Thursday, April 20, 2017

PAZA SAUTI YAKO JUU SANA



Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe!

Utangulizi

Hili ni somo la ki-maombi. Lengo la somo hili ni kukuwekea msukumo wa kuendelea kuomba zaidi juu ya jambo ambalo unataka Mungu akutendee hata kama umeomba mara nyingi na haujapata majibu. Msingi wa somo hili unatokana na kauli ya Yesu Kristo mwenyewe aliyotuagiza katika Luka 18:1 ya kwamba imetupasa kumwomba Mungu siku zote, wala tusikate tamaa. Maombi yangu kwa Mungu ni kuwa unapoendelea kusoma somo hili akufungulie mlango wa maombi yako na akupe nguvu ya kuendelea kupaza sauti yako juu sana.
Paza Sauti Yako

Biblia inatufundisha kuwa maombi ni suala linalohitaji uvumilivu wa ndani ya mwombaji unaotokana na imani yake kwa Mungu. Isaya 59:1 inatueleze kuwa “mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia”. Kwa hiyo tunajua wazi kuwa Mungu wetu yuko tayari kusikia na yuko tayari kutuokoa kila tunapohitaji msaada wake. Lakini ni ukweli ulio wazi kuwa kuna nyakati ambazo tumekuwa tukimwomba Mungu lakini hatupati majibu. Kutokujibiwa kwa maombi kunaweza kuwa kumesababishwa na mambo mengi sana ya kiroho na ambayo Biblia imeyawekea utaratibu wa namna ya kuyashughulikia. Mimi katika somo hili sitaki kuyaangalia mambo yanayozuia maombi kujibiwa. Lengo langu katika somo hili ni kukutia moyo na kukuambia ya kuwa Mungu anakusikia, endelea kupaza sauti yako tu.

Tukisoma Luka 18:35-43 kuna habari moja nzuri sana. Inasema:
Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.  Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.

Hii ni habari ya mtu kipofu ambaye alisikia tu habari za kuwa Yesu anapita. Aliposikia hilo akaona ndio wakati wa yeye kupana uponyaji wa macho yake. Akaanza kuita Yesu amsaidie. Watu waliomsikia akiita hawakumsaidia kumsogeza kwa Yesu bali wakamkemea ili anyamaze. Yeye hakukubali kunyamaza, bali akapaza sauti yake zaidi. Nataka tujifunze pamoja mambo kadhaa kutoka katika hii habari juu ya suala la maombi yetu kwa Mungu.
           
             Moja -  Imani ya huyu kipofu haikutokana na kumwona Yesu wala kuona miujiza aliyoifanya Yesu bali kwa kusikia habari za Yesu. Kumbuka huyu alikua kipofu na kwa maana hiyo alikua haoni. Hivyo basi tunajua hakika ya kuwa alikua hajawahi kumwona Yesu wala kuona akifanya miujiza. Lakini kilio chake cha kuomba msaada wa Yesu kinatufanya tujue ya kuwa aliwahi kusikia habari za Yesu. Sasa sikia! Warumi 10:17 inasema: “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”. Huyu mtu alikua amesikia habari za Kristo na hii ilimjengea imani ndani yake ya kuwa Yesu anaweza kumponya. Ndio maana utaona sasa katika ile Luka 18:42 Yesu anamwambia “imani yako imekuponya”.

Tunachojifunza hapa ni nguvu ya kusikia habari za Kristo na kuziamini bila kujali tumewahi kuona akitenda au la. Yawezekana umeomba mara nyingi na hujaona akitenda. Oooh suala sio kuona akitenda mpendwa, suala ni kusikia! Imani yetu haitokani na kuona bali inatokana na kusikia neno lake. Hata kama hujaona akitenda kwako cha muhimu jua kuwa anatenda na anauwezo wa kutenda tena na tena.

            Pili – Huyu kipofu hakuwasikiliza watu waliomkemea ili anyamaze bali alizidi kukaza kumwita Yesu. Nisikilize mpendwa wangu. Kuna wakati umeomba na mwishowe umesikia sauti ndani yako ikikwambia .. aaah Yesu hakusikii nyamaza tu! Au umeomba lakini watu wengine wanakuambia kuwa hilo jambo unaloomba haliwezekani maana hata wao waliomba na hawakujibiwa? Au unaomba lakini unaona mazingira ni magumu kiasi kwamba unahisi kama vile Yesu yuko mbali sana na hakusikii? Oohh nataka nikwambie mpendwa usikubaili kunyamaza. Usikubali kunyamaza! Usikubali kunyamazaaa! Paza sauti yako juu zaidi, endelea kuomba, endelea kuita jina la Yesu yeye anasikia hata kama watu wanakuambia hasikii. Yeye anasikia hata kama kuna kelele nyingi za shetani zinazokukwamisha. Endelea mpendwa! Endelea kuomba! Endelea kupaza sauti yako.

Huyu kipofu angekubali ushauri wa waliomwambia anyamaze, uwe na hakika Yesu angepita na asingemsaidia. Lakini alikataa kusikia vikwazo ‘aka-focus’ kwenye nia ya moyo wake mpaka alipoipata. Mpendwa wangu, ‘focus’ kwenye hitaji lako kwa Yesu. Acha kusikiliza kelele za maisha. Acha kusikiliza makwazo yanayokuzuia usiendelee kuomba. Wewe kazana kupaza sauti yako zaidi. Nakuhakikishia Yesu anasikia na atakujibu.

            Tatu – waliomkataza kipofu ili anyamaze ndio hao walikuwa wakimtukuza Mungu baada ya kipofu kupokea uponyaji wake. Hii inatufundisha kuwa, hatima ya maombi yako inabebwa na wewe mwenyewe mwenye hitaji. Watu wengine hawawezi kuelewa uzito wa hitaji lako hata kidogo. Wewe ndiye mwenye jukumu la kukazana hadi upokee hitaji lako. Hao wanaokupigia kelele za kunyamaza leo watageuka kesho na kumtukuza Mungu watakapoona umevuka hapo ulipokwama. Kwa hiyo wewe kazana. Paza sauti yako.

Zaburi 81:10 inasema hivi:
'Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza'.

Angalia neno la Bwana kwenye huo msitari: “fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza”. Huu ni ujumbe wa Mungu kwa mwombaji. Kwamba kadiri unavyoendelea kupaza zauti yako kwa kuomba ndivyo Mungu anavyozidisha wema wake na fadhili zake kwako na kukujaza baraka. Sasa ninaposema kupaza sauti sana simaanishi kupiga kelele, la hasha! Ninachomaanisha ni kuendelea kuliitia jina la Bwana bila kukata tamaa.

Napenda nikutie moyo mpendwa wangu kuwa, usiache kuomba. Usikate tamaa. Usinyamaze. Wokovu wa Mungu wako u karibu nawe zaidi sasa kuliko ulivyoanza kuita. Kwa hiyo usiishie njiani. Endelea hadi uufikie ushindi. Yesu akubariki sana.

1 comment: