Thursday, November 20, 2014

Mwanzo Sura ya 3

Mwanzo Sura ya 3

Udanganyifu wa shetani kwa mtu

Sura hii inaanza kwa utambulisho wa ajabu sana kuliko sura mbili zilizotangulia; wakati sura ya 1 na ya 2 zikianza kwa kuonesha uumbaji wa mbingu na nchi na kukamilika kwake, sura ya 3 yenyewe inaanza kwa kumtambulisha kiumbe mmojawapo kati ya viumbe aliowafanya Mungu. Kiumbe huyu anaitwa nyoka sawa na jina alilopewa na Adamu kwenye Mwanzo 2:19-20. Sura hii ya 3 inamtambulisha kiumbe huyu kuwa ni kiumbe aliyekuwa “mwerevu” kuliko wanyama wote wa mwitu aliokuwa amewafanya Bwana Mungu. Kwa hiyo kwa lugha rahisi ni kuwa nyoka ndiye aliyekuwa amewekwa awe juu ya kundi la wanyama wa mwitu na ndio maana alipewa akili kuliko wengine wote.

Kinachoshangaza ni uwezo wa huyu nyoka kuzungumza na mwanamke kwa jinsi ambavyo waliweza kuelewana; hakika hili linahitaji tulichunguze vizuri zaidi. Kwa faida yako msomaji, msitari wa kwanza unasema hivi:

Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?

Hili neno “alikuwa” lililotumika kwenye msitari huu, tafsiri ya kiebrania imetumia neno “hayah” ambalo kwa kiingereza linamaanisha “to become” au “to come into being” ambayo kwa Kiswahili linamaanisha “kufanyika” katika hali fulani. Kwa hiyo Biblia inaposema nyoka alikuwa mwerevu, maana yake alifanyika mwerevu kuliko wanyama wengine wote. Tunataka tuone huku kufanyika alikofanyika kulitoka kwa nani na ni kwa kusudi gani alipata huu werevu. Kabla hatujaenda mbele sana turudi kidogo kwenye uumbaji tuone Mungu alipoumba nyoka nini kilifanyika.

Mwanzo 1:24-25 ndiyo inayohusika na siku nyoka alipoumbwa, inasema hivi:
Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

Nyoka alifanywa kwenye kundi la wanyama wa mwitu (maana ndivyo Mwanzo 3:1 inavyosema) na Mungu alipomfanya nyoka katika kundi hili aliona kuwa ni vyema. Swali tunalojiuliza hapa ni: Je, ule werevu alioutumia nyoka kumdanganya mwanamke alifanywa nao au kuna kufanywa kwingine kulikotokea baadae ambako hakuhusiani na uumbaji wa Mungu? Biblia inajibu vizuri sana swali hili.
Matthew 10:16 Yesu anasema hivi: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua” (msisitizo umeongezwa). Huu msitari unatufunulia kuwa nyoka alipofanywa na Mungu alipewa busara na wala sio werevu. Yesu hakusema iweni ‘werevu’ kama nyoka bali alisema iweni na ‘busara’ kama nyoka. Kwa nini Yesu alitaka tufanane na nyoka kwenye suala la busara na wala sio werevu? Kwa sababu alijua dhahiri kuwa Mungu alipomfanya nyoka hakumfanyia werevu bali alimpa busara ili awe juu ya wanyama wengine wa mwitu kama tulivyotangulia kusema hapo kabla. Ni ile busara aliyofanywa nayo nyoka ndiyo Mungu aliyoiona kuwa “vyema” pale Mwanzo 1:25; huu werevu ulikuwa na chanzo kingine ambacho hakika hakuwa Mungu maana Mungu alimfanya nyoka awe na busara lakini sio werevu.
Neno “mwerevu” lililotumika kumweleza nyoka kwenye Mwanzo 3:1, Biblia za kiingereza zimetumia neno “subtil” au “cunning” kuelezea sifa hii ya nyoka. Sisi tungependa tuichambue sifa hii kwa kulitumia neno “cunning” kama lilivyotumika kwenye tafsiri ya New King James Version. Msitari huu wa Mwanzo 3:1 kwenye tafsiri hii ya NKJV unasomeka hivi:

Now the serpent was more cunning than any beast of the field which the LORD God had made….
Cambridge Advanced learners Dictionary (3rd Edition) wana jambo la kutuonesha kuhusu maana ya neno hili. Wanasema hivi:

Cunning “describes people who are clever at planning something so that they get what they want, especially by tricking other people, or things that are cleverly made for a particular purpose” (msisitizo umeongezwa)

Maana yake ni kuwa neno “cunning” hutumika kuwaelezea watu ambao wako makini sana katika kupanga vitu ili wapate kile wanachokitaka, hasa hasa kwa kuwalaghai (kuwadanganya) watu wengine. Hakika hiki ndicho kilichokuwa ndani ya nyoka; hakutumia busara aliyoumbiwa na Mungu bali alitumia werevu (yaani uwezo wa kupanga vitu ili upate unachokitaka hasa hasa kwa kuwadanganya watu wengine). Nyoka alifanikiwa kupata alichotaka kwa kutumia uongo na ulaghai. Swali tunalojiuliza hapa ni: huu werevu aliutoa wapi?

Tumeona hapo juu kuwa werevu unaozungumzwa kwenye hii Mwanzo 3:1 ulikuwa ni udanganyifu uliopangiliwa sawasawa ambao ulikuwa na lengo fulani maalumu nyuma yake. Kama nyoka alifanikiwa kupata alichotaka kwa kupitia uongo basi ni wazi sasa kuwa nyoka yule hakuwa nyoka wa kawaida, bali alikuwa nyoka ambaye ni baba wa uongo. Katika Yohana 8:44 Yesu anasema hivi:
Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (msisitizo umeongezwa)

Yesu anamtaja Ibilisi kama mwuaji tangu mwanzo na ambaye hajawahi kusimama katika kweli. Kweli ni neno la Mungu; Yesu alisema “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli (Yohana 17:17).” Ikiwa kweli ni neno la Mungu, basi Yesu anaposema kuwa Ibilisi hakusimama katika kweli tangu mwanzo maana yake ni kuwa tangu mwanzo Ibilisi hakuwahi kusimama sawa na neno la Mungu. Hakika hiki ndicho alichofanya kwenye Mwanzo 3:4-5, maana wakati Mungu alisema kuwa mkila matunda ya mti mliozuiliwa mtakufa, nyoka yeye akasema kuwa hakika hamtakufa bali mtakuwa sawa na Mungu.

