Thursday, January 26, 2017

KUGEUKIA UKUTANI (SEHEMU YA NNE)

Mwandishi: Anderson Leng'oko

Utangulizi
Mpendwa msomaji hili somo linaendelea na hii ni sehemu ya nne. Nakusihi pata muda usome sehemu zilizotangulia ili upate mtiririko mzuri wa mambo yanayozungumziwa humu. Hapa tumefikia mahali pa kuongelea mifano mbalimbali ya watu kwenye biblia ambao walimgeukia Mungu wakasema naye wakati wa magumu naye akawatoa katika shida zao. Na lengo ni kuonesha umuhimu wa kuwa na mahusiano binafsi na Mungu na mara zote kutafuta kuyatengeneza pale yanapotokea. Kama haujasoma tangu mwanzo na ungependa kusoma sehemu zilizotangulia bonyeza hapa.

Mfano wa nabii Yona na mji wa Ninawi
Tuhamie kwa nabii Yona, mara baada ya kwenda kwa kujilazimisha kuuonya mji wa Ninawi. Unaona kabisa kuwa Yona mwenyewe alikuwa anatamani sana mji wa Ninawi uangamizwe. Yona 4:2-3

Akamwomba Bwana, akasema, Nakuomba, Ee Bwana; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya.
Basi, sasa, Ee Bwana, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.

Lakini kwa yale aliyoyafanya mfalme wa Ninawi, yalimfanya Mungu aamue kuusamehe mji ule, kisha safari ya Yona ikawa ni ya faida. Kwa sababu Mungu unadhani angefaidika nini kama angetumia gharama zote zile za kumtuma Yona halafu akaishia kuuangamiza mji wa Ninawi?

Angalia gharama alizotumia Mungu kumleta Yona Ninawi, aliichafua bahari ili Yona atupwe majini ashindwe kuendelea na safari yake ya kwenda Tarshishi, aliwapa hasara wale wenye meli ambao walilazimika kutupa shehena zao baharini ili meli isizame; na bado Mungu akalazimika kumtuma samaki ammeze Yona ili ampeleke pwani akamtapike ili akili zimrudie na alirudie kusudi la Bwana.
Yona 1:4-17


Lakini Bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.

Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.

Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.

Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.

Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?

Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.

Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa amewajulisha.

Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.
Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.

Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana.

Basi wakamlilia Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda.

Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.
Ndipo wale watu wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka nadhiri.
Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.

Hayo yote ni mambo ambayo Mungu aliamua kuingia gharama ili kuufanya mji wa Ninawi kumgeukia.

Mfalme wa Ninawi hakuwa na mpango wa kuongea na Yona tena baada ya Yona kufikisha ule ujumbe. Yeye tena angethubutu kwenda kumng’ang’ania Yona yumkini angekutana na makubwa kuliko yaliyomkuta Sauli kwa Samweli, kwa sababu tunaona hapa kuwa ni dhahiri Yona alikuwa anatamani sana Ninawi uangamizwe.

Kiukweli mfalme wa Ninawi angetegemea huruma za Yona asingepona, angekufa papo hapo. Lakini mfalme wa Ninawi aligeukia ukutani, akamlilia Mungu wake, siye yeye peke yake aliyefanya hivyo, bali na watu wote aliokuwa nao katika mji ule; hadi wanyama.

Yona 3:4-10

Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.

Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.

Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.

Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;

bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake.
Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?

Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

Hiki ni kitu ambacho nilikwambia hapo juu kwamba Sauli angekifanya, nani ajuaye kuwa Mungu asingeghairi yale mabaya aliyomtajia kupitia Samweli?

Basi mpendwa, tumuige mfalme wa Ninawi, ambaye hata hakujisumbua kujua Yona yuko wapi baada ya kuyasikia maneno yake, yeye alijisumbua kujua Mungu yuko wapi baada ya kusikia yale maneno ya balaa yaliyotamkwa na Yona alipokuwa ‘amepaniki’ kwa kulazimishwa kufanya kazi ambayo asingependa kuifanya.


Mtafute Mungu mpendwa, usiwatafute akina Yona ambao kwanza wanatamani uangamie hata leo; usipate nafasi ya kutubu; usije ukachana mavazi yao kwa kuwalazimisha wakuombee wakakulaani kama Samweli alivyomlaani Sauli.

Bado unaweza kujidhili mbele za Bwana na akakuhurumia na akawatumia kina Isaya haohao kukuletea neno la ushindi kama ambavyo Isaya alimpelekea Hezekia habari za kuongezewa miaka. Haleluya!


Usikose kuendelea na sehemu zinazofuata kwa ajili ya tafakari zaidi kuhusu habari hizi za kugeukia ukutani. Unaweza pia kusambaza somo hili na kuwaalika wenzio wengine walisome.

No comments:

Post a Comment