Tuesday, June 10, 2014

UWEZA WA KUFANYIKA MWANA WA MUNGU

OUR DAILY MANA


UWEZA WA KUFANYIKA MWANA WA MUNGU
HALELUYA!!

Karibu tena ndugu yangu katika mfululizo wa masomo haya yenye lengo la kufungua na kupanua ufahamu na uelewa wetu juu ya neno la Mungu. Katika somo lililopita tuliangalia juu ya kasi ya shetani kuwapeleka watu kuzimu na tukaona kuwa watu wa Mungu wanachukuliwa kuwa mateka wa nguvu za giza kwa kukosa maarifa ya neno la Mungu. Leo nataka tuangalia juu ya nguvu au uweza unaombadilisha mtu na kumfanya mwana wa Mungu.

Ukisoma Biblia yako vizuri utagundua kuwa, kabla mtu hajaookoka anakuwa akitumikia mambo ya dunia na anasa zake na kufanya mambo yanayomchukiza Mungu lakini saa anapookoka na kujikabidhi kwa Bwana, Mungu huleta badiliko kamili kwenye maisha yake na kumwingiza katika mfumo mpya wa maisha. Mtume Paulo katika Tito 3:3 anasema:
“Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.”

Maandiko haya yanatuonesha aina ya maisha ambayo mtu huishi kabla hajampokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake. Paulo anasema kuwa hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili. Akili inayozungumzwa hapa ni suala la kumtafuta Mungu na kuishi sawa na mapenzi yake, mtu akiacha kumtafuta Mungu na kuenda katika njia zake mwenyewe, Biblia inasema huyo ni mjinga na hana akili. Zaburi 53:1 inasema “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna atendaye mema.Kwa hiyo yule asemaye kuwa hakuna Mungu, na wale watendao uovu na ufisadi na kuchukiza na kuacha kutenda mema, Zaburi inasema ni wapumbavu. Vile vile Mithali 6:32 insema “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.” Kwa hiyo wanzinzi wote Biblia inasema hawana akili kabisa kwa sababu wanafanya jambo litakalowaangamiza wenyewe. Cha ajabu zaidi ni kuwa Biblia inawafananisha watu wa namna hizi (yaani wasio na akili na wapumbavu kama maandiko yasemavyo) na wanyama wapoteao. Zaburi 49:20 insema “Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.

Nimekupitisha kwenye maandiko hayo ili uone kuwa Mungu anawafananisha watu walio nje YA Kristo, wale watendao maovu, na wanayama wapoteao. Kwa hiyo suala la kumpa Yesu maisha yako ni suala la muhimu sana kama kweli unataka kuishi sawa na mpango wa Mungu kwako.
Baada ya kuangalia jambo hilo sasa tuende kwenye kiini cha somo letu. Lengo la somo hili ni kutaka kuangalia ni kitu gani muhimu sana kinachomwezesha mtu kuendelea na maisha ya wokovu baada ya kuwa amempokea Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wake.

Utakubaliana name kuwa kuna idadi kubwa sana ya watu ambao waliopookoka walikuwa na kiu sana ya kukua kiroho na kuishi katika utakatifu lakini wengi wameanguka tena katika dhambi na wengine wameshindwa kabisa kusimama tena. Mi binafsi ninawafahamu watu kadhaa waliookoka vizuri sana lakini walishindwa kuendelea na maisha ya kiroho na kurudi katika dhambi. Hii ikanipa kujiuliza sana juu ya nini kinachohitajika ili mtu aliyeookoka aendelee kusimama imara katika Kristo. Ndipo neema ya Mungu iliponifunulia kujua kuwa kuishi katika utakatifu wa kristo ni jambo linalohitaji kitu fulani zaidi ya kuokoka tu. Na hicho ndicho tunachotaka tujifunze sasa.

