Mwenyezi
Mungu kwa neema yake anaendelea kutufundisha katika namna ambayo tunapata
kuuelewa wema wake na kupata sababu za kutokumkosea. Ni imani yangu kuwa watu
wakielewa hasa maana na uzito wa dhambi wanazofanya itawasaidia kuziacha na
kumgeukia Mungu. Karibu tuendelee kujifunza somo hili; kama ulikosa sehemu
zilizotangulia bonyeza hapa upate mtiririko mzuri zaidi.
Zinaa ni kukosa upendo kwa
unayezini naye
Kwa kawaida mtu unayempenda, utathamini utu wake na
kuheshimu asili yake. Utataka apate mema tu na wala siyo mabaya. Upendo wa
Agape (upendo wa kiMungu) ndio ambao wanadamu tumeumbiwa. Upendo huu ni
kutambua kuwa mwanadamu ameumbwa na Mungu na Mungu ana mpango wa kuyatumia
maisha ya kila mwanadamu ili kukamilisha malengo yake (Mungu) katika kujenga
ufalme wake.
Hivyo kama wewe unampenda mwenzio; utajitahidi
kuhakikisha kwamba yale ambayo Mungu ameyapanga yafanyike katika maisha yake
yanafanyika kikamilifu kwa sababu; Mungu atamleta hukumuni huyu mtu kama
hatatekeleza yale mambo ambayo Mungu angetamani kuyaona huyu mtu anafanya. Lakini
siyo hilo tu, Mungu anatamani sana kuona huyu mtu anaishi katika mapenzi ya
Mungu ili mtu huyu aweze kuurithi uzima wa milele.
Vipo vitu ambavyo vinamtenga mtu na Mungu wake, vitu hivi
ndizo dhambi. Mungu anapomuumba mtu hataki kabisa dhambi imtawale au ikae ndani
yake kwani anajua kuwa dhambi ndicho kikwazo cha kumfikisha mtu huyu katika
makusudi ya Mungu katika maisha yake hivyo anajitahidi kumuelekeza na kumlinda
mtu huyu asidanganyike na dhambi.
Upendo hapa unakuja kuwa na kusudi jema. Upendo wenye
kusudi jema hapa ni ule unaomsaidia mwanadamu kwanza, kuimarisha uhusiano wake
na Mungu na pili, kuyafanya yale ambayo Mungu angetamani kuyaona mtu huyu
anayafanya. Yaani makusudi ya Mungu aliyoyaweka ndani ya mtu.
Hivyo tunaona kwamba mtu anayekuja kuzini na mwenziwe
anamrudisha mwenziwe nyuma na kumharibia kabisa mahusiano yake na Mungu, yaani
anamfarakanisha na Mungu na kusababisha mahusiano ya mtu huyu na Mungu kupotea,
na yale makusudi ya Mungu juu ya mtu huyu pia yanakufa na kupotea kabisa.
Kwa hiyo licha ya kuwa watu husema kuwa wanampenda
msichana/mwanamke fulani au mkaka/mwanaume fulani hadi wanaamua kuzini naye,
hicho kitu si cha kweli kwani upendo siyo kumtenga mtu na Mungu wake bali
upendo, kwa sababu ni mwema, huzaa chema. Upendo usio mwema huzaa uovu na
upendo ulio mwema huzaa mema; amani, furaha na mafanikio katika Kristo.
Unaweza kusema, ‘sasa mbona mtu huyu ananililia na
kuning’ang’ania ili nizini naye, sasa mimi kwa kuwa nampenda na sitaki kuona
akiteseka, ni lazima nimhurumie na kumpa anachotaka,’ Kiukweli hiyo ni hoja ya
kibinadamu. Acha kufanya hivyo, kumbuka mtoto anapolilia wembe wewe kama mzazi
unatakiwa kumzuia kwa kumchapa. Kwani ukimpa ukamkata gharama ya kumtibia
majeraha aliyoyapata kwa kujikata na huo wembe itabaki kwako. Kwa hiyo, hiyo unayofanya
siyo huruma, bali ni ukatili kwani unamuangamiza, na siyo unamsaidia.
Hivyo basi dhana ya kwamba kufanya zinaa ni ishara ya
kuoneshana upendo inatoka kwa baba wa uongo-ibilisi na shetani na huo ni
UPOTOSHWAJI WA UPENDO.
