Saturday, April 15, 2017

KWA HABARI YA ZINAA (SEHEMU YA SABA)


Mwandishi: Anderson Leng'oko
Mwenyezi Mungu kwa neema yake anaendelea kutufundisha katika namna ambayo tunapata kuuelewa wema wake na kupata sababu za kutokumkosea. Ni imani yangu kuwa watu wakielewa hasa maana na uzito wa dhambi wanazofanya itawasaidia kuziacha na kumgeukia Mungu. Karibu tuendelee kujifunza somo hili; kama ulikosa sehemu zilizotangulia bonyeza hapa upate mtiririko mzuri zaidi.




Zinaa ni kukosa upendo kwa unayezini naye
Kwa kawaida mtu unayempenda, utathamini utu wake na kuheshimu asili yake. Utataka apate mema tu na wala siyo mabaya. Upendo wa Agape (upendo wa kiMungu) ndio ambao wanadamu tumeumbiwa. Upendo huu ni kutambua kuwa mwanadamu ameumbwa na Mungu na Mungu ana mpango wa kuyatumia maisha ya kila mwanadamu ili kukamilisha malengo yake (Mungu) katika kujenga ufalme wake.

Hivyo kama wewe unampenda mwenzio; utajitahidi kuhakikisha kwamba yale ambayo Mungu ameyapanga yafanyike katika maisha yake yanafanyika kikamilifu kwa sababu; Mungu atamleta hukumuni huyu mtu kama hatatekeleza yale mambo ambayo Mungu angetamani kuyaona huyu mtu anafanya. Lakini siyo hilo tu, Mungu anatamani sana kuona huyu mtu anaishi katika mapenzi ya Mungu ili mtu huyu aweze kuurithi uzima wa milele.


Vipo vitu ambavyo vinamtenga mtu na Mungu wake, vitu hivi ndizo dhambi. Mungu anapomuumba mtu hataki kabisa dhambi imtawale au ikae ndani yake kwani anajua kuwa dhambi ndicho kikwazo cha kumfikisha mtu huyu katika makusudi ya Mungu katika maisha yake hivyo anajitahidi kumuelekeza na kumlinda mtu huyu asidanganyike na dhambi.

Upendo hapa unakuja kuwa na kusudi jema. Upendo wenye kusudi jema hapa ni ule unaomsaidia mwanadamu kwanza, kuimarisha uhusiano wake na Mungu na pili, kuyafanya yale ambayo Mungu angetamani kuyaona mtu huyu anayafanya. Yaani makusudi ya Mungu aliyoyaweka ndani ya mtu.

Hivyo tunaona kwamba mtu anayekuja kuzini na mwenziwe anamrudisha mwenziwe nyuma na kumharibia kabisa mahusiano yake na Mungu, yaani anamfarakanisha na Mungu na kusababisha mahusiano ya mtu huyu na Mungu kupotea, na yale makusudi ya Mungu juu ya mtu huyu pia yanakufa na kupotea kabisa.

Kwa hiyo licha ya kuwa watu husema kuwa wanampenda msichana/mwanamke fulani au mkaka/mwanaume fulani hadi wanaamua kuzini naye, hicho kitu si cha kweli kwani upendo siyo kumtenga mtu na Mungu wake bali upendo, kwa sababu ni mwema, huzaa chema. Upendo usio mwema huzaa uovu na upendo ulio mwema huzaa mema; amani, furaha na mafanikio katika Kristo.

Unaweza kusema, ‘sasa mbona mtu huyu ananililia na kuning’ang’ania ili nizini naye, sasa mimi kwa kuwa nampenda na sitaki kuona akiteseka, ni lazima nimhurumie na kumpa anachotaka,’ Kiukweli hiyo ni hoja ya kibinadamu. Acha kufanya hivyo, kumbuka mtoto anapolilia wembe wewe kama mzazi unatakiwa kumzuia kwa kumchapa. Kwani ukimpa ukamkata gharama ya kumtibia majeraha aliyoyapata kwa kujikata na huo wembe itabaki kwako. Kwa hiyo, hiyo unayofanya siyo huruma, bali ni ukatili kwani unamuangamiza, na siyo unamsaidia.

