"UMUHIMU WA MAOMBI YA MUDA MREFU"
Neno la somo Efe 3:20 & Yak 5:16b
Kuna
idadi kubwa ya wakristo ambao wanaona kuwa maombi ya mtu hayawezi
kuchukua muda wa zaidi ya saa moja,na watu wa aina hii wengi wao maombi
yao huwa hayazidi muda wa dakika 30 au dakika 45. Watu wenye mawazo kama
haya wanaweza kuwa ni wale ambao ni wavivu kuomba au hawajaisoma vizuri
BIBLIA na hawajui biblia inasemaje kuhusu muda wa kutumia katika
maombi.
YESU KRISTO alipokua Gethsemane aliwasihi wanafunzi wake wakeshe pamoja naye katika maombi Math 26:37-38. Alipotoka kuomba akawakuta wamelala aliwauliza "... je, hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?" Math 26:40.
Swali hili halimaanishi kuwa wanafunzi hawakuomba hata
kidogo,inawezekana kabisa kuwa waliomba ila ambacho YESU anatuambia ni
kwamba maombi yao yalikua chini ya muda wa saa moja.
Sasa kama waliomba, kulikuwa na umuhimu gani YESU awaambie waombe
"hata" kwa saa moja?. suala lililopo ni kwamba YESU aliipima nguvu ya
rohoni iliyotokana na maombi yao na kuona kuwa isingetosha kuwawezesha
kumshinda adui. Ndio maana akawaambia "... kesheni, mwombe, msije
mkaingia majaribuni." Math 26:41.
Maana yake ni kwamba jaribu lililokuwa mbele yao wasingeweza kulishinda
pasipo maombi ya muda mrefu ambayo yangewapa nguvu kamili ya kushinda.
Na kwa sababu hawakuomba ndio maana jaribu lilipofika yaani wakati wa
kukamatwa YESU ulipofika, wanafunzi wote walimkimbia na hata Petro
ambaye alijitahidi kumfuatilia naye wakati ulifika ambapo alimkana YESU.
Wanafunzi wa YESU walimkimbia si kwa sababu walikuwa waoga bali ni kwa
sababu suala la kumkiri YESU na kumtetea mbele za watu ni jambo
linalohitaji ujasiri wa rohoni. Ujasiri huu hutokana na nguvu za rohoni
ambazo mtu huzipata kutokana na maombi anayofanya.Kwa hiyo kadri mtu
anavyotumia muda mwingi katika maombi ndivyo anavyopata nguvu zaidi.
Kukosekana kwa nguvu hii katika watu wengi kumepelekea watu
kushindwa kujitangaza kuwa wameokoka na wengine hata kuanguka kabisa na
kuacha wokovu. Kitu cha namna hii ndicho kiliwafanya mitume waombe MUNGU
awape ujasiri pale walipotaka kuanza rasmi utume. Matendo 4:29-31.
Kwa sababu ya mambo hayo na mengine kama hayo ndio maana ipo haja
tujifunze umuhimu wa kuwepo maombi ya muda mrefu kwa mkristo.
Katika kitabu cha waefeso 3:20 imeandikwa "basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa "kadri" ya nguvu itendayo kazi ndani yetu."
Biblia ya kiingereza imeandika Now to him who by the power at work within us is able to do far more abudantly than all that we ask or think {ephesians 3:20 RSV}
Maneno haya ya mtume Paulo yanatudhihirishia kuwa kuna kitu kiitwacho nguvu itendayo kazi yaani power at work. Nguvu
hii maana yake ni mamlaka na uwezo wa kiroho ambao mtu anakuwa nao
katika kumwezesha kufanya vitu vya kiroho. Kwa hiyo unapoona mtu
anakemea pepo na anatii ujue kuwa mtu huyo anakitu cha ziada kinachoitwa
nguvu ya rohoni, ambacho ndicho MUNGU anakitumia katika kufanya vitu
vya rohoni.
