Mwandishi: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Somo hili ni mwendelezo wa sehemu mbili zilizotangulia.
Tunaongelea habari ya kubaki wewe na Mungu wako na kuongea naye katika nyakati
ambazo unahitaji msaada wa lazima na wa haraka; hii huokoa muda na kurahisisha
mambo kuliko kutafuta mtu wa kati wa kukuunganisha na Mungu. Wakristo lazima
waweze kuwa na mawasiliano binafsi na Mungu. Mawasilianoya moja kwa moja na
siyo kutafuta mtu wa kati. Kila mtu anatakiwa kumjua Bwana na nguvu zake.
Tunaangalia mifano kadha wa kadha katika biblia ya maisha ya watu ambao kwa
maisha yao tunajifunza umuhimu wa kuwa na mahusiano binafsi na ya moja kwa moja
na Mungu. Kama hujasoma sehemu zilizotangulia; tafadhali bonyeza hapa ili upate
mtiririko mzuri.
Mfano mwingine unaojitokeza katika Biblia ni ule wa Samweli na
Sauli.
1
Samuel 15:17-29
Basi Samweli akasema,
Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha
kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.
Kisha Bwana akakutuma
safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi,
upigane nao hata watakapoangamia.
Mbona, basi, hukuitii
sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?
Sauli akamwambia
Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa
Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
Ila watu waliteka
nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi
wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
Naye Samweli akasema,
je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti
ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya
beberu.
Kwani kuasi ni kama
dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa
neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
Ndipo Sauli
akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na
maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.
Basi sasa, nakuomba,
unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.
Samweli akasema,
Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye
amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.
Naye Samweli
alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.
Basi Samweli
akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako,
aliye mwema kuliko wewe.
Tena Yeye aliye Nguvu
za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata
ajute.
Hiki ni kisa cha mfalme Sauli alipokiuka maagizo ya Mungu ya
kuteketeza kila kitu alipoenda vitani kupigana na Amaleki. Jambo la kujifunza
hapa ni kuwa Sauli hakuwa na uhusiano mzuri kati ya yeye na Mungu, alikuwa
karibu zaidi na watu kuliko alivyokuwa karibu na Mungu, na matokeo yake
akawaogopa watu kuliko Mungu, watu wakamkosesha.
Lakini jambo ninaloliona hapa pia ni kuwa Sauli hakuwa anajua
namna ya kumgeukia Mungu yeye kama yeye isipokuwa tu kupitia Samweli. Laiti
kama Sauli angejinyenyekesha mbele za Mungu na kutangaza kufunga katika Israeli
yote kwa mfano, nayeye akaacha mambo mengine yote na kujidhili mbele za Bwana
bila hata kumbugudhi Samweli, kama alivyofanya Isaya, yumkini Mungu angemsamehe
Sauli na kuuendeleza ufalme wake. Lakini juhudi za Sauli ziliishia tu katika
kumbembeleza Samweli na matokeo yake anachana nguo ya Samweli na kupelekea
unabii wa kutisha dhidi yake.
1
Wafalme 21:20-29
Ahabu akamwambia
Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu
umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
Angalia, nitaleta
mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume,
aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli.
Kisha nitaifanya
nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya
Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata
kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli.
Tena Bwana alinena
habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli.
Mtu wa nyumba ya
Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani
watamla.
(Lakini hapakuwa na
mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe
alimchochea.
Akachukiza mno, kwa
kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza
mbele ya wana wa Israeli.)
Ikawa, Ahabu
alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake,
akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.
Neno la Bwana likaja
kwa Eliya Mtishbi, kusema,
Huoni jinsi Ahabu
alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta
yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo
juu ya nyumba yake.
Unaona hapa habari za Ahabu, hakukuwa na mtawala mbaya kama Ahabu
katika Israeli kama neno lilivyosema hapo juu. Baada ya kukosa mbele za Mungu,
Ahabu aliisikiliza adhabu yake iliyokuwa inatajwa na adui yake Eliya. Eliya
hakukataa kwamba yeye alikuwa adui na Ahabu, na kama kanuni za biblia
zinavyosema adui wa mtumishi wa Mungu ni adui wa Mungu.
