Friday, October 24, 2014

MWANZO SURA YA KWANZA


KITABU CHA MWANZO

Utangulizi

Hiki ni kitabu kinachoweka msingi wa mambo yote tunayoyasoma, kuyasikia na kuyaona yakifanyika katika vitabu 66 vya Biblia. Inatajwa kuwa Kiliandikwa na Musa, na japo tunajua kuwa Musa alizaliwa miaka mingi baadae kuliko yale yanayozungumzwa katika kitabu cha Mwanzo, bado ufunuo wa maandiko haya unabaki kuwa halisi na wenye kweli halisi ya Mungu juu ya kile kilichofanyika kabla ya Musa mwenyewe kuwepo; “Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu. (2Petro 1:21)”

Sura za mwanzo kabisa za kitabu hiki, hasa sura ya 1 na ya 2, zinafunua kwetu asili ya kila kitu tukionacho leo duniani na jinsi kilivyopata kuweko. Sura zinazofuata baada ya hapo zinatufunulia mazingira yaliyopelekea mambo mabaya, kama dhambi, kifo, huzuni, misiba, mahangaiko, magonjwa na mengine kama hayo, kutokea na kutupata hadi leo. Utagundua kuwa kila alichofanya Mungu kwa mkono wake, au kwa neno lake, kilikuwa chema na cha kupendeza, lakini Mtu alipoanza kufanya yake tofauti na vile alivyoagizwa na Mungu ndipo mabaya haya yakatupata. Kama vile maandiko yasemavyo: “… Kwa sababu walimwacha Bwana … wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao. 2 Nyakati 7:22”(msisitizo umeongezwa). Hii inatupa moyo kuwa neno la Mungu ni uzima udumuo na kama tukiishi kwa neno la Mungu basi hatutapatwa na mabaya, bali tutakuwa na uzima wa milele ndani yetu. Hivyo ni heri kuishi kwa neno la Mungu kuliko kuishi kwa neno la wanadamu.

Kitabu hiki pia kinatufunulia maisha ya watu waliomtumaini Mungu katika nyakati hizo za mwanzo. Tunawaona Ibrahimu, Isaka, Yakobo, na uzao wao baada yao jinsi walivyoishi kwa Imani mbele za Mungu. Lakini tunaona pia kitabu hiki kikitufunulia matukio ya uasi wa ajabu uliofanywa na wanadamu enzi za Nuhu na nyakati za Sodoma na Gomora. Kama tutakavyoona kwenye tafakari za mambo hayo tutakapofika kwenye sura hizo, Mungu wetu hapendezwi na uovu wa namna yoyote ile, na hataacha kuadhibu kwa hasira kali wale wote wafanyao maovu, na machukizo. Lakini wale wote wampendezao yeye huwapa rehema na Baraka tele. Sasa tuzitafakari sura za kitabu hiki cha Mwanzo pamoja.

Mwanzo Sura ya 1

Maneno matatu ya kwanza kabisa katika Biblia ni: “Hapo mwanzo Mungu.” Ni jambo la kufurahisha sana na kututia nguvu sana katika Imani Biblia inapoanza na maneno haya. Hakika Biblia ilitaka tujue kuwa Mungu wetu ndiye mwanzo na mwisho wa kila jambo lililopata kuwepo au kufanyika katika ulimwengu huu, ikiwa ni jema. Maneno haya pia yanatufunulia kuwa yatupasa kuanza na Mungu katika kila jambo katika maisha yetu. Hebu jiulize kama Biblia ingeanza na habari za Ibrahimu na wanawe halafu baadae ndipo ikamtaja Mungu; hivi kati ya Mungu na Ibrahimu unafikiri watu wangemwamini nani zaidi. Basi tangu leo usiwatangulize watu katika maisha yako bali mtangulize Mungu kwanza. Fanya Mungu wako ajulikane kwanza na kutukuzwa yeye kwanza halafu ndipo wajulikane wanadamu.

Kuumbwa Kwa Mbingu na Nchi

Msitari wa 1 unasema “Hapo Mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Eeeeh kumbe! Kumbe mbingu na nchi (dunia) havina umilele ndani yake; vilikuwa na mwanzo, na mwanzo huo ulikuwa ni Mungu mwenyewe. Nasi tunajua kuwa kila chenye mwanzo kina mwisho wake pia; basi kumbe mbingu na nchi pia zina mwisho wake. Hii ni kweli kabisa maana Ufunuo 21:1 unasema Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.” Mungu aliweka maneno haya kwenye msitari wa kwanza kabisa wa Biblia ili kutufundisha kuwa yote tutakayoyaona baada ya hapo tujue kuwa yana mwisho wake. Mungu hakutaka kutuficha jambo hili bali aliliweka wazi kabisa kwa kila mtu, tena kwenye msitari wa kwanza kabisa wa Biblia, kuwa mbingu na nchi (dunia) vina mwanzo wake na kwa hiyo pia vina mwisho wake. Mungu hakutaka tuishi kwenye dunia bila kujua kuwa itaisha.

