Friday, July 1, 2016

MAMBO SITA (6) UNAYOPASWA KUYATAFUTA HAPA DUNIANI



… tafuteni, nanyi mtaona … (Mathayo 7:7)

Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe!

Leo katika darasa letu la maandiko nataka tuangalie juu ya mambo ambayo Biblia inatuafundisha kuwa tunapaswa kuyatafuta tungali hapa duniani. Pia mwishoni tutaangalia mambo ambayo Biblia inatuonya tusiyatafute wala kuyahangaikia. Karibu ushiriki nasi kujifunza siri hii Mungu aliyotufunulia kwa majira haya!

Utangulizi

Katika kitabu cha Mathayo 7:7 Yesu alituelekeza juu ya vitu vitatu vya kufanya: kuomba, kutafuta na kubisha. Kila kimoja katika vitu hivi ni somo tosha na linalojitegemea – ila kwa madhumuni ya somo hili tutaangalia hiki kipengele cha “tafuteni, nayi mtaona.”

Jambo la ajabu sana la kujua mapema ni kuwa Yesu alipotuambia “tafuteni, nanyi mtaona” hakusema tutafute nini! Anachofanya ni kutupa uhakika kabisa kuwa tukitafuta tutaona lakini hatuambii ni kitu gani hicho ambacho tunapaswa kukitafuta ili tukione. Lakini jambo moja ambalo tuna uhakika nalo ni kuwa Yesu hawezi kutoa ahadi hewa! Ikiwa alituambia “tutafute nasi tutaona” basi ni dhahiri kuwa liko jambo au mambo aliyotaka kutujulisha kuwa yapo na tunauwezo wa kuyaona endapo tutaamua kuyatafuta. Kwa msingi huo basi ni jukumu la kila anayeamini katika neno la Kristo kuweka bidiii ya kutaka kujua ni mambo gani haya ambayo Yesu mwenyewe ametuhakikishia kuwa tukiyatafuta tutayaona. Msingi wa somo hili ni kutaka kukufunulia baadhi ya mambo ambayo Biblia imetuagiza tuyatafute na faida zake pale tutakapoyatafuta.


 
Kwa nini ni muhimu kujifunza nini cha kutafuta?


Somo hili ni muhimu kwa sababu tusipojua yale yatupasayo kuyatafuta tukiwa hapa duniani basi tutajikuta tumepoteza muda mwingi kuhangaikia vitu ambavyo mwisho wake itakuwa ni mauti kwetu. Mithali 16:25 inasema “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.” Maana ya msitari huu ni kuwa kuna wakati mwanadamu huwa anafanya vitu akifikiri kuwa yuko sahihi lakini mwishowe vitu hivo humwangamiza.
Labda bado hujaelewa ninachotaka uone hapa! Hebu sikiliza maneno haya mfalme Sulemani:
Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu. Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo. (Muhubiri 1:12-14)

Sulemani alijaliwa hekima na Mungu, na yeye akaitumia hekima aliyopewa ili atafute kujua mambo yote yanayotendeka duniani (chini ya mbingu). Baada ya kutafuta yote na kuyavumbua akaishia kusema kuwa “yote ni ubatili na kujilisha upepo.” Kwa lugha rahisi ni kuwa aliwekeza nguvu nyingi kutafuta mambo ya dunia hii na mwisho wake hakupata faida yoyote katika mambo hayo aliyoyagundua. Kwa hiyo kwa muda wote aliotumia kutafuta ufahamu huo ilikua amepata hasara. Sasa unaweza ukaelewa ni kwa jinsi gani ilivyo muhimu kwa sisi tuliofikiwa na miisho ya zamani hizi kujitia bidii katika kutafuta kujua kile ambacho Mungu mwenyewe amesema tukitafute. Ni muhimu sana kujua Mungu ametuagiza tutafute nini muda tungalipo duniani ili tusije tukatumie muda wetu kutafuta vitu ambavyo mwishoni tutagundua kuwa ni “ubatili na kujilisha upepo.” Sasa ungana nami katika kujifunza mambo haya ambayo Bibilia imetuagiza tuyatafute.

