Sunday, March 25, 2018

MADHARA YA UMWAGAJI DAMU KATIKA NCHI (KIBIBLIA)

“…kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake…” (Hesabu 35:33)

Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe,
Utangulizi

Tunamtukuza Mungu Baba yetu kwa neema aliyotupa kupitia Mwana wake pekee Yesu Kristo kutupa nguvu za Roho wake Mtakatifu ili tupate kuyatafakari maandiko pamoja. Leo tunaangalia suala moja muhimu sana katika uhai na ustawi wa taifa (nchi), nalo ni: Madhara ya umwagaji damu katika nchi. Msitari tuliouweka hapo juu unatupa mahali pa kuanzia katika kulitafakari suala hili muhimu. Ili tuende pamoja vizuri katika somo hili, ngoja tuangalie mistari kadhaa katika Biblia.

Mwanzo 9:4-6, Mungu aliagiza hivi juu ya damu ya uhai wa mwanadamu:
Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.

Kisha katika Hesabu 35: 30, 33-33 Mungu akasema:
Mtu awaye yote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu hata akafa… Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga. Kwa hiyo msiitie unajisi nchi muiketiyo, ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi Bwana nakaa kati ya wana wa Israeli.

Nimekuwekea mistari hii ya utangulizi ili uone mambo yafuatayo:
  1. Damu ni uhai wa mtu. Kumwaga damu ya mtu ni sawa na kumwaga uhai wa mtu huyo.
  2. Damu ikimwagika mahali popote inaanza kudai malipizi (kisasi).
  3. Gharama ya damu kumwagika ni damu nyingine tena imwagike (atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu).
  4. Damu ya mtu ikimwagika katika nchi inaitia hiyo nchi unajisi.
Mambo haya yanatupa kujua kuwa damu ya mtu ina thamani kubwa sana mbele za Mungu, na Mungu hayuko tayari kuona damu isiyo na hatia ikimwagika. Mwanadamu aliyefanywa na Mungu, anapaswa kuondolewa na Mungu mwenyewe, sio na mwanadamu mwingine. Damu ni uhai wa mtu. Uhai huu mtu alipewa na Mungu kupitia pumzi yake. Mwanzo 2:7 inasema: “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai”. Mtu alifanyika nafsi hai baada ya pumzi ya Mungu kupulizwa ndani yake. Pumzi ya Mungu ndiyo iliyoamsha uhai wa kila kitu ndani ya mtu. Hivyo kumwaga damu ya mtu ni kuingilia kazi ya Mungu aliyoifanya, na kufanya hivyo kuna madhara makubwa sana.

Madhara yatokanayo na kumwaga damu katika nchi

Biblia inatuongoza vema kabisa juu ya madhara yanayoweza kuipata nchi kutokana na damu ya mtu kumwagwa juu yake. 

  1. Nchi kukataa kuwafanikisha wanaoikaa
Kaini alipomuua ndugu yake Habili, Mungu alimwambia hivi: “umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani” (Mwanzo 4:11-12).
Dhambi ya umwagaji damu ilileta laana juu ya Kaini katika ardhi. Ardhi ni kiashiria cha vyanzo vya uzalishaji (means of production) ambavyo Mungu amemwekea mwanadamu. Damu ya Habili ilipomwagika katika ardhi, kukatokea uhasama kati ya ardhi na Kaini. Ardhi ikazuiliwa kumpa Kaini mazao yake. Mazao ya ardhi inamaanisha mafanikio yatokanayo na njia za uzalishaji (prosperity). Kaini alipomwaga damu akajiingiza kwenye laana ya kutokufanikiwa katika ardhi.
Damu ya mtu yeyote inapomwagika juu ya ardhi, ardhi inafunga milango yake ya mafanikio. Ndio maana maeneo mengi yenye matukio ya umwagaji damu wa aina yoyote ule duniani, hayana mafanikio makubwa.

  1. Kuzuiliwa kwa maombi yanayohusu taifa (nchi) mbele za Mungu
Neno la Mungu katika Isaya 1:15 linasema: “Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu”.
Kwa sababu ya mikono ya watu kujaa damu, Mungu anajificha kila wakati watu hao wanapokunjua mikono yao mbele zake na pale wanapoomba maombi yao yeye hasikilizi. Taifa lolote ambalo damu zisizo na hatia zinamwagika ndani yake linakosa uhalali wa kusikilizwa mbele za Mungu. Watu wanaweza kuomba maombi mengi kwa ajili ya nchi, lakini kama kuna hatia ya damu juu ya nchi hiyo, Mungu hasikilizi.