Kwa kuwa nguvu hii ni jambo la rohoni basi ni wazi kabisa kuwa hata kuipata ni lazima itoke katika ulimwengu wa roho.
katika Yakobo 5:16b "...kuomba
kwake mwenye haki kwa faa sana akiomba kwa bidii." Hapa biblia
inazungumzia bidii katika kuomba, jambo hili tunaweza kulifananisha na
pale YESU alipokuwa akiwaambia wanafunzi wake waombe angalau kwa saa
moja.Maana yake alikuwa anawasisitiza waombe kwa bidii. Mathayo 26:40
Bidii hii alianza kuionesha YESU pale alipofunga na kuomba kwa muda wa siku 40. Math 4:1-2,
tunaona YESU mwenyewe pamoja na kuwa Mungu lakini alianza kwa maombi ya
muda mrefu. Maana yake ni kuwa YESU alijua wazi kabisa kwamba kazi
iliyokuwa mbele yake asingeishinda bila kuwa na nguvu ya kutosha ndani
yake. Lakini pia biblia inatuonesha mara kwa mara YESU akienda kusali.Luka 9:28, Luka 6:12
Luka 22:44
Bidii hii tunaiona pia pale kanisa lilipomwomba mungu kwa ajili ya Petro alipokuwa gerezani Matendo 12:5 inasema " Basi Petro akalindwa gerezani nalo kanisa likamwomba mungu kwa juhudi kwa ajili yake".
Sasa tujiulize swali kwa nini biblia inatueleza kuhusu kuomba kwa
bidii, kuomba kwa juhudi na mahali pengine inasema ombeni bila kukoma?.
Jambo tunalotakiwa kujua ni kwamba utendaji kazi wa MUNGU juu ya haja
yako au juu ya huduma fulani unayoifanya hutegemea sana nguvu ambayo
wewe unaiachilia. Ephesians 3:20
"... by the power at work within us is able..." maneno haya yanaonesha
kuwa nguvu itendyo kazi ndani yetu ndio inayomwezesha MUNGU kufanya
unalolitaka.
Sasa biblia ya kiswahili inasema kwa kadri, maana
yake ni kuwa kwa kiwango au kiasi. Kwa hiyo kwa kiasi cha nguvu iliyomo
ndani ya mtu ndivyo kwa kiwango hicho hicho MUNGU atatenda miujiza
kupitia mtu huyo. kwa maana hiyo kama nguvu ya mtu ni ndogo basi MUNGU
atashindwa kufanya kazi au MUNGU atajibu lakini majibu hayo hayataleta
ushindi kamili juu ya jambo hilo.Na ndio maana unaweza kukuta mtu mmoja
amemwombea mgonjwa hakupona lakini akaja mwingine akamwombea mgonjwa
huyo akapona.
Kwa hiyo unapoomba kwa bidii au kwa juhudi maana yake ni lazima
utatumia muda mrefu, au unapoomba bila kukoma maana yake utaomba mara
kwa mara ambapo tayari utakuwa umetumia muda mrefu.
Haya yote kazi yake ni kuhakikisha kuwa inapatikana nguvu ya kutosha ili kumfanya Mungu AIINGIE KAZINI kwa ajili yako.
Jiulize ni kwa nini Mungu hakumtoa Petro gerezani mpaka pale kanisa
lililpoomba, na kwa nini MUNGU alimwacha Yohane mbatizaji gerezani mpaka
akakatwa kichwa? Sababu ni kuwa ili MUNGU atende jambo duniani
anategemea nguvu za kiroho za watu walioko duniani ndizo zimruhusu
kufanya kazi efe 3:20.kwa hiyo
Petro alitoka gerezani kwa kuwa walipatikana watu walioachilia nguvu
iliyomwezesha MUNGU kutenda kazi lakini Yohane hakuapata watu wa
kumsaidia katika hili.