Hivyo basi dhana ya kwamba kufanya zinaa ni ishara ya kuoneshana upendo inatoka kwa baba wa uongo-ibilisi na shetani na huo ni UPOTOSHWAJI WA UPENDO.

MTU ANAYEZINI HAJIPENDI MWENYEWE
Tumeona hapo juu kwamba mtu anayezini hampendi yule anayezini naye, lakini hapa tutaona pia mtu anayezini hajipendi mwenyewe; angalia mstari huu;
Yohana 12:25
Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.

Yesu anasema kuwa aipendaye nafsi yake ataiangamiza, hii ina maana kuwa nafsi inatamani vitu visivyofaa katika dunia, na kuipenda ina maana ni kuishibisha na kila ovu inalotamani. Ndiyo maana mahali pengine wanasema:

1Timotheo 5:6
Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.

Hii ina maana kwamba nafsi siku zote yatamani mambo mabaya na mtu anatazamiwa kuizuia ili aishi. Sasa mtu anayeipenda nafsi yake ni yule ambaye hataki kuona nafsi yake inakosa kile inachotamani; yaani ni kama mtu ambaye hataki kuona mwanae ananyimwa kile ambacho anatamani na anajitahidi kumpa kila kitu anacholilia maana hataki kuona mtoto yule analia.

Kwa hiyo basi, ikishatokea kwamba mtu huyu anaidekeza nafsi yake na kuipa kila inachotaka, ataipoteza kwa sababu, nafsi ina udanganyifu na udhaifu mwingi ndani yake na ndiyo maana Paulo katika Timotheo anasema tunatakiwa kuizuia.

Sasa yule anayeipenda nafsi yake, haizuii na inampeleka katika matendo mabaya ya uharibifu ikiwemo zinaa. Mtu huyu haipendi nafsi yake, haipendi kwa sababu ataipoteza, ataipoteza kama Yesu alivyosema; kuipenda kwake hakufai kwani mwisho wa siku ataishia kuipoteza kama maandiko hapo juu yalivyosema. Atakufa katika upotevu na nafsi yake haitapona. Ndiyo maana dhambi ya zinaa ni mara nyingi sana imezaa mauti.

Watu ‘waliozipenda’ nafsi zao na kuzistarehesha katika uzinzi wameishia kuzipoteza kwani wanapata magonjwa na kupoteza uhai, wengine wanauawa kwenye mafumanizi au wanauana kwa kuchomana visu na kupigana risasi au hata kurogana wakigombania wanawake au wanaume.

Ndiyo maana hapo juu tumeona kuwa kama mwenzio anakulazimisha kuzini na kukubembeleza sana, huyo ameipenda nafsi yake hivyo ataiangamiza pamoja na yako pale atakapofanikiwa kuzini na wewe, hivyo kwa kuzini naye haumsaidii wala haujisaidii, bali ulitakiwa kuichukia nafsi yake na yako ili uziokoe nafsi hizi mbili hata uzima wa milele.

Watu wazinifu licha ya kuwa walizipenda nafsi zao wakazidekeza na kuzipatia zile tamaa zilizotamaniwa na nafsi hizo, wanaishia kuzipoteza. Lakini tumekwisha kuona hapo juu kwamba upendo ni kitu chema. Na kitu chema chochote ili tupate kujua kuwa ni kitu chema tunakipima kwa matokeo. Basi sasa, kwa kuwa hawa watu walikuwa na ‘upendo’ kwa nafsi zao na kuzipa kile ambacho nafsi hizo zilihitaji, kwa kuangalia matokeo ya upendo wao tunaona kuwa haukuwa upendo kwani matokeo yao ni kifo, magonjwa ya zinaa na vifungo vya mwili na roho au uadui na hata ndoa kuvunjika. Hivyo kwa tafsiri halisi ya upendo wenye matokeo mema, watu hawa hawakuzipenda nafsi zao bali WALIZICHUKIA.

Naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
Hapa yesu anatufundisha kuwa kuichukia nafsi ni kuizuia nafsi kupata kile ambacho inakitamani ambacho ni kibaya. Mtu anayeizuia nafsi yake, ndiye aliye hai kwelikweli kama tulivyosoma kwamba mtu asiyeizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai. Hivyo basi, tunaona kuwa Upendo wa kweli una matokeo mazuri, kwa kuwa tumeona kuwa yule ‘aliyeipenda’ nafsi yake na kuishibisha kwa tamaa ameishia kupotea, tuliona matokeo mabaya hivyo ule haukuwa upendo halisi kwa nafsi yake. Lakini tazama huyu anayeizuia nafsi yake na kuinyima tamaa zake ziletazo mauti, huyo kutokana na matokeo ya matendo yake, anaisalimisha nafsi yake hata uzima wa milele, kwa hiyo huyu hapa tunaona kuwa NDIYE MWENYE UPENDO WA KWELI  kwa nafsi yake.

uchambuzi; Mtu anayezini anaichukia nafsi yake, hajipendi na anajichukia mwenyewe kwani anajipoteza na kujifarakanisha na Mungu wake na kwa hakika atapotea duniani na mbinguni kwani atapata matatizo ya zinaa hapa duniani kwa kupata magonjwa, kuwa na uadui na watu, kuishi maisha ya chuki, aibu, fedheha na wasiwasi na hata kuuawa, kwa mfano kama nilivyokwisha sema ni mara nyingi nimesikia watumishi wa Mungu wakiuawa kwenye mafumanizi, na akisha kufa mtu huyu anaingia jehanamu moja kwa moja.

Kama tulivyoona hapo juu kwamba anayeichukia nafsi yake na kuinyima tamaa zake ataisalimisha hata uzima wa milele; ‘anayeipenda’ na kuipa zinaa ina maana atahukumiwa katika moto wa milele. Kwa hiyo zinaa ni UPOTOSHWAJI WA DHANA HALISI YA UPENDO. Anayezini, hampendi anayezini naye hata kumuangamiza, lakini pia hajipendi mwenyewe hata kujiangamiza, tazama mstari huu:

Mithali 6:32
Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo LITAKALOMWANGAMIZA NAFSI YAKE.

Tukirudi kwenye zile dhana zetu za upendo endelevu na usio endelevu, tunaona kuwa aipendaye nafsi yake na kuipa mahitaji ya mwili yasiyoendana na makusudi ya Mungu, huyo anajipenda, lakini hajipendi upendo endelevu. Anajitumia kwa maslahi ya muda mfupi tu ambapo baada ya maisha haya ya sasa atapotea.

Matumizi endelevu ya nafsi na mwili na roho yako ni yale yanayokupa maslahi ya kudumu duniani na mbinguni, yaani upate raha na amani hapa duniani na upate uzima wa milele huko mbinguni, ndicho Yesu anachosema katika mistari hii

Marko 10:29 Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,
 30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

Kwa hivyo kama unaipenda nafsi yako na hautaki kuipoteza, inabidi uipende upendo endelevu, utakaoifaidisha hapa duniani na mbinguni. Usiipende nafsi yako upendo usio endelevu.
Unapofanya zinaa na asiye mkeo, yaani mke wa mtu, wewe unaipenda nafsi yako kwa upendo usio endelevu, kwani unaweza kufa katika njia yako hiyo ukaenda kuzimu moja kwa moja, pia utakuwa umeacha familia na watoto wako watahangaika.

Ukifanya hilo la mke wa mtu pia; unachukua magonjwa hata kama hutauawa, magonjwa yataitesa familia yako hasa mkeo, na ukiwa ni Ukimwi, utalazimika kufa mapema na kuwaacha watoto wangali wadogo! Ni kweli uliipenda nafsi yako na kuipa kile inachotaka, lakini uliipenda upendo usio endelevu.

Tena unapozini na mke wa mtu, unafanya chukizo mbele za Mungu na kujiletea laana katika familia yako ambapo mambo mengi yatavurugika kiuchumi na kijamii na hamtakuwa na furaha na mkeo kama zamani. Afya ya ndoa yako inazorota na watoto hawatakuwa na furaha kama inavyotakiwa kwani furaha ya watoto ni kuwaona wazazi wanaishi kwa amani na upendo.

Tuendelee kujifunza zaidi mambo haya katika sehemu zijazo; unaweza kusambaza somo hili ili wengine nao wajifunze zaidi. Ubarikiwe na Bwana.


No comments:

Post a Comment