Mwandishi: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Mpendwa
msomaji, upo wakati ambapo unabaki peke yako katika maisha yako ya huduma, kazi
au familia. Hapa unatakiwa kupata msaada toka kwa Mungu wako. Ndipo ambapo
unatakiwa kugeukia ukutani umlilie Mungu ili akusaidie. Katika sehemu hii ya tano
ya somo hili, tunaendelea kuangalia watumishi mbalimbali ambao walimgeukia
Mungu naye akawasaidia.Kwa kusoma sehemu nyingine zilizotangulia bonyeza hapa.
Ipo
hadithi ya mfalme Daudi, ambapo mfalme Daudi alimpenda mke wa mtumishi wake,
mke wa Uria, akalala naye akampa mimba. Akafanya mpango wa kumuua Uria ili
amuoe yule mwanamke, kweli akamuoa na akawa naye. Lakini Mungu hakupenda,
akaahidi kumuadhibu Daudi. Daudi hakung’ang’ania kuomba msamaha kupitia
Nathani, ambaye alikuwa ni nabii ambaye Bwana alikuwa anamtumia kuwasiliana na
Daudi wakati ule. Daudi aligeukia ukutani akamlilia Bwana hadi mahusiano yake
na mkewe mpya Bathsheba, yakakubaliwa na Bwana. Tusome wote hadithi hii kwenye
kitabu kifuatacho
2Samweli
12:1-25
Ndipo Bwana akamtuma Nathani
aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika
mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.
Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi
sana;bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye
amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu
ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake
kama binti.
Hata msafiri mmoja akamfikilia
yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa
ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali
alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu
aliyemfikilia.
Ndipo hasira ya Daudi ikawaka
sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda
jambo hili, hakika yake astahili kufa;naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara
nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma.
Basi Nathani akamwambia Daudi,
Wewe ndiwe mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe
mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli;
nami nikakupa nyumba ya bwana
wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya
Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha.
Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya
yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa
mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.Basi, sasa
upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria,
Mhiti, kuwa mke wako.Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika
nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani
yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.Maana wewe ulifanya jambo
lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele
ya jua.
Daudi akamwambia Nathani,
Nimemfanyia Bwana dhambi.Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi
yako; hutakufa.Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi
kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.
Naye Nathani akaondoka kwenda
nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia
Daudi naye akawa hawezi sana.
Basi Daudi akamwomba Mungu kwa
ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini.
Nao wazee wa nyumba yake
wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini
hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.
Ikawa siku ya saba, yule mtoto
akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana,
walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye,
asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto
amekufa?
Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake
wananong'onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza
watumishi wake, Je! Mtoto amekufa?Nao wakasema, Amekufa.
Ndipo Daudi akainuka pale chini
akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa Bwana,
akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye
akala.
Watumishi wake wakamwambia, Ni
neno gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa
hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula.
Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nalifunga,
nikalia; kwa maana nalisema, Ni nani ajuaye kwamba Bwana atanihurumia, mtoto
apate kuishi?Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena?
Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.
Naye Daudi akamfariji Bath-sheba
mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake
Sulemani. Naye Bwana akampenda;
akapeleka kwa mkono wa Nathani,
nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya Bwana.
Tunaona katika mifano ndani ya masomo yaliyopita
kwamba watumishi wa Mungu hawa walikuwa na mahusiano binafsi na Mungu na
walimgeukia Mungu wao wenyewe hadi Mungu akabadilisha na kuigeuzia mbali hasira
yake na kuwasamehe.
Usipende sana kutumia mtu wa kati ili kumfikia
Mungu, Mungu yupo kwa ajili yako na anakusikiliza kila siku, kazi yako ni
kumuomba na kumtumikia kwa uaminifu.
Waombaji wengi kwa sasa wamekuwa siyo waaminifu na
dunia imejaa watumishi hewa kila mahali hivyo hautakiwi kutegemea mtu mwingine
akuunganishe na Mungu. Mtu mwenye nafasi nzuri kabisa kuliko wote ya kusema na
Mungu kuhusu maisha yako ni wewe mwenyewe.
Jenga mahusiano binafsi na Mungu ili nyakati
zinapokuwa ngumu uweze kugeukia ukutani na kusema naye na kuyapata majibu yako
mara moja.