Huyu nyoka anayejitokeza hapa katika Mwanzo 3:1 hakika alikuwa ni Ibilisi mwenyewe aliyejiingiza tu katika umbo la nyoka. Shetani hakuwa na njia ya kuwasiliana na mtu isipokuwa kwa kutumia moja ya vitu ambavyo mtu mwenyewe alikuwa anavifahamu na amevipa majina yeye mwenyewe tena vimewekwa chini yake. Biblia inatufunulia wazi kujua kuwa yule nyoka aliyezungumza na Hawa alikuwa ni Ibilisi mwenyewe. Ufunuo 12:7-9 unasema hivi:

“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” (msisitizo umeongezwa)

Msitari huu wa Ufunuo unataja kuhusu nyoka wa zamani ambaye kazi yake ni kuudanganya ulimwengu wote; na jina lake anaitwa Ibilisi na Shetani. Hili neno ‘nyoka wa zamani’ halijitokezi sehemu nyingine yoyote ya Biblia isipokuwa katika Ufunuo 12:9 na Ufunuo 20:2. Kwa hiyo matumizi ya neno hili yanatuashiria kuwa hiyo “zamani” inayotajwa ni ile ambayo Yesu anaitaja kama “tangu mwanzo”. Hivyo tunajua sasa kuwa nyoka wa zamani anayetajwa kwenye kitabu cha mwisho cha Biblia ni yule aliyemdanganya Hawa kwenye kitabu cha mwanzo cha Biblia.

Hivyo basi, yule nyoka mwerevu aliyezungumza na Hawa alikuwa ni Ibilisi na Shetani ambaye tu alilitumia umbo la nyoka wa kawaida ili kupata njia ya kumfikia mtu. Kosa la nyoka mwenye busara (yaani nyoka aliyefanywa na Mungu) kuruhusu atumiwe na Ibilisi ili kumwangamiza mtu lilipelekea adhabu kali kwa nyoka halisi na uzao wake wote, kama ambavyo Mungu hamwachi bila adhabu mtu yeyote anayeruhusu atumiwe na shetani katika kuharibu kusudi la Mungu. Shetani ndiye alikuwa mwanzilishi wa uasi na dhambi katika uzao wa mtu. Kuna mbinu alizotumia kulifanikisha hili; acha tuone alivyofanya.

Hatua ya kwanza ilikuwa ni kulitupia wasiwasi neno la Mungu. Hebu sikia anavyosema: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu … (msisitizo umeongezwa).” Mungu alikuwa ameshasema na ametoa amri yake bila kuficha kitu, alikuwa wazi kabisa kuwa “walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika (Mwanzo 2:17).” Ibilisi alitaka kuharibu kweli ya Mungu kwa kujaribu kujifanya kama hakusikia vizuri, hivyo akaleta uongo wake kwa njia ya swali ili asigundulike mapema. Kitu cha ajabu ni kuwa hakujipeleka kwa mwanaume na huu ujanja wake bali alimwendea mwanamke. Kwa nini alifanya hivi?

Utagundua kuwa Mungu alipokuwa anatoa agizo la kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya mwanamke alikuwa bado hajafanywa. Agizo hili lilitolewa katika Mwanzo 2:17 na mwanamke alifanywa rasmi katika Mwanzo 2:22; kwa hiyo ni wazi kuwa Hawa alijifunza agizo hili kutoka kwa Adamu, maana hatuoni Mungu akilirudia tena baada ya Hawa kufanywa. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa Adamu alikuwa na uelewa mzuri zaidi wa neno la Mungu kuhusu agizo hili kuliko hawa, na shetani alijua hilo hivyo akachagua kutumia kiungo kilicho dhaifu ili kupenyeza uasi. Biblia iko wazi kabisa kuhusu hili jambo; Paulo anasema hivi:

“Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo” (msisitizo umeongezwa) (2 Kor 11:3). Soma pia 1 Timotheo 2:14.

Kwa hiyo aliyedanganywa hakuwa Adamu bali Hawa, na kudanganywa kwake kulitokana na shetani kujua kuwa Hawa hakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya kile Mungu alichokuwa ameagiza. Lilikuwa jukumu la Adamu kumlinda mkewe na kumjulisha kweli ya Mungu jinsi ilivyokuwa. Inawezekana kuwa Adamu alimfundisha sawasawa ila Hawa ndo akajichanganya au Adamu ndiye hakumfundisha mkewe sawasawa. Maana utakuta majibu ya Hawa kuhusu kile Mungu alichosema yakitofautiana kabisa na kile Mungu alichoagiza. Mungu alisema kuwa “msile” lakini hawa anasema wameambiwa “msile wala msiguse”. Hakuna mahali ambapo Mungu alitoa agizo la ‘msiguse’. Hii ilitokana na ufahamu mdogo aliokuwa nao Hawa juu ya neno la Mungu. Ni rahisi sana kuingia kwenye mtego wa shetani ikiwa hauna neno la Mungu la kutosha ndani yako. (Fimbo ya Musa Ministry tunaandika kitabu kuhusu hila za shetani katika kanisa, ndani yake tunaeleza vizuri zaidi jinsi ambavyo kutokufahamu neno la Mungu kunavyompa shetani nafasi nzuri ya kukudanganya na kukushinda; tutawajulisha kikiwa tayari).

Shetani ili apenyeze uharibifu wake kwenye jamii au kanisa daima anatafuta nani aliye dhaifu ili amtumie. Akiishapata mtu aliye dhaifu basi ni rahisi sana kuwashambulia walio imara kwa sababu anakuwa tayari ameingia katikati yao kupitia yule mtu dhaifu. Udhaifu wa Hawa ulimpa shetani nafasi ya kumpoteza hadi Adamu ambaye alikuwa imara. Vivyo hivyo kwenye makanisa na sehemu za ibada shetani huwa anatafuta ni nani kati yenu ni dhaifu; akiishampata huyo basi humtumia yeye kuwamaliza wengine walio imara. Ndiyo maana ni muhimu sana kuimarishana kiroho kwa sababu udhaifu wa wenzako unaweza kutumiwa na shetani kukupoteza wewe uliye imara. Usifurahi hata kidogo kuona watu unaofanya nao huduma au watu wa kanisani wanakutegemea wewe tu kwa mambo yote ya kiroho; hii ni hatari kwako maana shetani akipata mpenyo kati yao inakuwa kwake ni njia ya kukufikia na wewe kirahisi zaidi. Kama unaona kuwa Mungu amekupa neema ya kuwa na ufahamu wa neno la Mungu na mambo ya kiroho zaidi ya wenzako basi jitahidi kuwaimarisha na wenzako ili nao wawe msaada kwako wakati utakapokuwa umepungukiwa nguvu. Hiki ndicho Yesu alichomwagiza Petro baada ya kumwombea; alisema:

… Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.” (msisitizo umeongezwa) [Luka 22:31-32].

Katika jibu lake kwa shetani Hawa aliongeza kitu ambacho hakikuwepo kwenye neno la Mungu. Biblia iko wazi kabisa kuwa kuongeza neno au kupunguza neno kwenye maneno ya Mungu ni kosa kubwa linalostahili adhabu (Ufunuo 22:18-19). Kwa hiyo si ajabu kuwa adhabu ya mwanamke ilikuwa chungu mno kuliko ya mwanaume kwa sababu ya kosa la kuongeza kwenye maneno ya Mungu. Ni vema sana kulishika neno la Mungu kwa usahihi na kama lilivyo bila kuongeza yako au kupunguza.

Ile kuongeza neno kwenye maneno ya Mungu kulimpa shetani kujua kuwa Hawa alikuwa ni njia rahisi ya kupenyeza uovu wake. Hatua ya pili sasa ilikuwa ni kulikataa kabisa neno la Mungu. Katika msitari wa 4 shetani anasema hivi: “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa.” (msisitizo umeongezwa) Hii ni ajabu sana, Mungu alikuwa ametangaza na ameweka wazi kabisa kuwa ikiwa mtu atajiingiza katika kulihalifu agizo la Mungu na kuasi kwa kula matunda ya mti aliokatazwa hakika atakufa. Shetani anainuka na kulikana waziwazi hili neno la Mungu na kusema “hakika hamtakufa.”

Ni kazi ya shetani kulipindua neno la Mungu kwa uongo na kuwapoteza watu wa Mungu. Leo hii tunasikia imani na makanisa kadhaa yakiibuka na kutoa mafundisho ambayo ni kinyume kabisa na neno la Mungu. Kwa mfano, Mungu ameagiza wazi kabisa kuwa mtu yeyote atendaye dhambi ataangamizwa katika jehanamu ya moto, lakini wapo watu wanaosema kuwa Mungu hawezi kumwumba mtu halafu akamtesa tena kwa moto hata kama mtu huyo amekosea vipi. Ni shetani yule yule aliyepindua kweli ya Mungu na kumdanganya Hawa ndiye anaendelea kuwadanganya watu kuwa jehanamu ya moto haipo ili watu waendelee kutenda dhambi. Ndugu msomaji wetu tunapenda kukufahamisha kuwa Mungu wetu hushika daima neno lake wala hataacha kuadhibu kwa hasira kali na ghadhabu wale wote watakaofuata udanganyifu wa Ibilisi na kuicha kweli halisi ya Mungu.

Kosa la kutaka kuwa kama Mungu

Katika msitari wa 5 shetani anaendeleza hila zake kwa kusema: “Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Shetani aliamua kuhalalisha uongo wake kwa kumwambia Hawa kuwa Mungu alikuwa amewazuia wasile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya kwa sababu alikuwa hataki wawe kama yeye [Mungu] wakijua mema na mabaya. Fahari ya nje ndiyo aliyokuwa anataka kuwaonyesha pale bustanini ili aharibu uhusiano wao na Mungu.

Kwa kujua mema na mabaya mtu angekuwa kama Mungu, japokuwa asingefikia kiwango cha kuitwa Mungu, lakini angefanikiwa kuwa kiumbe anayejitegemea na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi yake mwenyewe. Hatua hii ilikuwa na madhara makubwa sana kwa sababu badala ya mtu kuwa mwakilishi wa Mungu katika sura na mfano wa Mungu sasa alitaka awe na uwezo wake yeye mwenyewe. Hii ilimuondolea uwezo wa kumpinga shetani tangu hapo hadi pale Yesu alipokuja kumnyang’anya shetani na kuturudishia tena uwezo huo kwa gharama kubwa ya damu yake.

Tamaa ya ujuzi wa mema na mabaya na kutaka kuwa kama Mungu ndivyo vilivyomwondolea mtu uwezo wake wa ki-Mungu aliokuwa amepewa na muumba wake. Ni kweli angepata kujua mema na mabaya lakini asingepata nguvu ya kuzuia mabaya ili apate mema tu. Na matokeo yake alikosa mema akawa mtumwa wa mabaya. Katika Yohana 8:34 Yesu alisema hivi: “…Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.” Dhambi ya kuasi agizo la Mungu haikuwa na nguvu ya kumpa mtu uwezo wa kuwa huru tena, bali ilimweka awe mtumwa wa hiyo dhambi daima.

