Mwanzo Sura ya 4
Kuzaliwa
kwa Kaini na Habili
Sura ya 3 ya kitabu hiki cha
Mwanzo imeishia na habari mbaya ya uasi wa Adamu ambao unapelekea kufukuzwa
kutoka kwenye bustani ya Mungu na kuambiwa aende akailime ardhi ambayo kwa hiyo
alitwaliwa. Sasa mtu alikuwa amepoteza ule uhusiano na ushirika wa mwanzo
uliokuwapo kati yake na muumba wake; alikuwa sasa anatakiwa ajitegemee katika
kuishi kwake kwa kuilima ardhi. Katika hali hii ya kutengwa mbali na uso wa
Mungu ndipo tunapokuta mwanadamu wa kwanza anazaliwa. Msitari wa 1 wa sura ya 4
unatujulisha kuwa baada tu ya kufukuzwa kutoka bustanini Adamu alianzisha
maisha mpya nje ya bustani na mtoto wa kwanza kuzaliwa huko nje alikuwa ni
Kaini. Katika kuzaliwa kwake Kaini, Hawa alidhani kuwa ni mtoto aliyepewa na
Bwana. Maana tunamsikia Hawa akisema “Nimepata mtoto
mwanamume kwa Bwana.” Hatuambiwi Adamu alisema nini juu ya kuzaliwa kwa huyu
mtoto, lakini inaonesha dhahiri kuwa Adamu alijua kuwa huyu mtoto hakutoka kwa
Bwana hivyo akaamua kukaa kimya. Kwa mara nyingine tena Hawa anakurupuka na
kujifanya anajua sana mambo ya Mungu kuliko Adamu. Hawa anadhani kuwa Kaini
alitoka kwa Bwana, lakini akasahau kuwa Kaini alizaliwa nje ya uwepo wa Bwana
na hivyo hakutokana na Mungu. Hivi ndivyo Biblia inavyosema juu ya Kaini kuwa
alitokana na dunia. 1 Yohana 3:11 - 12 inasema:
“Maana, hii ndiyo
habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi;si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua
ndugu yake…”
Maneno haya ya 1
Yohana 3:12 kwenye tafsiri ya kiingereza ya New World Translation yameandikwa
hivi: “…not like Cain, who originated
with the wicked one and slaughtered his brother…” Hii tafsiri inasema Cain originated with the wicked one;
maana yake ni kwamba Kaini chanzo chake
ilikuwa ni yule mwovu, ndiyo maana tafsiri yetu ya Kiswahili imesema kuwa Kaini alikuwa wa yule mwovu.
Kumbe Kaini alizaliwa
kutoka kwenye uovu ambao Adamu na Hawa walikuwa wameufanya pale Edeni. Kuzaliwa
kwake hakukumwepusha na hii dhambi ya wazazi wake na hivyo yeye kama mzaliwa wa
kwanza, na kama lango la uzao wa mwanadamu alibeba laana ya uovu wa wazazi
wake. Kwa sababu ya kuzaliwa kwake katika hali ya uovu Kaini aliishi maisha
yasiyo safi mbele za Mungu na hatimaye aliua. Ndivyo ilivyo kazi ya uovu; Yesu
anasema hivi kuhusu watu walio dhambini:
Ninyi ni wa baba
yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala
hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo,
husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu
yeye ni mwongo, na baba wa huo. [Yohana 8:44]
Hivi ndivyo shetani
alivyojipambanua tangu mwanzo; alimwingia nyoka kule Edeni na akajimbanua kuwa
yeye ni mwongo na baba wa huo, maana alimdanganya Hawa hata akaingia katika
hali ya kuasi; alimwingia Kaini tangu tumboni na kujipambanua kuwa yeye ni
mwuaji tangu mwanzo, maana Kaini kwa sababu ya matendo yake kuwa mabaya akamwua
ndugu yake. Hivi ndivyo 1 Yohana 3:12 inavyomweleza Kaini;
inasema:
…si kama Kaini
alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya,
na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
Akiisha kumzaa Kaini
katika hali ya uovu, Adamu aliongeza tena akamzaa Habili ndugu yake Kaini.
Msitari wa 2 wa Mwanzo 3 umenyamaza kimya juu ya kile wazazi wa Habili
walichosema kuhusu kuzaliwa kwa mtoto huyu. Si Adamu wala Hawa aliyethubutu
kusema chochote juu ya kuzaliwa kwa Habili. Inawezekana kabisa kuwa katika
kipindi cha kukaa na Kaini kabla Habili hajazaliwa waliziona tabia za Kaini na
kugundua kuwa walikosea kusema kuwa ametoka kwa Mungu. Sasa hivi walipompata
Habili hawakuwa na uhakika tena kuhusu kauli zao juu ya watoto wanaowazaa hivyo
waliamua wasiseme chochote juu ya huyu mtoto. Ni katika Mwanzo 3:25 ndipo tunamsikia Hawa akisema kitu tena juu ya mtoto aliyemzaa
baada ya Sethi kuzaliwa. Ni vyema sana wazazi wakajua kusudi la kuzaliwa kwa
watoto wao na hali ya kiroho waliyozaliwa nayo ili wajue namna ya kukaa nao na
kuwalea.
Sadaka ya Habili na Kaini
Msitari wa 2 wa sura
hii ya 3 unatueleza pia ajira ambazo wana hawa wawili wa Adamu walikuwa
wamejipatia. Habili alikuwa mchunga kondoo na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
Katika ajira zao hizi walifika wakati wakamkumbuka muumba wao na kuamua
kumtolea sadaka. Haionekani moja kwa moja ni wapi walipopata ufunuo huu wa kuwa
Mungu hupenda sadaka za watu wake,lakini tutaona hapo baadae kuwa suala hili
lilikuwa na msingi fulani wa kiroho ndani ya watoto hawa wa Adamu na msingi huo
ndio ulikuja kutofautisha utoaji wao wa sadaka.
Hakika hatutaki
kujikita sana katika tafakari hii juu ya masomo ya utoaji sadaka ila tunataka
tu tuweke ndani yako somo moja la msingi juu ya utoaji wako wa sadaka. Jambo
lenyewe ni kuwa utoaji wa sadaka huambatana na imani aliyonayo atoaye sadaka
kwa Mungu anayepokea hiyo sadaka. Sadaka inayotolewa bila imani huwa haipati
kibali mbele za Mungu; wacha tujifunze hili kwa undani kidogo hapa. Mwanzo 4:3-5 inasema:
Ikawa hatimaye Kaini
akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta wazao wa kwanza
wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali,
wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.
Hawa ndugu wawili
walienda mbele za Mungu kutoa sadaka kila mtu kwa kadiri ya ajira aliyokuwa
nayo. Cha ajabu ni kuwa aina ya sadaka za wawili hawa zilitofautiana kwa jinsi
ya ajabu sana; Kaini alileta tu mazao ya ardhi kwa Bwana, hatuelezwi yalikuwa
na thamani gani au hata hadhi gani machoni pa Kaini mwenyewe. Bwana
hakumtakabali Kaini wala sadaka yake katika mazingira yale ya utoaji wake.
Habili yeye alileta sadaka ambayo Biblia inaielezea sifa zake kuwa walikuwa ni
wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama; hii sasa Mungu
aliitakabali na akamtakabali Habili pia. Hili jambolikainua ghadhabu ndani ya
Kaini hapo hapo.
Swali tunalojiuliza
hapa ni kuwa Habili alipata wapi ufunuo huu wa aina ya sadaka aliyopaswa kuitoa
na kwa nini Kaini hakuwa na ufunuo huo? Hakika sadaka ya hawa ndugu ilikuwa ni
njia yao ya kutaka kumwendea Mungu na kutengeneza nae baada ya wazazi wao
kuvuruga. Katika kutafuta namna gani wamwendee Mungu ndipo wazo la kutoa sadaka
lilipokuja ndani yao, lakini utoaji wao wa hiyo sadaka ukatofautiana. Utoaji wa
sadaka wa Habili unatufundisha mambo matatu makubwa tofauti na ule wa Kaini.
1.
Kwanza ni kuwa sadaka inayompendeza Mungu ni ile inayotokana na
kitu kisicho na hatia. Tumeona kuwa Habili alikuwa mchunga kondoo na Kaini
alikuwa mkulima wa ardhi. Utakumbuka kuwa Kaini alikuwa anailima ardhi ambayo
ilikuwa inabeba laana ya makosa ya Adamu. Ardhi haikuwa tena sehemu ya Baraka
katika uzao wa mtu maana ilikuwa laana kwa ajili ya makosa yake. Kaini kwa
ujinga wake akaamua kumletea Mungu sadaka iliyotokana na kitu kilicholaaniwa.