JAMBO LA KWANZA:
Utafute ufalme wa Mungu na haki yake

Hili ni jambo la kwanza kabisa ambalo Yesu mwenyewe aliagiza tulitafute. Utashangaa kugundua kuwa suala hili la kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake ni Yesu mwenyewe aliyesema kuwa ni la kwanza. Mathayo 6:33 inasema: “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Yesu anatuwekea mpangilio wa vipaumbele vya vitu vya kutafuta tukiwa hapa duniani na cha kwanza anasema ni kuutafuta ufalme wake na haki yake. Sasa utaniuliza: ufalme wa Mungu ni nini na unautafutaje? Majibu yapo kwenye Biblia yenyewe iliyosema tuutafute! Luka 17:20-21 inasema:
Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.

Kwa mujibu wa maneno hayo ya Yesu ni kuwa ufalme wa Mungu uko ndani yetu. Lakini sasa swali la kujiuliza ni kuwa kama ufalme wa Mungu uko ndani yetu ni kwa nini atuambie tena tuutafute? Hii inatupa kujua kuwa kuna kitu ambacho inabidi tukitafute ambacho hicho ndicho kinachoashiria uwepo wa ufalme wa Mungu ndani yetu. Mtume Paulo katika Warumi 14:17 anasema hivi:
Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.

Tena katika 1 Kor 4:20 anasema: “Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.” Mtume Paulo anatupa kujua kuwa maana ya ufalme wa Mungu ni “haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” Kwa hiyo Yesu aliposema ufalme wa Mungu uko ndani yetu alikuwa anamaanisha kuwa pale tunapokuwa na “haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu” hapo ufalme wa Mungu unakuwa uko ndani yetu. Sasa mambo haya matatu –haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu- hayapatika kwa maneno matupu bali kwa nguvu. Ndio maana sasa utaona ile 1 Kor 4:20 Paulo anasema “ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.” Kumbuka pia maneno ya Yesu katika Mathayo 11:12 kuwa: “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.”

Kwa hiyo ufalme wa Mungu – ambao ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu – unapatikana nguvu na ni wenye nguvu tu ndio wanaouteka. Sasa hii inaanza kutupa picha ya kwa nini Yesu amesema tuutafute ufalme wake na haki yake. Utakumbuka kuwa katika Mathayo 6:33 Yesu alisema tuutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake kisha mengine tutazidishiwa. Sasa utajiuliza kuwa haya mengine nitazidishiwa kutokea wapi?

Misitari inayotangulia kabla ya hiyo Mathayo 6:33 inaonesha Yesu akiwaonya watu wasijisumbue juu ya wale nini au wanywe nini au wavae nini – kwa sababu hata mataifa huyasumbukia hayo. Kimsingi harakati zote za mwanadamu katika maisha yake anahangaika ale nini, avae nini, anywe nini. Sasa ukichunguza kwa makini utangundua kuwa haya mambo ambayo mwanadamu anayahangaikia lengo lake ni ili awe na amani na furaha ya maisha. Sasa haki, amani na furaha ni vitu ambavyo viko vimehakikishwa [guaranteed] kwenye kifurushi [package] ya ufalme wa Mungu (rejea Warumi 14:17).

Kumbe tunagundua kuwa vitu ambavyo mwanadamu anajisumbua kuvitafuta kila siku na anapata shida sana kuvipata anaweza kuvipata kwenye package aliyowekewa na Mungu kwenye kifurushi kinachoitwa “ufalme wa Mungu.” Kumbe ndio maana Yesu anatuambia tutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake – akiwa na maana kwamba pindi tutakapoupata ufalme wa Mungu basi tutakua tumeyapata na mengine yote tunayoyasumbukia kila siku. Hebu sikiliza haya mazungumzo ya Yesu na Petro:
Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele. (Mathayo 19:27-29)

Sasa jambo la kuzingatia hapa ni kuwa huu ufalme wa Mungu unapatikana kwa nguvu na ni wenye nguvu ndio wanaouteka. Hapa sasa ndipo utakapoelewa ni kwa nini tuna walokole wengi wanaomwamini Yesu lakini hali zao za maisha sio nzuri. Hiyo ni suala la kiwango cha nguvu itendayo kazi ndani ya Mtu husika (Waefeso 3:20). Katika sala ya Bwana moja mbinu ambazo Yesu alitufundisha kuomba ni ile ya kuomba ufalme wa Mungu uje! Alituwekea hii mbinu kwenye sala ya Bwana ili tutambue kuwa ufalme wa Mungu (yaani nguvu ya Mungu) isipokua ndani yetu hatuwezi kupata tunayotafuta. Hili ni jambo la kuzingatia sana kuwa kama nguvu inayozalisha ufalme wa Mungu haiko ndani yako basi ni ngumu sana kufaidika na Baraka zilizomo katika ufalme wa Mungu hata kama wewe umeookoka. Ndio maana sasa Paulo katika Waefeso 6:10 anasema “Hatimaye mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.”