Vivyo hivyo watu wote wanaofanya dhambi huwa watumwa wa hiyo dhambi. Hata kama mtu alifanya dhambi kwa kujaribu, dhambi ile huwa haimwachi awe huru tena bali humfanya mtumwa ikimtumikisha katika tamaa na uasi kila siku. Ni katika damu ya Yesu peke yake na kuamua kuokoka ndipo mtu huwekwa huru tena mbali na dhambi wala dhambi haina nguvu tena kwao walio katika Kristo Yesu, kwa kuwa “Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli (Yohana 8:36).”
Mtego wa shetani ulikuwa umesukwa kiwerevu sana maana msitari wa 6 unasema

“Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” (msisitizo umeongezwa)

Shetani alichagua kumdanganya mtu kupitia mti ambao ulikuwa una mvuto kwa mambo ya mwili. Ulikuwa ni mti wa “kupendeza” na “wa kutamanika.” Lakini shetani anasema kuwa mti ule ulikuwa pia unavutia kwa ajili ya kuwa kama Mungu. 1 Yohana 2:15-16 inasema:

“Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.” (msisitizo umeongezwa)

Yohana anasema tamaa ya mwili, tamaa ya macho, na kiburi cha uzima havitokani na Mungu bali na dunia. Ndicho kilichowapata Adamu na Hawa, maana waliingiwa na tamaa ya macho, tamaa ya mwili, na tamaa ya utukufu wa kutaka kuwa kama Mungu (kiburi cha uzima) ambavyo vyote havikutoka kwa Mungu bali vilitoka katika dunia. Mvuto wa haya mambo ya dunia ulimshinda mwanamke kiasi ambacho aliamua kufanya tofauti na Mungu alivyoagiza; alitwaa matunda aliyozuiliwa akala, kisha akampa na mumewe ambaye naye kwa kusahau nafasi yake kama kichwa cha mkewe alikubali mkewe amuongoze, naye akaingia katika kuasi.

Shetani hutumia vitu vya dunia ambavyo vina mvuto kwa macho na kutamanika kwa mwili ili apate nafasi ya kumwingiza mtu dhambini. Mara nyingi amekuwa akimtumia mwanamke kama mlango wa kupitia, na hii inatokana na wanawake wengi kupenda vitu vya dunia kuliko vitu vya Mungu. Ndio maana utaona mambo mengi yenye mvuto katika dunia hii, kama mavazi, vito vya thamani n.k. huwahusu wanawake. Tamaa ya vitu vya dunia ilimwingiza Hawa katika kuasi naye akamwingiza mumewe katika dhambi. Ni vizuri kwa wanawake kuwa makini sana na vitu vya dunia hii hata kama vina mvuto mkubwa kiasi gani, na ni vizuri pia kwa wanaume kuchunguza kwanza uamuzi unaofanywa na wake zao kabla hawajaamua kuwafuata. Maana uzembe wa Adamu, kama kichwa cha mkewe, ulimwingiza katika uasi wa daima.

Matokeo ya uasi

Baada ya kuasi agizo la Mungu, sasa mtu alikuwa mwenye dhambi katika hali ya uasi. Msitari wa 7 unatuambia kuwa sasa macho yake yalifumbuliwa akajua kuwa yu uchi. Elimu ya ujuzi wa mema na mabaya aliyoipata kutoka katika ule mti sasa ilimwelekeza kwamba kuwa uchi ni jambo baya hivyo akatafuta namna ya kusitiri ubaya huo. Kutokana na ukweli kuwa ujuzi wa mema na mabaya walioupata haukuwa na nguvu za kuwasaidia kuyashinda mabaya ili wapate mema, sasa mtu alijikuta akitafuta njia zake mwenyewe za kuuficha ubaya wake ambao hata yeye alikuwa akiuona.

Ndivyo ilivyo siku zote; mtu yeyote akianguka dhambini huwa anafahamu kuwa nimefanya dhambi ila kwa sababu ya utumwa wa ile dhambi huwa hakumbuki kumtafuta muumba wake bali huwa kwanza anatafuta namna ya kuuficha uovu wake ili usijulikane. Bahati mbaya kwa Adamu na mkewe ilikuwa ni kuwa hapakuwa na mahali pa kujificha mbali ambapo Mungu asingewaona. Uovu wao uliwapelekea kujificha sasa kwa kutumia majani ya miti ya bustani ile ile ambayo Mungu aliwapa iwe baraka yao. Sasa waligueza baraka ya Mungu kuwa laana ya kuficha uovu wao. Bahati mbaya sana ni kuwa hata njia yao ya kuficha uovu wao haikuwa ya uhakika, maana walishona majani ya mtini ili kutengeneza nguo. Kwa wale wanaoufahamu mtini wanajua hakika kuwa majani ya mtini ni membamba na laini sana kiasi kwamba ni rahisi sana kuharibika. Hii ni kweli kabisa kuwa nguo walizojifanyia ili kuficha uchi wao hazikuweza kuwasaidia maana utakuta kwenye msitari wa 10 Adamu akikiri kuwa “mimi ni uchi.”

Msitari wa 8 unatuambia jambo jingine alilofanya Adamu na mkewe baada ya uasi wao; walimsikia Mungu akitembea bustanini kisha wakaamua kujificha ili Mungu asiwaone. Walidhani kuwa wanaweza kumficha Mungu uovu walioufanya, kama ambavyo watu wengi wakishafanya dhambi badala ya kurudi kwa Mungu kwa toba, wanaamua kwenda kujificha wakidhani kuwa Mungu hawaoni. Biblia inasema hivi:

“Ole wao wanaojitahidi kumficha Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?” (msisitizo umeongezwa) [Isaya 29:15]

Adamu na mkewe walifikiri wanaweza kumficha Mungu matendo yao ya giza; yawezekana walisema mioyoni mwao kuwa “tujifiche maana Mungu hakutuona kuwa tu uchi.” Lakini kilichowapata ni kile kilichonenwa na Nabii Ezekieli kuwa:

“Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misunobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo wote uliofanana naye kwa uzuri. Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu. Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake; mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake.” [Ezekieli 31:8-11] (msisitizo umeongezwa).

Licha ya Adamu kutafuta kujificha kwenye miti ya bustani ya Mungu, Biblia inasema miti ile ya bustani haikuweza kumficha. Ezekieli anasema kuwa kabla ya uasi wake, Adamu alikuwa mzuri mno kiasi kwamba miti yote ya Edeni ilimwonea wivu, lakini kwa kuwa moyo wake uliinuka kwa urefu na kutaka kuwa kama Mungu, basi Mungu alimfukuza kwa sababu ya uovu wake (Mwanzo 3:24). Maneno haya yanatufundisha kuwa hakuna namna ambavyo unaweza kuuficha uovu wako mbali na Mungu. Hata vitu utakavyotaka vikufiche navyo havitakubali uovu wako bali vitakufichua.

Mungu kumtafuta mtu wake

Msitari wa 9 wa sura hii ya 3 unamuonesha Mungu akiwa katika harakati za kumtafuta mtu wake aliyeanguka dhambini na kuamua kuenda kujificha ili muumba wake asimuone. Dhambi ya Adamu ilimnyima ujasiri wa kusogea tena uweponi mwa Mungu na kusimama mbele za muumba wake. Katika hali hiyo Mungu angeweza kumwacha tu Adamu na mkewe katika dhambi yao au hata kuwaangamiza kabisa. Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake na wingi wa rehema zake kwa mtu wake; anaenda kumtafuta huko alikojificha. Kwa sababu ya kujificha kwake Adamu alipoteza nafasi aliyokuwa amewekwa na Mungu hivyo tunaona sasa swali la kwanza la kitabu cha Agano la Kale ikiwa ni Mungu akimtafuta mtu wake. Swali la kwanza kabisa la Biblia ni Mungu akisema “Uko wapi?”

Tangu kuulizwa kwa hili swali la “uko wapi,” kitabu chote cha Agano la Kale kinajaribu kujibu hili swali bila mafanikio. Adamu alijaribu kujibu kwa kujitetea lakini katika harakati za kujitetea kwake akajikuta akiufunua uovu wake; akasema “mimi ni uchi.” Vitabu vyote vya agano la kale vinaonesha maisha ya mtu akijaribu kujitetea juu ya mahali alipo lakini hakufanikiwa kumgeukia Mungu na kutembea nae sawasawa. Tunapofika mwisho wa Agano la Kale tunakuta kitabu cha Malaki kikionesha jinsi mtu alivyoshindwa kujirudisha kwenye nafasi aliyokuwa amepewa na Mungu, na kitabu hiki kinaishia na kuonesha jinsi Mungu alivyokuwa amechoshwa na kujificha kwa mtu wake. Maneno ya mwisho ya Agano la Kale ni Mungu akisema “… nisije nikaipiga dunia kwa laana.” [Malaki 4:6] Utaratibu wa Mungu kumtafuta mtu wake kwenye Agano la Kale haukuweza kumtengeneza mtu arudi kwenye nafasi aliyoumbiwa, kila mara mtu alirudi kwenye uasi na dhambi, hivyo Mungu anamaliza Agano la Kale kwa kutaja laana.

Tunaanza kitabu cha Agano Jipya kwa kukuta jambo la tofauti sana. Swali la kwanza linalojitokeza kwenye Agano Jipya ni watu wakimtafuta Mungu badala ya Mungu kuwatafuta watu kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale. Utakuta swali la kwanza la Agano Jipya likisema “Yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi?” (msisitizo umeongezwa)

Wakati swali la kwanza la Agano la Kale alikuwa ni Mungu akimtafuta mtu wake kwa kusema “Uko wapi?” swali la kwanza la Agano Jipya ni watu wakimtafuta Mungu kwa kusema “Yuko wapi?” Kitabu chote cha Agano Jipya kinajaribu kujibu swali hili la watu kusema “yuko wapi… mfalme wa wayahudi”, na tunakuta mwisho wa kitabu hiki cha Agano Jipya Yesu akijifunua kwa watu wake na kuwakaribisha kwake. Utakuta Ufunuo 22:13 Yesu akisema “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.” Halafu katika Ufunuo 22:20 anamalizia kwa kusema “Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu”

Hii inatufunulia kuwa baada ya mtu kumwasi Mungu mpango wa wokovu wake haukuwa ndani ya mwingine yeyote isipokuwa katika Yesu Kristo. Pia tunagundua kuwa suala la kuokoka na kuachana na dhambi limo katika uamuzi wa mtu mwenyewe anapoamua kumtafuta na kumrudia muumba wake. Mungu aliamua kumtafuta Adamu wakati ambao Adamu alikuwa hajaamua kumrudia muumba wake, na matokeo yake tunaona maisha yote ya Agano la Kale yakiishia na laana. Lakini Agano Jipya linatufunulia kuwa pindi mtu anapoamua kumtafuta muumba wake aliko, basi Mungu huwa anajifunua kwake na mwisho wake ni maisha ya ushindi. Ndugu msomaji wetu tunapenda ujue leo kuwa suala la kubadili mwenendo wako na kumrudia Mungu liko mikononi mwako na Mungu alishafanya sehemu yake kwa kumtoa mwana wake pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele (Yohana 3:16). Kama bado unaishi katika dhambi chukua uamuzi leo wa kumpa Yesu maisha yako ili uanze kuishi tena kwenye bustani ambayo Mungu alikuwekea.

Lawama za mtu kwa Mungu wake

Baada ya Adamu kukiri kuwa yu uchi, Mungu, kwenye msitari wa 11 anamuuliza Adamu kuwa umejuaje kwamba u uchi, je umekula matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Katika kujibu swali hili Adamu anamrushia Mungu lawama juu ya kosa alilofanya; anasema:

“Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.”
Ni kama vile Adamu alikuwa anamwambia Mungu kuwa ‘kama usingenipa huyo mwanamke awe pamoja nami basi haya yote yasingetokea.’ Mungu hakumuuliza Hawa moja kwa moja swali hili japokuwa alijua kuwa Hawa ndiye aliyekuwa wa kwanza kula matunda ya mti waliokatazwa. Hii ilitokana na ukweli kwamba Mungu alikuwa amemweka Adamu ndiye awe kichwa cha mkewe hivyo alitakiwa ndiye awe wa kwanza kuwajibishwa kwa kila litakalotendeka kati yao. Adamu akijua hilo, akaamua amrushie Hawa lawama lakini kwa upande mwingine akamlaumu na Mungu kwa kumpa huyo mke awe pamoja nae.

