Thursday, June 1, 2017

NI KWELI… LAKINI…


Mwandishi: Anderson Leng'oko

Utangulizi
Katika maisha ya kila siku huwa kuna vitu viwili, mazingira halisi na mambo yanayowezekana kufanywa kulingana na mazingira hayo. Watu huwa wanatumia mazingira halisi kutabiri na kufahamu mustakabali wao. Kama kwa mfano mtu amefeli mitihani yake ya kidato cha nne, hawezi kuendelea na kidato cha tano. Ukweli humfanya mtu afanye uamuzi ambao unaendana na ukweli huo. Hata hivyo, yapo mambo ambayo hutokea licha ya mazingira kuwa yamelazimisha vingine. Kuna uwezekano mkubwa sana katika maisha wa mambo kutokea kinyume na wengi walivyotarajia. Kwa mazingira kama hayo, watu wanashauriwa katika somo hili kutokukatishwa tamaa na mazingira au hali halisi katika maisha yao bali wamgeukie Mungu ambaye ndiye msemaji wa mwisho asiyeathiriwa na uhalisia wala mazingira.
Karibu tujifunze pamoja katika somo hili, “Ni kweli… Lakini…”

2 Wafalme 19:17-19
Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao,
na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu.
Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako.


Mistari hiyo hapo juu inahusu habari za mfalme mmoja wa Yuda aliyejulikana kwa jina la Hezekia. Mfalme huyu alitawala Yuda katika nyakati ambazo mataifa yalikuwa yana chuki na uhasama ambapo kila taifa lilitakiwa kuwa na nguvu fulani ya kuliwezesha kupigana na kulishinda taifa lingine na kulifanya lile taifa lililoshindwa liishi kwa kulipa kodi kwa taifa lililoshinda. Ni kama katika historia ya nchi yetu au bara letu la Afrika ambapo watu zamani walikuwa wanaishi kwa kupigana na kunyang’anyana mali ambapo wenye nguvu walikuwa wanawavamia wadhaifu na kuwatawala.

Sasa hapa kuna wafalme wanatajwa katika mistari tuliyoisoma, wanaitwa wafalme wa Ashuru. Hawa walikuwa wababe, wababe sana; biblia inatuambia kuwa waliwaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni.

Huo ulikuwa ni ukweli ambao haupingiki, na ndiyo maana huyu Mfalme Hezekia anaanza na neno ‘Ni kweli’.

Hata hivyo haikuwa inamaanisha kuwa mfalme wa Ashuru angeweza kuwapiga Yuda kisa tu amewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni. Hezekia alijua kuwa Yuda ilikuwa ni habari nyingine! Mungu wa Yuda alikuwa ni habari nyingine na wala isingewezekana kumfananisha Mungu wa Yuda na ile miungu iliyotupwa motoni.

Mungu ni Mungu mwenye wivu
Hapa Mungu alijua kabisa kwamba jina lake lilikuwa liko hatarini. Ukitaka kumuamsha Mungu kutoka huko aliko basi wewe ongelea uwezo wake juu ya miungu mingine. Uwezo wa Mungu juu ya miungu mingine ukihojiwa, hapo lazima Mungu aamke na kutenda.

Kama tulivyoona hapo juu, Mungu huamka na kutenda yanapotokea mashindano ya miungu. Mfalme wa Ashuru alikuwa amemkosea sana adabu Mungu wa Yuda na Israeli kiasi cha kumfananisha na Miungu mingine ambayo baba zake wafalme waliotangulia wa Ashuru walikuwa ameitupa motoni; eti:
Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe?
Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari?
Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, na wa Hena, na wa Iva?
Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana.
(2 Wafalme 19:10-14)

Hapo ndipo mfalme wa Ashuru alikosea sana, kumfananisha Mungu wa Hezekia na Miungu ya watu wengine aliokuwa amewapiga kabla. Sasa somo letu lina kichwa cha habari kisemacho Ni kweli … lakini…

Kwa maana kuwa hapo ilikuwa ni kweli kuwa wafalme wa Ashuru walikuwa wameiangusha miungu mingi, lakini unapoongelea habari ya Mungu Jehova, aisee! Usijaribu kuchezea huo moto! Hebu tuangalie yaliyowapata hawa jamaa wa Ashuru baada ya kuleta kiherehere chao cha kuifananisha miungu mingine mibovubovu na Mungu Jehova:
2 Wafalme 19:32-37
Basi Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake.
Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema Bwana.
Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.
Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia.
Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi.
Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.

Hiyo ndiyo habari ya watu wote washindanao na Mungu wa kweli na kumfananisha na miungu mingine mibovumibovu.

Hapo tunaona kuwa;
Ni kweli mfalme wa Ashuru alikuwa na wanajeshi wengi kuliko Yuda lakini cha ajabu hata wanajeshi wa Yuda hawakusumbuka kupigana naye.
Ni kweli mfalme wa Ashuru alikuwa ameiangusha miungu mingine yote ya wafalme wengine lakini Mungu wa Yuda alikuwa ni Mungu wa kweli, ambaye alikuwa hawezi kufananishwa na miungu mingine ya uongo.

Sasa mfalme wa Ashuru hakujua kuwa alikuwa hapigani na Yuda, bali alikuwa anapigana na Mungu wa Yuda ambaye ni Jehova.

Rudi kwenye maisha yetu ya kila siku; yapo mambo mengi sana ambayo kiuhalisia yanatutishia.

Ni kweli kwamba masomo yamekuwa magumu na wengi sana wanafeli, lakini hiyo haina maana kuwa na wewe lazima ufeli.

