Thursday, November 20, 2014

NGUVU YA MAOMBI YA KUNENA KWA LUGHA KATIKA KULETA MAJIBU YA MAMBO MAGUMU

Our Daily Mana



UTANGULIZI

Mpendwa msomaji wetu, tunapenda kukushukuru kwa moyo wako wa dhati wa kuendelea kujifunza neno la Mungu kupitia mtandao huu wa Fimbo ya Musa. Napenda kukutia moyo kuwa kadiri unavyoendelea kufuatilia masomo haya Mungu atakuwa anafanya vitu visivyo vya kawaida maishani mwako ambavyo hata watu wengine watakushangaa umewezaje! Tumemwomba Mungu kuwa masomo haya yawe na “UPAKO” wa kukutoa hatua moja kiroho hadi utukufu wa juu ambao Mungu amekukusudia. Kama haujapata nafasi ya kusoma masomo yetu yaliyotangulia tafadhali chukua muda uyasome kwa umakini maana iko hazina ya pekee ambayo Mungu ameweka ndani ya masomo yote yanayoletwa kwako kupitia mtandao huu. HALELUYA!  




Leo nataka nilete kwako jambo muhimu sana kuhusu maombi ya watakatifu wa Mungu. (Hebu sema “maombi ya watakatifu wa Mungu!”) Jambo hili ni juu ya “Maombi ya Kunena kwa Lugha”.

Kuna mitazamo tofauti – tofauti miongoni mwa makanisa ya Kikristo juu ya suala la maombi ya kunena kwa lugha. Wako ambao wanasema hakuna kitu kama hicho katika maisha ya maombi. Hoja yao inajengwa kwenye msingi kuwa mtu hawezi kunena kitu asichokifahamu mwenyewe halafu akasema eti ni Roho Mtakatifu! Wengine wanapinga suala la kunena kwa lugha kwa hoja kuwa Roho Mtakatifu alipowashukia mitume walinena lugha ambazo watu waliokuwa wakiwasikiliza walizielewa, (Matendo 2:5-13) sasa kwa nini siku hizi watu wanena kwa lugha lakini wanaowasikiliza hawaelewi?

Sitaki kutumia somo hili kama njia ya kujibu hoja za watu wanaopinga kunena kwa lugha, kwa hiyo nitajikita katika kueleza ujumbe wa Roho Mtakatifu kuhusu maombi ya kunena kwa lugha. Utakapokuwa ukisoma somo hili na kulifuatilia kwa makini wewe mwenyewe utaona kama kweli kunena kwa lugha kupo au hakupo.

MSINGI WA KUNENA KWA LUGHA

Kunena kwa lugha kwa kiingereza ni “speaking in tongues,” maana yake kunena kwa ndimi tofauti. Kunena kwa lugha kuna misingi yake katika agano la kale kisha ikaja kuwa dhahiri kwa watu wa agano jipya kupitia ujazo wa Roho Mtakatifu.

Agano la Kale                              

Isaya 28:11 inasema:

“La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa lugha nyingine atasema na watu hawa

Msitari huu kwenye kiingereza unasema hivi; Isaiah 28:11

“For with stammering lips and another tongue, He will speak to this people. (NKJV)”

Nataka tuyaangalie maneno haya “with stammering lips and another tongue” kidogo halafu ndipo tuendelee mbele. Neno “stammer” kwenye Encarta Dictionary (2009) limetafsiriwa hivi (nitatoa tafsiri kama ilivyo kwenye kiingereza kisha nitakueleza maana yake):

…... a speech condition that makes somebody speak with involuntary hesitations and repetition of consonants or syllables.



.... speak, or say something, with many quick hesitations and repeated consonants or syllables because of a speech condition or a strong emotion

Ule msitari unasema “with stammering lips and another tongue, he will speak to this people”. Sasa tafsiri iliyoko hapo juu kuhusu neno “stammer” inamaanisha kuwa

“ni hali ya kuongea kwa haraka bila hiari, kwa kurudia-rudia maneno kunakosabishwa na msukumo mzito wa ndani. (speak with many quick involuntary hesitations and repetition of consonants or syllables because of a speech condition or a strong emotion.)”