Ardhi ilikuwa imelaaniwa hivyo isingeweza kuwa ni chanzo kizuri cha Baraka kwa
mtu, lakini Kaini aliamua kuitumia hiyo hiyo kuwa chanzo cha sadaka yake.
Matokeo yake ilikuwa ni kukataliwakwa yeye na sadaka yake.
Habili yeye alileta
sadaka kutoka katika mnyama safi – kondoo. Tunajua alikuwa kondoo kwa sababu
yeye alikuwa mchunga kondoo na Biblia inatuambia kuwa alitwaa sadaka katika
wanyama wake. Tungeambiwa stori nyingine kabisa kama Habili naye angeamua
kuleta sadaka ya nyoka kwa Mungu. Kondoo hakuwa na hatia yoyote kwa sababu hata
Mungu alimtumia kule Edeni kumtafutia Adamu nguo za kuficha uchi wake. Hivyo
sadaka ya Habili ilikuwa safi na hivyo ikapata kibali mbele za Mungu.
2.
Pili ni kuwa kutengeneza uhusiano uliovunjika kati ya mtu na Mungu
ni lazima damu imwagike. Kaini na Habili wote waliamua kutoa sadaka kama njia
ya kutengeneza uhusiano wao na Mungu baada ya wazazi wao kuwa wamekosa. Suala
la kurejesha uhusiano huo linafunuliwa kuwa lilitakiwa kufanyika kwa damu isiyo
na hatia, na Habili alipata ufunuo huu lakini Kaini hakugundua.
Kwa mara nyingine
tena suala la wokovu wa ulimwengu kupitia damu ya Yesu linatabiriwa tena katika
hatua za mwanzo kabisa katika maisha ya mtu baada ya kuasi. Utoaji wa sadaka ya
Habili ulihusisha sadaka ya kondoo wa kuchinjwa ili dhambi zake zifutwe na
atengeneze tena na muumba wake. Kitabu cha Ufunuo kinanena hivi juu ya Yesu:
Astahili Mwana-Kondoo
aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na
utukufu na Baraka. [Ufunuo 5:12]
Na watu wote wakaao
juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha
uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia. [Ufunuo 13:8]
Biblia inataja kuwa
Yesu ni Mwana-Kondoo aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia. Maana yake ni
kuwa tangu dhambi ilipoingia tu duniani, Mungu alimwandaa mwanae kama kondoo wa
kuchinjwa ili iwe dhabihu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Habili alijua
hili japokuwa Yesu alikuwa hajafunuliwa katika mwili wakati ule. Kaini
hakugunudua hili na hivyo akadhani kuwa suala la kutengeneza uhusiano wake na
Mungu lingefanyika tu kwa kumlaghai Mungu kwa sadaka za kawaida. Maana sadaka
ya Kaini ilikuwa ni kama mtu aliyekosa halafu akajaribu kufuta kosa lake kwa
kumletea zawadi yule aliyekosewa. Mungu hakuhitaji zawadi kutoka kwa watu bali
alihitaji unyenyekevu na moyo wa kweli wa kutaka kutengeneza.
3.
Tatu ni kuwa utoaji wa sadaka usioambatana na imani huwa dhambi
mbele za Mungu. Unaposoma Biblia utakuta kitabu cha Warumi 14:23 ikisema: “…Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.” Utoaji wa sadaka
uliofanywa na Habili ulikuwa wa tofauti na ule wa Kaini kwa sababu ya imani.
Katika Waebrania
11:4 Biblia inasema:
Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu
iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka
zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena.
Imani ya Habili ndiyo
imani ya kwanza kuandikwa kwenye Biblia; kabla ya hapo hakuna aliyewahi kuishi
au kutenda jambo kwa imani. Lakini Biblia inasema “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo
[Warumi
10:17]. Swali la kujiuliza hapa ni: Habili alipata wapi kusikia neno
la Kristo lililompa kuwa na imani?
