Monday, October 24, 2016

KWA HABARI YA ZINAA (SEHEMU YA TANO)

MWANDISHI: Anderson Leng'oko

DONDOO FUPI KUHUSU ZINAA

Utangulizi
Yapo mambo kadha wa kadha ambayo leo tunayaweka katika kipengele kimoja na kuyaongelea tofauti tofauti chini ya kichwa cha habari hiki. Ni mambo ambayo ni muhimu sana kuyafahamu katika safari yetu hii ya kuyaelezea mambo ya zinaa. Karibu uendelee kubarikiwa na kama unaanza leo kusoma somo hili basi bonyeza HAPA ili upate mtiririko mzuri wa somohili. Na ukimaliza kusoma usambaze ili wengine nao wapate kusoma. Barikiwa sana.

Zinaa ni dhambi kubwa sana kibiblia
Biblia inaitaja zinaa kama dhambi kubwa sana ambayo mwanadamu anatakiwa kuikimbia.

1Wakorintho 6:18
Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.

Hayo maneno yanayosema juu ya mwili wake mwenyewe, ukiyaangalia kwenye biblia za kiingereza utakuta maneno ‘against his own body,’ ambayo maana yake ni kwamba mtu huyu anafanya dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe, ambapo biblia inasema akifanya dhambi nyingine zote anaifanya nje ya mwili wake, yaani haiingii ndani yake.


Kwa hiyo tutoe mfano wa mauaji, kama yakifanyika nje ya nyumba yako, siyo mbaya kama ambavyo yangefanyika ndani ya nyumba yako. Kwa hiyo kwa mujibu wa biblia kufanya dhambi nyingine zote ni kama mauaji kutokea nje ya nyumba yako au nje ya mji wako, wakati kuzini ni kama kufanya mauaji ndani ya nyumba yako au ndani ya mji wako.

Au kwa maneno mengine kama dhambi ni nyoka, basi kufanya dhambi nyingine ni kumsogeza nyoka ukawa uko karibu naye ila usimuingize ndani ya mwili wako, wakati kuzini ni kama kumchukua nyoka na kummeza akaingia ndani ya mwili wako, jambo ambalo matokeo yake ni kifo.

Hivyo tunaona kuwa zinaa inaharibu mwili, kwani inaunajisi na inatenda dhidi yake. Inauua na kuufanya usiwe na thamani. Lakini ikumbukwe kuwa hapo awali tuliona kuwa kufanya zinaa ni kuiangamiza nafsi. Lakini sasa kwa hapa tunaona kuwa ni kuuangamiza mwili pia. Kwa hiyo zinaa inaua siyo nafsi tu, bali na mwili pia. Mwili na nafsi vikishakufa, na roho nayo itakufa. Hivyo zinaa ni kitu cha kukiogopa sana kwani ni aina fulani ya mauaji ya hiari ambayo mtu anajiua mwenyewe.

Ndoa ni kwa ajili ya zinaa
1Wakorintho 7:2
Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.
Hapa ni dhahiri kuwa biblia inatufundisha kuwa ndoa ni kwa ajili ya zinaa. Hivyo ili ndoa iimarike wanandoa hawana budi kuimarika katika tendo la ndoa na kuridhishana. Ndoa inasaidia kuleta suluhu la kuwafanya watu wasizini na kumaliza tamaa zao za mwili ili wapate kutulia mbele za Bwana.
Hivyo mwanandoa analazimika kukidhi mahitaji ya mwili ya mwenzie ili mwenzi huyo apate ule utulivu unaotakiwa katika ibada na maisha kwa ujumla; Ili asizini, yaani asiende kufanya mapenzi nje na mpango wa Mungu.
Sehemu kubwa ya wanandoa wanatoka nje ya ndoa kwa sababu wenzi wao hawakuwaridhisha kimapenzi au wamekaa mbali nao kwa muda mrefu sana. Hakuna kitu kinachotakiwa kuwa karibu sana na wewe kama mwanandoa mwenzako, ndiyo maana watu wakikuona unakuwa karibu na mtu mwingine wa jinsia tofauti mbali na mwanandoa wako wanaanza kujiuliza maswali.
Hivyo tuache kuwa na masuala ya kuingiza mambo ya rohoni wakati masuala mengine tunaweza kuyatatua kimwili. Wanandoa wanatakiwa kutumia muda wao na akili zao kuwaridhisha wenzi wao kimwili, na hii ni kibiblia kabisa, kama unataka ufafanuzi soma hiyo sura nzima niliyokutajia ya Wakorintho.
Yupo mwanamke mmoja alikaa na mumewe mwaka mzima bila kufanya naye tendo la ndoa, kisha mwanamke huyo akagundulika kuwa ana mimba. Alipoulizwa na mumewe ameipataje hiyo mimba akadai ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Basi ile ndoa haikwenda popote, ilivunjika na yule mwanamke amekutana na maisha ya dhiki sana kwani amemsingizia Roho Mtakatifu na ghadhabu ya Mungu katika hilo ni kubwa sana. Anakuwa amefanya machukizo.
Ndoa imara haiwezi kuwepo bila tendo la ndoa imara.
Zinaa ni ibada ya sanamu
Watu kwa kawaida hufikiri wanapokaa kanisani na kuimba nyimbo za kuabudu na kusifu ndipo wanapomwabudu Mungu peke yake, lakini sivyo ilivyo, uhalisia ni kwamba kila jambo unalolifanya ni ibada. Likiwa jema basi hiyo ni ibada kwa Mungu na likiwa baya basi hiyo ni ibada kwa shetani (sanamu). Hilo linathibitishwa na Paulo anaposema katika mstari huu;

Wakolosai 3:5 Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu.