Wakati biblia ya kisw ahili inasema kuomba kwa juhudi au kwa bidii,
ile ya kiingereza inasema kuwa maombi haya huwa na nguvu kubwa katika
matokeo yake James 5:16b "the prayer of a rightious man has great power in its effects"
Hapa
maana yake ni kwamba unapoomba kwa bidii yaani kwa muda mrefu unakuwa
unaachilia kitu ambacho hutoa nguvu kubwa katika matokeo yake. Kwa hiyo
unapoomba kidogo ndivyo na nguvu ya matokeo itavokua kidogo.
Watu wengi sana wamekua wakilalamika kuwa maombi yao hayajibiwi na
wengine kufikia hatua ya kusema kuwa MUNGU anaupendeleo. Lakini
nikwambie jambo, Mungu hana upendeleo; Matendo 10:34-35
Tatizo
liko kwa waombaji wenyewe ambao wengi wao hudhani kuwa suala la MUNGU
kujibu maombi ni kitu rahisi tu. Lakini nakwambia pima jambo
unaloliombea na muda wako katika kuliombea kisha angalia kama kweli muda
huo unatosha kuachilia nguvu ya kumfanya MUNGU alete ushindi kamili.
MUNGU huwa anapima tatizo au jambo unaloliomba na nguvu unayoachilia
kwenye maombi yako, kama akiona bado nguvu haitoshi ili kuleta ushindi
kamili basi huikusanya nguvu yako siku kwa siku hadi pale itapotosha
ndipo aitumie.
Hiki ndicho kilimpata Danieli, Dan 10:1-4,11-13.
Katika msitari wa 12 inaoneshwa kuwa maombi ya Danieli yalisikiwa tangu
siku ya kwanza ya kuomba kwake na malaika akatumwa. Msitari wa 13
inaonesha kuwa malaika alizuiliwa na roho ya mkuu wa uajemi kwa siku 21.
msitari wa 2 inaoneshwa kuwa Danieli aliomba majuma matatu kamili {siku
21}.
Tunachoweza kugundua ni kuwa kwa muda wote ambao malaika alikuwa
amezuiliwa, Danieli aliendelea kuomba mpaka pale malaika alipoachiwa.
Sasa tujiulize maswali yafuatayo:
=>je, inamaana kuwa mkuu wa uajemi alikuwa na nguvu kuliko malaika?
=>je, MUNGU hakuona kuwa malaika wake amezuiliwa? na kama alijua ni kwanini hakumtuma Mikaeli mpaka siku zote hizo?
=>ni kwa nini Danieli aliendelea kuomba kwa muda wote huo?
Majibu yake ni kwamba, mkuu wa uajemi hakuwa na nguvu kuliko malaika,
ila ni kwamba roho ya uajemi ndio iliyokuwa ikitawala anga lile na
hivyo kupita kwa malaika katika eneo lile kulitegemea kuwepo kwa nguvu
ndani ya Danieli ambayo MUNGU angeitumia katika kuuangusha utawala wa
mkuu wa uajemi na kusimamisha kusudi la Mungu. Hapa tunajifunza kuwa
kuna wakati mwingine huwa tunalalamika kuwa MUNGU hajajibu kumbe majibu
yetu yanakuwa yamezuiliwa na nguvu za ibilisi na yanahitaji maombi zaidi
ili kuyakomboa.
Pili ni kwamba MUNGU alijua kabisa kuwa malaika wake amezuiliwa lakini
suala ni kwamba jukumu la kuachilia nguvu ya kumsaidia malaika ili atoke
hapo halikuwa la MUNGU bali ilimpasa Danieli aombe kwa muda mrefu ili
kuachilia nguvu ambayo MUNGU angeitumia kumtoa malaika pale kizuizini.
tunachojifunza hapa ni kwamba ni jukumu la muombaji kuhakikisha kuwa anaomba mpaka pale anapoona ushindi.