  1. Kuondoa uwepo wa Mungu katika nchi
Hesabu 35:33-34 inasema: “Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga. Kwa hiyo msiitie unajisi nchi muiketiyo, ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi Bwana nakaa kati ya wana wa Israeli”.
Neno la Mungu hapa linatuonya waziwazi kuwa damu huitia nchi unajisi. Madhara ya unajisi ni kuwa unamwondoa Mungu asikae mahali hapo. Kwa hiyo damu ya mtu inapomwagika inatia nchi katika unajisi ambao unamfanya Mungu ashindwe kukaa pamoja na taifa hilo. 

  1. Kuzalisha chuki na visasi kati ya watu
Damu ikimwagika inadai kisasi. Damu ya Habili ilimlilia Mungu kutoka katika ardhi (Mwanzo 4:10) ikidai kisasi. Abneri alipomuua Asaheli ndugu yake Yoabu, Yoabu nae alimuua Abneri kwa ajili ya damu ya Asaheli (2 Samweli 3:27). Mfalme Yoashi alipomuua Zekaria mwana wa Yehoyada, watumwa wake mfalme Yoashi nao wakamfanyi fitna mfalme wakamwua kitandani pake ‘kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada’ (2 Nyakati 24:20-25).
Kwa hiyo nchi inapomwaga damu ya mtu mmoja ni kuwa inaanza kuzalisha vizazi vyenye chuki na visasi moyoni. 

Tanzania na damu zilizomwagika ndani yake

Nchi ya Tanzania imeshuhudia damu za watu zikimwagika katika maeneo mbalimbali ya nchi. Watekelezaji wa matukio hayo kwa sehemu kubwa hawajajulikana. Lakini madhara ya umwagaji damu hizo yanaweza kuliathiri taifa pasipo kujali kama wahalifu wanajulikana au hawajulikani. Kadiri matukio haya yanavyoongezeka katika nchi, ndivyo nchi inavyozidi kujitenga na mfumo wa baraka zake kutoka kwa Mungu. Watu wanaweza kufanikiwa katika ngazi ya mtu binafsi (individual wise) lakini mafinikio ya ngazi yakitaifa yanaweza kukosekana kwa sababu ya wingi wa damu zinazodai visasi katika nchi. Pia taifa linaweza kujikuta linapoteza kabisa umoja na amani yake kwa sababu ya chuki na visasi mioyoni mwa watu vinavyotokana na madhara ya umwagaji damu za watu.

Nini kifanyike?

Hesabu 35:33-34 inasema: “Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga’.

Kwa kuangalia maneno yaliyokolezwa hapo juu utaona kuwa ili kufuta madhara ya umwagaji damu basi lazima damu ya huyo iliyeimwa pia imwagike. La hasha! Sasa tunayo damu ya Yesu Kristo. Yeye ambaye amekufa na kufufuka ili aziondoe laana zote. Tukinyenyekea chini ya msalaba wa Yesu kama taifa na kuuitia damu yake ipate kututakasa basi tunaliokoa taifa letu na madhara ya damu zilizomwagika ndani yake.

Ili hayo yafanyike, lazima tukubali kama nchi kutubu na kuomba rehema za Mungu. Maombi ya kitaifa yanathamani sana mbele za Mungu pale kiongozi mkuu wa taifa anapotambua dhambi yake na ya watu wake na kuamua kwa dhati kabisa kutafuta rehema za Mungu. Wana wa Israeli walipokua jangwani wakafanya ndama, wakaiabudu, Mungu alitaka kuwaangamiza. Lakini Musa kama kiongozi wa taifa lile alisimama mbele za Mungu akaomba rehema kwa ajili ya watu wake (Kutoka 32:1---).
Tanzania inamhitaji Yesu wakati huu kuliko nyakati zote ilizowahi kupitia. Toba na kunyenyekea kuanzia kwa Rais wa nchi mpaka kwa raia wa kawaida kunahitajika sana wakati huu ili kuomba rehema za Bwana Mungu wetu juu ya nchi yetu.

Mungu irehemu Tanzania,
Jina lako Mungu wa mbinguni litukuzwe daima katika Kristo Yesu.
Amen.

No comments:

Post a Comment