Wakati Eliya akienenda kama adui wa Ahabu, Mungu alienenda kama
rafiki wa Ahabu kwa sababu inaonekana Mungu aliendelea kufuatilia nyendo za
Ahabu hadi ‘akaona’ jinsi Ahabu alivyojidhili mbele zake.
Akamwambia Eliya ambaye hakuwa hata na mpango wa kufuatilia maisha
ya Ahabu, na labda pengine akifurahia adhabu iliyotolewa dhidi ya adui yake
Ahabu, lakini Mungu alivyo na rehema na asivyomuacha mtu hata kama yule mtu
anakuwa muovu sana mbele yake, akamuonesha Eliya kitu alichokiona cha kuvutia
cha Ahabu; kule kujidhili, akaamua kumpunguzia Ahabu adhabu na kughairi mabaya
aliyokuwa ameyakusudia kwa Ahabukwa kiwango kikubwa.
Mungu ana tabia ya kughairi mabaya, ana huruma sana na si mwepesi
wa hasira. Hatukatai kwamba mtu au mwanadamu anaweza kukosea, lakini kitu
anachofanya mtu baada ya kukosea kina umuhimu mkubwa sana na kinaangaliwa sana
na Mungu kuliko alichofanya mtu kabla ya kukosea. Unaweza kumkosea Mungu
uwezavyo, lakini unachofanya baada ya Mungu kukupa adhabu bado kinaweza
kukusaidia sana na kikaepusha mambo makubwa sana mabaya ambayo yangekupata.
Unaweza pia kupata ufahamu zaidi kuhusu jambo hili kupitia Petro
na Yuda. Petro alipomkana Yesu alijutia dhambi yake akalia sana akatubu. Lakini
Yuda alipokosea, alijutia dhambi yake akarudisha zile fedha alizopewa za
kumsaliti Yesu, akaenda zake akajinyonga. Yuda alibakisha suala moja tu katika
yale mambo sahihi anayotakiwa kuyafanya mtu pale anapomkosea Mungu, angemalizia
kurudisha zile pesa akaenda akajifungia na kumlilia Mungu mambo yasingekuwa
kama yalivyo.
Mathayo 27:3-5
Kisha Yuda, yule
mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia
wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa
nilipoisaliti damu isiyo na hatia.
Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi?
Yaangalie haya wewe mwenyewe.
Akavitupa vile vipande
vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.
Wakuu wa makuhani na wazee walimuuliza Yuda swali la kufaa sana
ambalo kama Yuda angekuwa siyo mtu wa kutahayari, angelifanyia kazi. Pale
walipomuuliza ‘Basi, haya yatupasani
sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.’ Yuda alitakiwa kuyaangalia yale majuto
aliyojuta mahali pa kuyapeleka na wala siyo kuwapelekea wakuu wa makuhani na
mafarisayo. Majuto hayo alitakiwa ayapeleke mbele za Mungu, akalia mbele za
Bwana na Bwana angesema naye vinginevyo. Alitakiwa ayaangalie kwa umakini mambo
yale, ajue njia sahihi ya kufanya ili damu ile aliyoisaliti isimsababishie
mauti ya milele.
Mwanadamu, maadamu bado unaishi, usikate tamaa, endelea kurudi kwa
Bwana hata wakati ule ambao kila kitu ndani yako na kila kitu kinachokuzunguka
kinakwambia ukate tamaa, hapo ndipo utamke kwa ujasiri “Sitakata tamaa na kwa
hakika nitashinda” Haleluya!
Mtu anaweza kusema kwamba inabidi uwe umevuviwa na Roho wa Mungu
ili upate ule ufahamu wa kufanya toba mbele za Mungu, lakini hali hiyo kwa
mifano tuliyokwisha iona hapo juu haina ukweli kwa kiasi kikubwa. Kwa hasira
alizokuwa nazo Mungu dhidi ya Ahabu isingekuwa rahisi Mungu tena kumtumia Roho
wa kumshawishi atubu, ila Ahabu alitumia juhudi binafsi na uwezo na nafasi
ambayo Mungu humpa kila mtu baada ya kukosa,hadi akapewa
neema ya kutokuyaona yale mabaya ambayo Mungu alikuwa ameyataja dhidi yake.
Usikose kufuatilia sehemu inayofuata, waalike wengine pia wapate baraka za somo hili. Mungu akubariki sana
No comments:
Post a Comment