Monday, May 4, 2015

MAMBO MATANO AMBAYO SHETANI HUFANYA ILI KUKUTOA KWENYE MPANGO WA MUNGU

OUR DAILY MANA

MAMBO MATANO AMBAYO SHETANI HUFANYA ILI KUKUTOA KWENYE MPANGO WA MUNGU
UTANGULIZI
Jambo la msisitizo kwenye somo hili ni kuwa kila mtu ambaye Mungu amempa nafasi ya kuwepo kwenye dunia hii anakusudi ambalo Mungu amemleta nalo na ambalo anapaswa kulitimiza bila kujali amekuja duniani kupitia njia gani au familia gani, au bila kujali kuwa alichukuliwa mimba hatiani au la!

Ninasema hivyo kwa sababu kama Mungu angeona hauna sababu ya kuletwa duniani asingeruhusu uzaliwe halafu uje tu kuongeza idadi ya watu. Au kama Mungu anaona kuwa sababu ya kuwepo kwako duniani imeshaisha basi angekuwa ameshakuondoa. Matendo 13:36 inasema “Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala….” Kwa hiyo mtu yeyote ambaye amekamilisha kazi aliyoitiwa kama Daudi, Mungu humwondoa, Hivyo tunapoona bado unaishi tunajua wazi kuwa kuna kazi ya Mungu ambayo bado inakungoja ndio maana Mungu anaendelea kukutunza.
Huwa ninatafakari gharama ambazo Mungu anatumia kunitunza kwa siku, halafu huwa nakosa majibu. Yaani nikifikiria gharama ambayo Mungu anatumia kuhakikisha kuwa napumua, sipatwi na mabaya, nasafiri salama, nakula, nasoma nafanikiwa, nafanya kazi zangu bila taabu, na mengine mengi halafu nikifikiri kama akiniambia nilipie hata senti moja kwa siku kama nitaweza, nabaki tu kujiambia moyoni mwangu kuwa ni lazima kuna sababu kwa nini bado sijafa. Na hii sababu ndiyo ninayoiita “kusudi la Mungu juu ya mtu.”

Ngoja nikuambie jambo hili mapema kabisa, kuwa: kabla wewe hujazaliwa Mungu alifanya kusudi la wewe kuwepo halafu ndipo Mungu akaruhusu wewe uzaliwe. Kabla Adamu hajaumbwa Mungu alitafuta kwanza kusudi na kazi ambazo Adamu angetakiwa kufanya. Ukisoma Biblia yako utaona Mungu akimuumba Adamu kwenye Mwanzo sura ya 2, lakini kazi na majukumu ya Adamu vilitangazwa Mwanzo 1:26-27. Kwa hiyo tunachogundua hapa ni kuwa kumbe kabla sijawekwa rasmi kwenye ulimwengu huu, Mungu alitangulia kunifanya kwenye ulimwengu wa Roho na akaweka na kazi nitakayofanya nikija duniani. Ndio maana anamwambia Yeremia “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Kwa hiyo Yeremia aliwekwa kuwa nabii hata kabla hajawekwa tumboni mwa mama yake. Jua na wewe leo kuwa kuna kusudi la Mungu kukufanya uishi hadi leo, na unatakiwa ulifahamu hilo kusudi ili uishi kwenye mpango wa Mungu.

Sasa jambo la kujua ni kuwa shetani naye anajua kuwa kila mtu ambaye Mungu amemweka duniani ana kusudi la Mungu ambalo mtu huyo anapaswa kulitimiza. Na kibaya zaidi ni kuwa wakati mwingine shetani anajua zaidi makusudi ya Mungu juu ya watu hata kuliko watu wenyewe. Sasa kutokana na shetani kuwa na uwezo wa kujua kuwa Mungu alikuleta kwa kusudi gani, kazi yake kubwa ni kupambana na wewe ili akutoe kwenye hilo kusudi. Lengo kubwa la shetani siku zote ni kuhakikisha kuwa anamtenganisha mtu na Mungu aliye hai, na ili afanikiwe katika lengo hilo silaha yake kubwa ni kumfanya mtu aache shauri (kusudi) alilopewa na Mungu na kumfanya atumikie shauri la shetani. Ndicho alichofanya kwa Adamu. Alipotaka kumtenga Adamu na Mungu wake cha kwanza alichofanya ilikuwa ni kumtoa Adamu kwenye nafasi aliyowekwa na Mungu na kumfanya akajifiche. Mwanzo 3:9-10 inasema:
Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.