FAIDA NYINGINE YA KUWA NA MAHUSIANO BINAFSI NA MUNGU
KUWEZA
KUPATA NENO LA WAKATI
Katika kila hali unayopitia mpendwa lipo neno la
wakati katika hali husika. Neno la wakati ni Mungu anasema nini kuhusu hali
yako na siyo watu wanasema nini katika hali yako unayopitia kwa sasa. Ni muhimu
sana kupata neno la wakati ili uweze kuwa na uelekeo utakao kufikisha mahali
panapostahili. Wana wa Israeli waliweza kudai mfalme kwa sababu hawakuwa na
neno la wakati ule, ambapo neno la wakati ule kutoka kwa Bwana lingewaambia
dhahiri kwamba haukuwa wakati wa kutafuta mfalme.
Yuda naye alijinyonga kwa sababu hakupata kulijua
neno la wakati. Utabiri ulikuwapo dhidi yake kwamba angemsaliti Yesu, lakini
haupo utabiri juu yake kuwa atajinyonga. Alichofanya Yuda ni ‘kujiongeza’
mwenyewe bila kutafuta neno la wakati ambalo lingetoka kwa Bwana kuja kumuokoa
katika saa ile. Huyu yeye alijikuta katika hali ambayo alikuwa amechanganyikiwa
akaona “he was too bad to turn to God,” yaani alikuwa mbaya sana kiasi cha
kutoweza kumgeukia Mungu. Hakuna nyakati kama hizo katika maisha yako mpendwa.
Hakuna umbali utakaofikia ambao utakuwa ni mkubwa sana kiasi kwamba huwezi
kumgeukia Mungu maadam bado uko duniani. Huwezi kumgeukia Mungu ukiwa umekufa
tu; hapo ndo huna namna.
Neno la wakati katika shida ni neno la wokovu, neno
la wakati katika vita ni amani na ushindi, ni maji katika kiu na chakula katika
njaa na dawa katika maradhi. Hivyo katika maisha yako na katika kila hali
unayopitia, lipo neno la wakati la kukupitisha hapo unapopitia na ni la ushindi
na amani. Tafuta neno la wakati sasa, na ni Mungu pekee anayeweza kukupa neno
la wakati wala siyo rafiki zako au mganga wa kienyeji. Kuwa na mahusiano
binafsi na Mungu ndiyo njia pekee ya kujihakikishia neno la wakati katika kila
hali unayopitia.
Lipo neno la wakati kwako wewe uliyeachwa na
mchumba, liko neno la wakati kwako wewe uliyedharauliwa na kushindwa kuishi kwa
amani na furaha. Liko neno la wakati hata kwako wewe unayetafuta kuolewa na
hujapata mume wa kukuoa.
Lipo neno la wakati hata kwako wewe ambaye madaktari
wamekwambia kwamba huo ugonjwa wako hauwezi kupona, lipo neno la wakati hata
kwako wewe dada unayejiona huvutii kiasi cha kutosha kuwa na mume.
Lipo neno la wakati kwako wewe mama mjane, lipo neno
la wakati kwako wewe uliyefiwa na watu uliowategemea, lipo neno la wakati kwa
yatima na masikini wa kutupwa.
Lipo pia neno la wakati kwa wale wenye viburi na
waliojawa na tamaa za dunia, lipo neno la wakati kwa wale wasiopenda kushaurika
na wanaodhani wao ndo wao na hii dunia wameshaiweka viganjani.
Lipo neno la wakati kwa wapendwa wasiotaka kuwajali
wengine kisa wao wameinuliwa na Mungu na hata kwa watumishi wa Mungu wenye
majivuno na wanaong’ang’ania dhambi na fahari za kidunia zisizo za kimungu.
Lipo neno la wakati kwa wale waliotengwa na makanisa
kwa kufanya dhambi zilizoonekana. Maana makanisani wanatengwa watu wanaofanya
dhambi za kuonekana na wanaachwa wale wote ambao bado dhambi zao hazijaonekana
hata kama ni kubwa kuliko zile zilizoonekana. Nao hao wafanyao dhambi
zisizoonekana na watu lipo neno la wakati kwa ajili yao Haleluya!
Lipo neno la wakati kwako wewe dada uliyeambiwa kuwa
ni mbaya, tazama Mungu analo neno juu yako maana ndiye pekee aliyekuumba na
anajua kama wewe ni mbaya au la, usiwasikilize wanaokuambia, nenda kwa Mungu
mwenye neno la wakati akwambie namna ulivyo mrembo!
