Mwandishi: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Mafundisho
ya Bwana Yesu ni ya ajabu sana, nayo yanaleta raha sana na kutufariji mara
tuyasomapo. Kila nisomapo mafundisho ya Bwana Yesu huwa ninajazwa nguvu mpya na
kuiona upya ile faida na furaha ya wokovu ulio ndani yangu. Yesu anatufundisha
mambo mengi sana ya msingi na sisi watu wake tunatakiwa kuyajali mafundisho
yake na kuweza kuyatumia kurutubisha roho zetu. Mafundisho ya Yesu yanatufaa
kama ambavyo chakula kifaavyo kwa mwanadamu; kama ambavyo maji yafaavyo kwa
wenye kiu na kama ambavyo pumzi ni muhimu kwa kiumbe hai.
TULIANGALIE
SOMO HILI
Katika
somo hili tumepewa kichwa cha habari kisemacho “Unafanya Ziada Gani?” maneno
haya yametolewa katika moja ya mafundisho aliyoyatoa Yesu kwa watu waliokuwa
wanamsikiliza kama ilivyokuwa kawaida yake; hebu tuiangalie mistari hiyo ili
tuone Yesu anafundisha kitu gani-
Mathayo
5:38-48
Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho
kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu;
lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye
kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu
atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.
Akuombaye, mpe; naye atakaye
kukopa kwako, usimpe kisogo. Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na,
Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye
huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
Maana mkiwapenda wanaowapenda
ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo
hayo?Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda
tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?
Basi ninyi mtakuwa wakamilifu,
kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
Yesu
alikuwa anawafundisha wanafunzi wake namna ya kuishi na watu na njia mpya ya
utakatifu. Nasema hii ilikuwa ni njia mpya kwa sababu wale watu kabla ya hapo
walikuwa wanaishi kwa kanuni ya jino kwa jino.
Kuna jambo la kupatikana na ziada
Katika
mistari hiyo hapo juu Mungu anahimiza sana ziada. Anasema lazima matendo yetu
kama Wakristo tuyafanye kwa uzuri uliozidi yale ya wa mataifa. Watu wengi
wamejaribu kuyafumbia macho mafundisho haya. Lakini ni kweli kuwa mafundisho
haya hayaepukiki.
Lakini
nadhani kama kanisa lingeyaishi mafundisho haya, ugomvi mwingi sana ungekuwa
unakwisha bila kuhusisha waamuzi. Yaani kama kila mtu angekuwa wa kwanza
kumsalimia na kumsaidia adui yake kama maneno yanavyosema hapo juu, basi
mapatano yangeenea kila mahali.
Ndicho
ambacho Yesu alileta duniani; Yesu alileta amani na ndiyo maana anaitwa Mfalme
wa Amani.
Yesu
anatamani kwamba kama kuna mambo ya kufanya yenye wema; Wakristo ndio watu
ambao wanatakiwa kuwa wamewazidi wanadamu wote kwa sababu wao wanafanya na
ziada. Kama ni wema; wakristo wanatakiwa kuwa wanawazidi wote wanaofikiri kuwa
wanafanya wema; kama ni huruma na upendo vilevile.
Wakristo
katika kusamehe pia wanatakiwa kuwa wamezidi; na hapa Yesu anatoa mfano wa
Mungu anapowaangazia jua wabaya na wema. Ni jambo la muhimu sana kujifunza kwa
maana kwamba Mungu kama mjenzi na anayeitunza dunia asingependa watu
wanaomchukia waendelee kuitumia dunia yake; lakini hajafanya hivyo; bali
ameendelea kuwaangazia jua wote wakorofi na wema; na zaidi ya hayo anawanyeshea
mvua wote bila kujali kuwa huyu ni mwema au ni mbaya.
Yesu
ameyarudiarudia sana hayo mafundisho yake katika kusisitiza hoja yake. Watu ambao
wanaweza kudhani kuwa Yesu alikuwa na maana nyingine katika mafundisho hayo
wanahitaji pia kusoma mistari ya ziada ili waweze kujiridhisha kwamba Yesu
alikuwa ana maana hiyo hiyo ya kufanya ziada. Yesu
alitaka wakristo wawe ni watu waliozidi katika wema na wasiojihusisha kabisa
katika ubaya.
Uitapo
watu karamuni
Luka
14:12-14
Akamwambia na yule aliyemwalika,
Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu
zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe
ukapata malipo.
Bali ufanyapo karamu waite
maskini, vilema, viwete, vipofu,nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha
kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.
Yesu
anaendelea kusisitiza utofauti na uziada katika matendo yetu sisi wateule wake.
Hapa anatuamuru tufanye ziada katika kuandaa karamu na kuwaalika watu. Anataka
tuwe na mtazamo tofauti katika lengo la kuandaa karamu. Hii ni ziada ya wema
anayotaka tuifanye; ya kuwaalika masikini, vilema na vipofu.