Msitari huu unatufunulia pia kuwa chanzo cha uumbaji wote ni Mungu. Kuna watu duniani wanaojifanya kuwa wajanja sana na wanasema kuwa Mungu hayupo. Wao wana falsafa zao wanazoziamini juu ya chanzo cha vitu na mtu. Lakini sisi (Fimbo ya Musa Ministry) tunaamini kwa akili, macho, moyo, roho, mwili, nafsi, na kila kitu kuwa Mungu ndiye asili ya vitu vyote mbinguni na duniani. Yeye peke yake ndiye akatiye katika umilele wake naye ni milele na milele. Isaya 57:15 inasema ‘Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.’(msisitizo umeongezwa) Kwa hiyo Mungu pekee ndiye akaaye milele, na wale wasemao kuwa hakuna Mungu ni wapumbavu tu; “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu” (Zaburi 53:1) (msisitizo umeongezwa)

Ikumbukwe hapa pia kuwa uwepo wa Mungu hautegemei kuwepo kwa mbingu na nchi na Mungu aliweza kuwepo kabla ya kuwepo mbingu na nchi ndiyo maana aliziumba ina maana yeye alikuwepo na mbingu ziliumbwa baadaye, kwa maeneo mengine ya biblia tunajifunza kuwa Mungu mwenyewe ameweka mbinguni kuwa kiti chake cha enzi, lakini Mungu hategemei mbinguni kama mahali pekee anapoweza kuishi kwani alikuwepo kabla mbingu na nchi kuwepo. “Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzika ni mahali gani?” Isaya 66:1 (msisitizo umeongezwa)

Neno Mungu lililotumika kwenye msitari wa kwanza Mwanzo 1:1 kwa kiebrania limetumika neno “Elohiym”. ‘Elohiym’ kwa kiebrania linamaanisha Mungu katika nafsi ya wingi na sio umoja. Tunafahamu kuwa Biblia, Agano la Kale, iliandikwa kwa lugha ya kiebrania kabla ya tafsiri za lugha zingine kutolewa; kwa hiyo hili neno la kiebrania litakuwa na maana kubwa sana katika matumizi haya ya msitari huu wa kwanza wa Biblia. Sasa kama “Elohiym” ni Mungu katika wingi, basi tunachogundua hapa ni kuwa kazi ya uumbaji ilifanywa na zaidi ya mmoja. Ndiyo maana utaona katika Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu…”  Ni dhahiri kuwa kweli kazi ya uumbaji haikufanywa na mmoja. Kama ni hivyo ni vema tukajiuliza na tukajua hao wengi waliofanya kazi hiyo walikuwa akina nani.

Mistari kadhaa ya Biblia katika Agano Jipya inafunua kuwa kuna “utatu mtakatifu” ambao ni “umoja.” Luka 3:21-22 inatufulia jambo kubwa sana; inasema:
“Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

Palikuwa na Yesu duniani, aliyekuja kwa ajili ya kufanya watu wawe viumbe vipya kwa kuumbwa upya katika damu yake, kisha Roho Mtakatifu alishuka juu yake ili aifanye kazi hiyo pamoja na Yesu, naye Mungu baba alikuwa pamoja nao kwa sauti yake kutoka mbinguni. Hivyo tunagundua kuwa uko “utatu mtakatifu” nao wanatenda kazi moja kwa umoja wala hakuna utofauti kati yao maana Yesu anasema wao ni “umoja” (Yohana 17:22) na kisha anasema “Mimi na Baba tu Umoja” (Yohana 10:30). Tunachogundua sasa ni kuwa: Mungu aliyeziumba mbingu na nchi alikuwa ni Mungu Baba, Mungu Mwana (Yesu Kristo) na Mungu Roho Mtakatifu. Biblia inakwenda mbele zaidi na kutuambia kuwa nguvu za uumbaji wa kila kitu zilikuwa katika “Neno” ambaye huyo alikuwa ndiye asili ya kila jambo, na kupitia yeye kila kitu kilifanyika kwa jinsi kilivyofanyika. Yohana 1:1, 3 inasema:
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu…Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”

Tunajifunza mambo mawili katika mistari hii: kwanza ni kuwa kila jambo katika maisha yetu linatakiwa litokane na neno la Mungu. Ni neno la Mungu tu ndilo lenye uweza wa kuumba vitu vyema na vya utukufu katika maisha yetu yote. Pili, tunaona kuwa Mungu aliweka nguvu ya vitu vyote kuwako ndani ya “Neno”; tunajifunza katika maandiko kuwa “Neno” ni Yesu kristo. Kwa hiyo Mungu aliweka nguvu yote ya uumbaji ndani ya Yesu Kristo na pasipo Yesu hakikufanyika chochote kilichofanyika. Nguvu hii haikuishia katika uumbaji tu bali Mungu ameweka ndani ya Yesu nguvu za kila jambo. Ameweka ndani ya Yesu nguvu ya wokovu, nguvu ya uzima, nguvu ya mafanikio, nguvu ya ushindi, na nguvu ya hukumu, kama vile alivyompa nguvu ya uumbaji. Heri kukimbilia kwa Yesu mapema maana yeye ndiye chanzo cha kila jambo.

Msitari wa 2, unatujulisha mambo matatu.
     
               1. Kuwa nchi (dunia) ilikuwa ukiwa na tena utupu. Biblia za kiingereza zimetumia maneno “void and without form”. Maana yake dunia haikuwa na kitu wakati wa kuumbwa kwake na haikuwa na umbo maalumu (without form). Hatuambiwi mbingu zilikuwaje, lakini tunachoambiwa ni juu ya nchi jinsi ilivyokuwa wakati wa kuumbwa kwake. Lakini licha ya kuwa nchi iliumbwa bila kitu na bila umbo maalumu Mungu hakuikusudia ikae hivyo siku zote.  

Katika Isaya 45:12 inasema kuwa: “…Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwaaliiumba ili ikaliwe na watu”. Kwa hiyo japokuwa nchi kwa mara ya kwanza ilikuwa ukiwa lakini Mungu alikusudia ikaliwe na watu tangu mwanzo alipokuwa anaiumba. Ahaa kumbe kuumbwa kwa mtu na vitu vingine vyote viijazavyo dunia ilikuwa tu ni mwendelezo wa kile Mungu alichokuwa amepanga kitokee tangu mwanzo. Katika maisha wako watu wanasema kuwa wao waliumbiwa magonjwa, umasikini, taabu na mikosi; lakini nataka kukwambia kuwa hukuumbwa ili uwe ukiwa, uliumbwa ili ujae na upendeze kwa kila kitu chema ndani yako. Usikate tamaa kwa ukiwa ulionao sasa, bali umtafute Mungu maana siku utakapomtafuta Mungu ukiwa wako utaondolewa na mafanikio yatakujia hadi watu washangae. Sikia Biblia inachosema: “Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha. 2 Nyakati 26:5” (msisitizo umeongezwa).
    