Tatu ni kwamba Danieli aliendelea kuomba maana bado alikuwa hajaona
ushindi katika hitaji lake.Tunachojifunza hapa ni kwamba usiache kuomba
mpaka umeona Bwana amefungua njia kwenye haja yako. Isaya 62:6-7.
kwani kama Danieli angekua ni mvivu wa kuomba basi ni dhahiri kuwa majibu ya maombi yake yasingemfikia.
Sasa tujiulize tena ni kwa nini ilimbidi Danieli aombe kwa muda mwingi kiasi hicho?
Jibu ni kwamba MUNGU alikuwa akitumia nguvu aliyokuwa akiachilia
Danieli katika kumshinda mkuu wa uajemi,kwa hiyo kiasi cha nguvu ambayo
ingetosha kilikuwa kinapimwa siku hadi na ilipofika siku ya 21 nguvu ya
kuleta ushindi kamili ndipo ilipopatikana. hii ina maana kuwa kama nguvu
ingetosha katika siku ya 10 basi malaika angekuja na maombi ya Danieli
yangeishia hapo.
Wakati mwingine mtu anaweza kuomba kwa muda mrefu lakini nguvu
anayoachilia ikawa bado haitoshi ili kumpa ushindi kamili. Katika
mazingira kama haya mtu huyu atahitaji watu wengine wainuke kumsaidia
kuomba.
Ukisoma, Kutoka 17:11-13,
utaona kuwa Israeli walikuwa wanapigana na waamaleki na Musa alikuwa
amebeba mzigo wa kuomba ili Israeli washinde (ile hali ya kunyanyua
fimbo wakati wa vita ilikuwa ni ishara ya Musa kuwa kwenye maombi).
Biblia inasema kuwa Musa aliponyanyua mikono Israeli walishinda na
aliposhusha mikono Israeli walishindwa.
Maana yake ni kwamba ile hali ya Musa kunyanyua mikono iliashiria
maombi aliyokuwa akiyafanya na hivyo alikuwa akiachilia nguvu ambayo
MUNGU alikuwa anaitumia ili kuwapa Israeli ushindi.
Musa aliposhusha mikono, ilikuwa ni alama ya kuacha kuomba na hivyo
ikawa inapunguza nguvu ile ambayo MUNGU aiihitaji ili kuwapa ushindi.
kupungua kwa nguvu hiyo kulimfanya MUNGU ashindwe kuwapigania Israeli na
ikawa wanashindwa.
MUNGU alipoona hivyo ikabidi amwinulie Musa watu wa kumsaidia kuomba.
Ile hatua walioichua Huri na Haruni ya kuiegemeza mikono ya Musa,
kibiblia ina maana ya hatua ya Huri na Haruni kumsaidia kuomba. Na ndipo
baada ya hatua hii tunaona ISARELI wakishinda.
Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa kama Danieli angepata watu wa kumsaidia
kuomba basi ni wazi kuwa asingelazimika kuomba kwa muda wa siku zote
alizotumia.
Kutokana na kwamba YESU alikuwa akijua umuhimu wa watu wengine
kumsaidia katika kuachilia nguvu itakayomwezesha kuitimiza kazi
aliyopewa ndio maana aliwachukua Petro,na wale wana wawili wa Zebedayo
akaendao mlimani kuomba,kisha akawaambia "roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa, kaeni hapa, mkeshe pamoja nami". Math 26:38. huzuni
nyingi aliyokuwa nayo YESU ni kwa sababu aliona kazi ngumu iliyohitaji
nguvu nyingi ikimsubiri mbele na hivyo ikambidi aombe wanafunzi
wamsaidie kubeba mzigo huo kimaombi.Na tunaona kuwa kwa sababu wanafunzi
hawakuomba ilimbidi YESU aombe jambo lile kwa mara tatu; hivyo
inawezekana kabisa kwamba kama wanafunzi wangeomba basi YESU
asingelazimika kuomba mara tatu. Math 26:44.
