“Maana neema
ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa”
(TITO 2:11)
Bwana wetu Yesu Kristo apewe sifa na utukufu daima!
Utangulizi
Ninamshukuru Mungu aliyeweka somo hili moyoni
mwangu na kunipa mwongozo wa kukushirikisha siri hii ya pekee. Somo hili
linalenga kukupa ufahamu wa nyakati tulizopo sasa (katika ulimwengu wa roho) na
namna inavyokupasa wewe kuishi ndani yake ili ufaidike na baraka za wakati huu.
Somo hili ni mwendelezo wa masomo ambayo Mungu amekuwa akinipitisha binafsi juu
ya umuhimu wa kutambua majira na nyakati zinazopita kwenye maisha ya mtu ili
aishi sawasawa na mapenzi ya Mungu kwenye nyakati hizo. Kitabu cha Luka
kinatupa picha ya madhara yanayoweza kutokea pale ambapo mtu/watu hawana hekima
juu ya muda waliopo na namna muda huo ulivyobeba maisha yao. Biblia inasema:
Alipofika karibu aliuona
mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo
amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako
watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;
watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya
jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako. (Luka 19:41-44)
“And they will dash you down to the ground, you
[Jerusalem] and your children within you; an they will not leave in you one
stone upon another, [all] because you did not come progressively to recognize and know and understand [from observation and experience] the time of your
visitation [that is, when God was
gracious toward you and offered you salvation through Christ].” Luke 19:44 (AMP)
Kwa tafsiri hii ya Amplified Bible tunapata kujua
kuwa madhara yatakayoupata mji huu wa Yerusalemu yanatokana na tatizo moja tu –
kutokujua/kutokuelewa/kutokutambua wakati ambapo Mungu alikuwa ameachilia neema
yake kupitia Yesu Kristo kwa ajili ya mji kuokolewa. Sasa utaelewa ni kwa nini
Mtume Paulo anaweka msisitizo mkubwa katika suala la kutambua muda/majira.
Ndani ya nyaraka zake mbili tofauti, Mtume Paulo anasisitiza jambo hili la
kutambua wakati japo yeye anatumia lugha ya kuukomboa wakati:
Basi angalieni sana jinsi
mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi
ni za uovu. (Waefeso 5:15-16)
Enendeni kwa hekima mbele
yao walio nje, mkiukomboa wakati. (Wakolosai 4:5)
Jumla ya mambo yote haya ni kuwa: muda/wakati ni
jambo la kiroho na Mungu anataka watu waishi kwa hekima sana kutegemea na
wakati waliopo. Pia, kwa kuwa muda ni (temporal) basi lazima uelewe kuwa mambo
yaliyobebwa kwenye muda hutoweka pale muda wake unapokwisha. Nataka kukwambia
kuwa katika vitu ambavyo shetani anafurahi sana kuviona ni pamoja na kuona watu
wa Mungu wanaishi pasipo kutambua wakati waliopo. Somo hili linataka kukutoa
hapo!
Neema ni kipindi maalumu
Nimemwomba Mungu anisaidie namna ya kukueleza jambo
hili kwa namna ambavyo utaelewa. Kama utakuwa na maswali juu ya eneo hili
tafadhari usisite kunitafuta kwa simu au email, au whatsapp au facebook.
Neema ni kitu anachopewa mtu pasipo kusitahili. Ni
upendeleo maalumu kutoka kwa mtu atoaye kwenda kwa anayepewa. Mtume Paulo
ametusaidia kuelewa maana ya neema kwa kutumia mfano wa mtu anayefanya kazi na
yule asiyefanya kazi. Anasema:
Lakini kwa mtu afanyaye
kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni
neema, bali kuwa ni deni. Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini
yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa
kuwa haki. (Warumi 4:4-5)
Paulo anasema kuwa ujira/mshahara wa mfanya kazi
hauwezi kuitwa neema – bali ni deni – kwa sababu kila mtenda kazi amestahili
ujira wake (1 Timotheo 5:18).
Lakini, kwa mtu ambaye hajafanya kazi ila akahesabiwa kuwa amestahili kuwepa
ujira/mshahara basi ule ujira wake sio deni bali ni neema. Naamini tunaenda pamoja!
