Saturday, March 18, 2017

KWA HABARI YA ZINAA (SEHEMU YA SITA)

Mwandishi: Anderson Leng'oko

Utangulizi

Mpendwa msomaji, tunaendelea na mwendelezo wa mafundisho yetu ya somo la Kwa habari ya zinaa, na sasa tupo sehemu ya sita; sehemu ya sita inaendelea kutoka tulipoishia kwenye sehemu ya tano. Na kama utakuwa umekosa sehemu zilizotangulia tafadhali bonyeza hapa ili uweze kupata mtiririko mzuri. Kuna watu wanaweza kuwa wanapata shida kuhusu mana ya neno zinaa linapotumika katika somo hili; lakini tunatumia neno zinaa kiujumla; ikumbukwe katika sehemu ya kwanza tuliweka utangulizi wenye kuelezea maana hii kama ifuatavyo:



ZINAA NI NINI?
Katika biblia zinaa inatumiwa kumaanisha tendo la kufanya mapenzi na mtu asiyekuwa mkeo wala mumeo, ukiwa tayari mwanandoa. Lakini katika somo hili tutatumia neno la zinaa kumaanisha kufanya mapenzi isivyo halali kwa ujumla, ambapo kuna wakati neno zinaa litatumika kumaanisha uasherati, yaani kufanya mapenzi kabla ya ndoa, kuna wakati litatumika kumaanisha pia tendo la kufanya mapenzi na mtu asiye mumeo wala mkeo wakati wewe umeoa au umeolewa.

Upendo endelevu na upendo usio endelevu
Wapo watu kwa kutokujua wanawapenda wenzi wao kiasi cha kuwapa kila kitu wanachohitaji. Huu nao ni upendo. Lakini ni upendo usio endelevu. Si endelevu kwani mwisho wake ni madhara kwetu na kwa tuwapendao; Au tuliweke hivi, tuchukulie ule upendo unaopelekea watu kuzini nao ni upendo, lakini tuuite upendo usio endelevu. Kisha ule upendo ambao ni wa kumfanya mtu atimize makusudi ya Mungu ni upendo endelevu. Upendo usio endelevu hupelekea matumizi yasiyo endelevu na upendo ulio endelevu hupelekea matumizi yaliyo endelevu. Ukimpenda mpenzi wako hadi ukaamua kuzini naye kabla ya ndoa wewe una matumizi yasiyo endelevu na ukimpenda mpenzi wako ukamheshimu na kumtunzia uhusiano wake na Mungu hadi mkafunga ndoa wewe una matumizi endelevu.
Mwenye matumizi yasiyo endelevu ni yule anayemtumia mpenzi wake kuzini; kwa sababu anamtumia, na anamfurahisha na kujifurahisha yeye, ila matumizi yale yanamfanya mwenzi wake asidumu na usitawi wake kiroho uathirike. Anachoka na kupoteza thamani mbele za Mungu na mbele za mwanadamu kwani ‘anapata jeraha na kuvunjiwa heshima, wala fedheha yake haitafutika’.
Lakini pia kuzini kusiko na baraka za ndoa ni matumizi yasiyo endelevu ya mwenzi wako kwani unaua umilele ndani yake, unaangamiza nafsi yake na kumfanya awe ni mtu ambaye ataishi tu hapa duniani na anakuwa amepoteza nafasi ya kuingia mbinguni. Sasa unapata picha ya kwanini tunasema kuzini kabla ya ndoa au nje ya ndoa ni matumizi yasiyo endelevu au upendo usio endelevu.
Hapa tunamaanisha kuwa upendo endelevu ni ule upendo ambao siyo tu unajali furaha ya mwenzi kwa wakati huu, bali kwa wakati ujao na milele yote, wakati kinyume na hapo, ndo kwenye upendo usio endelevu, ambao unajali tu furaha ya wakati huu.
Upendo usio endelevu ni kumpenda mwanafunzi na kumzinisha na kuharibu masomo yake na kumwacha analia.
Upendo usio endelevu ni kumpenda mtu na kumharibia ndoa yake na kuzini naye na kusababisha aachike arudishwe kwao wakati wewe uliyemponza mwenzio ndoa yako iko salama.
Upendo usio endelevu ni ule unaopelekea wewe kumfarikisha mtu na Mungu wake kwa kumtumbukiza katika zinaa na uasherati na kupelekea mwenzako kukosa Baraka za Mungu kwa sababu ya tamaa zako za muda mfupi.
Angalia; na utagundua kuwa watu wengi wanaingia katika mahusiano wakiwa na upendo usio endelevu.
Chunguza mahusiano yako, jaribu kuondoa kila kitu ambacho kina ishara ya upendo usio endelevu, na jaribu kuvunja kila mahusiano ambayo siyo endelevu kama mwenzi wako anakataa na kung’ang’ania tabia zisizo endelevu.
Upendo ulio endelevu ni upendo ambao unajali mafanikio ya mtu ya mwili na roho.
Upendo ulio endelevu hauegemei na kutegemea furaha za muda mfupi, ambazo hazina tija ya milele.
Upendo ulio endelevu una heshima, upendo ulio endelevu una subira, upendo ulio endelevu hautafuti mambo yake wenyewe, upendo ulio endelevu ndio hasa unaostahili kuitwa upendo na ndio ulioongelewa kwenye 1Wakorintho 13