Mungu anapomuuliza Adamu “Uko wapi?” haimaanishi kuwa Mungu alikuwa haoni kuwa Adamu amejificha ila alikuwa anauliza juu ya nafasi aliyokuwa amepewa; maana Mungu aliona nafasi haina mtu. Watu wengi leo shetani amefanikiwa kuwadanganya na kuwatoa kwenye nafasi zao na wengi sana wako mafichoni. YESU AKUTOE HUKO LEO KWA JINA LA YESU KRISTO ALIYE HAI
NJIA ZA SHETANI KUKUTOA KWENYE KUSUDI LA MUNGU
Ili shetani aweze kufanikiwa kwenye mpango wake wa kukutenga na Mungu ni lazima awe na njia au mkakati wa kufanikisha azma hiyo. Sasa ndiyo maana tunataka tuangalie mambo matano ambayo shetani anashughulika nayo sawasawa ili kukutoa kwenye mpango wa Mungu.
Waamuzi 16:4-5, 15-16, 18-19
4 Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila.  5 Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja…. 15 Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi….16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa…. 18 Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. 19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka…. 21 Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.
Ukisoma hayo maneno kwenye mistari hiyo hapo juu vizuri kuna habari ya kushangaza sana. Tunamwona Samsoni, mnadhiri wa Mungu, akimpenda mwanamke wa kifilisti jina lake Delila. Na wafilisti walipoona ya kuwa Delila amepata nafasi kubwa moyoni mwa Samsoni ikabidi watengeneze mkakati wa kumtumia ili kuweza kumwangamiza Samsoni. Wakamwambia “mbembeleze ili upate kujua asili ya nguvu zake nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa….”
Nia ya wafilisti iko wazi kabisa – ni kumfunga na kumtesa. Wafilisti hawakumficha Delila nia yao – walimwambia wazi kabisa na wakamweleza jukumu lake na mshahara ambao wangemlipa kwa kazi hiyo. Ukisoma maandiko utagundua kuwa vita ya Samsoni na wafilisti inaanza nyuma kidogo kabla ya hapo. Na walikuwa wamemwinda kwa style na mbinu nyingi sana bila mafanikio. Ghafula wakagundua mpango wa ajabu sana wa kumtumia mwanamke; wakagundua kuwa katika mambo ambayo yanaweza kukusaidia kumwangusha mwanaume kirahisi ni kwa kumtumia mwanamke. Walijua kuwa Samsoni si mtu wa kawaida na kwamba hata nguvu za wanajeshi wao haziwezi kumshinda Samsoni maana alikuwa ameshawapiga mara nyingi tu – alikuwa ameshapambana na simba akamrarua vibaya sana – alikuwa amewafunga mbweha mia tatu mikia akawawasha moto akawapitisha kwenye mashamba ya wafilisti. Kwa hiyo wafilisti walijua wazi kuwa Samsoni hawezi kushikika kirahisi, kwa hiyo ilibidi watafute “super plan.”
Ghafula wakagundua kuwa iko nguvu ya ziada ndani ya mwanamke. Swali la msingi la kujiuliza kawaida ni kuwa katika vitu vyenye nguvu ya kuleta mabadiliko duniani ni wanawake. Kama unataka mabadiliko ya aina yoyote ile duniani – yawe mema au mabaya we anza na wanawake tu. Ndani ya mwanamke Mungu aliweka nguvu ya kuzalisha na kuzidisha yaani “power of multiplying.” Sasa hiyo waliyopewa inaweza kutumiwa kuzalisha mema au kuzalisha mabaya. Mungu anataka awatumie wanawake kuzalisha vya kwake na shetani naye anawawinda wao ili wamsaidie kuongeza uovu duniani. Ndio maana utakuta timu nyingi sana za maombi zimejaa wanawake lakini pia utaona kuwa kichocheo kikubwa cha maovu duniani ni wanawake. Ndio maana vita waliyonayo wanawake kwenye ulimwengu wa roho ni kubwa sana.