=> KUNA FAIDA GANI YA KUWA NA MAOMBI YA MUDA MREFU?
Zipo faida nyingi sana za kuwepo maombi ya muda mrefu kwa mtu anayetaka kuona MUNGU akimpigania katika mambo yake.
1) Maombi
haya yanatoa nguvu ya kutosha ambayo humfanya MUNGU atume malaika zake
waje kushughulika na haja yako.
Efeso 3:20
Yakobo 5:16b, Matendo 12:5-11
Danieli 10:1-2,11-14.
Kutokana
na utaratibu wa MUNGU wa kutenda kutokana na nguvu wanazoachilia watu
wake basi ni muhimu kuwa watu waombe kwa muda mrefu ili wajenge nguvu
ambayo MUNGU anapoitumia unakuja ushindi.
= Namna nyingine za kuachilia nguvu za kiroho tofauti na maombi.
· Kusoma sana NENO LA MUNGU.
Katika
neno la Mungu unapata msaada na mwongozo wa kiimani ambao huo unakupa
mbinu za kuishi maisha matakatifu. Unapoishi katika utakatifu ndipo
unapojenga mazingira mazuri ya MUNGU kusikiliza maombi yako na
kukuhudumia.
1 Petro 3:12, Zaburi 16:3
2 Nyakati 7:14-16.
>Neno la Mungu hukupa nguvu ya kushinda majaribu,na unaposhinda
jaribu kwa neno unakuwa tayari umeachilia nguvu ambayo MUNGU anaitumia
kukufungulia baraka zingine. Mathayo 4:1-10.
· Kutoa SADAKA
Hii
ni moja ya njia muhimu sana katika kuachilia nguvu ya kiroho. Unapotoa
sadaka unaigusa madhabahu ya MUNGU na kumfanya ashuke kukuhudumia.
Malaki 3:10, Matendo 10:30-31.
Hapa
Mungu anatusihi tumjaribu kwa sadaka ili afungue milango ya baraka
kutumwagia; hiki ndicho alichofanya kornelio na Mungu akamkumbuka.
· KUSIFU kwa hali ya juu na katika roho.
Mungu
wetu ni Mungu anayependa kusifiwa, kwa hiyo unapotoa sifa kwake
unauburudisha moyo wake na kumfanya ashuke kukuhudumia haja yako.
Matendo 16:25-26
· USHUHUDA wa matendo makuu ya Mungu.
Hapa unamwinua Mungu na kumuaibisha shetani hivyo MUNGU anatukuka na kukusaidia zaidi ili uendelee kumshuhudia na kumtukuza,
Ufunuo 12:11a
2) Maombi haya yanakupa nguvu ya kutosha kuweza kupambana na milango ya kuzimu.
1 Petro 5:8-9a
Kuna
wakati unaweza kujiuliza ni kwa nini unaandamwa na roho chafu au nguvu
za giza licha ya kwamba umeombea jambo hilo hata kwa muda mrefu.
Unachoyakiwa kujua ni kwamba nguvu unayoachilia bado haijatosha
kuyaangusha malango ya kuzimu yanayokuandama;hivyo inakupasa uombe zaidi
hadi uone ushindi.
Mtumishi mmoja alikuwa akishudia jinsi alivyoandamwa na roho ya uzinzi
kwa muda mrefu, akasema niliomba sana lakini roho hiyo haikuniacha. Baada
ya hapo nilifunga kwa muda wa mwezi mmoja lakini sikupata ushindi,ndipo
nikaenda kuwashirikisha wanamaombi wenzangu na wakafunga siku tano,
ndipo MUNGU akatoa maono kwamba ukoo wetu unaandamwa na uzinzi hivyo
alikuwa amenipa mzigo mimi wa kuomba mpaka roho hiyo itakapoachia ukoo; alisema.