             2. Kwamba giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Inaonekana kuwa nchi hapo mwanzo ilikuwa ni maji tupu kila mahali na hapakuwa na mahali pakavu pasipo na maji. Juu ya uso wa maji haya lilitawala giza, na kwa hiyo haikuwezekana kuonekana chochote kilichokuwa ndani ya dunia. Kumbuka giza halikuwa kila mahali ila tu ‘juu ya uso wa vilindi vya maji.’ Kwa hiyo kule alikokuwa Mungu, hakukuwa  na giza kwa sababu Mungu ni nuru (Zaburi 27:1)

Kwa hiyo giza lilizuia vitu mbalimbali visidhihirike, na ndio maana tunaona Mungu baadae akiamuru giza lipishe nuru. Kwa nini ilikuwa hivi; tutaona jambo hili kwenye msitari wa tatu na wa nne. Wakati mwingine giza limetanda kwenye maisha ya watu wengi na kuwazuia wasizione Baraka ambazo Mungu amewawekea na kwa sababu hiyo wengine wamedhania kuwa ndivyo walivyoumbwa. Lakini, mngoje Bwana na umtumaini maana uko wakati wa kuliamuru giza liondoke na kuipisha nuru unakuja.

        3. Kwamba Roho ya Mungu ilitulia juu ya uso wa maji. Tumekwisha kuona kuwa kazi ya uumbaji ilimuhusisha Mungu katika “utatu mtakatifu” na hapa tunaona Roho ya Mungu ikiwa kazini juu ya uso wa maji. Tuna jambo la kujiuliza hapa, nalo ni: Roho ya Mungu ilikuwa inafanya kazi gani juu ya uso wa Maji?

Mwanafalsafa aitwaye Herbert Spencer alipata kusema kuwa: ‘ili vitu vyenye maumbo halisi vitokee panahitajika muda (time), nafasi (space), nguvu (force), mada au kitu (matter), na mwendo (motion).’ Mambo haya matano yamejitokeza wazi katika sura hii ya kwanza ya kitabu cha Mwanzo ili kuidhihirisha kazi ya uumbaji katika maumbo halisi. Biblia inatufundisha kuwa Roho Mtakatifu ni kani/nguvu ya utendaji wa Mungu (work force of God); soma Matendo 1:8.

Roho ya Mungu ilikuwa ikitembea (maana kiingereza kinasema ‘And the Spirit of God moved upon the face of the waters’) juu ya uso wa maji ili kuhakikisha kuwa kile Mungu atakachokisema kifanyike basi kinafanyika kama alivyosema. Ndio maana utagundua kuwa katika sura hii maneno “Mungu akasema… ikawa hivyo” yametumika sana katika kuelezea suala la uumbaji wa Mungu. Tunachojifunza ni kuwa Roho ya Mungu inatenda kazi katika dunia ili kuhakikisha kuwa Neno la Mungu linatimia kama alivyosema na wala si vinginevyo (Isaya 55:11). Roho ya Mungu ilikuwa juu ya uso wa maji yaani duniani na wala si mbinguni. Kwa hiyo ili Mungu atimize mpango wake duniani alituma Roho yake ili ihakikishe kuwa kila Mungu anachosema kinafanyika. Ndivyo ilivyo hata leo kwa wale tulio ndani ya Yesu. Roho Mtakatifu ameletwa na Mungu ndani yetu ili kuhakikisha kuwa anaithibitisha kweli ya Mungu kwa ulimwengu wote. Yohana 16:8 inasema “Naye akiisha kuja (Roho Mtakatifu), huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu”. Heri wenye Roho Mtakatifu ndani yao. Anapokuja Roho wa Mungu katika maisha yako anatembea na kuona mapungufu yaliyo ndani yako na kwa kutekeleza yale yaliyoagizwa na Mungu anayaondoa hayo madhaifu(giza)

Kutengwa kwa Nuru na Giza

Msitari wa 3 na 4, Mungu anaifanya nuru na anatenga nuru na giza. Ni ajabu sana kugundua kuwa giza halikufanywa na Mungu wala Mungu haonekani mahali popote katika sura hii ya uumbaji akisema ‘iwe giza’ bali anaonekana akisema ‘iwe nuru’. Msitari wa pili umetuambia tu kuwa kulikuwa na giza juu ya uso wa maji lakini hautuambii lile giza lilitokea wapi au lilifanywa na nani. Hii itakuwa na sababu ya msingi na litakuwepo jambo ambalo Mungu alitaka kutufundisha kutoka kwenye mambo haya. Kwa kuwa giza halikufanywa na Mungu basi ni dhahiri kuwa Mungu hakukusudia giza liwepo ila yeye aliikusudia nuru ndiyo iwepo, ndio maana kile alichokikusudia kiwepo alisema kiwepo, yaani nuru na sio giza.

Mungu anatufundisha hapa kuwa yeye hajaumba giza kwenye maisha yetu wala hakukusudia tuishi ndani ya hilo giza. Giza la magonjwa, umasikini, laana, kutokufanikiwa, kufeli, kutopendwa na watu, mikosi, kusumbuliwa na nguvu za giza, kutozaa, na mengine kama hayo yote, Mungu hakuyakusudia kwetu wala siye aliyeyaumba maana yeye hakuumba giza. Na kwa upendo wake amemtuma mwanawe Yesu Kristo ili awe Nuru kwetu na kututoa katika giza. “Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza (Yohana 1:5).” Mpokee Yesu leo naye atakuangazia nuru yake utoke gizani.