Katika kisa hiki siri ya uasi wa mtu kwa mara nyingine inafichuliwa. Mtu akifanya dhambi au kosa fulani, basi kama hatakana kosa hilo au dhambi hiyo, atatafuta mtu wa kumtupia lawama na ikiwezekana hata kumlaumu Mungu. Tumesikia mara nyingi watu wakifanya dhambi na kusingizia kuwa shetani alinipitia. Wengine wamekuwa wakisingizia hali za maisha, na wengine hata kumlaumu Mungu wao kuwa kama angewatetea wasingeanguka katika uasi huo. Hii haijaanza leo, ilianzia kwa Adamu ambaye ndiye aliyefungua mlango wa dhambi kuingia.

Baada ya kutoka kwa Adamu swali lililofuatia lilimhusu Hawa. Mungu alimuuliza ni nini hili ulilofanya? Hawa hakuulizwa “uko wapi?” kama Adamu alivyoulizwa bali alihojiwa kuhusu kosa alilokuwa amefanya. Swali la ‘uko wapi?’ lililenga kuonesha kuwa Adamu alikuwa ametoka kwenye nafasi aliyokuwa amepewa na Mungu. Hawa hakuulizwa swali hili kwa sababu Hawa alipofanywa na kuletwa kwa Adamu, usitawi wake ndani ya ile bustani ulitegemea nafasi aliyokuwa nayo Adamu. Hawa hakupewa nafasi ya peke yake mle bustanini bali alipelekwa kwa Adamu ili awe msaidizi. Msaidizi hufanya kazi kulingana na nafasi mkuu wake aliyonayo. Nafasi ya Hawa pale Edeni ilitegemea sana Adamu yuko wapi. Kwa hiyo Mungu alipokuta Adamu yuko nje ya nafasi haikumsumbua kuuliza Hawa yuko wapi. Kama mme ndo kichwa cha familia basi nafasi ya mke hutegemea sana mme wake yuko wapi. Ndiyo maana wanawake wengi wanaoolewa na wanaume walevi au wapenda anasa nao hujikuta wamekuwa hivyo kwa sababu ya nafasi ya waume zao.

Hawa alipoulizwa ‘ni nini hili ulilolifanya?’ jibu lake nae halikutofautiana sana na lile la mume wake; naye aligeuzia lawama kwa nyoka kuwa ndiye aliyenidanganya. Ni kweli kuwa nyoka alikuwa amemdanganya lakini swali la Mungu halikuuliza kuwa ni nani aliyekwambia kula, Mungu aliuliza ni nini hili ulilolifanya? Lakini Hawa kwa kutaka kukwepa kuwajibishwa, akamgeuzia nyoka lawama. Cha ajabu ni kuwa nyoka hakuulizwa swali lolote na Mungu kama ilivyokuwa kwa wengine, alipogeukiwa yeye ilikuwa ni kutangaziwa adhabu tu.

Adhabu ya Mungu juu ya uasi

Maneno ya Mungu katika msitari wa 14 yanatoa adhabu kwa kizazi chote cha nyoka; huyu alikuwa nyoka wa kawaida aliyeruhusu kutumiwa na shetani. Kwa kuwa yeye ndiye alikuwa chanzo cha uovu ule kupita, nyoka anashusha hadhi yake na kufanywa awe chini ya wanyama wote na chini ya hayawani wote wa mwitu. Anapewa adhabu ya kula mavumbi, mavumbi ambayo katika hayo mtu alifanywa. Kwa namna fulani Mungu alikuwa anampa nyoka adhabu ambayo ilitakiwa imwangukie mtu; maana mtu ni mavumbi na kwa hivyo suala la nyoka kupewa adhabu ya kula mavumbi linamaanisha alikuwa anachukua adhabu fulani ya mtu ambayo angestahili aipate Adamu.

Adhabu anayopewa nyoka kwenye msitari wa 15 inaashiria kuwa haikumuhusu nyoka wa kawaida tena ila ilikuwa juu ya Ibilisi shetani ambaye alikuwa amemtumia nyoka kuleta uharibifu ule. Mungu hakutaka kumwacha shetani bila adhabu kwa kosa la kumkosesha mtu wake. Adhabu anayotoa kwa shetani ni kuweka uadui kati yake na mwanamke, na kati ya uzao wake na uzao wa mwanamke. Inahitaji kufikiri vizuri ili kugundua kitu ambacho Mungu alikuwa anafanya hapa. Uzao wa shetani unaotajwa hapa ni roho zote za uasi zenye asili yake, na hizi zote zimewekwa katika uadui mkubwa na uzao wa mwanamke.

Kwa kutaja kuwa uzao wa mwanamke utamponda shetani kichwa, ni wazi kuwa Mungu alikuwa anatujulisha kuwa mkombozi atakuja siku moja kutuokoa kutoka katika uangamivu wa shetani naye atamwangamiza shetani kabisa, yaani “atamponda kichwa.” Mungu alitangulia kutaja habari za kuja kwa Yesu tangu mwanzo mara tu dhambi ilipofanikiwa kuingia ulimwenguni. Kazi ya Yesu ilikuwa ni kuja kumponda kichwa shetani, lakini kabla ya Yesu kumponda kichwa shetani, shetani alipewa kumgonga kisigino. Yesu mwenyewe alinena kwa habari hii akasema: “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu [Yohana 14:30].” Shetani si kitu mbele za Yesu ndivyo Bwana wetu alivyosema.

Kuna mambo manne yanayotujulisha kuwa uzao wa mwanamke uliotakiwa kumponda kichwa shetani alikuwa si mwingine bali Yesu peke yake.

1.                  Katika suala la uumbaji wote, tangu mtu mpaka kwa viumbe wengine wote, uzao hufuata mwanaume na si mwanamke. Lakini hapa Mungu anazungumzia kitu ambacho kilikuwa kinyume na utaratibu wa kawaida, kuleta uzao kupitia mwanamke. Ni wazi kabisa kuwa hata kuzaliwa kwa Yesu hakukufuata utaratibu wa kawaida, maaana bikira asiyemjua mume alipata mimba akazaa mwana.

2.                  Tangazo la kupatikana kwa uzao wa mwanamke lilitolewa kabla ya uzao wa mwanamume kuwepo. Adamu alikuwa sio wa uzao wa mwanamume kwa maana yeye alikuwa moja katika vitu vya uzao wa mbingu na nchi. Uzao wa mwanaume ulianzia kwa Kaini na bahati mbaya ulikuwa uzao uliojaa uovu kwa maana Kaini naye alifanya dhambi ya kuua. Mungu alitangulia kuutaja huu uzao wa mwanamke kwa sababu haukutakiwa kuhesabiwa kama uzao wa kibinadamu, Yesu alikuja kama Adamu wa pili japokuwa yeye alijitaja kama mwana wa Adamu. Yesu alikuja katika uzao wa tofauti ili awaongoze watu katika haki ya Mungu tofauti na uzao wa mwanaume ambao uliwaongoza watu katika uasi.

3.                  Uadui kati ya uzao wa nyoka na uzao wa mwanamke ulitakiwa kuisha kwa ushindi wa uzao wa mwanamke, yeye angemponda kichwa nyoka. Kichwa ndiyo sehemu yenye werevu na utashi wote. Suala la Yesu kumponda kichwa shetani lilimaanisha kukomesha biashara ya shetani kuwadanganya watu na kuwapoteza. Ni Yesu peke yake aliyeweza kufanya hili, maana uzao wote wa mwanaume ulishindwa kumponda shetani, hata Musa alifika mahali akakosea. Yesu ndiye Bwana wa vita dhidi ya shetani na hila zake, yeye anajua namna ya kumponda kichwa.

4.                  Mwisho ni kwamba Mungu alitanguliza kuonesha kuwa ushindi huo ulikuwa na gharama na maumivu. Mtu aliyewahi kugongwa na nyoka ataelewa vizuri hiki tunachosema hapa, lakini yatosha tu ujue kuwa maumivu ya kugongwa na nyoka ni makali sana na yaweza kusababisha kifo. Katika kutembea, kisigino huwa ndiyo sehemu ya kwanza kabisa ya mguu wako kukanyaga chini. Nyoka alitakiwa kumgonga kisigino yule mzao wa mwanamke. Ni kweli kuwa ni pale tu Yesu alipokanyaga duniani ndipo alipopata maumivu. Hakuwahi kupata maumivu akiwa mbinguni, lakini alipokanyaga duniani kama kisigino kitanguliavyo kukanyaga chini ndipo alipopata maumivu, tena maumivu ya mijeledi na kupigiliwa misumari. Ilikuwa ni gharama aliyotakiwa kulipa Bwana wetu ili apate ushindi wa kumponda nyoka kichwa. Ashukuriwe Yesu kwa kuwa alilipa gharama na ushindi tumeupata, sasa hatuko tena chini ya udanganyifu wa shetani.

Baada ya kutoa adhabu kwa nyoka, ilikuwa sasa ni zamu ya mwanamke. Adhabu yake ilikuwa na pande mbili; moja, kuzaa kwake kungekuwa kwa uchungu siku zote; na pili, aliwekwa chini ya mumewe kwa kila jambo. Siku hizi kumekuwa na jitihada za kila namna kutaka kupingana na hiki Mungu alichoagiza kama adhabu. Kumekuwa na harakati zinazoitwa harakati za ukombozi wa mwanamke. Tumesikia kampeni za kutaka haki sawa kati ya mwanamke na mwanaume na kutaka mwanamke alingane na mwanaume kwa kila kitu. Hii imepelekea kuharibika kwa maadili katika jamii na msingi wa jamii (social order) umevurugika. Suala lililoamuriwa na Mungu sasa mwanadamu anataka ashindane nalo ili ikiwezekana alibadilishe; hakika sisi hatutaki kuwa sehemu ya upinzani huo juu ya Mungu.

Zamu ya Adamu ilipofika adhabu yake inatoa fundisho la ajabu kidogo; alikuwa amesikiliza sauti ya mkewe na kuacha agizo la Mungu sasa alitakiwa kuadhibiwa kwa hilo. Mtu yeyote anayeacha agizo la Mungu na kufuata sauti za watu lazima awe na adhabu kwa Mungu. Ardhi ililaaniwa kwa ajili ya Adamu. Ni wazi kuwa adhabu ya laana ilitakiwa imwangukie Adamu, lakini kwa jinsi Mungu alivyompenda mtu wake aliipindisha laana ile na kuielekeza kwenye ardhi. Sasa ardhi ilipewa kiburi juu ya mtu; haikutakiwa imzalie mtu bure kama ilivyokuwa mwanzo. Sasa ilimpasa Adamu ailime ardhi tena kwa jasho na kwa uchungu ndipo apate mazao yake. Ardhi hii pia ilipewa kumpokea mtu katika kifo chake, maana sasa neno la Mungu lilikuwa likitimizwa ya kwamba ‘siku utakapokula mtunda ya mti huo hakika utakufa.’ Kifo sasa lilikuwa ni jambo ambalo Adamu asingeweza kuliepuka. Ni katika hatua hii Adamu anaamua kumwita mkewe jina la Hawa.

Fumbo la kuvikwa ngozi

Adamu na mkewe walijaribu kuuficha uchi wao kwa nguo zilizoshonwa kutokana na majani ya mtini. Mungu alikuwa ameahidi kuja kwa uzao wa mwanamke ambaye angemponda nyoka kichwa na kukomesha kabisa hila za shetani juu ya mtu. Ujio huu wa mwokozi, Mungu alianza kuudhihirisha tangu katika kitabu cha Mwanzo na jinsi ambavyo wokovu huo ungetokea. Mungu aliamua kumchinja mojawapo ya wanyama waliokuwa bustanini ili awashonee nguo ya ngozi watu wake. Uovu wa Adamu na mkewe haukuweza kufichwa kwa majani isipokuwa kwanza kwa kumwaga damu.

Hakuna namna ambavyo ngozi hii ingepatikana isipokuwa kwanza kuna kifo cha mnyama fulani. Ndivyo alivyokuwa akitangulia kutujulisha Mungu kuwa hakuna namna dhambi zetu zingeweza kufichwa isipokuwa kuna kifo cha mtu fulani na damu yake imwagike kwa ajili ya dhambi hizo. Ni wazi kuwa mnyama aliyechinjwa na Mungu pale bustanini ili akina Adamu wapate nguo hakuwa na hatia iliyomsitahili mauti yale. Lakini kwa ajili ya upendo wa Mungu kwa mtu, damu isiyo na hatia ilimwagwa ili mtu apate kuepukana na aibu yake.