Kwa kuwa imani chanzo chake ni
kusikia, uwe na uhakika kabisa kuwa kuna mahali ambapo Habili alisikia kuhusu
aina ya utoaji wa sadaka ambao ndio uliotengeneza imani hiyo ndani yake. Majibu
ya swali hili tunayapata kwanza kwa kuangalia aina ya sadaka aliyotoa, ambayo
kimsingi ndiyo iliyobeba imani yake. Habili alitoa sadaka ya kuchinjwa, ambayo
tumesema ilikuwa ni kwa ajili ya kutengeneza uhusiano wake na Mungu. Mpaka hapa
sasa tunajua kuwa sadaka ya Habili ilikuwa ni kwa ajili ya kuondoa dhambi zake
na kumpatanisha na Mungu wake.
Sasa utakumbuka kuwa Mungu
mwenyewe ndiye aliyeanzisha mfano wa utoaji wa sadaka ya kuchinjwa ili kufunika
uovu wa watu wake pale Mwanzo 3:21. Katika msitari huo tuliona kuwa
Mungu alimchinja mnyama asiye na hatia ili kuficha uchi wa Adamu na Hawa, na
tulichambua kwa undani kidogo jambo hili kwenye tafakari yetu ya sura ya 3.
Sasa ni wazi kuwa Adamu aliwasimulia wanawe kuhusu kile Mungu alichowafanyia
pale walipokosea na jinsi Mungu alivyochinja mnyama asiye na hatia ili kuficha
aibu yao. Stori hii ya baba kwa watoto wake ilimpa Habili fundisho la kujua
kuwa uovu wao unaweza kufutwa tu kwa kumwaga damu isiyo na hatia; na katika
hili fundisho alilolisikia kwenye stori za baba yake akajenga imani ambayo
ndiyo iliyomtofautisha na jinsi Kaini alivyotoa sadaka yake. Haaaa! Kumbe kweli
imani huja kwa kusikia. Ni ajabu sana kwamba Kaini licha ya kusikia mambo
ambayo Mungu alifanya kutoka kwa baba yake bado hakutaka kuishi kwa imani bali
akataka kumlaghai Mungu kwa zawadi za mazao ya ardhi. Hakika kweli Kaini alikuwa wa yule mwovu.
Lakini maisha ya
Kaini hayatofautiani sana na watu wengi kwenye ulimwengu wa leo ambao licha ya
kusikia matendo ya Mungu na rehema zake kwetu, bado hawataki kumtegemea na
kuishi kwa imani katika Kristo. Imani ya Habili ilimfanya apewe haki mbele za
Mungu ijapokuwa alizaliwa na wazazi walikuwa wamemwasi Mungu. Kumbe hata kama
nimezaliwa katika hali ya uovu bado ninaweza kuwa mwenye haki mbele za Mungu
kwa imani tu. Basi tangu leo usijilaumu eti ulizaliwa nje ya ndoa au kwamba
ulizaliwa na wazazi waovu, maaana kwa imani sasa tunahesabiwa haki katika
Kristo Yesu - kondoo wa kuchinjwa. Tunakupa shauri usiende katika njia ya Kaini
kama Yuda 11inavyotuonya.
Hasira ya Kaini na kufukuzwa kwake
Msitari wa 5-7 wa
sura ya 4 unaachilia fundisho juu ya hasira ya mtu aliyekataliwa na Mungu
katika namna yake ya kumwendea Mungu. Kaini baada ya kukataliwa na sadaka yake
kukataliwa akawa na ghadhabu kubwa sana juu ya Mungu na uso wake ukakunjamana.
Tunajuaje kuwa hasira yake ilikuwa juu ya Mungu; ni kwa kuangalia wa kwanza
kuiona hiyo hasira. Kaini alimwonyesha Mungu waziwazi kuwa ana hasira nae na
Mungu kwa upendo akamwelekeza Kaini nini cha kufanya. Yale maneno ya msitari wa
7 yanatufunulia upendo wa Mungu ulivyo hata kama tuko dhambini. Mungu akasema:
Kama ukitenda vyema,
hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo
inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.
Mungu alimwonya Kaini
mapema kabisa juu ya dhambi iliyokuwa mbele yake na kumweleza kuwa imempasa
aishinde. Suala la kushinda dhambi sio la Mungu, ni suala lako binafsi na
nijukumu lako kuishinda dhambi. Mungu kwa upendo alimweleza Kaini nini cha
kufanya ili aishinde dhambi na hasira iliyokuwa imemjaa moyoni. Alimwambia
atende vyema ili apate kibali. Ni kama vile kulikuwa na sadaka nyingine ambayo
Mungu alikuwa akimwelekeza Kaini aitoe ila Kaini akagoma na kwa mara ya kwanza
tunaona neno “dhambi” likijitokeza kwenye Biblia. Neno ‘dhambi’ halijitokezi
tena mpaka tunapolikuta kwenye Mwanzo 13:13 Biblia inapoeleza
juu ya dhambi nyingi walizokuwa wamefanya watu wa sodoma. Kutokea hapo neno
hili linajitokeza mara nyingi sana kwenye Biblia kuonesha jinsi maisha ya mtu
kuanzia kwa Kaini yalivyokuwa mabaya. Ni katika Yesu tu ndo tunapata ushindi wa
kweli juu ya dhambi.