Tunachojifunza
hapa ni kwamba wakati mwingine hupati majibu ya maombi yako kwa sababu
umebeba mzigo mkubwa ambao unahitaji nguvu kubwa kuutua,hivyo unapoona
hali kama hizo omba msaada wa watu wengine wakusaidie kuachilia nguvu
iletayo ushindi.
3) Maombi haya humkumbusha MUNGU kuhusu hitaji lako ulilowahi kumwomba.
Isaya 62:6-7,1 Samweli1:10-12,20
Luka 1:5-20.
Kuna
wakati unapoomba, unajibiwa lakini MUNGU anakuwa anasubiri kuiona
juhudi yako katika kufuatilia maombi unayoomba. Kwa hiyo usipoomba mara
kwa mara unakuta majibu yanachelewa kwa kutokukumbushia kwako.
4) Maombi haya hukupa nguvu ya kuweza kushinda majaribu.
Kuna
wakati watu hujiuliza ni kwa nini watumishi wa Mungu wanaanguka na
kuacha wokovu? Suala ni kwamba unapookoka unatangaza vita na shetani
hivyo kila wakati anakuwa anakuwinda akuangushe,na hivyo anatuma majeshi
yake kukushambulia. Sasa unapokosa nguvu ya kutosha ndipo unakuta mtu
anazidiwa na nguvu za ibilisi na hatimaye anaanguka.
Hii ndio sababu iliyomfanya YESU awasisitize wanafunzi wake waombe ili wasiingie majaribuni, Mathayo 26:41.
5) Maombi haya hukujengea mazingira ya kukaa katika utukufu wa MUNGU na kukuwezesha kukaa mbali na dhambi.
Unapokaa
katika maombi kwa muda mrefu, moyo wako unakua unafunikwa na roho
mtakatifu na hivyo muda wako mwingi utakuwa unamtafakari MUNGU na hii
itakuweka mbali na kuzifikiria tamaa za ulimwengu huu.
6) Maombi haya huubadilisha utu wa kale na kuleta utu ambao ni wa utukufu.
Mtu
kabla hajaokoka anakuwa amefungwa kwenye roho mbalimbali chafu,
anapookoka anasafishwa na kupewa utu upya lakini kuna roho nyingine
unakuta zina maagano makubwa na hivyo suala tu la kuokoka haliziondoi
roho hizo ndani ya mtu.
Mtu huyu atahitajika kuomba kwa muda mrefu au watu wengine wamsaidie
ili kuachilia nguvu ya kutosha itakayotumika kumfungua.
Wakati tuko shule kuna binti mmoja tulimfanyia huduma, naye alikuwa
anaandamwa na magonjwa ya kila mara tena yasioeleweka. tulipokuwa
tunamwombea alikuwa anafunguliwa lakini baada ya siku chache tu alikuwa
akirudia hali zilezile. Hatukukata tamaa na hatimaye MUNGU akasema kuwa
kuna mambo elfu moja yaliokuwa yamemfunga na baada ya kuomba kwa miezi
kama saba Mungu akasema limebakia jambo moja na iwapo tukilishinda hilo
atakuwa huru kabisa.
Sasa unaweza kuona jinsi ambavyo ni hatari kufanya maombi kwa ufupi.
Kuna wengine wakati hawajaokoka walikuwa wazinzi au walevi, wanapookoka
unakuta roho hizo bado zinawaandama, na wengine waanza kuona kuwa
hawauwezi wokovu. suala ni kwamba watu hawa wanatakiwa waendelee kuomba
zaidi ili MUNGU apate nguvu ya kutumia ili awafungue.
7) Maombi haya hukupa amani ya kristo ambayo hukusaidia katika kufanya maamuzi sahihi juu ya mambo yako.
Kuna
wakati watu hufanya maamuzi ambayo baadae huja wakayajutia, na wakati
mwingine unaweza kukuta walimwomba MUNGU. Sasa tujiulize ni kwa nini
wafanye uamuzi ambao baadae wanaujutia?.
