatendea adui zako hata kama kitendo wanachofanya kinakuangamiza; yeye akiwa katika kupigwa mawe, na akijua kabisa kwamba kwa kitendo hiki yeye alikuwa anapoteza uhai, aliwaombea wale watu msamaha…
Matendo ya mitume 7:59-60
Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.
Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala.
Huko ndiko kufanya ziada mpendwa, kama tukiwawazia adui zetu kama ambavyo mataifa wengine wanawawazia, sisi Wakristo tutakuwa hatuna tofauti nao. Kama tusipokuwa na ushirika na Roho Mtakatifu kama ambavyo mataifa walivyo; sisi walokole tutakuwa na ziada gani? Kama tusipokuwa waombaji na wafungaji zaidi ya wamataifa, tutakuwa na ziada gani?

Kama wakristo tutaogopa na kuishi kwa hofu kama wasiomwamini Mungu, je, tutakuwa na ziada gani? Mkristo ni mtu ambaye ana ziada; na yuko juu zaidi ya watu wengine wote katika mambo mema yote; na yuko nyuma na hajihusishi na mabaya yote.

Warumi 16:19 Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.


                                           Ziada katika kuona.

Katika kujadili suala hili, tuangalie kidogo jinsi Stefano alivyokuwa anaona;

Matendo ya Mitume 7:55 Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.
Tunakuja kwa kuiangalia mistari hii kugundua mambo aliyokuwa nayo Stefano ambayo wale watesi wake hawakuwa nayo; nayo ni
Kujawa Roho Mtakatifu na
Kuona utukufu wa Mungu.
Katika kujawa na Roho Mtakatifu, Stefano alikuwa na nguvu za kimungu ambazo zilikuwa zinamuwezesha kuona vitu ambavyo wale makutano hawakuwa wanaweza kuviona. Lazima ieleweke hapa kuwa haya mambo yote tuliyojadili na tunayotaka kufanya ya ziada hatuwezi kuyafanya ikiwa hatutakuwa na uwezo wa kufanya ziada; tunaona hapo juu kuwa huyu mtu Stefano, alikuwa na nguvu za Roho Mtakatifu ambazo, kwa kujaa ndani yake ziliondoa uchungu na hasira na kisasi; zikampa unyenyekevu wa kukubali kushindwa na wale watu; akapewa kuwapenda na kuwasamehe wakati uleule, hata asiombe Moto kutoka mbinguni uje uwaangamize, bali aliomba Mungu awasamehe! Hapa tunaona kuwa Stefano alikuwa na nguvu za Roho Mtakatifu ambazo zilimpa kuona vitu ambavyo makutano walikuwa hawavioni. Macho ya Stefano yaliona ushindi, yaliona mbingu zikifunuka; naye akifurahia kule kuacha dunia ya taabu na mateso na kuingia mbinguni kwenye raha na uzima wa milele; hakuona haja ya kuwakandia hawa waliomuwezesha/waliomharakisha kuingia kwenye hiyo raha ya milele zaidi ya kuwaombea!
Ili ufanye ziada lazima uone ziada, uwe na ziada katika kuona, kuwaza na kuwa na malengo.

Lakini kile kimjazacho mtu, ndicho kimtokacho

Mathayo 12:34-35
Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya.
Wapendwa katika Bwana, kila jambo ambalo mtu hulifanya, huwa linaanzia moyoni mwake. Ili mtu afanye mema, atende mema, lazima moyo wake uwe umejaa mambo mema. Hivyo kama ziada yetu tunataka ipatikane katika matendo; lazima ziada hiyo iwepo moyoni kwanza ili iweze kutoka katika uhalisia.
Watu wengi wanashindwa kusamehe kwa sababu mioyo yao imejaa chuki na visasi; ili moyo wako uweze kuachilia lazima uujaze mambo mema na upendo utokao kwa Mungu ambapo utatakiwa kuishi katika mazingira ambayo yanaruhusu au yamejaa mambo mema ili moyo wako ujizoeze katika hayo. Kama unakaa na watu wanaopenda visasi na chuki na fitina lazima moyo wako utaambatana nao na kuwa na tabia hizohizo. Kaa na wenye hekima, wanaoongelea mambo mema na wanaopenda mapatano; nawe utakuwa na uwezo wa kutenda mema na kutenda mema ya ziada.
Jambo hili aliliona Mungu ndiyo maana aliwahimiza wanadamu kulinda sana mioyo yao kuliko yote wayalindayo;

Mithali 4:23 Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
Sasa kwa sababu moyo unalishwa na mazingira, ambapo mazingira ni aina ya watu unaokaa nao na kuishi nao kwa muda mrefu; Biblia hapo imekuelekeza kutafuta na kuwa mchaguaji sana wa watu wa kuwa nao karibu, yaani marafiki; wanasema nioneshe rafiki zako nami nitakwambia tabia yako ‘show me your friends and I will tell you your behavior.’

Mithali 13:20 Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Sababu pekee ambayo ilimfanya mwandishi wa mithali kukusihi uenende na wenye hekima ni kwa sababu alijua moyo wako una tabia ya kuiga na kupenda kila kitu ambacho kinafanywa na watu unaowapenda, moyo unatakiwa kutiwa moyo na kushawishiwa kufanya kitu, na watu wenye kuushawishi moyo wako ni wale wa karibu yako, ulio nao na unaowapenda sana. Yupo mwanamke mmoja labda anakuwa na imani ya dini fulani, ila unashangaa akimpenda mwanaume wa imani nyingine naye yule dada anabadili imani yake na hata kuanza kuikashifu ile imani ya kwanza. Haishii hapo tu, yule mwanamke hujikuta anapenda na vitu vyote vinavyopendwa na huyo mkaka hata kama ni vibaya na vina madhara kwa maisha yake; hivyo ni muhimu sana kuwa makini katika kuchagua marafiki kwa ajili yetu na kwa ajili ya watoto wetu na tunatakiwa sana kumuomba Mungu aingilie kati.

Pamoja na kuepukana na marafiki wabaya, bado unatakiwa kuangalia sana ni vitu gani unavihifadhi moyoni, ili moyo wako usikuangushe katika safari yako ya maisha matakatifu. Uukataze na kuusimamia kwa maana siyo nyakati zote moyo wako utakusapoti katika kumtafuta Mungu na kutenda mema. Na mwongozo mkuu wa nini na nini moyo wako unatakiwa kupenda au kuchukia ni Biblia takatifu; hii itakusaidia kukupa namna ya kuulea na kuusimamia moyo.

Yeremia 17:9 Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

Ili tuweze kufanikiwa katika kutenda mema, basi tuusimamie moyo ili usiote chipukizi/shina la uchungu na kisasi na tamaa mbaya. Tuudhibiti na kuuadibisha kwa utakatifu tukiwa na lengo la kutenda ziada ili tuweze kuurithi uzima wa milele.

Usikose kuendelea na mfululizo huu wa somo hili kwa tafakari zaidi … Unaweza kusambaza ili wengine nao wabarikiwe. Mungu awe nawe.

No comments:

Post a Comment