Kaini alipoulizwa na
Mungu kuhusu hasira yake hakutaka kujibu chochote; ilikuwa ni kama vile alikuwa
akisema moyoni mwake kuwa “kama wewe Mungu ningekuwa na uwezo wa kukufikia
ningekuua leo.” Kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kumfikia Mungu, hasira ya Kaini
ilimgeukia Habili ambaye alikuwa amekubaliwa na Mungu. Ndivyo shetani alivyo.
Akishindwa kukuangamiza wewe kwa sababu una nguvu kuliko yeye basi hutafuta ni
nani umpendaye sana halafu humpiga huyo. Kwa wakati huu Habili ndiye aliyekuwa
mtu anaeupendeza moyo wa Mungu, maana Adamu na mkewe walikuwa wameshapoteza
sifa hiyo. Shetani aliyekuwa ndani ya Kaini alipoona kuwa hawezi kupigana na
Mungu sasa aligeuzia hasira yake kwa Habili, mwenye imani wa Mungu. Ni muhimu
sana kuhakikisha unaweka ulinzi wa kiroho juu ya watu wako wote na vitu vyako
vyote, maana shetani akikushindwa wewe atatafuta cha kwako anachokiweza ili
akipige hicho.
Bila kujua hasira
iliyokuwa ndani ya nduguye, Habili alikubali ombi la kwenda uwandani na huko
nduguye akamwinukia akamwua. Kwa kumwua nduguye, Kaini anadhihirisha jinsi
alivyokuwa wa uzao “wa yule mwovu” maana Yesu alisema shetani ni mwuaji tangu
mwanzo naye ni baba wa uongo. Alijidhihirisha kama mwongo kwenye sura ya 3 na
hapa sasa anajidhihirisha kama mwuaji.
Kama ilivyo kawaida
ya Mungu kutokutoa hukumu bila kumhoji mtuhumiwa ndivyo alivyofanya na kwa
Kaini pia. Msitari wa 9 na wa 10 Mungu anamhoji Kaini juu ya alichofanya na
aliko ndugu yake. Bila kuonyesha hata tone la hofu kwa Mungu, Kaini
anadhihirisha uovu wake kwa kusema “Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
Hakika alidhani kuwa anaweza kumficha Mungu uovu wake; kama ambavyo wazazi wake
walidhani kuwa wanaweza kumficha Mungu uovu wao kwa majani ya mtini. Lakini
kama vile mti ya bustani ilivyoshindwa kuuficha uovu wa Adamu na Hawa ndivyo na
damu ya Habili pia ilivyoshindwa kunyamaza juu uovu wa nduguye; sasa damu ile
ilimlilia Mungu kutoka ardhini.
Kilio cha damu ya
Habili kilipelekea laana juu ya Kaini kwa kuongezea katika laana aliyokuwa
ameirithi kutokana na dhambi ya wazazi wake pale Edeni. Sasa Kaini alilaaniwa
yeye mwenyewe katika ardhi. Katika kosa la Adamu ardhi ilibeba laana badala
yake, lakini kosa la Kaini lilisitahili laani hii imwangukie yeye mwenyewe na
Mungu akamfarakanisha na ardhi iliyofungua kinywa chake ipokee damu ya ndugu
yake [Mwanzo 3:11-12].