Kitabu cha Yohana 1:12 kinasema hivi:
Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.
Haya maandiko yanatuambia kuwa wale waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Jambo ninalotaka uone hapa ni juu ya kile kinachoitwa “UWEZO WA KUFANYIKA”. Haya maneno yametafsiri kwenye baadhi ya tafsiri ya kiingereza kama “POWER TO BECOME” au “AUTHORITY TO BECOME”.
Haya maneno yanatufunulia kuwa suala la watu hawa kuwa wana wa Mungu halikutokana na wao kumpokea Kristo ila lilitokana na uwezo waliopewa na Mungu wa kufanyika watoto wa Mungu. Lile neno “kufanyika” linatupa picha ya kuwa uwezo waliopewa watu hawa ulikuwa na nguvu ya kuwabadilisha kutoka kwenye utu wao wa kwanza na kuwafanya watoto wa Mungu. Kwa hiyo kumbe sio kwamba kuokoka ndiko kunakomfanya mtu awe mwana wa Mungu, ila kuokoka ni hatua ya kwanza inayomruhusu Mungu kukuletea juu yako uwezo wa kubadilishwa ili uwe mwana wa Mungu.
Naona hujaelewa sawasawa. Hebu ngoja tujifunze kutoka kwa Yesu. Soma pamoja name kitabu cha Luka 3:21-22. Biblia inasema hivi:
Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.
Nimeamua kukoleza sehemu za maneno haya kwa makusudi ya kukuonesha kile kilichofanyika pale Yordani. Biblia inasema Yesu alipokwisha kubatizwa alianza kuomba. Alikuwa anaomba nini? Biblia haituambiii alikuwa anaomba nini, lakini majibu ya maombi yake yanatupa kujua kuwa alikuwa anaomba juu ya kuhitaji kwake kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu. Sasa cha ajabu ni kuwa Roho aliposhuka juu yake tu na Mungu akatangaza hapo hapo kuwa huyu ni mwanangu mpendwa wangu.
Swali la kujiuliza hapa ni kuwa Mungu alitaka kutuonesha nini? Kwa nini asinyamaze tu kimya maana tayari kwenye kuzaliwa kwake tulikwisha ambiwa kuwa ni mwana wa Mungu. Na kwa nini Mungu asitangaze hivyo kabla ya Roho Mtakatifu kuja juu yake? Ni nini kilichomfanya Mungu asubiri kwanza Roho Mtakatifu ashuke juu ya Yesu ndipo akatangaza kuwa huyu ni mwanangu?
Maswali haya yanatufungua macho kujua kuwa Mungu alitaka tujue kuwa ni uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu ndio unaomwezesha kufanyika kuwa mototo wa Mungu. Mtu anaweza akaokoka lakini asipojazwa Roho Mtakatifu mtu huyo anakuwa bado hajafanyika mototo wa Mungu. Ndiyo maana Biblia inasema waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Na Yesu mwenyewe anatuambia kuwa uwezo huo ni nguvu ya Roho Mtakatifu. Luka 24: 45 Yesu anasema: “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Yesu aliwazuia wanafunzi wake wasitoke mjini mpaka wamevikwa uwezo utokao juu. Jambo la kujiuliza ni kwa nini aliwazuia? Tunachogundua ni kuwa bila Roho wa Mungu hatuwezi kuishinda dhambi wala hauwezi kumpendeza Mungu. Rumi 8:8 inasema “Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.” Na Warumi 8:14 inasema “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu”
Kwa hiyo kama mtu haongozwi na Roho wa Mungu huyo hawezi kumpendeza na Mungu na hawezi kuwa mwana wa Mungu. Sasa hauwezi kuongozwa na Roho wa Mungu, kama Roho wa Mungu hayuko ndani yako. Ni lazima kwanza Roho aje juu yako ndipo anaweza kukufanya uwe mwana wa Mungu. Warumi 8: 15 inasema “… bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.”
Kumbe ni Roho wa Mungu ndiye anayetufanya wana wa Mungu. Kuokoka ni hatua ya kwanza ya kumruhusu Roho wa Mungu apate nafasi ndani yetu, kisha pindi tunapovikwa Roho wa Mungu hapo ndipo tunapopewa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Katika wagalatia 4:6 Paulo anasema “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.”
Ooooh kumbe ni uwezo wa Roho Mtakatifu ndio unaotuwezesha kuwa wana wa Mungu kweli kweli na kutuwezesha kuishi bila dhambi. Ikiwa hatuna Roho wa Mungu basi nguvu yetu ya kumshinda shetani inakuwa kidogo sana na baada ya muda mchache mtu hujikuta ameanguka na kumwasi Mungu. Ili uishi katika wokovu na kumpendeza Mungu basi ni lazima uombe Roho wa Mungu aje juu yako. Yesu anatupa mfano mzuri. Yeye alipokwisha tu kubatizwa alianza kumwomba Mungu na Mungu akamvika Roho Mtakatifu aliyekuja juu yake na kumfanya kuwa mwana wa Mungu.
Watu wengi leo wanaokoka na kisha kuanguka kwa sababu walipookoka hawakujazwa Roho Mtakatifu hivo wakakosa nguvu ya kufanyika watoto wa Mungu. Watumishi wengi hupenda kuwahubiria watu waokoke lakini wakiisha kuokoka husahau kuwaombea nguvu ya Roho Mtakatifu ili wafanyike kuwa watoto wa Mungu. Katika Matendo 19: 2, 6 Paulo anatuonesha umuhimu wa watu kumpokea Roho Mtakatifu wanapookoka. Biblia inasema
akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia… Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.
Kwa hiyo uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu ndio uwezo pekee unaomfanya mtu huyo kuweza kuishi katika utakatifu na kumpendeza Mungu na kuwa mwana wa Mungu.
NAKUOMBEA UMPOKEE ROHO MTAKATIFU SASA KWA JINA LA YESU.
YESU NI BWANA

2 comments:

  1. Natowa asante kwa mafundisho

    ReplyDelete
  2. Asante Mutumishi Kwa mafundisho yako,inaeleweka vizuri.

    ReplyDelete