Kwa hiyo Isaya alipotoa unabii juu ya kusema kwa midomo ya watu wageni na kwa lugha nyingine alikuwa anazungumza habari za Mungu kuzungumza na watu wake kupitia “stammering lips and another tongue.” Mungu aliweka utaratibu wa kuzungumza na watu wake kupitia njia hii ya kuongea kwa haraka bila hiari ya anaezungumza na kwa kurudia-rudia maneno kupita mguso mzito ndani ya mtu huyo (strong emotion).
Sasa linganisha tafsiri hii na kile ambacho wanaonena kwa lugha hufanya. Utagundua kuwa mambo yafuatayo huwa yanawatokea:

  1. Hujikuta wanazungumza lugha wasiyoifahamu, sawasawa na Isaya 28:11 kuwa atasema na watu hawa kwa midomo ya watu wageni. Jambo hili la kunena lugha usiyoifahamu limetajwa tena katika agano jipya. Matendo 2:4-5, 7-11 inasema:
“4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. 5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu… 7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? 8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? 9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, 10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, 11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Biblia inatufundisha kuwa mitume wote waliokuwa wamejazwa Roho na wakaanza kunena kwa lugha walikuwa wagalilaya. Lakini walinena lugha zote za watu waliokuwa wakiwasikiliza. Jambo la kushangaza ni kuwa Biblia haisemi kuwa mitume walikuwa wakielewa lugha walizokuwa wakizinena ila inasema watu waliokuwa wanasikiliza ndio walioelewa kuwa kila mtu lugha yake imenenwa. Ok labda hujanielewa vizuri!

Nasema hivi; kulikuwa na mitume kumi na wawili waliokuwa wakiomba, na wote walikuwa wagalilaya. Kwa hiyo kwa hesabu rahisi tu ni kuwa mitume walikuwa wanafahamu lugha ya kigalilaya na hiyo ndiyo ambayo wangetegemewa waitumie kwenye maombi yao. Lakini Biblia inasema waliposhukiwa na Roho, eneo lile walilokuwepo lilikuwa limetembelewa na watu wa kila taifa duniani ambao walienda kuadhimisha sikukuu ya Pentekoste. Walokole wengi wanachanganya hapa wakifikiri kuwa Pentekoste inamaanisha ujazo wa Roho Mtakatifu; haaaaa hapana kabisa. Pentekoste ilikuwa ni sikukuu ya kiyahudi ambayo watu wa maeneo yote duniani walikuwa wanakusanyika Yerusalemu kwa ajili ya kuadhimisha sikukuu hiyo.

Sasa ni katika siku hii watu wa mataifa yote walipokuwa Yerusalemu ndipo Roho alipowashukia mitume. Walipojazwa walianza kusema kwa lugha nyingine za watu waliokuwa wamekusanyika pale Yerusalemu. Lugha hizi mitume hawakuzifahamu wala kuzielewa lakini watu waliokuwa wakisikiliza ndio waliofahamu kila mmoja wao kuwa na yeye lugha yake imetajwa.

Watu wengine husema kuwa kama kweli ni Roho kwa nini lugha hizo hazifanani wakati mnaomba? Hii ni ajabu sana. Hebu tujiuliza swali; kulikuwa na mitume kumi na wawili waliokuwa wakinena lakini walinena lugha ya kila taifa duniani. Je, lugha hizo zilikuwa zinafana? Watu kumi na wawili waliwezaje kusema lugha zote? 1Kor 14:21 “Imeandikwa katika torati, Nitasema na watu hawa kwa watu wa lugha nyingine, na kwa midomo ya wageni, wala hata hivyo hawatanisikia, asema Bwana.”