1Wakorintho 13:1-8a
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.
Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.
Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.
Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;
haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;
haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
Upendo haupungui neno wakati wo wote;
Huo unaoongelewa hapo juu ndio upendo endelevu, kwa misingi ya imani lakini pia ukiutumia upendo huu katika kila sehemu, ni aina ya upendo inayolipa sana.
Tukisema upendo huvumilia, hatutaki mtu anayejifanya anakupenda na anataka akuoe na anataka azini na wewe leoleo. Huyo atakuwa amekosa uvumilivu. Tena anakuwa amekosa kuwa na adabu; tena huyo atakuwa anatafuta mambo yake mwenyewe, tena haoni uchungu kama wewe unaweza kupotea na kuishia kuzimu, halafu pia anafurahia udhalimu na kuikataa kweli. Sawa dada?
Kama mtu unamwambia kuwa unamwamini Mungu na hujamjua mwanaume na hutaki mjuane kabla ya ndoa, halafu hakuamini, huyo hakupendi, kwani upendo huamini yote.
Ndiyo maana watu wengine wanakuwa wanashangaa sana kwamba mbona mtu fulani ni malaya na tumeshamwambia mumewe amuache lakini tunashangaa hamuachi, lazima mjue kuwa upendo huamini yote, na yule mwanaume anaamini yote anayoambiwa na mkewe kwamba yote hayo mnayosema siyo ya kweli.
Kwa hiyo katika somo letu hili, tunauita upendo ulio endelevu upendo na upendo usio endelevu ni chuki, japo inaonekana kama ni upendo. Ukimpenda mtu halafu ukamfanyia mambo yasiyo endelevu kama kuzini naye, basi wewe umemchukia.

Hiyo ndiyo maana halisi ya upendo ndugu; usitumie neno upendo vibaya, ujichunguze upendo ulio nao kama hautokani na upendo wa Mungu kwetu, bado siyo upendo. Rudi msalabani ili Yesu akutengeneze na kukupa maana halisi ya upendo, kwani yeye ni Pendo na hakuna maana sahihi ya Upendo inayoweza kupatikana isipokuwa katika Yeye.

Usikose kufuatilia sehemu zinazofuata za somo hili kwani bado Mungu ana mengi ya kusema nasi; pia uwasambazie na wengine ili nao waipate kweli hii iwajenge mwili na roho.

No comments:

Post a Comment