Ni kweli wasichana wanapata mimba na safari yao kitaaluma na kiajira inakuwa ngumu sana kwa sababu ya wingi wa vishawishi, lakini hiyo haina maana kuwa na wewe utashindwa kufanikiwa.

Ni kweli kuwa maisha ni magumu sana na siku hizi hela haipatikani, lakini hiyo haimaanishi kuwa wewe utabaki kuwa masikini.

Ni kweli mchumba amekuacha na umekosa amani na matumaini, lakini hiyo haimaanishi kwamba hautapata mwingine umpendaye na kuendelea na maisha.

Ni kweli kuwa una huzuni nyingi sana kwa sasa kiasi kwamba unapoteza matumaini ya kufarijika tena, lakini hiyo haimaanishi kuwa hutafurahi tena.

Yupo wa kukufurahisha wewe uliyeandamwa na huzuni ya muda mrefu
Yupo wa kukufariji wewe uliyeandamwa na misiba ya muda mrefu
Yupo wa kukutajirisha wewe uliyedhulumiwa mali na kufilisiwa
Yupo wa kukuajiri wewe uliyefukuzwa kazi
Yupo wa kukupa mume wewe uliyeachwa na mumeo
Yupo wa kukupenda wewe uliyechukiwa
Yupo wa kukukumbatia wewe uliyekataliwa

Usijiumize kana kwamba umejileta mwenyewe duniani, yeye aliyekuleta anajua sababu ya kukuleta, Mgeukie yeye kama Mfalme Hezekia alivyomgeukia.
Ni nyaraka ngapi umeandikiwa kuhusu maisha yako?
Je umekuwa ukizipeleka mbele za Bwana kama Hezekia alivyofanya?

Kama umefeli sana mtihani na kupata 1/10, nenda na hilo karatasi mbele za Bwana ukamuoneshe! Anajua kusoma, kampe alione halafu uone kama tena utarudia kupata hiyo alama, Haleluya!

Kama umepewa majibu ya Afya yako na ukaambiwa uko HIV positive mpelekee Bwana hayo majibu ukayakunjue mbele yake; yeye ni mponyaji, waombaji wote wanaoponya watu wanatoa nguvu kwake, ukienda moja kwa moja kwake utapata majibu haraka kuliko kupitia kwa mtu; nenda ukamweleze kuwa unasikia anaponya kila gonjwa na wewe unataka kumuona akikuponya Ukimwi!
Ni kweli Ukimwi hauna dawa, ni kweli watu wengi hata Wakristo wenyewe hawaamini kuwa Mungu anaponya Ukimwi, lakini yeye ni mtenda miujiza, na hilo la kuponywa ukimwi nalo ni muujiza, nenda kaulilie; ni nani ajuaye kuwa hutaponywa?

Kama aliweza kugawanya bahari ya Shamu, hilo ni lipi asiloliweza? Kama aliweza kumfufua mtu aliyeoza (Lazaro) kwanini ashindwe kukuponya wewe ambaye hata kufa bado hujafa???
Kwani jambo rahisi kuamini ni lipi? Kwamba Mungu anaponya Ukimwi au kwamba Mungu anafufua wafu? Bila shaka lile la kwanza ni rahisi zaidi, sasa huyu Mungu tunayemtafuta na tunayemtumikia, anafufua wafu, hawezi kushindwa kukuponya gonjwa lolote, nasema tena gonjwa lolote.

Usisikilize watu, ni kweli kuna watu walikuwa na imani nzuri kuliko wewe lakini walishindwa kupita hapo, hiyo wewe isikukatishe tamaa kwani wakati wanaandikiana mikataba yao na Mungu wao kwenye chumba cha ndani wewe hukuwepo; ukweli kwamba Musa alikuwa na nguvu ya Mungu na kibali kikubwa zaidi kuliko Joshua haikumfanya Joshua adhani kuwa hawezi kuwafikisha Israeli Kaanani; yumkini angewaza kama wewe angeweza kuogopa, kuwa hawa watu wana mioyo migumu sana, kama Musa anayeongea ana kwa ana na Mungu amewashindwa mimi nitawaweza wapi, lakini hilo halikumsumbua Yoshua, alijua Musa ni mwanadamu kama yeye hakujisumbua kuangalia historia ya Musa, yeye alimuangalia Mungu, akamsikiliza Mungu na akafanya ya Mungu, haleluya!


Sikiliza, hatuambiwi kuwa Joshua na Kalebu ndiyo walikuwa karibu sana na Mungu kuliko wapelelezi wote walioenda Kaanani, ila tunaambiwa tu kuwa wapelelezi wengine wote waliwatisha watu wakawaogopesha hadi watu wakaamua kurudi Misri, lakini Kalebu na Joshua hawakuangalia CV za wale waliowaogopesha watu, walimuangalia Mungu, Jehova wakauona uwezo wake, kwamba hauishii kwenye fahamu za binadamu, yeye anatenda siyo kama aliyowahi kutenda zamani, anao uwezo hata wa kutenda yale ambayo sikio halijawahi kusikia wala akili haijawahi kuwaza!

1 comment:

  1. Pokies Casino Bonus Codes 2021
    Pokies Casino Bonus Codes 암호화폐란 2021 - 저녁밥 추천 Get Up to €/$1000 포커 용어 Welcome Bonus at the best casino 유니 벳 online! Sign up, deposit €/£20 and receive 바카라 검증 20 free spins upon registration.

    ReplyDelete