Tofauti na Adamu
ambaye alifukuzwa ili akailime ardhi na kula kwa jasho baada ya kuteseka katika
ardhi, kwa Kaini adhabu ilikuwa ngumu sana. Kaini mwenyewe anakiri katika
msitari wa 13 kuwa “Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.” Ardhi sasa
ilipewa kiburi juu ya Kaini ambaye ajira yake ilikuwa ni mkulima; haikutakiwa
tena kumpa mazao yake hata kama angeilima vipi. Maisha yake sasa yaligeuka kuwa
ya mtu mtoro na asiye na makao maalumu. Tangu enzi za Kaini hata leo mtu yeyote
mwenye dhambi asipotubu huwa analalamika juu ya ukubwa wa adhabu ya Mungu na
kuona kuwa adhabu hiyo siyo haki. Lakini Biblia nzima inataja hukumu za Mungu
kuwa ni za haki; kwa hiyo malalamiko ya akina Kaini hayaondoi uhalali wa adhabu
za Mungu wala hayamzuia Mungu kuadhibu. Ni heri kuokoka leo na kubadili maisha
yako kuliko kukaa na kumlaumu Mungu.
Uzao wa Kaini na maisha yake nje ya uwepo wa Mungu
Baada ya ardhi kuzuiwa
isimpe mazao, Kaini aliona kuwa maisha yake yalikuwa hatarini na ya kwamba
angeweza kuuawa wakati wowote. Licha ya yeye kuwa mwuaji, kumbe naye hakupenda
kufa. Ndivyo ilivyo siku zote, watu watendao mabaya hupenda sana wao kutendewa
mema; Kaini alitaka watu wamtendee mema wakati yeye alimtenda mabaya ndugu
yake. Kwa huruma Mungu alimwekea Kaini alama ya utambulisho ili mtu yeyote
asije akamwua. Kimsingi Mungu alitegemea Kaini angetubu na kuomba rehema,
lakini kama vile wazazi wake walivyopewa adhabu wakakaa kimya na kuondoka usoni
pa Mungu ndivyo na mtoto wao nae alivyofanya. Msitari wa 16 unasema “Kaini
akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.”Adamu alifukuzwa atoke mbele za Bwana
lakini Kaini aliondoka mwenyewe. Ni sahihi kabisa kusema kuwa kwa mwenye
dhambi uwepo wa Mungu ni mateso makali.
Msitari wa 17 unaanza
na jambo jingine jipya kwenye historia ya Biblia; ni juu ya uzao wa mwanadamu
mbali na wale Mungu aliowafanya mwenyewe. Kabla ya msitari huu ndoa pekee iliyokuwepo
ilikuwa ni ile ya Adamu na Hawa, na msitari huu unatuambia Kaini alipofika
katika nchi ya Nodi alimjua mkewe na akazaa mzaliwa wake wa kwanza, Henoko.
Swali linalojitokeza mara nyingi miongoni mwa wakristo hapa ni: mke wa Kaini
alitoka wapi?
Wengine wamekuwa
wakisema kuwa Kaini alioa mke kutoka katika wana wa nchi ya Nodi na kuwa
kulikuwa na uzao mwingine huko ambao ulikuwa sio wa Adamu. Sisi hatuamini hivyo.
Bibli inasema “Kaini akamjua mkewe…” haisemi Kaini akaoa mke katika nchi ya
Nodi, maana kama ingekuwa hivyo Biblia ingesema wazi. Kinachoonekana ni kuwa
kati ya kuzaliwa Habili na kuzaliwa Sethi kwenye Mwanzo 4:25, Adamu alikuwa
amezaa watoto wengine ijapokuwa Biblia haikutaka kuwazungumzia. Ni katika
watoto hawa ndipo Kaini alipojitwalia mke akaenda nae nchi ya Nodi alipoondoka
mbele za uso wa Bwana. Maana kimsingi haiwezekani kwamba Adamu alikuwa hazai
wakati Kaini anapata watoto na wajukuu na vitukuu.
Mzaliwa wa kwanza kwa
Kaini alikuwa ni Henoko na msitari wa 18 unaeleza vizazi vya Kaini mpaka kufika
kwa Lameki. Inaonekana kuwa kwa watoto wengine hakukuwa na jambo kubwa sana la
kuhitaji Biblia ilizungumzie ila ilipofika kwa Lameki Biblia ikabidi isimame
kidogo kueleza kilichotokea kwa huyu mtu.
Lameki ndiye
aliyekuwa wa kwanza kuvunja utaratibu Mungu aliouweka wa mtu kuwa na mke mmoja.