Neno la wakati linapatikana tu kwa kugeukia ukutani
na kukutana na Muumba ambaye halali wala hasinzii na macho yake yapo duniani
kuwaangalia wamtafutao kwa bidii ili awatatulie mahitaji yao. Kama ambavyo
msomi anahangaika na bahasha kutafuta kazi ndivyo ambavyo Mungu anahangaika
duniani akibisha milangoni mwa watu wanaotafuta neno la wakati awahudumie!
Haleluya…
Anagonga toka mlango hadi mlango akiwa na maneno ya nyakati ya kila
mmoja wetu, hata la kwako wewe unayesoma somo hili! Kazi yako ni kufungua tu na
kulipokea neno lako.
Maana Mungu naweza tena kumfananisha na muuza samaki
au muuza bidhaa anayetembea mtaani akitangaza samakiii! Unachotakiwa wewe ni
kumuita tu na anakupatia bure kabisa! Haleluya!
Wakati nikiwa advance nilikuwa nakaribia kufanya
mtihani wa kidato cha sita, mama yangu mzazi alifariki dunia. Ugonjwa uliomuua
ulikuwa ni kansa na nilimshangaa Mungu sana. Unajua wakati huo Mungu alikuwa
yupo karibu na mimi kwa namna ya ajabu sana na kitu cha mama yangu kufariki ni
kitu ambacho kilinishitua sana maana sikukitegemea hata kidogo. Hii ni kwa
sababu Mungu alikuwa amenitumia pamoja na watenda kazi wa Fimbo ya Musa
kufungua magonjwa ya kila aina, kupitia sisi wenye kansa walikuwa wanapona,
wenye uvimbe tumboni, wenye appendix walikuwa wote wanafunguliwa hapohapo
tunapoomba.
Lakini katika suala la mama tulikuwa tumeomba mara
kadhaa bila mafanikio. Tulipoamua siku moja kwenda kukutana na mama ana kwa ana
ili tumuombee, tulifika nyumbani na tukakuta umati wa watu wenye huzuni na
maombolezo, kaka yangu aliangua kilio na kuniambia kuwa nilikuwa nimefika tu na
mama anafariki. Sikumuelewa Mungu kabisa.
Wakati huo ulikuwa ni mwezi mmoja tu kabla ya
kufanya mtihani wa form six na nilikaa siku nne tu za maombolezo nikarudi
shule. Watu waliosikia habari za msiba ule na yaliyonipata-wanafunzi wenzangu
walikuwa wanaogopa kukutana na mimi kwani walijua kuwa hali yangu ilikuwa mbaya
sana na walidhani pengine ningekuwa nalia muda wote.
Siyo wao tu, hata mimi mwenyewe nilifikiri kuwa
nikisharudi shule ningekuwa na muda mwingi sana wa kulia kuliko kufanya jambo
lingine lolote. Cha ajabu ni kwamba tangu siku niliyoondoka nyumbani hadi siku
niliyofanya mtihani; sikuwahi hata kulengwa na machozi kuhusu suala la mama.
Hii ni kwa sababu Mungu hakuniacha katika wakati husika na aliniletea neno la
wakati kupitia ndoto.
Siku moja nikiwa nimelala nilijikuta ndotoni niko
nimekaa na mtu kama ambavyo mtoto anavyopakatwa na baba yake, nilimlilia mtu
huyu ambaye nafsi yangu ilikuwa imeongozwa kuwa ni Mungu, naye alikuwa
akinifariji na kuniambia maneno ya kunibembeleza kuwa alielewa hali yangu na
jinsi nilivyoumia na alikuwa ana mawazo mema na mimi na kamwe hataniacha.
Nililia sana kwenye ile ndoto, na hatimaye ndoto
iliisha na nikawa na amani tangu pale hadi watu waliokuwa wananiona wakawa
wanakiri mbele yangu kuwa walikuwa wanashangazwa jinsi nilivyokuwa na moyo
uliochangamka katika kipindi kigumu kama kile.
Ashukuriwe Mungu ambaye alijua kuwa nilikuwa
nahitaji neno la wakati na hii ni kwa sababu nilikuwa na mazoea ya kugeukia
ukutani na kukutana naye moja kwa moja kwanza kabla sijamsikiliza mtu mwingine
yeyote kuhusu hali husika.
Umeona sasa? Neno la wakati ni kila kitu katika maisha yako.
Neno la wakati ndiyo dira na kila mtu analihitaji. Geukia ukutani sasa utafute
neno la wakati. Yule alijinyonga na yule mwingine alikunywa sumu kwa sababu
alikosa neno la wakati.
No comments:
Post a Comment