Ni sura ya dhahiri kabisa ambayo Mungu alikuwa anaionesha juu ya kile ambacho kingeleta ukombozi wa dhambi. Yesu anaitwa mwana-kondoo wa kuchinjwa, alichinjwa na kuuawa kwa ajili ya deni ambalo yeye hakuwa na hatia nalo wala hakushiriki kulifanya. Kama vile mnyama yule wa bustanini ambavyo hakuwa na hatia bali alichinjwa kwa ajili ya Adamu, ndivyo na Yesu naye alivyokufa na kutolewa awe sadaka kwa ajili ya dhambi zetu.

Ukomo wa maisha ndani ya Edeni

Inasikitisha sana kuona kwa jinsi gani mtu aliishi muda mfupi kwenye kusudi aliloitiwa na Mungu. Sasa Adamu alikuwa amepata ujuzi wa mema na mabaya, lakini bila nguvu yoyote ya kumwezesha kuyapata hayo mema bali akivutwa daima kuyendea mabaya. Mungu akaliona hili, ya kuwa huyu mtu sasa anajua mema na mabaya lakini hana uwezo wa kuyashinda mabaya na kuyapata mema. Katika hali hiyo Mungu akasema:

“…Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.” [Mwanzo 3:22-23]

Mti wa uzima ulikuwa haujaondolewa katika bustani, na bado Adamu alikuwa na uwezo wa kuufikia akatwaa matunda yake akala. Hii ingempa kuishi milele, lakini katika hali ya uovu. Mungu hakutaka hilo litokee hivyo alimfukuza Adamu atoke pale bustanini aende akailime ardhi ambayo kwa hiyo alitwaliwa. Na pia Adamu, asingeruhusiwa kutwaa matunda ya mti wa uzima akayala kwani angefanya hivyo neno la Mungu aliloahidi kama adhabu kwa Adamu la ‘hakika utakufa’ lisingetimia. Na kama unavyojua moja kati ya sifa kuu za Mungu wetu ni kutogeuka, yeye siyo kigeugeu na akisema amesema.

Msitari wa mwisho wa sura hii una fundisho jingine kubwa sana. Mungu alipogundua kuwa Adamu angeweza kula mtunda ya mti wa uzima akaishi milele kwenye uovu wake, hakuamua kuukata mti wa uzima, bali alimfukuza Adamu atoke bustanini na akaweka makerubi wailinde njia ya mti wa uzima. Swali la kujiuliza hapa ni kwa nini Mungu asingeukata tu mti wa uzima, halafu akamwacha Adamu aendelee kuishi Edeni?

Kitabu cha Ufunuo kinatueleza mambo kadhaa kuhusu mti wa uzima na sababu kwa nini Mungu hakuukata. Ufunuo 2:7 inasema:

“Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.” (msisitizo umeongezwa)

Hapa kitabu cha Ufunuo kinatuambia kuwa matunda ya mti wa uzima ulio katika bustani ya Mungu yalitunzwa ili iwe zawadi kwa wale watakaoshinda ya ulimwengu. Bustani ya Edeni ilikuwa ni mahali pema ambapo Mungu alitaka mtu afurahie ushirika wake na Mungu hapo. Ikiwa Adamu angebaki katika ile bustani basi uhalisia wa ile bustani na uthamani wake usingekuwepo tena. Ufunuo 22:2 inatueleza jambo lingine, inasema:

“…Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.” (msisitizo umeongezwa)

Hii ni habari ya mji mpya ambao Mungu amewaandalia watu wake wale ambao wameushinda ulimwengu na tamaa zake. Ndani ya huo mji Mungu anaurudisha tena mti wa uzima, ambao majani yake huwaponya mataifa. Ni wazi kuwa huu mti wa uzima ni Yesu Kristo maana yeye ndiye atuponyaye. Ikiwa Mungu angeukata mti wa uzima pale Edeni basi hiyo ingekuwa ni ishara ya kuwa tusingekombolewa kutoka dhambini. Ashukuriwe Mungu ambaye alituwekea uzima huu tangu kale.
Tumeona kuwa baada ya Adamu kufukuzwa atoke pale bustanini, njia ya mti wa uzima ilizuiwa ilindwe na makerubi pamoja na upanga wa moto. Hii haina maana kuwa hatuwezi kuufikia tena huo mti wa uzima, maana kitabu cha Ufunuo 22:14 kinasema hivi:

“Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.” (msisitizo umeongezwa)

Maneno haya yanatufundisha kuwa wale waliofua nguo zao, maana yake waliotakaswa kwa damu ya mwana-kondoo Yesu, wanayo amri ya kuuendea huo mti wa uzima. Maana yake ni kuwa watakatifu wa Yesu, na wale tunaoishi katika kweli ya Kristo tunayo amri ambayo kwa hiyo tukiwa tunauendea huo mti wa uzima ule upanga wa moto unatupisha na yule kerubi anatupigia saluti huku akituelekeza mti wa uzima ulipo. Ni raha iliyoje kupata kujua fumbo hili kubwa, ya kuwa mti wa uzima ulitunzwa na unalindwa kwa ajili yetu sisi tulio wake Kristo Yesu. Ndugu msomaji wetu kama hujampa Yesu maisha yako, chukua uamuzi leo wa kuokoka na kuziacha dhambi zako ili uungane nasi pamoja na Bwana arusi Yesu Kristo katika safari ya kuuendea mti wa uzima. Maana tunapokula mtunda ya mti huo tunaishi milele. Yesu alisema:

“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”  [Yohana 6:54]

Je, unataka kuwa na uzima wa milele ndani yako? Je, unataka nawe ufufuliwe na Yesu siku ya mwisho? Njia ni moja tu njoo uule mwili wa Yesu na kuinywa damu yake. Yaani OKOKA LEO. Mungu akupe neema ya kumpokea Yesu leo.

Endelea kufuatilia mfululizo huu kwa ajili ya sura ya 4.

DOWNLOAD MWANZO SURA YA 3

No comments:

Post a Comment