Ieleweke katika neno hilo hapo juu kuwa ibada ya sanamu siyo ile wanayofanya wakatoliki wanapoinama mbele ya msalaba wenye sanamu ya Yesu. Ibada ya sanamu ni matendo anayoyafanya mtu. Ni upotoshaji mkubwa kuwalaumu wakatoliki wakati wewe mwenyewe ni mzinifu.

Mtu mmoja alisema kuwa wakatoliki wanachofanya ni kuamsha hisia tu na kuvuta uhalisia juu ya masuala ya mateso ya Kristo, lakini hawafanyi kama waisraeli waliofanya ndama kule jangwani ambapo wana wa Israeli walimwambia Haruni awatengenezee ndama kwani haijulikani ni jambo gani lililokuwa limempata Musa na Mungu wake.

Walipokwisha kutengenezewa ndama wakasema (wakiiambia ile ndama) “Sikia ee Israeli Hii ndiyo miungu yako iliyokutoa Misri katika nchi ya utumwa…”

Hapa ifahamike kabisa kuwa wana wa Israeli walikuwa wanaiambia ndama, wanaiabudu, na kuichezea; kwa maneno mengine ni kama mlokole wa leo anavyomwambia Mungu, nakuabudu nakusifu nakutukuza, ndivyo ambavyo wana wa Israeli waliiambia ile ndama kwamba ee ndama tunakusifu, tunakutukuza, wewe ndiwe uliyetutoa Misri na jina lako lihimidiwe.

Hicho siyo kitu wanachofanya wakatoliki, kwani wao hawaabudu ule msalaba, hawaabudu ile sanamu, bali wanaabudu Mungu na kutumia ile sanamu kama kikolezo cha hisia zao kuwapeleka mbele za Mungu, kama ambavyo watu huimba wimbo wa kuabudu kabla ya kuomba, ni ili kuleta zile hisia na msisimko kwa ajili ya kumuabudu Mungu.

Kama wakatoliki wangekuwa wanaabudu zile sanamu basi sanamu ingekuwa moja dunia nzima. Ni sawa na masuala ya maisha ya kila siku. Mtu ukitaka kumzinisha huwezi kumletea biblia, utamwambia maneno ya kuamsha hisia zake au hata kumuonesha video za kumuamsha hisia zake na kumpeleka kwenye kusudi lako la kumzinisha.

Huwezi kumfunulia biblia na kumuombea wakati unataka kuzini naye. Vilevile tunapokuwa ibadani tunaweza kutumia vitu ambavyo vinatusogeza karibu na Mungu, hatuviabudu vile vitu bali tunavitumia kutusogeza karibu na Mungu! Ndiyo maana sisi Fimbo ya Musa Ministry hatutapoteza muda hata siku moja kukashifu dini au dhehebu la mtu, bali daima tutamtangaza Mungu wa biblia tu. Lakini ifahamike kuwa biblia inasema kila mtu hufanya jambo aonalo kuwa sahihi machoni pake, bali Mungu huiangalia mioyo.

Na mimi najua kwa hakika kuwa moyo wa mkatoliki hauiabudu ile sanamu, unamuabudu Mungu aliye juu, Haleluya!

Basi, turejee kwenye mada yetu…

Kwa maana kila tendo alifanyalo mwanadamu, huwa lina utukufu. Utukufu huo huwa ni wa aina mbili, utukufu kwa Mungu, au utukufu kwa shetani. Hivyo basi kila tendo alifanyalo mwanadamu ni ama linapeleka utukufu kwa Mungu au linapeleka utukufu kwa shetani. Kwa hiyo basi, kama tendo linalofanywa halina utukufu mbele za Mungu, basi hilo linamtukuza shetani.

Mungu anaabudiwa kwa matendo tunayoyafanya siku zote na siyo ule utakatifu na utulivu tunaouonesha tu kanisani, au mbele ya mchungaji, au mbele ya padre au mbele ya muinjilisti, bali mbele ya Roho Mtakatifu.


Usikose kuendelea katika sehemu ya sita ambapo tutaendelea kujadili mambo haya kwa kina kwa neema ya Mungu. Barikiwa sana.

1 comment:

  1. Mume wangu amerudi!!! Baada ya miaka 1 ya ndoa iliyovunjika, mume wangu aliniacha na watoto wawili na maisha yangu yalivunjika. Nilitaka kuyamaliza, nusura nijiue maana alituacha bila chochote. Nimekuwa nimevunjika kihisia wakati huu wote na maisha yanaonekana kutokuwa na maana. Siku moja mwaminifu, nilipokuwa nikivinjari mtandao, nilikutana na baadhi ya shuhuda kuhusu Dk DAWN. Baadhi ya watu walishuhudia kwamba alimrudisha mpenzi wao wa zamani, wengine walishuhudia kwamba anarejesha tumbo na kuponya magonjwa kwa mimea. Nilipendezwa zaidi na upatanisho na mume wangu, ambao Dk. DAWN aliwezesha kumrudisha mume wangu ndani ya siku 3. Sasa mume wangu amerudi na tumekuwa tukiishi kwa furaha tangu wakati huo. Shukrani zote kwa Dk DAWN. Hapa, ninaacha mawasiliano yake kwa kila mtu. Maana kuna changamoto za aina yoyote,
    Barua pepe ( dawnacuna314@gmail.com )
    Whatsapp: +2349046229159

    ReplyDelete