Yeremia 31:22 inasema “…. Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.” Hii ni kitu ya ajabu sana maana kitabu cha Mwanzo kinatuambia kuwa Mungu alipomaliza kazi yake ya uumbaji aliona kila alichokifanya kuwa ni chema na akapumzika, akafunga kazi ya uumbaji. Lakini cha ajabu ni kuwa anakuja kumtumia Yeremia kutuambia kuwa kuna jambo jipya Mungu ameumba tena ya kuwa mwanamke amlinde mwanaume. Kwa nini Mungu alileta jukumu hili kwa mwanamke?
Mungu alipokuwa ameweka jukumu la ulinzi chini ya mwanaume, shetani alifanikiwa kumtumia mwanamke kumwangusha mwanaume.  Hivyo Mungu akaamua ampe mwanamke mwenyewe jukumu hili la kumlinda mwanaume. Hili jukumu shetani analijua vizuri sana na anajua kuwa ili ampate mwanaume basi inabidi atumie mwanamke Fulani. Angalia watumishi ambao walikuwa vizuri kihuduma halafu wakaanguka, utagundua kuwa kuna mwanamke aliyetumiwa kuleta anguko hilo. Sasa shetani akifanikiwa kumkamata mlinzi (mwanamke) basi shetani anakuwa amepata nafasi nzuri ya kumwangusha mwanaume. Hicho ndicho wafilisti walichofanya.
Sasa ile Waamuzi 16:15-16 inasema “Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.”
Tunachojifunza hapa ni kuwa licha ya Delila kuwa na nguvu ya kumshawishi Samsoni, hakufanikiwa kupata alichokitaka kwa mara moja tu. Ila alikua na moyo na kufuatilia hadi apate anachokitaka. Biblia inasema Delila alimsumbua Samsoni kwa maneno yake kila siku hadi roho ya Samsoni ikadhikika hata kufa.
Jambo la Kwanza
Kukusumbua kwa mashambulizi ya kila namna ambayo yatakukatisha tamaa hadi uachane na Mungu wako
Maandiko yanatuambia Delila alimsumbua Samsoni kwa maneno yake kila siku hadi alipokata tamaa na kuamua kutoa siri ya nguvu zake. Jambo ninalojiuliza hapa ni kuwa hayo maneno aliyokuwa anamwambia yalikuwa maneno ya namna gani? Zaburi 10:7 inasema “Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu.” Huu msitari unatuambia kuwa ulini wa mtu unaweza kubeba madhara na uovu. Hiki ndicho kilichompata Samsoni; ulimini mwa Delila kulikuwa kumejaa maneno ya uovu na madhara ambavyo vililenga kumwangamiza Samsoni. Na Biblia inatuambia kuwa yale maneno yalimsumbua Samsoni kiasi ambacho roho yake ilifika mahali ikachoka.
Yale maneno ya Delila hayakumpa Samsoni nafasi ya kupumzika. Tafsiri za kiingereza zinasema kuwa “she gave him no peace” yaani hakumpa nafasi hata ya kupumzika bali alimsumbua kila siku. Kwa hiyo adui alimzingira kwa maneno ya kumkosesha amani kila siku hadi alipochoka. Hiki ndicho shetani hufanya anapotafuta kukutoa kwenye mpango wa Mungu. Atahakikisha amekusumbua kwa kila aina ya matatizo na mikosi na kushindwa na kila jambo la kukatisha tamaa hadi uchoke. Atatafuta ni eneo gani la maisha yako linalokupa furaha kisha atashambulia hilo eneo hadi uone Mungu amekuacha. Atakachofanya ni kuisumbua roho yako ikose nafasi ya kumtafuta Mungu. Ndio maana watu wengi wakiwa kwenye matatizo huwa wanakosa hata hamu ya kuomba au hata kwenda kwenye ibada. Hii si kitu ya kawaida, shetani anawinda kukukosesha amani ili apate mwanya mzuri wa kukumalizia.
