Mwandishi: Anderson Leng'oko
UTANGULIZI
Mada hii ni mada inayoogopwa na watu wengi au tuseme
labda inazuiwa na watu wengi. Pia kanisa halijihusishi sana na kuliongelea
suala hili, lakini biblia inatuhimiza kufundisha ili watu waimarike katika
kweli yote.
Walengwa wa somo hili ni watu wote, waliookoka na hata
wasiookoka, watu wa dini zote na madhehebu yote, watu wa kila rika na kila
imani. Inafaa sana kuyasoma mambo haya kwa kila mtu. Kama una rafiki yako
ambaye hajalisoma somo hili tafadhali sana mpe alisome bila kujali imani yake,
tabia zake, wala rika lake. Ujumbe huu unatakiwa kusikika kwa kila mwenye uhai
hivyo ukibahatika kuusoma usikae nao, mwambie na mwenzio ausome.
Somo hili linatolewa kwa lengo la kujenga, maneno
yaliyotumiwa au mambo yaliyoelezewa yanatumika kwa ajili ya kulijenga kanisa na
si vinginevyo. Muda mwingi sana umetumika kuandaa somo hili. Roho Mtakatifu
amekuwa akitoa vitu vingi karibu kila siku vya kuongezea hata ikaonekana
dhahiri kuwa kama somo hili lisipoanza kutolewa ili kulisubiri liishe, yumkini
halitaisha.
Kwa wakati huu nakupa sehemu ya kwanza ya somo hili
lakini sehemu nyingine zitaendelea kukujia ambazo nazo zina ujumbe muhimu sana
kwako kama kanisa la Kristo. Mungu akikujalia kuyasoma maneno haya na kuyatumia
vizuri hakika yake utashinda kila changamoto unayokutana nayo kuhusu zinaa
katika maisha yako.
Natumaini na kumuomba Mungu kuwa kila neno lililoandikwa
katika somo hili litakufaa kwa kuyajenga maisha yako katika roho na
kukuimarisha hata uzima wa milele.
ZINAA NI NINI?
Katika biblia zinaa inatumiwa kumaanisha tendo la kufanya
mapenzi na mtu asiyekuwa mkeo wala mumeo, ukiwa tayari mwanandoa. Lakini katika
somo hili tutatumia neno la zinaa kumaanisha kufanya mapenzi isivyo halali kwa
ujumla, ambapo kuna wakati neno zinaa litatumika kumaanisha uasherati, yaani
kufanya mapenzi kabla ya ndoa, kuna wakati litatumika kumaanisha pia tendo la
kufanya mapenzi na mtu asiye mumeo wala mkeo wakati wewe umeoa au umeolewa.
FURAHA YENYE GHARAMA KUBWA
Hapa duniani, kila jambo la kufurahisha lina gharama
zake. Kwa mfano, kunywa maji huleta raha kwa mwili, maji haya yanauzwa na
lazima ufanye kazi ndipo upate hela ya kukuwezesha kunywa maji. Vivyo hivyo
kula chakula, kuna gharama zake ambapo usipokuwa na fedha hauwezi kula. Hata
vijijini unapata chakula baada ya kuwa umehangaika mashambani na kupata mazao
ambayo ndiyo unayoyatumia kama chakula.
Katika burudani, kutazama mpira kwa mfano, kuna gharama
zake, ambapo mtu hulipa kiingilio kwa ajili ya kwenda kuangalia mchezo wa mpira
wa miguu. Hata katika uwanja wa mpira wa miguu hasa katika ligi kuu, kuna
viingilio, kuonesha kwamba huwezi kufurahia kuangalia mchezo wa mpira wa miguu
bila kulipia gharama, na ukiingia kule ndani uwanjani pia, kuna viwango vya
mahali pa kukaa kwa ajili ya kuitazama hiyo mechi ambapo kama ulilipa pesa
nyingi utapata kukaa sehemu nzuri zaidi na kinyume chake, ina maana kwamba
uzuri wa sehemu na utamu wa kuangalia unapokuwa mzuri zaidi, ndipo na gharama
ya kuangalia inapozidi kuwa kubwa sana.
Pia suala la kupata mtu wa kuishi naye, hapa tuongelee
suala la kupata mke kwa mfano, ni gharama kubwa sana. Wanaume wengi watakumbuka
jinsi ilivyokuwa taabu kwao kuwapata wenzi wao, hasa wakati wanachumbia. Kuna
wengine walikuwa wanatukanwa hadi wanalia na kushindwa kula. Wanawake waliokuwa
wanawataka walikuwa wakali sana na wanaowakatisha tamaa. Lakini kwa uwezo wa
Mungu wanaume hawa wakiisha kutumia nguvu nyingi sana wanawapata wapenzi wao
hawa na kuwa na mahusiano.
Lakini bado kuna gharama za uchumba. Ambapo wachumba
wanalazimika kujichunga na kuhakikisha wanaondoa mapungufu yao kitabia, ili
tabia zao zisiathiri mahusiano yao au hata kuyavunja. Baada ya uchumba ni ndoa.
Upande wa mwanaume hutoa mahari, hugharimika kununua shela na kumpamba bi
harusi, ndoa nyingi hutumia mamilioni ya fedha kufanyika. Na kwa maisha ya
mkristo wa kweli haiwezekani kuoa bila kufunga ndoa, hali hii huleta gharama
kubwa sana lakini zisizoepukika.
Baada ya ndoa gharama za maisha huanza, mwanamke
atatakiwa kula, kuvaa na kunywa, kutibiwa akiugua na kutunzwa katika kila hali
na mahitaji aliyonayo. Hapa naongea kwa mtazamo wa kibiblia ambapo mwanaume
ndiye baba wa familia na kichwa cha nyumba.
Mwanaume ndiye anayetakiwa kuhakikisha kuwa mke yupo
salama, anapata mahitaji yote. Na ndugu wa mke nao wanakuwa karibu kuhakikisha
kuwa mtoto wao anatunzwa vizuri kule alikoolewa. Basi kuna wakati mwingine kana
kwamba mzigo wa mwanamke pekee hautoshi, mashemeji nao huenda kwa zamu au kwa
pamoja kuishi kwa 'shemegi’ yao.
Unaweza kufikiri kwanini mtu akimfumania mkewe ‘akichepuka’
anaweza kuua mtu? Ni kwa sababu ya gharama hizi tulizoziona hapo juu. Mwanamke
avishwe apendeze, alishwe, atibiwe, na akishapendeza na kuwa na mvuto, ndipo
mwanaume mwingine anakuja na kumuiba. Yaani akiwa mahututi hospitali, ni wa
mumewe, akipona na kunawiri, anakuwa wa wote; inachukiza sana; haifai na
usingependa kuona inatokea kwako, kwa hivyo usiifanye kwa mwingine. Kumbuka
kuwa jambo lile usilopenda kufanyiwa, usimfanyie mwenzako.
Hizo hapo juu tulizoziona ni gharama za mke. Kwa hiyo
tumeona kuwa huduma ya kuwa na mke ni ya gharama kubwa sana. Kwa sababu thamani
ya huduma hiyo ni kubwa sana, ndivyo na gharama yake inavyokuwa kubwa. Njia
yoyote ya mkato ya kuipata huduma hiyo, yaweza kusababisha mauti. Hilo halina
ubishi, kwani mara ya mwisho nilisikia huko nyanda za juu kusini mchungaji
alikutwa anazini na mke wa mtu akauawa.
Mwingine anawaza na kusema ‘mbona mwalimu unaongelea
wanaume kutunza wanawake tu, wakati siku hizi kuna wanawake wanawagharimia
waume zao,’ ni sawa, hiyo nayo ipo. Na inapokuwepo, tunaihesabu nayo kama
gharama ambayo huyu mwanamke anaitoa kumgharimia mumewe, na asingependa
kusalitiwa, ndiyo maana kuna wanawake huwa wanajiua pale wanaposalitiwa.
Kwa mifano hiyo na mengine tutakayoendelea kuiangalia
tunaona kuwa kila huduma yenye kuleta tija au burudani kwa mwili au kwa
mwanadamu inalipiwa na kadiri huduma hiyo inavyozidi kuwa nzuri na kubwa sana
ndipo gharama yake inavyokuwa kubwa pia.
Gharama ya nafsi
Nafsi ya mwanadamu, ambaye ni mwanadamu mwenyewe ni ya
thamani kubwa sana. Thamani ya nafsi ya mwanadamu hailinganishwi na kitu
chochote kile, dhahabu hata ikijazwa duniani kote na kuongezewa maradufu
haiwezi kufikia thamani ya nafsi ya mtu.
Kwa kuona thamani ya nafsi ya mwanadamu Mungu baba
aliamua kumtoa Yesu Kristo afe msalabani ili kuikomboa nafsi ya mwanadamu na
dhambi. Yohana 3:16.
Zinaa inagharimu nafsi
Licha ya kuwa nafsi ina thamani kubwa sana kiasi cha
kumfanya Mungu atumie kila mbinu kuikomboa nafsi yako na hata kwa kumtoa mwanae
afe msalabani, bado zinaa inaweza kubatilisha kazi kubwa iliyofanywa na Mungu
ya kumtoa mwanawe pale msalabani kwani zinaa ina gharama kubwa sana ambayo ni
nafsi yako. Yaani kwa maneno mengine ni kwamba huduma ya zinaa, kama ingekuwa
inauzwa dukani, mtu angekuwa anatoa nafsi yake ili apatiwe huduma hiyo. Na
katika ulimwengu wa roho ndivyo ilivyo, kwamba huduma hii haitolewi bure, na
bei yake ni nafsi ya mwanadamu anayepatiwa huduma hiyo, hivyo kila ufanyapo
zinaa unalipa, na malipo yake ni kuitoa nafsi yako na haiwi yako tena, unakuwa
umeipeleka kwa yule mtoa huduma.
Tazama biblia inavyosema kuhusu jambo hili la zinaa kuwa
na gharama ya nafsi
Mithali 6:32Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.
KWANINI WATU WANAZINI/WANAKUWA
WAZINIFU?
No comments:
Post a Comment