Ni kwa nini Mungu aliamuru ‘iwe nuru’ na akatenga giza na nuru? Kwa nini Mungu hakutaka giza na nuru vikae pamoja au basi hata kuwe na mchanganyiko wa nuru na giza kwa pamoja? Hakika isingewezekana; giza lilipokuwa juu ya uso wa nchi lilificha kila kitu Mungu alichokikusudia kwa ajili ya nchi kikawa hakionekani. Ndio maana msitari wa pili umetuambia kuwa nchi ilionekana kuwa ‘ukiwa na utupu’. Giza lilificha kila kitu Mungu alichotaka kiweko duniani, na hivyo ilihitajika nguvu ya kupambana na giza ili vitu Mungu alivyovikusudia vitokee. Ndio maana kabla ya kufanya kitu kingine chochote, Mungu alitaka kwanza ‘nuru ije.’ Kumbuka kuwa Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza; kwa hiyo nguvu pekee ya kulishinda giza ni kwa njia ya nuru. Ndiyo maana huwezi kumshinda shetani kwa kwenda kwa shetani. Shetani na wafuasi wake ni malaika wa giza ambao wanazuia Baraka na mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Ili tuweze kuwashinda ni lazima tuiruhusu nuru iingie mahali hapo, na pindi nuru inapodhihirika giza lote linatoweka. Yesu anasema hivi:
“Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima (Yohana 8:12) Kisha anasema: ‘Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.’ (Yohana 12:46)”

Kwa nini isingewekezana nuru na giza kukaa pamoja au kuchanganyika? Tunapaswa kujua kwanza maana ya nuru ili tujibu swali hili. Neno ‘nuru’ kwenye Biblia za kiingereza limetumika neno ‘light.’ Kuna tafsiri nyingi tu za kamusi zinazoweza kutumiwa kueleza maana ya ‘light’ na pia wanasayansi wana maelezo yao kuhusu jinsi ‘light’ inavyotokea na chanzo chake na maana yake. Sisi hatutajikita katika maelezo hayo ya kibinadamu, maana hakuna tafsiri nzuri ya neno la kibiblia kuliko ile iliyotolewa na Biblia yenyewe. Biblia inatafsiri neno ‘nuru’ kwa kusema: “…maana kila kilichodhihirika ni nuru. (Efeso 5:13)” (msisitizo umeongezwa). Kumbe nuru ni kudhihirishwa kwa vitu, hivyo jambo lolote lilofichwa au kusitirika hilo sio nuru bali ni giza.

Tumetangulia kusema kuwa giza halikufanywa na Mungu, na giza lilikuwa limeyaficha mambo aliyoyataka Mungu ili yasitokee. Ili mambo hayo yatokee basi ilibidi Mungu afanye nguvu ya kuyadhirisha na nguvu hiyo ndiyo ‘nuru’. Isingewezekana vitu hivi kukaa pamoja maana hata Mtume Paulo anasema hapana ushirika wowote kati ya nuru na giza (2 Kor 6:14). Mungu alivitenga vitu hivi viwili mwanzoni kabisa mwa uumbaji wake ili kutufundisha kuwa ili tuzione Baraka za Mungu kwenye maisha yetu ni lazima tujitenge na giza. Ili tuuone uzuri wa Bwana lazima tujitenge na mambo ya uchafu na giza huku tukiyavaa matendo ya nuru katika Kristo Yesu Bwana wetu na mwokozi wetu.

Mchana na Usiku vinafanywa

Msitari wa 5, unakuja kuonesha matokeo ya kutengwa kwa giza na nuru. Biblia inasema nuru iliitwa mchana na giza likaitwa usiku. Na hapa ndipo tunaona mwanzo wa kuhesabu siku ukitokea. Tunachotaka uone hapa ni kuwa kabla giza halijaondoka katika maisha yako, siku zako zinakuwa sawa na bure tu. Ni pale giza linapoondoka maishani mwako ndipo unapoanza kuona uthamani wa wewe kuishi na unaona raha ya siku zako duniani. Ndio maana watu wanapookoka huwa wanarudi na kusema “aisee natamani ningeokoka zamani.” Kweli kama unataka kuona raha ya siku zako hapa duniani, okoka leo na umkabidhi Yesu maisha yako, awe nuru, nawe utaona kama vile siku zako ndo zinaanza kuhesabiwa upya.

Kumekuwa na mawazo tofauti ya wanatheolojia juu ya uhalisia wa mchana kuumbwa siku ya kwanza halafu jua linalotawala mchana likaumbwa siku ya nne. Sisi tunaona huu mkanganyiko hauna sababu ya msingi kwa kuwa jua halikutajwa kuwa ndilo chanzo cha nuru itawalayo mchana. Tukumbuke kuwa hii ilikuwa ni nchi ambayo dhambi ilikuwa haijaingia bado na kwa hiyo “mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:23)” (msisitizo umeongezwa). Yesu Kristo ndiye nuru ya kwanza na ya msingi katika jambo hili, wala giza halikufukuzwa na jua bali na nuru ya utukufu wa Mungu ulio katika Mwana-Kondoo Yesu. Tutaliangalia vizuri jambo hili katika msitari wa 14-17.