  1. Hujikuta wakizungumza kwa haraka bila hiari yao na kwa kurudia-rudia maneno. Tumeona maana ya neno “stammering lips” lilotumika kwenye Biblia ya kiingereza kuwa limaanisha hali ya kuzungumza kwa kurudia-rudia na bila hiari, yaani involuntary hesitations and repetition of words.
Ukifuatialia vizuri watu wanaonena kwa lugha utakuta kuwa kile kinachoitwa “stammering lips” huwa kinatokea. Utakuta mtu anazungumza maneno kwa haraka kama vile kafungiwa mota kwenye ulimi na mara nyingi utaona anongea kwa kurudia-rudia herufi (repetition) kwenye maombi yale na wakati mwingine huwa kana kwamba ana kigugumizi Fulani (hesitations). Wakati mwingi watu wanaonena kwa lugha huonekana kuwa kama vichaa kwa wale wasiolewa habari hizi na wala sio kosa lao maana Paulo anasema

Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini … (1Kor 14:22)

Katika moja ya tafiti za kisayansi juu ya uhalisia wa kunena kwa lugha waligundua kuwa mtu anapokuwa akinena kwa lugha ubongo wake unakuwa umelala na hivyo hakuna kabisa msukumo wa fikra za kibinadamu juu ya nini atamke na nini aache. Ni maneno yasiyo ya hiari kama jinsi inavyoelezwa kwenye Isaya 28:11 juu ya “stammering lips”, Mmoja wa watafiti, Dr. Andrew Newberg, alisema hivi:

“When they are actually engaged in this whole very intense spiritual practice their frontal lobes tend to go down in activity. It is very consistent with the kind of experience they have, because they say that they’re not in charge. [They say] it’s the voice of God, it’s the spirit of God that is moving through them,”

Kwa hiyo ni dhahiri kuwa Isaya alikuwa anazungumza habari za kunena kwa lugha pale alipotabiri juu ya Mungu kusema na watu kwa ulimi wa watu wageni na kwa lugha nyingine. Maana tafsiri ya msitari huo imetuonyesha kuwa kilichokuwa kinazungumzwa na Isaya ndicho kile kinachotokea watu wanaponena kwa lugha.

Agano Jipya

Ufunuo wa utabiri wa Isaya unakuja kuwa dhahiri na halisi katika agano jipya. Katika Marko 16:17 Yesu mwenyewe ndiye aliyeweka msingi wa kunena kwa lugha. Anasema:

Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya….

Yesu anasema wale waaminio watasema kwa lugha mpya. Ahaaa kumbe ni suala la imani. Ikiwa mtu anaamini kuwa amepewa kipawa hiki na Yesu mwenyewe basi kwake huyo kipawa hiki kinakuwa dhahiri, na kwa yule asiyeamini yeye ataona kuwa kunena kwa lugha ni ulevi kama wale watu walivyodhani kuwa mitume wamelewa asubuhi-asubuhi (Matendo 2: 13).

Ukisoma kitabu cha Matendo ya mitume utaona kuwa kunena kwa Lugha ni ishara namba moja ya uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu. Okay hebu tuone mifano michache hapa.

Matendo 2: 1- 4, mitume waliposhukiwa na Roho Mtakatifu kitu cha kwanza walichopewa ni kunena kwa lugha hata kabla hawajaanza kuhubiri. Matendo 10:44 – 46, Kornelio na wenzake walipoamini tu wakajazwa Roho Mtakatifu na wakaanza kunena kwa Lugha hata kabla hawajabatizwa. Kama Yesu alivyosema “… hao waaminio … watasema kwa lugha mpya.” Matendo 19:6, wale wanaume kumi na wawili walipobatizwa kwa jina la Yesu na Paulo akaweka mikono juu yao walipokea Roho Mtakatifu na jambo la kwanza ilikuwa ni kunena kwa lugha. Kwa hiyo ishara ya nje kabisa ya uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu ni kunena kwa lugha. Katika 2Kor 14:18, Paulo anasema:

Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote

Kwa hiyo Paulo alikuwa naye akinena kwa lugha tena zaidi ya watu wengine wote. Najua kuna mtu mwingine ataniuliza kuwa; mbona Yesu hakuwahi kunena kwa lugha? Ntakujibu swali hili kwenye sehemu inayofuata.

KAZI YA MAOMBI YA KUNENA KWA LUGHA

Katika kusoma kwangu maandiko nimegundua kuwa kuna kazi kubwa tatu zinazofanywa na maombi ya kunena kwa lugha. Endelea kuwa nami hapa kwa umakini zaidi uone.

 Kazi ya Kwanza

Kuleta majibu ya maombi juu ya mambo yaliyoko sirini

Isaya 45:3 inasema

“nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.”

Mungu anazungumza habari ya kumpa mwanawe hazina za gizani na mali zilizofichwa mahali pa siri. Swali la kujiuliza hapa ni je, huko gizani ni wapi na huko sirini kuna nini na ni nani aliyeziweka hizo hazina huko gizani?
Jambo la kujua ni kuwa Mungu alipomuumba mtu alimwekea kila kitu anachohitaji kwa ajili ya maisha yake. Hakuna jambo ambalo mwanadamu analihitaji ambalo Mungu hakumwekea; ndio maana bustani ya Edeni haikupandwa na Adamu bali ni Mungu aliyeipanda kisha akamweka Adamu aitunze tu. Mwanzo 3:23-24 inatuonesha kuwa baada ya Adamu kuasi Mungu alimfukuza atoke kwenye bustani ya Edeni lakini bustani hakuiondoa bali aliweka makerubi wailinde kwa upanga wa moto.

Swali la kujiuliza hapa ni kama Mungu alikuwa ameona kuwa Adamu hana chake tena pale Edeni kwa nini asingeiondoa na bustani? Jibu lake ni kwamba kila kitu ambacho Adamu alikuwa anakihitaji kwa ajili ya kuishi vizuri kilikuwa ndani ya Edeni na kama Mungu angeiondoa Edeni basi ingempasa Mungu amwondoe na Adamu pia. Sasa kilichofanyika ni kuwa Mungu alibadilisha utaratibu wa Adamu kuvitumia vitu vilivyokuwa Edeni. Badala ya ule utaratibu wa mwanzo ambao adamu alikuwa huru muda wowote kuchukua anachokitaka, sasa ilibidi awe anaomba kwa Mungu halafu Mungu ndiye anamletea. Ndiyo maana utaona Adamu anafukuzwa Edeni kwenye Mwanzo sura ya tatu halafu wakaanza kuliitia jina la Bwana kwenye Mwanzo sura ya Nne (Mwanzo 4:26) Kwa hiyo ilibidi Adamu aliitie jina la Bwana ili aweze kupata mahitaji yake. Kwa nini? Kwa sababu hazina zake tayari zilikwisha kuwekwa sirini na zikawa zinalindwa na kerubi. Mungu aliamua kuziweka gizani na sirini ili kumzuia shetani asije akamdanganya tena Adamu halafu akapoteza vyote.

Huu ndio uhalisia wa maisha ya kiroho. Chochote unachokihitaji kwa ajili ya maisha Mungu amekuwekea tayari, lakini si kila kitu ambacho ni chako kiko kweupe. Jua wazi kuwa kuna hazina zako nyingi tu ambazo Mungu ameziweka gizani na anasubiri uliitie jina la Bwana kama Adamu alivyofanya ndipo upewe. Ndio maana Isaya 45:11 Mungu anatoa utaratibu wa namna ya kuzifikia hizo hazina za gizani. Anasema:

Bwana, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.