Utaona hata ukienda kwa wapendwa wenzio unaona kama wanakung’ong’a, ukirudi nyumbani unaona kama familia ni chungu, ukienda kazini unakuta umefukuzwa kazi au wafanyakazi wenzio hawako pamoja na wewe. Yaani unakuta kila kitu hakiendi sawa. Ukiona hivyo anza kukaa sawa na Mungu maana ni dalili ya mashambulizi ya shetani kukutoa kwenye mpango wa Mungu. Shetani akiona kuwa hawezi kukupata wewe moja kwa moja atakachofanya ni kushambulia vitu vinavyokupa amani. Utakumbuka habari za Ayubu na jinsi shetani alivyoshambulia mifugo yake, mashamba yake, watoto wake na mwisho akampa majipu makali sana. Shetani alikuwa hatafuti mashamba wala watoto wala afya ya Ayubu, yote hayo yalikuwa mashambulizi yaliyolenga kumtoa kwenye mpango wa Mungu. Shetani anajua akikusumbua sana utapoteza network yako kwa Mungu.
Jambo la Pili
Shetani atakuletea usingizi wa kiroho ili iwe rahisi kwake kutimiza mpango wake
Waamuzi 16:18-19 inasema “Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.  Naye akamlaza usingizi magotini pake…”
Mathayo 13: 24-25 inasema “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.”
Swali kujiliza hapa ni kuwa kama Samsoni alikuwa ameshamwambia Delila siri yake yote kulikuwa na haja gani tena ya kumlaza usingizi? Jibu lake ni wazi kabisa. Delila alijua wazi kabisa kuwa suala la kumnyoa Samsoni vishungi vya nguvu zake lisingewezekana kama Samsoni angekuwa macho maana ni lazima angepigana na wafilisti wasingefanikiwa. Shetani anajua wazi kuwa hawezi kukutoa kwenye mpango wa Mungu ikiwa rohoni uko macho maana utapambana naye na utamshinda. Kwa hiyo anatakachofanya ni kukufanya ulale kiroho ndipo aje kukumaliza. Shetani anajua kuwa akija wakati uko macho utamwona na utapambana nae, kwa hiyo atakuvia wakati ambao kiroho umelala.
Shetani anajua kuwa kanisa ambalo lina waombaji waliomacho hawezi kulishinda hivo atatafuta daima namna ya kuwalaza usingizi ili aweze kuwashinda. Katika dunia ya leo shetani amefanikiwa kuwalaza usingizi watu wengi kwa njia nyingi sana. Kuna watu walikuwa waombaji wazuri lakini walipopata kazi (ajira) wakawa busy na kazi na wakaacha kabisa kusoma neno la Mungu na maombi wakasahau kabisa. Ukiwauliza watakuambia kuwa wako busy na kazi. Lakini hawajui kuwa shetani ametumia kazi zao kuwalaza usingizi ili wasimtumikie Mungu. Wengine shetani amewalaza usingizi kwa kupitia teknolojia. Watu wengi wako tayari kuangalia TV hadi macho yakauma lakini ukiwaambia kusoma Biblia hata sura moja kwa siku watakuambia kuwa hawana muda. Watu wengi leo wanatumia simu ambazo badala ya kuwasaidia kumtafuta Mungu zinawasaidia kujitenga na Mungu. Unakuta mtu anamiliki simu ambayo inauwezo wa facebook, twitter, whats app, na pia ina uwezo wa kuwa na Biblia. Lakini utakuta ame-install program zingine zote lakini Biblia hajaweka. Au anayo lakini kila anapokuwa anakuwa anaipita tu kama haioni. Anakuwa busy na kwingineko kote lakini sio kwenye maandiko.
Nimezunguka kwenye makanisa mengi sana hapa nchini na kujionea hali za kiroho za makanisa hayo jinsi zilivyo. Nasikitika kusema kuwa hali ya kanisa sasa hivi ni ile iliyoandikwa katika Ufunuo 3:1
Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.