JAMBO LA PILI:
Utafute uso wa Bwana

Napenda ujue tokea mwanzo kuwa tunapozungumzia kuutafuta uso wa Bwana tunazungumzia kumtafuta Bwana. Mtu anayemtafuta Bwana pia anakua ameutafuta uso wa Bwana – kwa hiyo utakuta mara kadhaa Biblia inatumia maneno “mtafuteni Bwana” na “utafuteni uso wa Bwana” kwa kuumaanisha kitu kile kile ambacho msingi wake ni “kutafuta uwepo wa Mungu kati yetu.”
Napenda ufahamu mapema kabisa kuwa suala la kuutafuta uso wa Bwana ni agizo ambalo limetoka kwa Mungu mwenyewe. Zaburi 27:8, Daudi anasema:
Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.

Msitari huu hapo juu unatujilisha kuwa ni Mungu ndiye aliyesema watu wautafute uso wake, na Daudi anatii agizo hili akisema “Bwana uso wako nitautafuta.” Ukisoma Biblia yako vizuri utakuta maeneo mengi sana ambayo Mungu anawaita watu wake wamtafute.

Kwa nini lazima tuutafute uso wa Bwana

Isaya 55:6 inatuambia hivi: “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu.” Maneno haya yanatuambia jambo la ajabu sana kuwa Bwana anapatikana na tena yu karibu. Sasa kama Bwana yu karibu tena anapatikana, ni kwa nini tumtafute? Biblia inatupa kujua sababu za kwa nini tumtafute Bwana wake amesema anapatikana!

Sababu ya kwanza: Mungu ana sifa ya kujificha uso wake.

Isaya 45:15 neno la Mungu linasema hivi: “Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.” Labda wacha nikueleze jambo hili hapa ili tuende pamoja. Tangu mwanzo Adamu na Eva walimwasi Mungu na kuruhusu dhambi itawale, Mungu hamwamini mtu tena. Na kwa hiyo amejiweka mbali na wanadamu ili kwamba kila mtu amtakaye Bwana – amtafute!

Utaratibu wa kabla ya dhambi ilikuwa inampasa Mungu kuja kumtembelea Adamu bustanini kila siku, lakini baada ya dhambi kuingia utaratibu ukabadilika. Sasa Mungu anaonekana kwao tu wenye haja ya kumwona, na ndio maana inabidi tumtafute. Ngoja niseme hivi: sasa hivi Mungu anaonekana [by demand] – yaani kabla hajaonekana kwako lazima uwe umeonesha haja ya kwamba unamwitaji. Ndio maana Yesu akasema Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe (Yohana 7:37). Maana yake – asiye na kiu asije kwangu! Lazima uoneshe kiu yako ya kumwitaji Mungu ndipo Mungu aonekane kwako. Na hiyo kiu sasa ndio inayokusukuma kumtafuta Mungu. Ukiwa na kiu lazima uende – usije ukafikiri kiu yako tu inatosha kumfanya Mungu ajifunue kwako. Yesu hakusema “mtu kiona kiu, anyweshwe” bali alisema “mtu akiona kiu, aje kwangu anywe”. Kwa hiyo ni lazima wewe unayeona kiu uchukue hatua ya kuenda kwake ili unywe. Usipoenda utabaki kuwa na kiu yako na utakufa nayo wakati maji yalikuwepo.

Sababu ya Pili: ni ili uweze kuishi na kuwa na uzima ndani yako

Amosi 5:4,6,8 inasema hivi:
Maana Bwana awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi; Mtafuteni Bwana, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu, nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli. Mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina lake.

Mungu anaagiza watu wamtafute ili waishi. Maana yake mtu asiyetaka kuutafuta uso wa Bwana hana uhai ndani yake – amekufa ijapokuwa bado yuko duniani. Sasa hapa utaelewa kwa nini Yesu alisema “Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi (Yohana 11:25).”

Uhai unaozungumzwa hapa sio suala la kuishi hapa duniani bali ni uzima wa Mungu katika maisha yako ya sasa na uzima wa milele katika ulimwengu ujao. Tunapaswa kumtafuta Mungu ili tuwe na huu uzima ndani yetu. Matendo 17:26-28 inasema hivi:
Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu.

Mistari hii inatufundisha kuwa Mungu aliwawekea watu mipaka ya nyakati na makazi ili wamtafute hata kama ni kwa kupapasa-papasa kwa sababu ndani yake tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu. Kwa lugha rahisi ni kuwa tusipomtafuta Mungu tunakuwa tumejinyima haki yetu ya kuishi pamoja na Mungu na kwa hiyo tutaukosa uhai wetu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.
Sababu ya tatu: Ili Mungu akufanikishe na kukustarehesha
Biblia inatuambia kuwa kuna mafanikio ya wacha Mungu lakini pia kuna mafanikio ya wapumbavu. Lakini Mithali 1:32 inatuambia kuwa “kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.” Napenda kukusihi uwe makini na aina ya mafanikio unayotafuta, kwa sababu ukifanikiwa kipumbavu hayo mafanikio yatakuangamiza.

Zaburi 35:27 inatuambia kuwa Mungu anafurahishwa na amani (mafanikio) ya mtumishi wake. Na katika hilo Mungu anatamani sana ahusike kwenye mafanikio ya kila mtu aliyeko duniani. Mungu hataki ufanikiwe bila yeye kuwepo kwa sababu mafanikio yoyote nje ya Mungu yatakuangamiza. Ndio maana ameweka utaratibu wa watu kumtafuta ili awafanikishe. Wacha tuangalie mistari michache ya Biblia.

Mithali 8:17-21Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia. Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule. Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.”

2 Nyakati 14:2-7 Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa Bwana, Mungu wake; maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera; akawaamuru Yuda wamtafute Bwana, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu Bwana amemstarehesha. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta Bwana, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa.

2 Nyakati 26:3-5 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye. Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.

Nimekuwekea hii mistari ili uone jinsi ambavyo kumtafuta Mungu kunasababisha mafanikio ya watu wa Mungu. Asa aliwaamuru Yuda wote wamtafute Mungu na vile walivyomtafuta, Mungu akawafanikisha na kuwastarehesha. Tunaliona jambo hili pia kwa Uzia ambae alianza kumtafuta Mungu akiwa na miaka 16 na muda wote alipomtafuta Bwana Mungu alimfanikisha. Nataka uelewe kuwa huwezi kuendelea katika njia yako mwenyewe na kufanikiwa usipomtafuta Mungu na kumweka awe sehemu ya maisha yako.

Ndio maana Mungu alipokataa kutembea na Israeli kuelekea Kanani – akasema atawapa malaika aende nao, Musa naye aligoma kuondoka pale walipokuwa. Kutoka 33:15 Musa anamwambia Mungu “Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.” Kwa nini Musa alikataa kuondoka kama uso wa Mungu usingeenda nae? Ni kwa sababu raha ya Israeli na mafanikio yao yote yalitegemea uwepo wa Mungu kati yao. Angalia Mungu anachojibu kwenye Kutoka 33:14, anasema “uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.” Maana yake uso wa Mungu usingeenda pamoja nao wasingepata raha huko waendako. Sasa kwa nini wewe unataka kufanikiwa mwenyewe bila uso wa Mungu kuwa pamoja nawe?

JAMBO LA TATU
Tafuta kuwa na amani na watu wote

Kuna watu wanapenda kusema kuwa ‘huwezi kuwafurahisha watu wote duniani.’ Mimi huwa sikubaliani na msemo huu kwa sababu hii ni kauli ya watu wanaotaka kuhalalisha kuwa kwao na ugomvi na watu wengine. Biblia inapinga kitu hiki. Waebrania 12:14 inasema: “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote.”

Utaona katika msitari huu kuwa - amani na watu wote ni jambo linalopaswa kutafutwa kwa bidii. Kwa hiyo hatuwezi kuridhika na kauli kuwa ‘huwezi kuwafurahisha watu wote.” Biblia haisemi tafuteni kwa bidii kuwafurahisha watu wote bali inasema tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote. Kwa sababu hiyo sio vema kuwa na mafarakano na kuishi kwenye kutoelewana na watu wengine. Angalia jinsi mtume Petro anavyosema juu ya jambo hili katika 1 Petro 3:10-11
Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana.

Huu ni ujumbe wa ajabu sana – kwamba kila mtu anayependa maisha na kupenda kuona siku yake imekaa vizuri basi asinene mabaya bali atende mema na kutafuta amani, tena hii amani aitafute sana. Sasa utagundua kuwa Wakati Waebrania inatuambia kuwa tutafute amani kwa bidii, Petro anasisitiza kwa kutuambia kuwa tuitafute sana.

Kwa msisitizo huu ambao Biblia imeweka kwenye jambo hili tunapata kuelewa kabisa kuwa suala la kuwa na amani na watu wote sio suala la kupuuza – sio suala la kuchukulia kijuu-juu tu. Lazima tulipe uzito wake unaostahili na tuitafute hiyo amani sana na kwa bidii hadi tuipate.

Madhara ya kutokuwa na amani

Maisha ya watu wengi yamesimama pasipo kusonga mbele kwa sababu ya kutokuwa na amani. Kukosekana kwa amani kunaleta uchungu na huzuni ya moyo ambayo madhara yake ni kupunguza kasi ya mafanikio ya mtu huyo. Isaya 38:15 inasema:
Nitakwenda polepole miaka yangu yote, kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.

Utaona kwenye msitari huo hapo juu jinsi ambavyo suala la kukosa amani lilivyo na madhara makubwa. Huyu mtu anasema miaka yake yote atakwenda polepole kwa sababu ya uchungu wa nafsi yake. Kwa hiyo kwenye kila eneo la maisha yake ana [slow down] kwa sababu tu hana amani, na hii ni kitu anasema itamgharimu miaka yake yote. Huwezi kuelewa ubaya wa kukosa amani kama bado hujawahi kupita kwenye eneo hilo. Lakini nataka kukwambia kuwa kwenye eneo lolote lile ambalo hakuna amani mafanikio ya eneo hilo lazima yana [slow down].

Angalia nchi zenye vita, angalia familia zenye ugomvi, angalia makanisa yenye migogoro kote huko utagundua kuwa kama walikua wanakimbia kwa spidi fulani hapo mwanzo, ule ugomvi ulio kati yao umepunguza kwa kiasi kikubwa sana maendeleo na mafanikio yao. Ndio maana katika Yeremia 29:7 utaona Mungu anawaagiza Israeli akisema:
Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani.

Sasa utajiuliza ni kwa vipi Mungu awaagize Israeli wautakie amani mji ambao wao ni mateka. Ni kama vile anawaambia wawaombee wanaowatesa. Lakini utagundua kuwa hata kama walikuwa utumwani bado walihitaji kufanikiwa na kuendelea kuishi na hakuna namna ambavyo wangefanikiwa nje miji waliyokuwa wanaishi. Kwa hiyo ili wao wafanikiwe ilikuwa ni lazima miji wanayokaa ifanikiwe kwanza. Ili wao wawe na amani ilikuwa ni lazima miji wanayokaa iwe na amani kwanza.

Ninalotaka uone hapa ni kuwa suala la kutafuta amani na watu wote ni la muhimu sana. Usitunze kinyongo na watu. Usichochee ugomvi hata kama mliyegombana naye hataki mapatano bado Biblia inasema sisi wateule wa Mungu tumepewa huduma ya upatanisho kwa hiyo lazima tuyatafute kwa bidii hayo mapatano.

JAMBO LA NNE
Tafuta watu sahihi wa kushirikiana nao

Watu wote duniani ni wa muhimu kwako ila si watu wote duniani wamewekwa kwa ajili yako. Suala la watu gani unashirikiana nao ni suala la muhimu sana na la kuangalia kwa makini kwa sababu maandiko yanasema “adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake (Mathayo 10:36).

Nachotaka uelewe hapa ni kuwa huwezi kuchukua mtu yeyote tu unayemwona na kuamua kushirikiana nae. Biblia inakataza! Lazima ufuate vigezo vya ki-Biblia juu ya aina ya watu unaotakiwa kuwa nao, na neno la Mungu linasema hao watu lazima uwatafute. Angalia Yesu alichowaambia wanafunzi wake wakati anawatuma kwenda vijijini kuhubiri injili. Mathayo 10:11 anasema:
Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.

