Monday, January 9, 2017

KUGEUKIA UKUTANI (SEHEMU YA TATU)

 Mwandishi: Anderson Leng'oko

Utangulizi
Somo hili ni mwendelezo wa sehemu mbili zilizotangulia. Tunaongelea habari ya kubaki wewe na Mungu wako na kuongea naye katika nyakati ambazo unahitaji msaada wa lazima na wa haraka; hii huokoa muda na kurahisisha mambo kuliko kutafuta mtu wa kati wa kukuunganisha na Mungu. Wakristo lazima waweze kuwa na mawasiliano binafsi na Mungu. Mawasilianoya moja kwa moja na siyo kutafuta mtu wa kati. Kila mtu anatakiwa kumjua Bwana na nguvu zake. Tunaangalia mifano kadha wa kadha katika biblia ya maisha ya watu ambao kwa maisha yao tunajifunza umuhimu wa kuwa na mahusiano binafsi na ya moja kwa moja na Mungu. Kama hujasoma sehemu zilizotangulia; tafadhali bonyeza hapa ili upate mtiririko mzuri.


Mfano mwingine unaojitokeza katika Biblia ni ule wa Samweli na Sauli.

1 Samuel 15:17-29
Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.
Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.
Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?
Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.
Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.
Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.
Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.
Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.
Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.

Hiki ni kisa cha mfalme Sauli alipokiuka maagizo ya Mungu ya kuteketeza kila kitu alipoenda vitani kupigana na Amaleki. Jambo la kujifunza hapa ni kuwa Sauli hakuwa na uhusiano mzuri kati ya yeye na Mungu, alikuwa karibu zaidi na watu kuliko alivyokuwa karibu na Mungu, na matokeo yake akawaogopa watu kuliko Mungu, watu wakamkosesha.


Lakini jambo ninaloliona hapa pia ni kuwa Sauli hakuwa anajua namna ya kumgeukia Mungu yeye kama yeye isipokuwa tu kupitia Samweli. Laiti kama Sauli angejinyenyekesha mbele za Mungu na kutangaza kufunga katika Israeli yote kwa mfano, nayeye akaacha mambo mengine yote na kujidhili mbele za Bwana bila hata kumbugudhi Samweli, kama alivyofanya Isaya, yumkini Mungu angemsamehe Sauli na kuuendeleza ufalme wake. Lakini juhudi za Sauli ziliishia tu katika kumbembeleza Samweli na matokeo yake anachana nguo ya Samweli na kupelekea unabii wa kutisha dhidi yake.

1 Wafalme 21:20-29
Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli.
Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli.
Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli.
Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla.
(Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea.
Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)
Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.
Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema,
Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.


Unaona hapa habari za Ahabu, hakukuwa na mtawala mbaya kama Ahabu katika Israeli kama neno lilivyosema hapo juu. Baada ya kukosa mbele za Mungu, Ahabu aliisikiliza adhabu yake iliyokuwa inatajwa na adui yake Eliya. Eliya hakukataa kwamba yeye alikuwa adui na Ahabu, na kama kanuni za biblia zinavyosema adui wa mtumishi wa Mungu ni adui wa Mungu.
Wakati Eliya akienenda kama adui wa Ahabu, Mungu alienenda kama rafiki wa Ahabu kwa sababu inaonekana Mungu aliendelea kufuatilia nyendo za Ahabu hadi ‘akaona’ jinsi Ahabu alivyojidhili mbele zake.

Akamwambia Eliya ambaye hakuwa hata na mpango wa kufuatilia maisha ya Ahabu, na labda pengine akifurahia adhabu iliyotolewa dhidi ya adui yake Ahabu, lakini Mungu alivyo na rehema na asivyomuacha mtu hata kama yule mtu anakuwa muovu sana mbele yake, akamuonesha Eliya kitu alichokiona cha kuvutia cha Ahabu; kule kujidhili, akaamua kumpunguzia Ahabu adhabu na kughairi mabaya aliyokuwa ameyakusudia kwa Ahabukwa kiwango kikubwa.

Mungu ana tabia ya kughairi mabaya, ana huruma sana na si mwepesi wa hasira. Hatukatai kwamba mtu au mwanadamu anaweza kukosea, lakini kitu anachofanya mtu baada ya kukosea kina umuhimu mkubwa sana na kinaangaliwa sana na Mungu kuliko alichofanya mtu kabla ya kukosea. Unaweza kumkosea Mungu uwezavyo, lakini unachofanya baada ya Mungu kukupa adhabu bado kinaweza kukusaidia sana na kikaepusha mambo makubwa sana mabaya ambayo yangekupata.

Unaweza pia kupata ufahamu zaidi kuhusu jambo hili kupitia Petro na Yuda. Petro alipomkana Yesu alijutia dhambi yake akalia sana akatubu. Lakini Yuda alipokosea, alijutia dhambi yake akarudisha zile fedha alizopewa za kumsaliti Yesu, akaenda zake akajinyonga. Yuda alibakisha suala moja tu katika yale mambo sahihi anayotakiwa kuyafanya mtu pale anapomkosea Mungu, angemalizia kurudisha zile pesa akaenda akajifungia na kumlilia Mungu mambo yasingekuwa kama yalivyo.

Mathayo 27:3-5
Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.
 Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.
Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.

Wakuu wa makuhani na wazee walimuuliza Yuda swali la kufaa sana ambalo kama Yuda angekuwa siyo mtu wa kutahayari, angelifanyia kazi. Pale walipomuuliza ‘Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.’ Yuda alitakiwa kuyaangalia yale majuto aliyojuta mahali pa kuyapeleka na wala siyo kuwapelekea wakuu wa makuhani na mafarisayo. Majuto hayo alitakiwa ayapeleke mbele za Mungu, akalia mbele za Bwana na Bwana angesema naye vinginevyo. Alitakiwa ayaangalie kwa umakini mambo yale, ajue njia sahihi ya kufanya ili damu ile aliyoisaliti isimsababishie mauti ya milele.

Mwanadamu, maadamu bado unaishi, usikate tamaa, endelea kurudi kwa Bwana hata wakati ule ambao kila kitu ndani yako na kila kitu kinachokuzunguka kinakwambia ukate tamaa, hapo ndipo utamke kwa ujasiri “Sitakata tamaa na kwa hakika nitashinda” Haleluya!
Mtu anaweza kusema kwamba inabidi uwe umevuviwa na Roho wa Mungu ili upate ule ufahamu wa kufanya toba mbele za Mungu, lakini hali hiyo kwa mifano tuliyokwisha iona hapo juu haina ukweli kwa kiasi kikubwa. Kwa hasira alizokuwa nazo Mungu dhidi ya Ahabu isingekuwa rahisi Mungu tena kumtumia Roho wa kumshawishi atubu, ila Ahabu alitumia juhudi binafsi na uwezo na nafasi ambayo Mungu humpa kila mtu baada ya kukosa,hadi akapewa neema ya kutokuyaona yale mabaya ambayo Mungu alikuwa ameyataja dhidi yake.

Usikose kufuatilia sehemu inayofuata, waalike wengine pia wapate baraka za somo hili. Mungu akubariki sana


No comments:

Post a Comment