Thursday, March 9, 2017

MJUE YETHRO “MKWEWE MUSA”



Bwana Yesu Kristo Asifiwe!

Lengo la somo hili ni kukupanulia tu ufahamu wa watu mbalimbali katika Biblia na kukupa kuwajua kwa undani wao. Hii ni muhimu ili kukusaidia kuelewa namna Biblia inavyopangilia matukio na namna Mungu alivyokuwa akifanya kazi yake kwa kufuata vizazi.

Leo nataka nimlete kwako mtu mmoja kwenye Biblia ambaye yawezekana umesoma habari zake lakini hujapata kumfahamu vizuri – YETHRO “Mkwewe Musa”.
Kutoka 3:1 inasema: “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu”.

Msitari huu unataja mtu huyu aitwaye Yethro kwamba alikuwa ni kuhani wa Midiani lakini pia alikuwa ni mkwewe Musa. Jina “Yethro” linajitokeza mara 10 tu kwenye Biblia yote na mara zote hizo ni kwenye Kitabu cha Kutoka tu (Kutoka 3:1; 4:18; 18:1; 18;2; 18:5; 18:6; 18:9; 18:10; 18:12). Utaona hapo kuwa ni Mistari tisa (9) niliyoorodhesha lakini jua kwamba katika Kutoka 4:18 jina hili linajitokeza mara 2 kwenye msitari huo na hivyo kukamilisha idadi ya jina hili kujitokeza mara kumi (10) katika kitabu hiki cha Kutoka.
Lakini unapoifuatilia historia ya mtu huyu kwenye Biblia utagundua kuwa Yethro halikuwa jina la mtu bali ni cheo. Kama ningetaka kukueleza kwa kiingereza ningesema kuwa: “Jethro was not a name of a person but a title”. Unashangaa! Hivyo ndivyo ilivyo.

Ni kama neno Farao. Watu wengi wanafikiri kuwa Farao lilikuwa jina la mfalme wa Misri – hapana! Farao kilikuwa ni cheo cha mtu mwenye mamlaka ya kifalme juu ya Misri. Kwa hiyo mtu mwenyewe alikuwa na jina lake lakini cheo chake ndicho kiliitwa Farao. Ni kama ambavyo tunatumia neno “Rais” kwenye ulimwengu wa sasa. Neno "Rais" ni cheo na mtu anayekuja kutumikia cheo hicho anakuwa ana jina lake binafsi. Mfano, John Pombe Magufuli ni jina binafsi la Rais wa sasa wa Tanzania. Lakini Rais sio jina la John Pombe Magufuli ila ni cheo chake. Nimetaka kuliweka sawa hili jambo ili kukurahisishia kuelewa habari za Yethro kama Cheo na si kama jina binafsi la mtu.

Maana ya Yethro ni ipi?

Yethro kwa kiebrania ni ‘Yithrow’ ambalo kwa tafsiri ya kiingereza linamaanisha “his excellence” yaani mtukufu. Na kama tulivyoona kwenye Kutoka 3:1, mtu huyu alikuwa ni kuhani wa midiani. Kwa hiyo Yethro ilikuwa ni cheo kilichoambatana na nafasi yake kama Kuhani wa midiani. Hivyo kama asingekuwa kuhani wa midiani basi mtu huyu asingetambulishwa kama Yethro bali angetajwa kwa jina lake binafsi.

Lakini kuwa kuhani tu haitoshi kutueleza undani wa nafasi aliyokuwa nayo mtu huyu. 
Tumesema kuwa maana ya Yithrow ni his excellence – mtukufu. Sasa katika mazingira ya kawaida neno hili hutumika kuwatambulisha watu wenye mamlaka ya kifalme si makuhani. Huwa tunaona marais wanaitwa “Mtukufu Rais” au “Mtukufu Mfalme” n.k. lakini hatuoni neno mtukufu likitumika kuwataja makuhani. Hii inatupa kufikiri zaidi kuhusu huyu Yethro.

Kamusi kadhaa za Biblia zinaeleza kuwa licha ya kuwa kuhani, Yethro alikua pia ni mfalme wa Midiani. Kwa asilimia kubwa hii inaleta maana halisi ya neno Yethro. Sasa ukichukua nafasi yake kama kuhani ukachanganya na nafasi yake kama mfalme utapata kuelewa ni kwa nini Yethro alikuwa na hekima ya kumshauri Musa kuhusu masuala ya uongozi kule jangwani. Angalia jinsi Kutoka 18:13-24 inavyosema:

Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.

Hii hekima ya uongozi ambayo Yethro alimpa Musa inatuthibitishia kuwa lazima mtu huyu alikuwa ni kiongozi mahali fulani. Na kama tulivyoona hapo juu, mtu huyu anatajwa kuwa alikuwa ndiye mfalme wa Midiani. Na hivyo hekima aliyompa Musa lazima ilitokana na uzoefu aliokuwa ameupata kwa miaka yote aliyotumika kama mfalme wa midiani. Naamini tunaenda pamoja!

Jina la mkwewe Musa ni nani?