MTU ANAYEZINI HAJIPENDI MWENYEWE
Tumeona
hapo juu kwamba mtu anayezini hampendi yule anayezini naye, lakini hapa tutaona
pia mtu anayezini hajipendi mwenyewe; angalia mstari huu;
Yohana
12:25
Yeye aipendaye nafsi
yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu
ataisalimisha hata uzima wa milele.
Yesu anasema kuwa aipendaye nafsi yake ataiangamiza, hii ina maana
kuwa nafsi inatamani vitu visivyofaa katika dunia, na kuipenda ina maana ni
kuishibisha na kila ovu inalotamani. Ndiyo maana mahali pengine wanasema:
1Timotheo
5:6
Bali, yeye
asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.
Hii ina maana kwamba nafsi siku zote yatamani mambo mabaya na mtu
anatazamiwa kuizuia ili aishi. Sasa mtu anayeipenda nafsi yake ni yule ambaye
hataki kuona nafsi yake inakosa kile inachotamani; yaani ni kama mtu ambaye
hataki kuona mwanae ananyimwa kile ambacho anatamani na anajitahidi kumpa kila
kitu anacholilia maana hataki kuona mtoto yule analia.
Kwa hiyo basi, ikishatokea kwamba mtu huyu anaidekeza nafsi yake
na kuipa kila inachotaka, ataipoteza kwa sababu, nafsi ina udanganyifu na
udhaifu mwingi ndani yake na ndiyo maana Paulo katika Timotheo anasema
tunatakiwa kuizuia.
Sasa yule anayeipenda nafsi yake, haizuii na inampeleka katika
matendo mabaya ya uharibifu ikiwemo zinaa. Mtu huyu haipendi nafsi yake,
haipendi kwa sababu ataipoteza, ataipoteza kama Yesu alivyosema; kuipenda kwake
hakufai kwani mwisho wa siku ataishia kuipoteza kama maandiko hapo juu yalivyosema.
Atakufa katika upotevu na nafsi yake haitapona. Ndiyo maana dhambi ya zinaa ni
mara nyingi sana imezaa mauti.
Watu ‘waliozipenda’ nafsi zao na kuzistarehesha katika uzinzi
wameishia kuzipoteza kwani wanapata magonjwa na kupoteza uhai, wengine wanauawa
kwenye mafumanizi au wanauana kwa kuchomana visu na kupigana risasi au hata
kurogana wakigombania wanawake au wanaume.
Ndiyo maana hapo juu tumeona kuwa kama mwenzio anakulazimisha
kuzini na kukubembeleza sana, huyo ameipenda nafsi yake hivyo ataiangamiza
pamoja na yako pale atakapofanikiwa kuzini na wewe, hivyo kwa kuzini naye
haumsaidii wala haujisaidii, bali ulitakiwa kuichukia nafsi yake na yako ili
uziokoe nafsi hizi mbili hata uzima wa milele.
Watu wazinifu licha ya kuwa walizipenda nafsi zao wakazidekeza na
kuzipatia zile tamaa zilizotamaniwa na nafsi hizo, wanaishia kuzipoteza. Lakini
tumekwisha kuona hapo juu kwamba upendo ni kitu chema. Na kitu chema chochote
ili tupate kujua kuwa ni kitu chema tunakipima kwa matokeo. Basi sasa, kwa kuwa
hawa watu walikuwa na ‘upendo’ kwa nafsi zao na kuzipa kile ambacho nafsi hizo
zilihitaji, kwa kuangalia matokeo ya upendo wao tunaona kuwa haukuwa upendo
kwani matokeo yao ni kifo, magonjwa ya zinaa na vifungo vya mwili na roho au
uadui na hata ndoa kuvunjika. Hivyo kwa tafsiri halisi ya upendo wenye matokeo
mema, watu hawa hawakuzipenda nafsi zao bali WALIZICHUKIA.
Naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata
uzima wa milele.