Hili ndilo kanisa la sasa na watu wake jinsi tulivyo. Tumebaki na majina ya historia za jinsi tulivyokuwa zamani lakini sasa hivi wengi shetani amewalaza usingizi. Utasikia mtu anasema: enzi zangu banaaa… nilikuwa mwombaji sana, mwingine anasema nilikuwa nasoma sana neno la Mungu, mwingine nae anasema nilikuwa mfuatiliaji mzuri sana wa ibada n.k. Swali ambalo huwa najiuliza ni: huo uwezo umeenda wapi? Kuna watu wengi leo wanasema kuwa wanasali makanisa ya kiroho lakini wao wenyewe sio watu wa rohoni. Watu wengi wamelazwa usingizi na shetani.
Bahati mbaya ni kuwa ukiwa umelala usingizi hujui kinachoendelea juu yako. Na ndivyo walivyo watu wa leo, wengi wamelala usingizi kiasi kwamba hawajui hata kile shetani anachofanya kwenye maisha yao. Kutokana na usingizi waliolala wanajiona kuwa bado wanamtumikia Mungu kumbe shetani alishawamaliza nguvu zao.
Waefeso 5:14 inasema, “Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”
Jambo la Tatu
Shetani atahakikisha ameharibu chanzo cha nguvu zako za kiroho
Waamuzi 16:19 “…Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.”
Shetani atahakikisha kuwa ameua asili ya nguvu zako ili afanikiwe kukumaliza kabisa kiroho. Baada ya kukulaza usingizi wa kiroho kitakachofuata ni kuua msingi wa nguvu zako; maana akipiga chanzo anakuwa amekugeuza kutoka kwenye kuwa hai unabaki mkristo aliyekufa kiroho. Chanzo kikipigwa ndipo unakutana na watu wenye majina ya kuwa hai lakini wamekufa. Chanzo kikipigwa ndipo unaanza kusikia mtu anasema: “nilikuwa mwombaji sana” “nilikuwa mtu mzuri sana wa neno la Mungu” n.k.
Ukiona mtu anaanza kusimulia habari za utumishi wake wa nyuma ambao kwa sasa hawezi kuufanya ujue kuwa chanzo cha nguvu zake kimepigwa. Shetani akiisha kukuweka busy na shughuli za dunia na kufanikiwa kukulaza usingizi, atakachofanya baada ya hapo ni kunyoa vishungi vya nguvu zako ili usiwe na mtaji tena wa kusimama. Watu wengi leo shetani ameua vyanzo vyao vya nguvu za kiroho na wamebaki na historia tu kuwa waliwahi kufika mahali Fulani kiroho. Usiruhusu shetani anyoe chanzo cha nguvu zako, usiruhusu shetani aharibu mtaji wako wa kiroho. Kama asili yako ni maombi basi usiruhusu jambo lolote lile likuzuie kuomba; unahitaji kuchochea chanzo cha nguvu zako kila siku.
Jambo la Nne
Shetani atakuletea mahangaiko na mateso makali ya kimaisha ili uachane kabisa na imani yako kwa Mungu
Waamuzi 16:19 “… Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.”
Baada ya shetani kuwa amekusumbua kule mwanzo kwa mashambulizi ya kila namna na kukatisha tamaa, na baada ya kuwa ameshakulaza usingizi na kisha kuharibu chanzo cha nguvu zako, sasa atakachofanya ni kuleta juu yako mahangaiko na mateso ambayo yatakufanya usimkumbuke kabisa Mungu wako. Delila aliamua kumsumbua Samsoni baada ya kuwa amemnyoa vishungi vya nguvu zake ili kuhakikisha kuwa hakuna nguvu hata kidogo iliyosalia ndani ya Samsoni ambayo inaweza kumsaidia akainuka tena. Ndicho shetani anachofanya; akiishavunja chanzo cha nguvu zako ataendelea kuleta mashambulizi mengine mengi ili ukose kabisa nafasi ya kumrudia Mungu na ukose kabisa nguvu za kusimama tena kiroho.
Ndio maana 2Petro 2:20 inasema:
Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.
Hali yao mwisho inakuwa mbaya kwa sababu shetani akifanikiwa kukunasa kwenye mtego wake atafanya kila jambo ili kuhakikisha kuwa haurudi tena kwa Mungu wako.