Zingatia:  Kuna jambo la muhimu hapa ambalo tunataka ulizingatie tunapoendelea kuitafakari sura hii ya ajabu kuhusu uumbaji. Maneno “Mungu akaumba” yanatokea mara tatu katika sura hii ya kwanza. Tunayaona maneno kama haya kwenye msitari wa 1, 21, na 27. Kutoka kwenye msitari wa 1 hadi 21, Biblia inatumia maneno “Mungu akafanya.” Tunaamini kuna tofauti ya kimaudhui ambayo Mungu alitaka tuione katika utofauti wa kazi ya uumbaji. Maneno yaliyotumika kwenye kiingereza ni “God created” na “God made.” Tafsiri zake ni hivi “create” is to bring something into existence; yaani kukifanya kitu fulani kiwepo. Wakati “make” indicates forming or re-forming already existing matter; yaani kutengeneza kitu kutoka kwenye kitu kingine ambacho kipo. Kwa hiyo Mungu alipoumba, alikuwa anafanya kitu kipya ambacho hakikuwepo; lakini alipokuwa anafanya, alikuwa anatengeneza kitu kutoka kwenye kingine kilichokuwepo tayari.

Kumbuka kuwa Isaya 45:18 umetuambia kuwa Mungu hakuiumba dunia ukiwa, maana yake Mungu hakuiumba dunia ikiwa haina kitu kabisa bali vilikuwevyo ndani yake vikisubiri nuru ividhihirishe. Na ndiyo maana tunaona baada ya nuru kuweko ndipo na vitu vingine vinaanza kufanywa.

Anga linayatenga maji

Msitari wa 6-8, Mungu analifanya anga kwa ajili ya kuyatenga maji na maji. Tunamwona Mungu akiendelea na kazi ya kuvitenganisha vitu. Baada ya kulitenga giza na nuru, sasa anayatenga maji ili kuwe na maji ya juu na maji ya chini. Anatumia anga kuikamilisha kazi hii na lile anga akaliita ‘mbingu.’ Hivyo ndivyo siku ya pili ilivyomalizika.

Lakini pana jambo la kuchunguza kwa makini hapa. Tumeona kwenye msitari wa kwanza kabisa kuwa jambo la kwanza kabisa Mungu aliloumba ilikuwa mbingu na nchi, lakini hapa tunakuta akiliita lile anga lililotenga maji ya juu na ya chini, mbingu. Je, hizi mbingu ni kitu kile kile au ni vitu viwili tofauti. 2Petro 3:5 inasema:
“Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu.”

Maneno hayo yaliyokolezwa kwenye kiiingereza tafsiri mojawapo inasema hivi: … the heavens existed long ago…” Maana yake mbingu zilikuwepo tangu zamani kabla ya nchi kufanyizwa kutoka katika maji. Alichokuwa anakifanya Mungu ni kile alichosema mwandishi wa Mithali 8:27-29 kwamba:
Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi.

Ahaaa! Kumbe Mungu alipokuwa anatenga maji ya juu na maji ya chini kwa anga alikuwa anazithibitisha mbingu ambazo zilishakuwepo na kuiwekea nchi misingi yake na bahari mipaka yake. Maana yake ni kuwa Mungu alikuwa tu anatenganisha mbingu na nchi ambazo alikuwa amezifanya hapo kabla ili kujulikane mipaka ya kila kimoja, na lile anga alilolifanya ndilo aliliweka liwe mpaka kati ya mbingu na nchi. Kumekuwa na maswali kuhusu maji ya juu na ikiwa ndiyo yanaleta mvua na mahali yalipo huko juu. Ule msitari wa Mitahali 8:28 unasema kuwa “aliyafanya imara mawingu yaliyo juu katika siku alipozithibitisha mbingu. Maana yake ni kuwa yale maji ya juu Mungu aliyakusanya katika mfumo wa mawingu na akayafanya imara ili kwamba yasimame yasianguke (Ayubu 37:14-16). Wanasayansi wanasema kuwa mawingu ni chanzo kimojawapo cha mvua, na sisi tunaamini hivyo. Kuwa yale maji ya juu, Mungu aliyakusanya kama mawingu na ndiyo hayo huyaachilia kwa majira yake ili kuinyeshea nchi mvua.

Nchi kavu na Bahari vinatengwa

Msitari wa 9-13, Siku ya tatu tena Mungu aliendelea na kazi ya kutenganisha; hapa Mungu anaitenga nchi na bahari kutoka kwenye maji yale yaliyokuwa chini ya mbingu. Maji yaliamuriwa yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane na pale pakavu pakaitwa Nchi.

Mpaka kufika hapa tunaona Mungu akiwa amefanya mgawanyo wa aina tatu: kwanza, kutenga nuru na giza; pili, kutenga maji ya juu na maji ya chini; tatu, kutenga nchi na bahari. Katika mgawanyo huu wote Mungu aliona kuwa vyema. Kuna wakati mwingine Mungu huwa anaamua kuwatenga watu wake na watu fulani au na mambo fulani lakini mara nyingi watu huwa hawamwelewi Mungu na kuamua kuendelea kushikamana na vitu au watu ambao Mungu ameamua kuwatenga nao. Sikia Mpendwa, kila utengano ambao umefanywa na Mungu, Mungu ameona kuwa ni vyema; usijaribu kulazimisha kung’ang’ania umoja au muunganiko na vitu au watu ambao Mungu amekutenga navyo. Kwa mfano, Mungu amewatenga wanadamu wote na dhambi na uovu wa kila aina lakini watu wanaona kama vile Mungu amewaonea kwa kuwatenga na vitu hivyo na kwa hiyo wao wameamua kuendelea kushikamana navyo. Lakini fahamu kuwa kile Mungu alichokiona ‘chema’ wewe mwanadamu usikione kibaya na kile Mungu alichokiona ‘si chema’ wewe usikione kuwa chema.

Mimea inaoteshwa

Siku ya tatu haikuishia hapo bali Mungu aliendelea na kazi yake kwa kuruhusu nchi itoe majani, na miche, na miti ya matunda kwa jinsi zake. Nchi ikatoa na Mungu akaona pia kuwa ni vyema. Ni ajabu sana tunapogundua kuwa Mungu hakuifanya hii miche, na majani na miti, wala hakuiumba bali aliiagiza Nchi itoe nayo Nchi ikatoa. Nini maana yake? Maana yake ni kuwa mazao ya nchi yalikuwa ndani ya Nchi yenyewe pale Mungu alipoifanya na yaliwekwa tayari kwa ajili ya mtu ambaye Mungu alipanga kumweka katika hiyo nchi. Zaburi 104:14 inasema:
Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi.

Kwa hiyo nchi iliwekwa na ikaamuliwa itoe chakula kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu. Ndio maana suala la njaa katika nchi si suala la ki-Mungu kabisa kwa sababu nchi iliamuriwa itupe chakula. Hapa haimaanishi chakula cha tumboni tu bali ni kila aina ya mahitaji tunayohitaji kwa ajili ya kuishi, nchi iliamriwa itoe. Palitokea uharibifu wa mpango huu baadaye pale Adamu alipoasi, na hivyo nchi ikazuiliwa kutoa mpaka pale itakapolimwa, yaani kulazimishwa kwa jasho la mtu. Neema hii tunaipata tena katika Kristo Yesu, Paulo anasema:
Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu (Wafilipi 4:19)

Jambo jingine linalojitokeza kwenye misitari hii ni kuwa Mungu aliweka kanuni ya kuzaliana kwa kila mche, na majani, na miti katika mbegu kwa jinsi zake. Katika kanuni hii hakuna uzao wowote ambao ungeweza kuzaa jinsi nyingine maana Mungu alisema kila uzao wa mche, na majani, na mti utoe mbegu (maana yake uzaliane kwa jinsi) zake, na hili nalo Mungu aliona ni vyema. Lakini wanadamu kwa ugunduzi wao wamefanya mfumo wa vitu kuzaliana si kwa jinsi vilivyoamriwa na Mungu. Utaratibu wa kupandikiza mbegu (breeding) ulioanzishwa na watu umepelekea utaratibu wa Mungu kuvurugwa na kwa hiyo sasa watu wanakula vitu visivyo vyema. Sasa hivi kuna kuku wa kisasa, ng’ombe wa kisasa, mimea ya kisasa, mayai ya kisasa n.k ambavyo vyote si vyema na vimechangia sana kuleta magonjwa ya ajabu katika dunia. Ni kile tu ambacho Mungu alisema ni chema hicho ndicho chema kweli kweli.

Jua, Mwezi na Nyota vinafanywa

Msitari wa 14-19, Mungu anafanya mianga miwili mikubwa pamoja na nyota. Mwanga mkubwa aliuamuru utawale mchana na ule mdogo utawale usiku. Sasa utakumbuka kuwa kuna jambo tuliliona kule kwenye siku ya kwanza juu ya nuru kuitwa mchana na giza kuitwa usiku na tukasema tutaliangalia jambo hili vizuri tukifika siku ya nne. Ni kweli kuwa Mungu alifanya jua na mwezi na nyota katika siku ya nne na jua akalipa kutawala mchana na mwezi na nyota usiku. Msitari wa 17 na 18 inatufunulia kuwa mianga yate hii ilipewa kutia nuru juu ya nchi na kutenga nuru na giza. Sasa tukiyafananisha haya majukumu ya hii mianga na kile tulichokiona kwenye msitari wa 4 na 5, tunagundua kuwa chanzo cha nuru halikuwa jua wala mwezi wala nyota, bali hivi vyote vilipokea nuru kutoka katika ile nuru kuu iliyofanywa siku ya kwanza na vikapewa kuangaza mchana na usiku. Ndio maana licha ya kuwa mwezi uliwekwa utawale usiku, lakini huwa hautoi giza bali mwanga na kila wakati mwezi utoapo mwanga wake, giza hutoweka hata kama ni usiku.  Hii inatudhirishia kuwa chanzo cha mchana sio jua na wala chanzo cha usiku sio mwezi wala nyota, bali ni nuru na giza kama vilivyowekwa siku ya kwanza. Soma Yeremia 31:35

Kwa hiyo jua na mwezi viliwekwa vitawale mchana na usiku na ili viwe ni ishara na majira na siku na miaka. Kwa sababu hiyo tunayahesabu majira na siku na miaka kwa kufuata usiku na mchana. Vitu hivi viliwekwa ili kutambulisha mpango wa Mungu wa kufanya mambo yake kwa siku na majira aliyoyaamuru yeye mwenyewe. Mungu mwenyewe anaweka mfano wa jambo hili kwa kuumba vitu vyote kwa siku sita. Ingewezekana kabisa Mungu kukamilisha kazi ya uumbaji kwa siku moja nayo bado ingekuwa vyema, lakini alitaka kuweka utaratibu wa mambo kufanyika kwa kufuata nyakati na majira yake. Hivyo usijaribu kutaka mimea ioteshwe kabla nchi haijatengwa kutoka kwenye bahari. Muhubiri 3:1 inasema Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. (msisitizo umeongezwa)

Kuna jambo la ajabu kidogo, nalo ni pale Mungu anaposema kuwa mwezi na jua vimewekwa viwe “ishara”. Kuna maandiko kwenye Biblia yanayolionesha jambo hili kwa uhalisia wake; Joshua 10:12-14, 2 Falme 20: 8-11. Nayo Luka 21:25 inasema:
Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake.

Ni vema kukumbuka kuwa kitabu cha mwanzo sura ya kwanza hakitaji kabisa majina kama jua, na mwezi. Neno jua linakuja kujitokeza katika Mwanzo 15:12, wakati mwezi unajitokeza katika Mwanzo 37: 9. Tunaifahamu tu ile mianga kuwa ilikuwa ni jua na mwezi kwa kuangalia kazi zake tu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika siku ya nne na Mungu akaona kuwa ni vyema.

Viumbe hai waendao wanafanywa

Msitari wa 20-23, akiisha kumaliza kazi hiyo Mungu anaendelea sasa na uumbaji baada ya kuwa amefanya mimea na majani na miti. Hii ni siku ya tano sasa na Mungu tena anaingia kwenye kazi ya kuumba wanyama, na ndege, na kila kiendacho chenye uhai. Viumbe wote wanaopatikana katika siku ya tano, nchi wala bahari hazikuamuriwa ziwatoe bali Mungu mwenyewe aliwaumba naye akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu anavipa viumbe hivi agizo la kuzaa na kuongezeka. Ni katika msitari wa 21 tunapata neno “Mungu akaumba” kwa mara ya pili. Hii inatuonesha aina nyingine kabisa ya viumbe ambavyo Mungu alitaka viwepo. Ni katika siku hii ndipo Mungu anapoanza kufanya “kiumbe chenye uhai.” Hakika hatulioni neno ‘uhai’ likijitokeza kabla ya hapo. Biblia inatufundisha kuwa ‘uhai wa kiumbe’ uko katika damu yake. Mwanzo 9:4 inasema:Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. (msisitizo umeongezwa) Damu ina kawaida ya kuzunguka mwilini mwa kiumbe na ikiwa damu itasimama basi uhai wa kiumbe hicho nao unakuwa hatarini.

Ndio maana Mungu anaviita hivi viumbe vyenye uhai kuwa ni ‘viumbe viendavyo’ yaani ‘moving creatures.’ Ni ule uhai ndio unaovifanya vitembee. Ilikuwa ni lazima Mungu aingie kwenye kazi ya kuumba hapa kwa sababu kabla ya hapo hapakuwa na kitu chenye uhai ndani yake na uhai haukutoka katika nchi, kama ilivyokuwa kwa mimea, bali kwa Mungu mwenyewe. Mungu alitaka kutufundisha kuwa hakuna uhai katika mwingine awaye yote isipokuwa katika yeye tu; nchi, jua, mwezi, nyota, mbingu, mchana, au hata usiku, vyote havikuweza kutoa uhai kwa ajili ya viumbe hawa bali Mungu mwenyewe. Mimea iliyofanywa katika siku ya tatu haikuhitaji Mungu aumbe kwa sababu Nchi ilikuwa na uwezo wa kutoa, lakini haikuwa hivyo ilipofika zamu za kufanya ‘viumbe viendavyo.’

Maneno ya msitari wa 20 kwenye tafsiri nyingi za kiingereza yametumika maneno haya:
And God said, Let the waters bring forth abundantly the moving creature that has life, and fowl that may fly above the earth in the open firmament of heaven.

Yale maneno ‘bring forth’ kwa Kiswahili ni ‘izae’. Kwa hiyo Mungu alisema maji na yazae kwa wingi kila kiumbe kiendacho chenye uhai. Ni ajabu sana kuona hapa kuwa maji hayakuzaa hivyo vitu mpaka msitari wa 21 unapotuambia kuwa Mungu akaumba. Nini maana yake?

Katika misitari yote iliyotangulia, kila wakati Biblia inaposema “Mungu akasema…” inamalizia na “ikawa hivyo.” Lakini ni ajabu sana katika suala hili la uumbaji wa vitu vyenye uhai, maana Mungu aliposema “maji na yazae (au yajawe)” hatuoni ikiwa hivyo, na cha ajabu zaidi ni kuwa hata Biblia yenyewe haitumii  neno “ikawa hivyo” kwenye habari hii. Baada ya kimya cha maji kushindwa kuzaa kama Mungu alivyosema, tunaona msitari wa 21 ukianza kwa kusema “Mungu akaumba…” Kwa nini ilikuwa Hivyo?

Tumetangulia kusema kuwa suala la uhai halikujitokeza ndani ya kiumbe chochote kile kilichofanywa na Mungu kabla ya hapo, hivyo hata maji yenyewe yaliyoambiwa yazae viumbe wenye uhai hayakuwa na uhai ndani yake ndiyo maana yalipoambiwa yazae yalikaa kimya mpaka Mungu mwenyewe alipoingilia kati. Mungu alitaka kutufundisha kuwa hakuna uhai katika mwingine au kitu kingine chochote isipokuwa katika yeye mwenyewe tu. Mambo yaliyokufa katika maisha yako hayawezi kupata uhai katika mtu au kitu chochote kile isipokuwa kwa Mungu tu kupitia kwa Kristo Yesu. Usitafute uhai wako kwa waganga, bali tafuta kwa Mungu. Hii nayo Mungu aliona kuwa ni vyema, siku ya tano ikakamilika.

Wanyama wafugwao na wa mwitu

Msitari wa 24-25, katika mwanzo kabisa wa siku ya sita vitu venye asili na uhai kama vile vilivyofanywa katika siku ya nne vinafanywa. Tofauti ya hivi na vile vya siku ya tano ni kuwa: hivi vya sasa havikuumbwa bali vilifanywa kwa neno navyo vikawa. Tunaona tena maneno “Mungu akasema … ikawa hivyo” yakijitokeza katika uumbaji wa viumbe hawa, ambao ni wanyama wafugwao na wa mwituni. Hawa wanyama walikuwa na uhai ndani yao lakini haikuhitaji tena kuumba kwa sababu tayari uhai ulishaumbwa katika siku ya tano. Ni katika siku hii kumbe ndipo Mungu alipotofautisha wanyama wa mwitu na wale wafugwao. Kwa hiyo tunapoona ng’ombe anafugwa nyumbani huku simba akiwinda porini tunaelewa kuwa ni uumbaji wa Mungu huo; hebu mtukuze Mungu kwa uweza wake wa ajabu. Na hii nayo Mungu aliona kuwa ni vyema, kisha akaendelea na kazi.