Lile neno “Niulizeni” kwenye kiingereza limetumika neno “ask me” likiwa na maana ya “niombeni.” Kwa hiyo kwenye msitari wa tatu Mungu anatuambia kuwa kuna hazina zetu alizotufichia shetani asije akazigusa halafu kwenye msitari wa 11 anatuita tumwombe juu ya hizo hazina za gizani na mali zilizofichwa sirini.
Sasa jambo la kujiuliza hapa ni kuwa; nawezaje kumwomba Mungu juu ya kitu kilichofichwa na mi sijui kama kipo? Majibu ya swali hili ndiyo yanayotuleta kwenye point yetu ya maombi ya kunena kwa lugha. Paulo anasema hivi: 1Kor 14:2

Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.
He he heee!! This is amazing!

Kumbe kunena kwa lugha hakulengi kusema na watu, bali ni mazungumzo binafsi kati ya mtu na Mungu juu ya mambo ya siri katika roho yake. Okay, sasa hapa tunapata kujua kuwa kuna maombi ya siri na maombi ya wazi. Maombi ya wazi ni yale mnayotaka kujengana kama kanisa la kristo lakini maombi ya siri yanafanyika ndani ya roho ya mtu kwa njia ya kunena kwa lugha. Ndio maana Yesu alisema; Mathayo 6:6

Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

Yesu anasema unaposali ingia kwenye chumba chako cha ndani yaani katika roho, kisha funga mlango maana yake omba kwa jinsi ambayo wengine hawatasikia yaani kunena kwa lugha; halafu baba yako aonaye sirini maana yake aliye na hazina zako za gizani atakujazi. Kwa hiyo maombi ya kunena kwa lugha peke yake ndiyo yenye uwezo wa kuleta majibu ya mambo yaliyo sirini na yaliyofichika.

Tumewahi kuomba na dada mmoja huko Arusha na alikuwa amefungwa kwa mapepo na kila wakati yalikuwa yanamrudia. Siku moja mtu aliyekuwa akituongoza kwenye maombi yale akapewa ufunuo kuwa siku hiyo tuombe kwa kunena kwa lugha tu. Aisee haikuchukua muda yule dada akawa ameshafunguka na akawa mzima kabisa. Wakati mwingine unaweza kuwa unakemea pepo halafu likanyamaza kimya kabisa kama vile mtu amekufa. Ukiona hivo we usihangaike sana, ingia kwenye maombi ya kunena kwa lugha halafu utaona.

Ni maombi ya kunena kwa lugha ndiyo yanayoweza kukupeleka mpaka kwenye falme za shetani na ukawashinda. Maana Paulo anasema kuna lugha za wanadamu na za malaika (1Kor 13:1) Tunaponena kwa lugha tunanena lugha za ulimwengu wa roho kwa ajili ya vitu vya rohoni. Ndio tunatumia kunena kwa lugha kwenye maombi na sio kwenye mahubiri. Kama unataka ufaidi vitu vya rohoni omba upewe kunena kwa lugha…. And its simple…. AMINI TU NAYO YATAKUWA YAKO

Kazi ya Pili

Kukujenga na kukuimarisha kiroho

Maisha ya mwanadamu mara nyingi yametawaliwa na hofu na mashaka kutokana na vitu mbalimbali. Mashaka haya huwasibu watu hata kwenye maisha yao ya kiroho. Watu wengi wana mashaka juu ya kujitambulisha kwao kuwa wameokoka na wengine hawawezi hata kusema Bwana Yesu asifiwe kwa sababu ya mashaka waliyonayo. Hii inatokana na ukosefu wa nguvu na ujasiri wa kiroho. Moja ya tiba ya hofu na mshaka ya kiroho ni kunena kwa lugha. Kunena kwa lugha huleta ujasiri wa Roho Mtakatifu juu ya mtu kwa ajili ya ushuhuda wa kristo.

1Kor 14:4 inasema “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.” Kwa hiyo mwenye kunena kwa lugha hujijenga nafsi yake katika mambo ya kiroho. Ndio maana akina Petro kabla ya kujazwa Roho walikuwa na hofu sana na hawakuweza kuitangaza injili. Lakini pindi tu walipoanza kunena kwa lugha nafsi zao zikatiwa nguvu na wakaanza kuwahubiria wale wale waliokuwa wakiwasikiliza.
Nataka nikupe kiu leo ya kutafuta upako wa kunena kwa lugha kama kweli unataka kuwa imara katika Bwana. Uoga ulionao juu ya injili utapotea kama upepo siku utakapoanza kunena kwa lugha. Lakini pia suala la kuijenga nafsi yako kwa kunena kwa lugha linajumuisha vitu zaidi ya kimoja. Mtu anayenena kwa lugha kweli kweli hata dhambi haina nafasi ndani yake. Watu wengi leo wamebomoka kiroho kwa sababu hawaneni kwa lugha.
Kazi ya Tatu
Kuomba katika Roho
Liko somo lingine ambalo Roho amenipa nifundishe juu ya “tofauti ya kuomba kwa roho na kuomba kwa hisia.” Haya nitakayokueleza hapa yatakuwa kwa uchache tu lakini chakula kamili juu ya jambo hili fuatilia masomo haya utaona.
1Kor 14:14 inasema hivi: “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.” Huu ndio ukweli kuhusu kunena kwa lugha. Paulo anasema kuwa nikiomba kwa kunena kwa lugha hakuna suala la kuhusika kwa akili yangu bali ni roho yangu ndiyo huomba. Nimetangulia kukueleza utafiti uliofanywa na wanasayansi ambao wamethibitisha kuwa mtu akiwa kwenye kunena kwa lugha akili zake zinakuwa hazihusiki kabisa, na ndicho Paulo anachokisema hapa.
Maombi katika roho hayahusishi akili za mtu bali roho ya mtu ndiyo huwa katika kuwasiliana katika ulimwengu wa roho. Unaponena kwa lugha unakuwa una uhakika kabisa unachoomba ni sawa na mapenzi ya Mungu maana akili zako hazihusiki. Kuna wakati huwa ninaenda kwenye maombi na agenda zangu mwenyewe lakini nikiisha kumkaribisha Roho Mtakatifu huwa najikuta nasahau hadi agenda nilizokuwa nazo.
Wakati fulani Mungu alinionesha jambo ambalo lilikuwa linakuja mbele yangu na mimi nikawa sitaki lije. Hivyo nikaanza kuwa na maombi ya kukataa jambo hilo lisitokee lakini kila nilipokuwa nikienda kwenye maombi nilikuwa ninakamatwa kunena kwa lugha. Mwishowe jambo lile likatokea. Nilipokuwa najiuliza kwa nini Mungu aliliruhusu wakati mi sikulitaka, rafiki yangu mmoja akaniuliza “ulikuwa unanena kwa lugha wakati unaombea jambo hilo?” Nikajibu, “ndiyo.” Kisha akaniambia “wakati unaponena kwa lugha Roho hubatilisha mapenzi yako na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatendeke.”
TAFUTA UPAKO WA KUNENA KWA LUGHA WEWEEEEE
Ngoja nihitimishe kwa kukupa kile Paulo alichotuambia tufanye maana naona hapa hapanitoshi.
1Kor 14:5, 39 anasema “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha …. Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha.”
HALELUYAAAA

5 comments:

  1. Ooooh hallelujah nimeomba Sana leo hiyo Hali ya kuongea kqa lugha nisiyo ifahamu ikanuijia ahsante yesu wangu jwa ukombozi

    ReplyDelete
  2. Ameni barikiwa sana

    ReplyDelete
  3. Asante kwa somo zuli..

    ReplyDelete
  4. Bwana mungu akubariki Sana Sana mwalimu nitakufuatilia Mara kadhaa

    ReplyDelete