Jibu ni kwamba unakuta maombi aliyofanya mtu huyu hayatoi nguvu ya
kutosha kumfanya MUNGU ashiriki kwenye maamuzi yako. Hiki ndicho
kilimfanya YESU aombe usiku kucha alipotaka kuwachagua mitume na ndicho
kiliwafanya mitume waombe walipotaka kuwaweka wakfu Barnaba na Sauli.
Luka 6:12-13, Matendo 12:3-4.
8) Maombi haya yatakupa nafasi kubwa sana ya kusikilizwa mbele za Mungu.
Kuna
mambo mengine MUNGU anakuwa hana mpango wa kuyafanya lakini
unapozidisha kuliomba basi Mungu anaingia kazini kulishughulikia.
Yakobo 5:17-18.
NB: "Hakuna
kipimo kamili cha muda ambao mtu anatakiwa kuutumia katika maombi kwa
siku. Muda wa mtu kuomba utategemea msukumo wa roho mtakatifu ndani ya
mwombaji, lakini pia ni vizuri ukawa na utaratibu kwamba mwisho wa
maombi yako ni pale unapoona majibu ya maombi yako"
" VITU VINAVYOWEZA KUKUWEZESHA KUOMBA KWA MUDA MREFU "
Kuna
watu wengine wanapenda kuomba kwa muda mrefu lakini hawawezi, na
wanajiuliza kuwa wengine wanawezaje kuomba kwa saa zaidi ya moja?. vitu
vifuatavyo vitakusaida katika kujenga mazingira ya kuomba kwa muda
mrefu.
· Kufanya toba na kuokoka
Unapookoka
unatengeneza nafasi ya YESU kuja kukaa ndani yako naye YESU huja na
Roho Mtakatifu ambaye atakuwa na kazi ya kukufundisha na kukuongoza
jinsi ya kuishi maisha ya ushindi. Huyu Roho Mtakatifu hakai tu kwa kila
mtu bali kwa wale walio na YESU ndani yao, na ili uwe na Yesu ni lazima
uwe umemkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi yaani uwe umeokoka.
Pia unaweza kuwa umeokoka lakini ukatenda dhambi, sasa huwezi kufanya
maombi mazuri ukiwa katika hali hii; utahitaji kufanya toba ambayo
itarejesha uhusiano wako na Roho Mtakatifu.
Matendo 2:38
Hapa tunaona kuwa ukiokoka au kutubu utapewa kipawa cha Roho
Mtakatifu,hiki ndio ile nguvu ya roho ambayo itakusaidia katika kuomba
kwa kuwa hatujui kuomba jinsi itupasavyo.
Warumi 8:26,27.
Tunaona kuwa Roho Mtakatifu huwaombea watakatifu, sasa yawezekana
unashindwa kuomba kwa muda mrefu kwa kuwa hauko katika utakatifu.
· Kuwa na neno la Mungu la kutosha ndani yako.
Unaposoma sana biblia na kuwa na neno la kutosha ndani mwako, utaweza kujua kuwa MUNGU amenena vipi kuhusu haja yako na kwa kuwa
biblia inasema Mungu analiangalia neno lake ili alitimize
Yeremia 1:12, Isaya 55:11-
Basi hii itakuwezesha kuwa na hoja za kumwambia Mungu na unapojenga hoja ni lazima utumie muda mrefu.
Watu wengi hawaombi kwa muda mrefu kwa sababu hajengi hoja mbele za
MUNGU lakini nikwambie kuwa Mungu wetu ni Mungu wa hoja
Isaya 41:21
Aasante kwa fundisho la kuokoa na kufungua ufahamu
ReplyDeleteAhsante Sana Kwa fundisho zuri Sana hili Mungu akubariki Sana nimekuelewa sana
ReplyDeleteKuanzia leo nitaanza kumsumbua MUNGU
ReplyDelete