Jambo la Tano
Shetani akiisha kukukamata atakufanya ulitumikie shauri (kusudi) ambalo hukuitiwa
Waamuzi 16:21 “Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”
Tumejifunza mwanzoni kuwa kila mtu ambaye Mungu amempa nafasi ya kuishi amempa na shauri ambalo mtu huyu anapaswa kulitumikia. Lakini shetani akikukamata na kukuweka chini ya himaya yake atakutoa kwenya kazi ambayo Mungu alikuitia na kukupeleka kwenye kazi ambayo hukuitiwa kabisa. Samsoni aliwekwa awe mnadhiri wa Mungu na alipaswa kuwatetea waisraeli dhidi ya adui zao. Lakini shetani alipofanikiwa kumweka chini ya himaya yake alimfanya akalitumikie shauri la wafilisti kwa kusaga ngano gerezani.
Leo hii wapo watumishi wa Mungu wengi sana ambao shetani anawasagisha ngano gerezani badala ya kumtumikia Mungu. Wapo wachungaji wanaosaga ngano, wapo waimbaji wanasaga ngano, wapo walimu, mitume, manabii n.k. ambao wanajidai kuwa wanamtumikia Mungu lakini kimsingi wanasaga ngano kwenye magereza ya wafilisti. Ikiwa ni mtumishi wa Mungu kweli kweli hebu angalia sana huduma Mungu aliyokupa usije kuwa unadhani bado unamtumikia Mungu kumbe macho yako yametobolewa na unasaga ngano kwenye gereza la wafilisti.
Unaweza ukafikiri kwamba labda atakuvikwa kuwa mwenye dhambi wa kutupwa, lakini nataka kukwambia kuwa shetani atakutumikisha kwenye shauri lolote lile ambalo anajua kuwa litakufanya uunufaishe ufalme wake. Anaweza akakuacha uendelee kuwa muumuni wa kanisa lako lakini kazi yake ni kuvuruga kazi ya Mungu mahali hapo isiende mbele. Utaona mtu anakua mchonganishi na mwenye kuvuruga kila kikundi cha kihuduma kinachoinuka. Kwa vile aliwahi kuwa mtumishi mzuri basi watu wanamwamini sana kiasi kwamba hawadhani kama yeye ndiye anayesababisha vurugu. Lakini kila kikundi anachoenda kinakufa – oooh ujue huyo ni anaesaga ngano kwenye gereza la shetani.
NEEMA YA KUREJESHWA TENA
Muhubiri 3:15 inasema “Yale yaliyoko yamekuwako; na hayo yatakayokuwako yamekwisha kuwako; naye Mungu huyatafuta tena mambo yale yaliyopita.”
Maneno haya yanatufundisha kuwa licha ya wakati mwingine kuwa tumepoteza uhai wetu kwa Bwana, Mungu anao uwezo wa kuturejesha tena kwenye mpango wake maana yeye huyatafuta tena mambo yaliyopita ili atuinue tena. Ijapokuwa shetani anaweza akawa amekuangusha na kukutoa kwenye mpango wa Mungu nataka kukwambia kuwa kuna kuinuka tena. Samsoni alitobolewa macho, akanyolewa nywele zake, akasagishwa ngano gerezani lakini Mungu alimrejeshea tena ushindi mkubwa. Ayubu 22:29 inasema “Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.”
Waamuzi 16:22 inasema “Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.” Haya maneno yanatuonesha kuwa licha ya kunyolewa kwake, bado Mungu alikuwa ameacha mzizi wa nywele ndani ya Samsoni. Haijalishi walikuwa wamemnyoa kipara au aina gani ya kinyozi ila ninachokijua ni kuwa hawakunyoa hadi mzizi wa nywele. Nataka kukwambia hivi: ikiwa shetani amekunyoa nywele zako bado liko tumaini kwa Bwana. Mungu anao uwezo wa kukuinua tena na kukuinulia tena nguvu zako. Bado Bwana anayo nafasi ya kukusimamisha mbele ya adui zako na kuwaangamiza mbele yako. Mwisho wa huduma yako bado haujafika, Mungu anazo nguvu za kukusimamisha tena.
NAKUPA SHAURI MKUMBUKE MUNGU NAYE ATAKUINUA TENA



No comments:

Post a Comment