Ni
ziada kwa misingi kwamba; Yesu anajua kwamba watu hualikana kwenye karamu kwa
misingi ya kuweka akiba ili nao siku moja wafanyiwe hivyo; au huandaa karamu na
kuwaalika rafiki zao ili kuwalipa mema ambayo walishawahi kufanyiwa hapo kabla,
lakini Yesu anatufundisha kuwa licha ya kuwa kuwaalika rafiki zako karamuni au
kuwaandalia karamu ni jambo jema; lakini la kuwasaidia na kuwaita wale ambao
hawawezi kukusaidia ni vyema zaidi kwani wao hawawezi kukulipa. Kwa hiyo
tukifanya hivyo; yaani kuwaalika masikini karamuni, tutakuwa tumetenda ziada,
tukiwazidi watu wa kawaida ambao wao hualika rafiki zao tu karamuni.
Haki
yenu isipozidi ya mafarisayo
Hili ni
jambo jingine lililoonesha katika biblia kwamba Yesu anatafuta ziada ndani ya
wateule wake…Angalia hapa anasisitiza hadi anaonekana kuwa radhi kuwakosesha
wateule wake uzima wa milele kwa sababu tu ya kutokuwa na ziada katika wema na
matendo matakatifu. Sikiliza, ni kweli kwamba hatuwezi kujitengenezea haki kwa
matendo yetu lakini tunatakiwa kujivika utakatifu na kuwa matajiri katika
kutenda mema. Hebu tuiangalie hii habari ya kuwazidi mafarisayo…
Mathayo
5:20 Maana
nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo,
hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Lakini
hapa tunaweza kujiuliza neno moja, kwani mafarisayo walikuwaje?
Mathayo
23:2-33
Waandishi na Mafarisayo wameketi
katika kiti cha Musa;basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda;
lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.
Wao hufunga mizigo mizito na
kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.Tena
matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao,
huongeza matamvua yao;hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele
katika masinagogi,na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
Bali ninyi msiitwe Rabi, maana
mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.Wala msimwite mtu baba duniani;
maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.Wala msiitwe viongozi; maana
kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.Naye aliye mkubwa wenu atakuwa
mtumishi wenu.
Na ye yote atakayejikweza,
atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.Ole wenu waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi
wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.
Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa
mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata
hukumu iliyo kubwa zaidi. Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja
kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili
zaidi kuliko ninyi wenyewe.
Ole wenu viongozi vipofu, ninyi
msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya
hekalu, amejifunga. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana
ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa
madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo
kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka?
Basi yeye aapaye kwa madhabahu,
huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake.
Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa
hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa
kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake. Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha
mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa
kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.
Viongozi vipofu, wenye kuchuja
mbu na kumeza ngamia.Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa
mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na
kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha
kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.
Ole wenu, waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo
kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu
wote.
Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje
mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.
Ole wenu, waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba
maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi
tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya
manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya
kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba
zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka,
mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?
Tunaweza kuorodhesha sifa chache za mafarisayo
-
Walikuwa hawatendi wanachokihubiri
-
Walikuwa wanafiki
-
Walikuwa watu wa kujionesha kuwa wamekubalika
-
Walikuwa wanawazuilia wengine kumjua Mungu
-
Walikuwa hawamuogopi Mungu ndani ya mioyo yao
-
Walikuwa hawana mahusiano binafsi na Mungu
-
Walikuwa hawana mahusiano mazuri na waumini wao.
-
Walikuwa siyo watu wa kutenda haki
-
Walikuwa watu wa kupindisha mafundisho ili kujitengenezea
faida binafsi.
Kwa
hiyo Yesu alitamani wanafunzi wake na kila aliyetamani kuurithi uzima wa milele
kutenda zaidi ya mafarisayo ili astahili kuurithi uzima wa milele. Hii
inaonesha kuwa mafarisayo walikuwa hawawezi kuurithi uzima wa milele.
Mafarisayo walishika sheria zote za mafundisho ya kidini lakini walisahau
kuutafuta utakatifu na kuyaishi yale waliyokuwa wakiyafundisha.
Hili
jukumu la kufanya zaidi ya mafarisayo halikuishia tu kwa wanafunzi wa Yesu, bali
linaendelea hadi leo; naomba hapa usiniulize kama mafarisayo bado tunao,
maadamu tumeshaona hapo juu mapungufu yao basi ni kazi yako kuamua kama tunao
au la; ila kama usipowaona basi wewe tafuta kufanya zaidi ya mafarisayo
waliokuwa wakiishi wakati wa Yesu.
Niunge kwa group la wasap
ReplyDelete