Thursday, June 5, 2014

KASI YA KUZIMU KUWAMEZA WATU

OUR DAILY MANA



KASI YA KUZIMU KUWAMEZA WATU

Bwana wetu Yesu Kristo apewe sifa!

Karibu tena mpendwa katika Bwana katika safu hii ya kuyachunguza maandiko. Katika somo lililopita tuliangalia juu ya kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu na tukaona kuwa ni pale tu unapoamua kumweka Mungu mbele ndipo mambo yako yanapofanikiwa. Katika somo hili nataka tuangalie kitu kingine muhimu sana katika maisha yetu ya kiroho. Tunachojifunza leo ni juu ya kasi (speed) ambayo shetani anayo katika kuwavuta watu kuenda kuzimu.

Ni wazi utakubaliana nami kuwa kasi ya kuongeza maasi duniani hivi sasa ni kubwa kuliko miaka ya nyuma na cha ajabu ni kuwa kila siku zinaposogea ndivyo na maasi mengi yanavyogundulika na kuwavuta watu wengi. 1 Timotheo 4:1 inasema “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.” Mtume Paulo anazungumza na Timotheo kwamba siku za mwisho wengine watajitenga na imani; maana yake ni kuwa watu wengi wataacha kumfuata Mungu na kuamua kufuata tamaa za dunia na mambo ya mwili ambayo mengi yake ni mafundisho ya mashetani.

Leo hii ukiangalia na kuchunguza kwa makini utagundua kuwa asilimia kubwa ya watu kwenye kanisa wamerudi nyuma kiroho au hata wamepotea kabisa na kuamua kumwacha Mungu. Nimeshuhudia watu kadhaa ambao walikuwa vizuri sana kwa Mungu; walikuwa waombaji wazuri sana; walikuwa wahubiri wazuri sana; au hata walikuwa wakitumiwa na Mungu kwa ishara na miujiza mingi, lakini wameanguka katika dhambi hasa zinaa. Hii ikanifanya nianze kuchunguza ni nini kinaendelea kwenye ulimwengu wa roho.

Ufunuo 12:12 inasema hivi: “Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” Biblia inasema shetani alipofukuzwa mbinguni akashuka kwetu (duniani), akiwa na ghadhabu nyingi huku akijua kuwa ana muda mchache tu. Swali la kujiuliza ni kuwa shetani ana muda mchache wa kufanya kitu gani? Na ghadhabu yake ni juu ya kitu gani?

Kitabu cha Isaya 5:13-14 inasema: “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana. Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.”

Mungu anazungumza kwa uchungu akisema kuwa watu wangu wamechukuliwa mateka kwa kukosa maarifa na kwa sababu hiyo kuzimu kumeongeza tama yake, na kumefunua kinywa chake bila kiasi. Huu msitari umetafsiriwa hivi kwenye kiingereza:“therefore, sheol has enlarged itself, and opened its mouth beyond measure.” Hii unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili kwamba kuzimu imeongeza nafasi yake (au imejipanua), na imefungua kinywa chake kupita kiasi.

Hii ni ajabu sana, yaani shetani kwa kujua kuwa watu wa Mungu wamekosa maarifa ameamua kuongeza nafasi ya kuwapokea watu wanaoenda kuzimu na amefunua kinywa cha kuzimu kupita kiasi ili watu wote wasio na maarifa ya Mungu waingie humo. Hii ndiyo tunayojifunza kuwa ameshuka kwetu mwenye ghadhabu nyingi akijua kuwa ana muda mchache. Kasi ya shetani kuwavuta watu kwenye uovu ni kubwa kuliko kasi yetu tuliyonayo katika kumpinga. Yakobo 4: 7 inasema “mtiini Mungu, mpingeni shetani naye atawakimbia.” Hili neno mtiini kwenye kiingereza wametumia neno submit yourselves to God. Maana yake jikabidhi kwa Mungu kisha mpinge shetani naye atakukimbia.

Kanisa la leo linamezwa na kuzimu kwenye mambo mengi. Watu wameona wokovu kuwa ni mazoea. Wameona kuomba kuwa ni jambo la watu Fulani wanaoitwa eti wanamaombi. Watu maeomua kuutoa muda wao mwingi kufanya mambo ya dunia huku wakimsahau Mungu. Oooohh nakuambia ndugu hujajua kasi ya shetani kukushambulia ilivyo, maana laity ungalijua basi ungalikesha katika kumtafuta mungu. Jambo moja la ajabu ni kuwa “Mtu yeyote asiye mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo ni mateka wa nguvu za giza. Huo ndio ukweli na haijalishi awe anajijua au hajijui, awe anaamini au haamini ukweli ndio huo. Unaweza kuwa mateka wa nguvu za giza na shetani akawa anakutumia katika mipango yake bila wewe kugundua. Aliyesalama ni yule tu aliyemwaminifu kwa Bwana.”

Huduma za watu zimepotea, uzinzi umeongezeka katika kanisa, maasi yanazidi kuwa mengi lakini bado kanisa linaona ni jambo la kawaida tu. Watu wameona kuwa unaenda kwenye maombi kwa toba kila siku kuwa ni jambo la kawaida. Aisee Mungu atusaidie, maana shetani anafanya kazi akijua kuwa ana muda mchache lakini sisi tunampinga kwa uzembe tukufikiri kuwa tuna muda mwingi. Mitego ambayo shetani ameweka ili kuwaingiza watu kuzimu ni mingi mno lakini bado watu hawashituki. Kweli watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.

AMKA LEO JIFUNGE KIUME MAANA NI WAKATI WA HATARI
YESU PEKEE NI NGOME IMARA

1 comment: