Utangulizi
Tuliona
katika sehemu ya kwanza kuwa kuna umuhimu wa kufanya ziada; leo katika
kuendelea na somo letu, tutaangalia baadhi ya mambo ambayo tutafaidiwa sana
tukiyafanya kwa umuhimu na bidii kubwa. Vipo vitu katika maisha ni vya kuvipa
kipaumbele na kuvifanya kwa bidii, kwani matokeo yake huzidi kuwa bora
tunavyozidi kuvifanya kwa wingi. Kama hukusoma sehemu ya kwanza basi bonyeza
hapa ili upate mtiririko mzuri wa somo letu. Mungu akubariki unapoendelea
kujifunza nasi.
KUFANYA
ZIADA
Mambo
yafuatayo ni baadhi tu ya mambo ambayo unatakiwa kuyapa kipaumbele katika
kufanya ziada
-
Kuomba na kusoma neno la Mungu
Mambo
haya ukiyafanya zaidi ya mafarisayo na ukayafanya kwa kumaanisha; au
ukiyazidisha kuyafanya katika maisha yako, usiombe kwa unafiki, au ukazidisha
muda wa kuomba kwa kumaanisha, basi wewe unaurithi ufalme wa Mungu lakini pia
utaweza kuepuka mitego iliyowanasa mafarisayo. Pia katika kusoma neno la Mungu,
watakiwa kufanya ziada, yaani ‘zaidi ya kawaida’, au basi ukiweza, zaidi ya
wengine wote. Ndipo uwepo wa Mungu utakapojaa ndani yako na hutafukuzana na
dhambi bali dhambi itakukimbia.
-
Kutenda mema
Hapa
tena ndipo Yesu amesisitiza sana. Yaani kwamba utende mema zaidi ya wamataifa
watendavyo. Kuwapenda adui na kutokuwachukia watu kama tulivyoona. Lakini hapa
ikumbukwe kuwa huwezi kuyakamilisha haya kwa ukamilifu kama hautakuwa na ziada
katika kuomba, kufunga na kusoma neno la Mungu. Mambo haya yanategemeana. Kama
unataka kuwazidi mataifa katika jambo lolote lazima kwanza uanze kuwazidi
katika kuomba, kufunga, na kusoma neno la Mungu.
-
Kumtumikia Mungu
Unapomtumikia
Mungu usimtumikie kama mafarisayo, usitafute kujifaidisha wewe mwenyewe bali
utafute kuueneza ufalme wa Mungu pasipo na hila moyoni mwako. Angalia utumishi
wa mafarisayo anaouongelea Yesu;
Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha
mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa
kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.
Viongozi vipofu, wenye kuchuja
mbu na kumeza ngamia.
Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa
unyang'anyi na kutokuwa na kiasi.
Ewe Farisayo kipofu, safisha
kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.
Ole wenu, waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo
kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu
wote.
Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje
mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.
(Mathayo 23:23-28)
Hapo
tunajifunza kuwa mafarisayo wanafuata sheria sawasawa katika utumishi wao, na
dalili za nje za kuonekana; lakini wameachana na utakatifu. Yesu anawatajia
mafarisayo vitu muhimu vya kuwa navyo ambavyo hata wewe mtumishi wa Mungu
unatakiwa kuwa navyo ili kuifanya haki yako izidi kuwa zaidi ya ile ya
mafarisayo: adili, rehema na imani.
Mafarisayo
wanaonekana kwamba hawakuwa na utu wema wa ndani, hawakuwa na maadili wala
hawakuutafuta utakatifu. Ndicho ambacho Yesu anatamani sisi wanafunzi wake tuwe
nacho.
Yale mengine msiyaache
Licha
ya kuwa Yesu anawahimiza mafarisayo kuzingatia adili, rehema na imani;
anawasisitiza kuwa yale mengine wasiyaache. Hii ina maana kuwa vitu vyote vina
umuhimu wa kipekee katika kumtumikia Mungu. Mengine anayoyazungumzia Yesu ni
pamoja na zaka na kanuni zingine za imani kwa mujibu wa kanisa. Kwa sasa
watumishi wa Mungu wengi wanakutana na changamoto nyingi za kimaisha hadi
wanakuwa wanashindwa kuwa waaminifu kwenye suala la matoleo.
Hilo siyo jambo
jema na kamwe Mungu hafurahishwi nalo, Mungu anataka uwe msafi moyoni lakini
kanisani pia umtolee. Wengine wanakuwa wanafanya yote hayo lakini hawataki
kuwashuhudia wengine kwa habari ya Kristo wala hawataki wengine wajue kuhusu
imani yao, ni sharti la Ukristo kuungama mbele ya mashahidi wengi na kumtangaza
Kristo katika semina na uinjilishaji. Kwa hiyo wewe usiishie tu kuwa mkristo wa
kuokoka kwa siri, kama ambavyo wengi wanasema ‘wewe ukiokoka unajua wewe na
moyo wako usimwambie mwingine,’ hapana, usiwashe taa ukaiweka chini ya uvungu;
inuka uangaze…
Luka
8:16
Hakuna mtu ambaye akiisha washa
taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili
waingiao wapate kuona nuru yake.
Isaya
60:1
Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru
yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia.
ZIADA
HUKUPA UWEZO ZAIDI YA WENZIO
Waebrania
1:9 Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako,
amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.
Mungu anakuahidi furaha na shangwe kupita wenzio kama utachukia
maasi na kupenda haki. Hapa inatuonesha kuwa hao wenzio siyo lazima wawe
wapagani, ila inawezekana nao pia wanapenda haki, ila ukiwazidi katika kupenda
haki, na furaha yako itakuwa kubwa zaidi yao.
Unaweza kuzidi katika mambo kadha wa kadha, na katika kila jambo,
ukizidi, na furaha yako au matokeo yako yatawazidi wengine. Ni kama darasani,
kama utakuwa makini zaidi darasani na kufanya bidii zaidi ya wenzako na kuelewa
zaidi yao, matokeo yako yatakuwa bora zaidi. Na pia katika Mungu kama wewe
utakuwa mwombaji zaidi na mfungaji zaidi na mwenye kusaidia watu zaidi, baraka
zako zitawazidi wote unaowazidi kuomba na kufunga.
Fanya ziada ya kazi upate ziada ya matokeo; Mungu yupo na wewe
kukuzidishia wewe uliyezidi katika kumtafuta; Mungu yupo kukuzidishia nguvu
zake wewe uliyezidi katika kuomba na kufunga, Mungu yupo kukuzidishia uwepo
wake wewe unayemtafuta usiku na mchana. Mungu yupo kukupa hitaji lako wewe
uliyezidi katika kumtegemea na kumuamini yeye. Mungu yupo katika kukuokoa na
kukulinda wewe uliyezidi katika kuwasaidia wengine. Mungu yupo katika
kukubariki wewe uliyezidi katika kumtolea yeye na atahakikisha unazidi katika
kipato hadi watu washangae; fanya ziada ili upate ziada, apandaye haba atavuna
haba. Unafanya ziada gani?
Usikose sehemu
inayofuata ya somo hili, unaweza kulisambaza pia ili wengine nao wazidi
kubarikiwa na ujumbe huu. Ubarikiwe sana.
No comments:
Post a Comment