Hapa yesu anatufundisha kuwa kuichukia nafsi ni kuizuia
nafsi kupata kile ambacho inakitamani ambacho ni kibaya. Mtu anayeizuia
nafsi yake, ndiye aliye hai kwelikweli kama tulivyosoma kwamba mtu asiyeizuia
nafsi yake amekufa ingawa yu hai. Hivyo basi, tunaona kuwa Upendo wa kweli una
matokeo mazuri, kwa kuwa tumeona kuwa yule ‘aliyeipenda’ nafsi yake na
kuishibisha kwa tamaa ameishia kupotea, tuliona matokeo mabaya hivyo ule
haukuwa upendo halisi kwa nafsi yake. Lakini tazama huyu anayeizuia nafsi yake
na kuinyima tamaa zake ziletazo mauti, huyo kutokana na matokeo ya matendo
yake, anaisalimisha nafsi yake hata uzima wa milele, kwa hiyo huyu hapa tunaona
kuwa NDIYE MWENYE UPENDO WA KWELI kwa
nafsi yake.
uchambuzi; Mtu anayezini anaichukia nafsi yake,
hajipendi na anajichukia mwenyewe kwani anajipoteza na kujifarakanisha na Mungu
wake na kwa hakika atapotea duniani na mbinguni kwani atapata matatizo ya zinaa
hapa duniani kwa kupata magonjwa, kuwa na uadui na watu, kuishi maisha ya chuki,
aibu, fedheha na wasiwasi na hata kuuawa, kwa mfano kama nilivyokwisha sema ni
mara nyingi nimesikia watumishi wa Mungu wakiuawa kwenye mafumanizi, na akisha
kufa mtu huyu anaingia jehanamu moja kwa moja.
Kama tulivyoona hapo juu kwamba anayeichukia nafsi yake na
kuinyima tamaa zake ataisalimisha hata uzima wa milele; ‘anayeipenda’ na kuipa
zinaa ina maana atahukumiwa katika moto wa milele. Kwa hiyo zinaa ni
UPOTOSHWAJI WA DHANA HALISI YA UPENDO. Anayezini, hampendi anayezini naye hata
kumuangamiza, lakini pia hajipendi mwenyewe hata kujiangamiza, tazama mstari
huu:
Mithali
6:32
Mtu aziniye na
mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo LITAKALOMWANGAMIZA NAFSI YAKE.
Tukirudi kwenye zile dhana zetu za upendo endelevu na usio
endelevu, tunaona kuwa aipendaye nafsi yake na kuipa mahitaji ya mwili
yasiyoendana na makusudi ya Mungu, huyo anajipenda, lakini hajipendi upendo
endelevu. Anajitumia kwa maslahi ya muda mfupi tu ambapo baada ya maisha haya
ya sasa atapotea.
Matumizi endelevu ya nafsi na mwili na roho yako ni yale
yanayokupa maslahi ya kudumu duniani na mbinguni, yaani upate raha na amani
hapa duniani na upate uzima wa milele huko mbinguni, ndicho Yesu anachosema
katika mistari hii
Marko
10:29 Yesu
akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au
ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa
ajili ya Injili,
30 ila atapewa mara mia
sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na
mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.
Kwa hivyo kama unaipenda nafsi yako na hautaki kuipoteza, inabidi
uipende upendo endelevu, utakaoifaidisha hapa duniani na mbinguni. Usiipende
nafsi yako upendo usio endelevu.
Unapofanya zinaa na asiye mkeo, yaani mke wa mtu, wewe unaipenda
nafsi yako kwa upendo usio endelevu, kwani unaweza kufa katika njia yako hiyo
ukaenda kuzimu moja kwa moja, pia utakuwa umeacha familia na watoto wako
watahangaika.
Ukifanya hilo la mke wa mtu pia; unachukua magonjwa hata kama
hutauawa, magonjwa yataitesa familia yako hasa mkeo, na ukiwa ni Ukimwi,
utalazimika kufa mapema na kuwaacha watoto wangali wadogo! Ni kweli uliipenda
nafsi yako na kuipa kile inachotaka, lakini uliipenda upendo usio endelevu.
Tena unapozini na mke wa mtu, unafanya chukizo mbele za Mungu na
kujiletea laana katika familia yako ambapo mambo mengi yatavurugika kiuchumi na
kijamii na hamtakuwa na furaha na mkeo kama zamani. Afya ya ndoa yako inazorota
na watoto hawatakuwa na furaha kama inavyotakiwa kwani furaha ya watoto ni
kuwaona wazazi wanaishi kwa amani na upendo.
Tuendelee kujifunza zaidi mambo
haya katika sehemu zijazo; unaweza kusambaza somo hili ili wengine nao
wajifunze zaidi. Ubarikiwe na Bwana.
No comments:
Post a Comment