Mtu anaumbwa

Msitari wa 26-31, siku ya sita ndiyo ilikuwa kilele cha kazi ya uumbaji na ni katika siku hii ndipo Mungu alipoumba kitu chenye thamani na heshima na nguvu kuliko vyote alivyotangulia kufanya au kuumba. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” Hakika ni kwa sura yake na kwa mfano wa Mungu sisi tuliumbwa. Wacha tukuletee haya maneno ya mzaburi; Zaburi 8:4-6 inasema:
“Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima; Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.”

Ndivyo ilivyokuwa hakika katika Mwanzo 1:26-28. Yale maneno ya zaburi kuwa “Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu” yametafsiri na tafsiri kadhaa za kiingereza kwa kusema “You have made him a little lower than God” yaani umemfanya mdogo kidogo chini ya Mungu. Maandiko haya yanatufundisha kuwa Mungu kweli alimuumba mtu kwa sura na kwa mfano wake akamfanya tu awe mdogo chini yake asije akalingana na Mungu. Kisha akamvika taji ya utukufu na heshima, na kumtawaza juu ya kazi yote aliyoifanya Mungu, na akavitia vitu vyote chini ya miguu ya mtu huyo. Kama Mungu alivyosema “wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”

Maneno “Mungu akaumba” yanajitokeza tena kwa mara ya tatu katika msitari wa 27. Tunachogundua hapa ni kile kile kuwa hapakuwa na kitu kama kilichotangulia kufanywa na hivyo ilibidi Mungu aifanye kazi hiyo mwenyewe. Tunaona mashauriano ya Mungu katika ‘utatu mtakatifu’ akisema na tumfanye mtu. Hii inatuonesha kuwa hakuwa mmoja. Lakini pia inatuonesha kuwa mtu amefanywa kwa sura ya Mungu katika utatu wake, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hakika mtu alipewa neema ya kufanana na Mungu ndio maana Daudi anasema alimfanya awe mdogo kidogo tu kutoka kwa Mungu.

Katika kufanana huku na Mungu, mtu alipewa majukumu ya kufanya:
i)                    Kuzaa, na kuongezeka, (Be fruitful & multiply)
ii)                  Kuijaza nchi na kuitiisha(fill the earth and subdue it)
iii)                Kutawala(Have dominion)

Katika kutimiza majukumu haya, mtu anakuwa ametimiza kusudi ambalo Mungu alimfanyia na kwa hilo atapata kuishi na kufanikiwa. Wanasayansi na watafiti wa dunia wanajaribu kuupotosha ukweli huu wa kuwa mtu alitoka kwa Mungu na akapewa maagizo na Mungu ya jinsi ya kuishi. Maagizo hayo ya Mungu yanaweka wazi misingi ya kiroho, kimaisha, na kimaadili ambayo mtu anapaswa kuishi nayo. Lakini hawa wataalamu wa dunia wanajaribu kuupotoa ukweli huu ili kumtengenezea mtu mazingira ya kuihalalisha dhambi yake. Kile ambacho Biblia inakiita ‘dhambi’ wao wanakipuuza na kusema kuwa ni kujidhihirisha kwa ile asili ya unyama ambayo mtu alitoka kwayo. Watu wanapoanza kufanya zinaa kama wanyama wasio na akili, wao wanayatetea maovu haya kwa kigezo cha haki za binadamu; hakika watu hawa watajipatia hukumu iliyo kuu (Luka 20:47).

Mamlaka ya utawala aliyopewa mtu ni kubwa na inampa heshima na utawala kwa vitu vya rohoni na vya mwilini. Mungu alimuumba mtu ili apate kushirikiana naye katika kazi ya kuitawala na kusimamia mambo yote ya Rohoni na ya mwilini. Ilikuwa ni pale tu mtu alipoasi kwa dhambi ndipo akapoteza haki hii ya utawala. Ni neema ya Mungu kuwa haki hii tunarudishiwa tena katika Kristo Yesu.

Kuna jambo jingine linalojitokeza katika msitari wa 27 nalo ni kuwa Mungu aliwaumba mwanamke na mwanaume siku moja. Watu wengi wamekuwa na mtazamo kuwa mwanaume aliumbwa kwanza kisha mwanamke akaumbwa baadae. Hiki hakionekani kuwa hivyo kwa mujibu wa maandiko. Hebu ona Mwanzo 5:1-2 inachosema:
Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa.

Kwa hiyo wote waliumbwa siku moja, na jina lao wote waliitwa Adamu. Kinachotokea kwenye sura ya pili ni kudhihirishwa katika mwili kwa hawa wawili na hapo ndipo mwanamume anapotangulia. Kwa hiyo mwanamume na mwanamke ni kitu kimoja maana ule msitari wa 27 unaanza kwa kusema “… kwa mfano wake alimwumba (umoja)” halafu ndipo unasema “… mwanamume na mwanamke aliwaumba (wingi).” Maana yake ni kuwa kwanza aliumbwa mmoja lakini katika huyo mmoja walikuwemo mwanamke na mwanamume. Ndio maana hata kwenye kudhihirishwa kwa Hawa hatumwoni Mungu akiumba kitu kipya bali alimfanya kutoka katika mwanamume maana alikuwemo tayari ndani yake, na kuthibitisha hili Adamu hakushangaa wala kuuliza huyu ni nani pindi Mungu alipomleta mwanamke kwake.

Mistari ya mwisho ya sura hii inatufundisha kuwa majani na miche na miti na wanyama na kila kitambaacho juu ya nchi kiliwekwa kimsaidie mtu na kimtumikie mtu. Katika sura hii tunaona kuwa Mungu aliruhusu miche itoayo mbegu tu ndiyo iwe chakula cha mtu; japokuwa jambo hili anakuja kulibadili yeye mwenyewe katika habari za Nuhu.

Endelea kufuatilia mfululizo huu kwa ajili ya sura ya pili.  

 DOWNLOAD MWANZO SURA YA 1






1 comment: