MWANDISHI: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Mpendwa mfuatiliaji wa somo hili, tunashukuru kuwa Mungu
anaendelea kutujalia mafundisho mema kuhusu habari ya zinaa. Tunakushukuru wewe
ambaye kwa namna moja ama nyingine umekuwa ukifuatilia somo hili na kuombea
mwendelezo wake. Pia kwa msomaji mpya, bonyeza HAPA ili uweze kufuata mtiririko
mzima wa somo hili na ujifunze kwa undani yale ambayo Mungu amekuwa akisema
nasi katika sehemu tatu tulizopita. Leo tunaendelea na sababu zinazopelekea
watu waanguke kwenye uasherati na uzinifu. Mambo haya yapo mengi lakini kwa
namna moja ama nyingine kwa kuyasoma unapata mwanga wa namna ya kuepuka mambo
hayo na ushauri unatolewa ili hata kama yupo rafiki yako au ndugu anayepitia
hali hizo aweze kuziepuka. Endelea kubarikiwa…
Kanisa kuyakalia kimya mambo ya zinaa kana kwamba hayapo
Kanisa pia linatakiwa kuyawekea mkazo mambo haya na
kuwaelekeza vijana kuhusu maana, athari na matatizo mbalimbali yanayoambatana
na zinaa. Kama kanisa litakaa kimya juu ya athari zinazopatikana kwa kuzini
hakika yake waumini wataendelea kukosea na kuona kuwa zinaa ni kitu cha
kawaida.
Kama tunavyoelewa jamii nyingi za kiafrika haziongelei
sana mambo ya zinaa, hivyo hatuna budi kama kanisa kuongeza bidii ya
kuliongelea na kuwafundisha hasa watoto na vijana kuhusu mambo haya ili wawe na
ufahamu na uwezo wa kupambanua mambo wanapokutana nayo. Kuna usemi wa
kiingereza usemao ‘forewarned, forearmed,’
yaani ukionywa mapema, utajiandaa mapema.
Hosea
4:6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa
maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe
kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami
nitawasahau watoto wako.
Mwingine ameshituka nilipotaja watoto, lakini uhalisia
huko duniani ni kwamba kuna watoto wanapata mimba wakiwa darasa la tatu, nne na
tano. Inaonesha kanisa ‘linaibiwa zamu,’ yaani shetani anatuwahi kabla
hatujashituka. Rafiki yangu mmoja alishituka sana alipoona kupitia dirisha lake
asubuhi moja watoto wakifanya mapenzi, wakati mwingine alikuwa na miaka miwili
hivi, hawezi hata kuongea. Kama mtoto anajua kuhusu zinaa akiwa na miaka miwili
au hajajua kuongea vizuri, vipi kanisa linaweza kukwepa kuzungumzia zinaa kwa
watoto?
Proverbs
22:6
Mlee mtoto katika
njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.
Kukosa kazi ya kufanya
Wapo watu ambao wanakula na kushinda kwenye tv, wanakula
na kwenda vijiweni kukaa, watu hawa hujikuta wana muda mwingi wa kuwaza na
kuona maovu. Matokeo yake hujiingiza kwenye tabia hatarishi, ikiwemo zinaa,
ulevi n.k.
Sababu za kiuchumi
Wengine huzini kwa lengo la kujipatia fedha za kukidhi
mahitaji ya kimaisha. Katika kundi hili huingia makahaba ambao huwa wanajiuza
kibiashara, lakini pia wapo wake na waume za watu ambao wana tamaa za pesa na
kutokuridhika.
Hila za adui
Wengine huzini kwa sababu za kishirikina na kichawi au
kishetani, wanakuwa maajenti wa shetani wanaochochea ngono ili wamtawale mtu
kishirikina na kumtumia kichawi kama sehemu ya maagano na wakuu wa giza.
Wanawake washirikina hutumia ngono kuwanasa wanaume na kwa wale walio na ndoa huwafanya
wawaache wake zao na kuwa nao wenyewe, wengine huwa hawavunji ndoa, bali
wanamtawala yule mwanaume na kula pesa zake kiasi hata cha kumfanya yule
mwanaume awe radhi kuishindisha familia yake njaa.
Ikumbukwe pia kuwa shetani hutumia ngono ili kumtawala
mwanadamu katika vifungo mbalimbali vya kudumu. Katika kutimiza kusudi hili,
shetani huchochea ngono kwa kila hali, ambapo wakati mwingine hutuma mapepo
ambayo huvaa miili ya wanawake wazuri na kukaa kwenye kona za miji wakijiuza
kama makahaba.
Hiki ni kiwango cha juu cha utendaji kazi wa nguvu za
giza. Wahanga wa uchawi huu na hila hizi za giza mara nyingi hupoteza maisha
yao, au kuingia katika vifungo vya kudumu.
Kurejesha hisani
Wengine wanazini kwa lengo la kurejesha hisani baada ya
kufanyiwa wema, na wengine huzini kama sehemu ya rushwa ya kufanikisha jambo
fulani analolitaka toka kwa yule anayezini naye.
Kufuata mkumbo
Wengine huzini kwa kufuata mkumbo wa marafiki wabaya
wakiisha kuaminishwa kuwa kuzini ndiyo fasheni na ndiyo mtindo wa maisha kwa
kila kijana, mara nyingi hawa huwa ni vijana na wasichana wadogo wanaojikuta
wamezungukwa na makundi mabaya, au hata wanandoa wanaozungukwa na marafiki
wabaya, ambao huwa wanawaambia kuwa figa moja haliivishi ugali.
Migogoro ya ndoa
Wengine huzini kwa lengo la kulipa kisasi katika ndoa au
mahusiano; pale ambapo mwenzi wake anafanya usaliti, mtu huyu huamua na yeye
kutoka nje ya ndoa au kumsaliti mwenziwe kama sehemu ya kisasi na kumkomesha
mwenzake; hii inaweza kuwa ndani ya ndoa au kwenye mahusiano, na hata wengine
hufikia hatua ya kutembea na wenzi wa wale waliotembea na wenzi wao, mfano,
kama mwanamke akigundua kuwa rafiki yake wa kike anatembea na mumewe, mara
nyingi naye huamua kutembea na mume wa yule rafiki yake ili kumkomesha rafiki
yake. Hili siyo jambo la kulifanya hata kidogo.Mara nyingi watu wafanyao haya
hawafuati misingi sahihi ya maisha. Kutembea nje ya ndoa ni tatizo ambalo
haliigwi, kwani hupelekea mwanadamu kumuudhi Mungu na kuhatarisha maisha yake
na umilele war oho yake.
Hivyo unapoona mwenzako anaenda nje ya ndoa tafadhali
sana jaribu kutumia njia sahihi ya kukabiliana na tatizo na siyo kulipa kisasi
kwa wewe pia kutoka nje ya ndoa. Kwa waombaji, tumia muda huu kumsihi Mungu
kuhusu kuililia roho ya mwenzi wako huyu.
Kuna mtu mmoja aliwahi kusema mtu anayetoka nje ya ndoa
kisa ameona mwenzake anatoka huyo naye tabia hiyo anayo tangu mwanzo.
Ukitafakari kweli unaona inaleta mashiko makubwa sana. Kimsingi kama unafuata
misingi ya utakatifu huwezi kuamua kuikosa mbingu na kuhatarisha uhai wako kwa
kuwa mzinifu. Kwa kufanya hivyo unazidisha migogoro na kamwe hupati suluhu.
Kuna shuhuda nyingi ambazo tunakutana nazo kuhusu watu
ambao wamekuwa waaminifu katika ndoa zao, lakini kwa bahati mbaya wenzi wao
wamekuwa siyo waaminifu. Mwisho wa siku unakuta wale ambao walikuwa siyo
waaminifu wanapata UKIMWI na hata kupoteza maisha wakiwaacha wenzao hawana hata
huo UKIMWI.
Mungu ni mwaminifu sana, kamwe mzazi hatakula zabibu
halafu mtoto ndio aumwe meno
Ezekiel
18:2-9
Je! Maana yake ni
nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu
mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno?
Kama mimi niishivyo,
asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika
Israeli.
Tazama, roho zote ni
mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana
mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.
Bali kama mtu ni
mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki;
hakula juu ya milima,
wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi
mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake;
wala hakumdhulumu
mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang'anya mtu mali yake
kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi;
ambaye hakumkopesha
mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha
mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake;
tena ikiwa amezifuata
sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika
ataishi, asema Bwana MUNGU.
Hivyo tenda haki ili uishi, mtu asisababishe ukaangamia. Na uwe na
uhakika kama ukitenda haki, mabaya yake hayatakupata kwani Mungu atakutetea.
Udadisi
Kuna watu walioingia kwenye zinaa kwa lengo la kuona
jinsi ilivyo, kama kuna raha ni ipi, kama kuna faida ni ipi. Hao wanajikuta
wanazini wakiwa na lengo la kudadisi kama kile walichokisikia ni kweli kuhusu
zinaa au la.
Lakini Mungu hapendi mtu azini au afanye mapenzi yasiyo
halali kwa sababu iwayo yoyote ile. Hivyo ni kazi ya shetani kusababisha watu
wazini, siyo mpango wa Mungu mtu kuzini.
Usikose kuendelea na somo hili katika mambo yanayofuata,
ambayo Mungu atatuwezesha kuyajadili katika sehemu zijazo. Tafadhali, hakikisha
unalisambazaili wengine nao walione, walisome, wapate baraka ambazo umezipata.
Ubarikiwe sana.
No comments:
Post a Comment