Hebu cheki hapo! Yesu hawaambii waingie kwenye nyumba yoyote ile bali anawaambia watatute kwenye mji huo au kijiji hicho mtu aliye mwaminifu ndiye wakae kwake. Sasa fahamu kuwa Yesu aliwajua watu wote walikuwa na hicho kijiji au mji na angeweza kuwaelekeza moja kwa moja ni kwa nani waende lakini akawapa vigezo ila suala la kumpata mtu akawaachia wao wenyewe watafute.

Yusufu alipomfafanulia Farao ile ndoto alimweleza na nini cha kufanya, kisha akasema: “Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri (Mwanzo 41:33). Utaona hapa kigezo anachoweka Yusufu cha aina ya mtu atakayebeba maono aliyoyaona Farao ni awe mtu wa akili na hekima. Na Farao alipoona hicho kigezo akaona hakuna mtu mwingine mwenye sifa katika Misri yote isipokuwa Yusufu.

Tunajifunza kuwa suala la watu wa kushirikiana nao ni suala la ki-Mungu kabisa na Mungu ameliwekea utaratibu. Hii ni pamoja na suala la unaoa au unaoelewa na nani? Huwezi tu kumkubalia mtu yeyote anayekuja kutaka kukuoa au kuolewa na wewe hata kama ameokoka. Watu sahihi wanatafutwa katika mkono wa Bwana. Yeye ndiye anayeijua mioyo ya wanadamu na siri zao hivo hakuna namna utawapata watu sahihi wa kushirikiana nao bila kumshirikisha Mungu. Yesu mwenyewe kabla hajachagua wale Thenashara alienda mlimani akakesha huko usiku kucha akimwomba Mungu ndipo akawachagua wale kumi na wawili.

JAMBO LA TANO
Utafute unyenyekevu

Suala la unyenyekevu ni suala muhimu sana katika kutunza mahusiano ya mtu na Mungu lakini pia kutunza mahusiano kati ya mtu na mtu mwingine. Biblia inasema katika 1 Petro 5:5 kuwa:
Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.

Usipojifunza kunyenyekea kiburi kitainuka ndani yako, na pale kiburi kinapoinuka basi uwe na hakika Mungu lazima atakupinga. Ndio maana Zefania 2:3 anasema
Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana.

Kwa hiyo unyenyekevu una nguvu ya kukuletea neema na pia una nguvu ya kukuficha siku hasira ya Mungu ikiwaka. Kati ya vitu vilivyomtofautisha mfalme Daudi na mfalme Sauli machoni pa Mungu ni unyenyekevu wao mbele za Mungu. Sauli alipokosea alijitetea na kutafuta namna ya kuhalalisha kosa lake lakini Daudi alipokosea alianguka magotini pa Bwana kuomba rehema. Kiburi kinaleta kujihesabia haki na kwa mujibu wa maandiko hakuna mtu awezaye kujihesabia haki maana wote tunahesabiwa haki bure kwa njia ya imani katika Kristo Yesu (Warumi 3:25-27).

JAMBO LA SITA
Utafute mambo mema

Amosi 5:14-15 anasema hivi:
Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo Bwana, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.

Biblia inatujulisha kuwa mambo mema yanatafutwa na sisi kama wateule wa Mungu inatupasa kuyatafuta. Mambo mema ni yale yampendezayo Mungu – yale ambayo yeye ametuagiza tuyatende. Kila jambo Mungu alituzuia kulifanya basi hilo si jema kwetu na hatupaswi kulitafuta. Mtume Paulo yeye anasema kuwa “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko (Wakolosai 3:1).” Hatupaswi kuhangaika kuyatafuta mambo ya dunia hii kwani hayo yote yanapita bali tuyatafute yaliyo juu Kristo aliko kwani huko ndiko yaliko mema yote.

Mwisho

Kwa vile Biblia ilivyotuwekea mambo tunayopaswa kuyatafuta vile vile imetuwekea mambo ambayo hatupaswi kuyatafuta wala kuhangaikia. Mambo ya Walawi 19:31 inasema “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” Mungu anatuzuia kuwaendea wachawi wala kuwatafuta kwa sababu kufanya hivyo ni kutiwa unajisi. Kwa hiyo usiwategemee wachawi wala waganga – wewe weka tumaini lako kwa Bwana. Yako na mambo mengine ambayo Biblia inatuzuia kuyatafuta ila kwa leo tutaishia hapo. Tutayaangalia hayo wakati mwingine Mungu akitupa nafasi.

JIWEKE TAYARI YESU YU KARIBU KURUDI

No comments:

Post a Comment