Lameki alikuwa na wake wawili; yeye ndiye chanzo cha ndoa za wake wengi na
katika kosa hili tunaona uovu uliofuata juu yake. Msitari wa 23 na 24
unamwonesha Lameki akijisifu mbele za wakeze kwa kumwua mtu aliyekuwa
amemjeruhi na kumchubua. Aliyeuawa alikuwa ni kijana, na inaonekana kuwa
alikuwa amempiga Henoko nae akamwua ili kulipa kisasi. Tunajuaje kuwa alikuwa
analipa kisasi; maneno yake kwenye msitari wa 24 yanadhihirisha hili. Dhambi ya
Kaini sasa ilikuwa imeinuka tena katika kizazi cha nne tangu Kaini. Kumbuka Mungu
anasema:
…Bwana, Mungu wako,
ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana
maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao. [Kutoka 20:5]
Dhambi ya Kaini haikufutwa
hivyo illiendelea kufuatilia vizazi vyake na hatimaye ikapata mlango wa kutokea
kwa Lameki. Wako watu ambao dhambi zao ni kutokana na kupatilizwa kwa laana za
wazazi wao na wakijitahidi kushinda dhambi hizo kwa nguvu zao hawawezi. Ni damu
ya Yesu peke yake ndiyo iliyobeba laana zetu zote ili sisi tuwe huru. Ipokee
leo kwa kuokoka ili ikusafishe kabisa uwe safi.
Mwanzo wa kumiliki mali na ugunduzi
Katika uzao wa Lameki
tunapata fundisho jingine la pekee kidogo; huu ndio uzao wa kwanza duniani
kumiliki mali na kufanya ugunduzi mbali mbali. Mtoto wa kwanza wa Lameki ni
Yabali na msitari wa 20 unasema huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na
kufuga wanyama. Yabali ndiye baba wa wafugaji; kwa hiyo jamii ya wafugaji
ilianzia kwa Yabali mwana wa Lameki. Kuna tofauti kati ya kazi ya Yabali na ile
aliyokua akifanya Habili; Biblia inamtaja Habili kuwa alikuwa akichunga kondoo wakati Yabali alikuwa akifuga wanyama.
Katika enzi hizo kumiliki
mifugo ilikuwa ndiyo utajiri mkubwa, kwa hiyo uzao wa Yabali ndio walikuwa
waanzilishi wa kumiliki mali. Kwa upande wa pili nduguye Yabali alikuwa Yubali,
yeye ndiye baba yao wapiga kinubi na filimbi. Ahaa kumbe mwanzilishi wa muziki
hapa duniani alikuwa ni Yubali mwana wa Lameki. Ufundi wote wa sanaa na mziki
tunaouona leo ulikuwa na chanzo chake katika uzao huu wa Lameki. Katika wana wa
Lameki pia alikuwepo Tubal-kaini, yeye alikuwa mfua kila chombo cha kukatia,
cha shaba na cha chuma. Katika huyu sayansi ya matumizi ya chuma ilianza.
Tunaposoma historia kwenye shule zetu tunafundishwa kuwa mtu alianza kutumia
chuma kwenye kipindi cha zama za chuma baada ya zama za mawe kupita.
Inawezekana wazi kuwa enzi za akina Adamu mpaka Lameki zilikuwa ni zama za mawe
na ni kuanzia kwa Tubal-kaini ndipo zama za chuma (iron age) zilipoanzia.
Ugunduzi huu umeendelea kuwa mkubwa kila kila siku hadi kufikia kwenye zama za
sasa zinazojulikana kama “artificial intelligence.”
Mistari miwili ya
mwisho ya sura hii inaeleza juu ya uzao mwingine alioupata Adamu baada ya siku
nyingi. Alipomzaa Sethi, Hawa anajitokeza kwa mara nyingine tena akitabiri juu
ya kile mtoto yule alichobeba. Kwa sasa akajua kuwa Sethi alikuwa amezaliwa ili
kuziba nafasi ya Habili ambaye Kaini alimwua. Ni kweli kuwa Sethi alikuwa
amekuja kwenye nafasi ya Habili, maana ni baada ya Sethi kumzaa Enoshi ndipo
watu walipoanza kuliitia jina la Bwana hapo. Sethi alikuwa mtu wa imani kwa
Bwana kama Habili alivyokuwa. Ni furaha sana kuona jinsi sura hii
ilivyopangiliwa; inaanza kwa kuonesha uovu wa mauti lakini inamalizia kwa watu
kuliitia jina la Bwana. Hii inatufundisha kuwa hata kama tumeanza vibaya na
Bwana bado tunaweza kumaliza vizuri ikiwa tutaamua kuliitia jina la Bwana.
No comments:
Post a Comment