Kama Yethro sio jina la mtu bali ni cheo, basi ni vizuri tulijue jina sahihi la huyu mkwewe Musa. Kutoka 2:16-18 inatuambia kuwa jina la huyu kuhani wa Midiani ambaye Musa alioa mwanawe alikuwa anaitwa Reueli.
Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?
Kwa hiyo baba yao akina Sipora alikuwa anaitwa Reueli sio Yethro. Hesabu 10:29 inathibitisha jambo hili kwa kutuambia kuwa Reueli Mmidiani ndiye alikuwa mkwewe Musa. Reueli kwa kiebrania maana yake ni rafiki wa Mungu (a friend of God). Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa Reueli ndilo lilikuwa jina la baba-mkwe wake Musa na Yethro kilikuwa cheo chake kama kuhani na mfalme.

Reueli/Yethro ni uzao wa nani?

Kutoka 2: 15 inatueleza kuwa Musa alipokua anaukimbia uso wa Farao baada ya kumwua yule Mmisri alienda katika nchi ya Midiani. Kwa hiyo Midiani ilikuwa ni nchi inayojitegemea na ilikuwa na mfalme na kuhani wake aitwaye Yethro/Reueli. Kwa hiyo ili tuweze kufuatilia uzao wa Reueli vizuri lazima tuelewe hili taifa la Midiani lilitokea wapi.

Pana mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wanatheolojia juu ya alikotokea huyu Reueli. Lakini acha sisi tuangalie kile Biblia inachosema. Mwanzo 25:1-3 unasema hivi:
Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua.

Nataka tumuangalie huyo mtoto anayeitwa Midiani kwenye huo uzao wa Ibrahimu. Baada ya Sara kufa, Ibrahimu alioa mke mwingine aitwaye Ketura na akamzalia wana. Miongoni mwa wazao wa Ibrahimu waliopatikana kwa Ketura alikuwa ni huyu aliyeitwa Midiani. Sasa ukifuatilia Biblia vizuri utaona kuwa huyu Midiani naye alizaa wana na baadaye walikuja kujulikana kama jamii ya Wamidiani. Hawa Wamidiani ndio waliomnunua Yusufu mikononi mwa Waishmaeli wakaenda kumuuza kwa Potifa huko Misri (Mwanzo 37:28, 36).

Kwa mpangilio wa matukio ulivyo inaonekana kuwa Midiani ilikuwa karibu na Misri na ndio maana hawa Wamidiani waliweza kwenda kumuuza Yusufu huko Misri. Inawezekana ndio sababu pia Musa akakimbilia huko alipotoka Misri.

Sasa kama Midiani alikuwa ni mzao wa Ibrahimu, na Yethro alikuwa kuhani na mfalme wa Midiani maana yake ni kuwa mtu huyu aitwaye Yethro alikuwa ni wa uzao wa Ibrahimu. Ukilitazama jambo hili kwa jicho la rohoni utagundua kuwa kulikuwa na uhusiano wa kiuzao kati ya Musa na Yethro na ndio maana Mungu alimwongoza Musa akimbilie huko pale alipotoka Misri.

Ukitaka kuiona hii kitu kwa ndani zaidi jiulize Sipora – mkewe Musa- alipata wapi ufunuo wa kumtahiri mtoto pale Bwana alipotaka kumwua Musa? Kutoka 4:24-25 inasema:
Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, Bwana akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.

Sasa Biblia inatuambia kuwa agano la kutahiri watoto aliliweka Mungu kati yake na Ibrahimu na uzao wote wa Ibrahimu. Mwanzo 17:10-14 inasema:
Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele. Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.

Kwa hiyo suala la kutahiri watoto lilikuwa suala la Mungu na uzao wa Ibrahimu. Sasa swali la kujiuliza ni kuwa: Kama Sipora hakuwa wa uzao wa Ibrahimu alipata wapi ufunuo wa kujua kuwa jambo lililofanya Bwana atake kumwua Musa njiani ilikuwa ni kwa sababu ya kutokumtahiri mtoto wao? Hii inatufikirisha na kutufanya tuamini kuwa Yethro alikuwa wa uzao wa Ibrahimu kupitia kwa Midiani mtoto wa Ketura na kwa hiyo alikuwa amewafundisha watoto wake agano la Mungu na uzao wa Ibrahimu na hii ndiyo ilimpa Sipora kujua umuhimu wa kumtahiri mtoto.
Nimekueleza haya yote ili upate kujua kuwa Musa hakukimbilia kwa Midiani kwa bahati mbaya na wala hakukutana na Yethro kwa nasibu bali Mungu mwenyewe ndiye aliyekuwa anamuongoza.

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Yethro  
1. Karibisha wageni na uwe mkarimu kwa watu wote hata kama huwajui maana hujui wamebeba baraka gani ndani yao. -  Kutoka 2:20-21

2. Mfuate Mungu wa kweli popote aliko hata kama wewe ulikuwa na Mungu wako mwanzoni. – Kutoka 18:1-12

3. Tumia uzoefu ulionao ili kuwasaidia wengine waweze kuvuka mahali unapoona wamekwama. Kutoka 18:13-24

4. Wajulishe na uwafundishe watoto wako agano lililopo kati yako/yao na Mungu ili wajue namna ya kulisimamia na kulifuatilia. Kutoka 4:24-26

Yesu Kristo akubariki sana!
Endelea kufuatilia blog hii ili ujue nani anafuata katika mfululizo huu!

No comments:

Post a Comment