Sasa Biblia inatuambia kuwa Kristo alipokuja
alileta neema! Oooh hii ni habari njema. Yohana 1:17 inasema: Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa;
neema na kweli zilikuja kwa mkono wa
Yesu Kristo. Kwa hiyo katika mkono wa Yesu Kristo iko neema na kweli. Sasa kama neema ni kitu
unachopewa pasipo kusitahili na mkononi mwa Yesu iko neema, hii inamaanisha
kuwa mkononi mwa Yesu viko vitu vingi ambavyo tunaweza kuvipata ambavyo kwa
kawaida hatukustahili kuvipata.
Bibia inasema jambo la kutia moyo sana katika Tito 2:11, inasema: “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa”. Neema imefunuliwa. Haleluya haleluyaa!!
Huu msitari wa Tito 2:11 una jambo la ajabu sana
ambalo ndilo limebeba msingi wa somo hili. Paulo anasema “neema … imefunuliwa”.
Hili linatupa kujua kuwa neema hii ilikuwepo tangu zamani … lakini ilikua
haijafunuliwa. Ndiyo! Tangu Adamu na Hawa waasi pale bustanini, neema iliachiliwa
lakini haikufunuliwa. Watu wa agano la kale walitembea chini ya kipindi ambacho
neema ilikuwepo lakini ilikua imefichwa (Waefeso 3:1-5). Sisi watu tuliofikiwa
na zamani hizi tunaishi kwenye kipindi ambacho neema imefunuliwa.
Roho mtakatifu alinishirikisha siri hii ya ajabu siku
moja nikiwa katikati ya maombi. Nilisikia sauti ya Roho Mtakatifu akiniambia:
Ijapokuwa neema imefunuliwa
bado watu wengi hawataweza kufaidika nayo kwa sababu hawajatambua nyakati
zilizopo. Ndani ya neema kuna kila kitu unachokihitaji pasipo kuhitaji wewe
uhangaike kutafuta kwa sababu unapewa chini ya neema iliyopo. Lakini ipo hekima
inayohitajika ili mtu aweze kunufaika na wakati wa neema – akiikosa hiyo hekima
mtu huyo atakosa faida zote zinazopatikana kwenye neema.
Neema ni kipindi maalumu! Kuna kipindi neema
haikuwepo kabisa. Kuna kipindi neema ilikuwepo lakini ilikua haijafunuliwa.
Sasa hivi ni kipindi ambacho neema imefunuliwa. Kuna kipindi kinakuja ambapo
neema itaondolewa.
Nilimwomba Roho Mtakatifu anipe mfano rahisi wa
kuelewa jambo hili. Akanirudisha kwenye Kitabu cha Mwanzo kwa habari ya Yusufu
na ndoto ya Farao:
Ikawa, mwisho wa miaka
miwili mizima, Farao akaota ndoto; … Hata asubuhi roho yake ikafadhaika;
akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima
walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao
mambo hayo … Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu
amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu… Tazama, miaka saba ya shibe
inakuja, katika nchi yote ya Misri… Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada
yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu
nchi. (Mwanzo 41:1, 8, 25, 29, 30)
Ukipata nafasi soma sura hii ya 41 yote. Ila
ninachotaka uone hapa ni kuwa Farao aliota ndoto juu ya miaka saba ya shibe na
miaka saba ya njaa iliyokuwa inakuja katika dunia. Jambo la kujua ni kuwa hayo
majira yaliyokuwa yanakuja juu ya nchi Misri yalikuwa yanakuja juu ya dunia
yote hadi kule alikuwa anaishi mzee Yakobo – baba yake Yusufu.
Farao alipata neema ya kuambiwa juu ya majira na
nyakati zilizokuwa zinakuja katika dunia. Watu wa mataifa mengine hawakuambiwa.
Miaka saba ya shibe ilipokuja dunia yote ilikua na chakula cha kutosha ndio
maana huoni mataifa mengine yakienda Misri kununua chakula kwenye miaka hiyo ya
shibe. Ni kwa sababu neema ilikua
imeachiliwa kote. Kila mahali palikua na chakula cha kutosha. Hata wale
ambao walikua hawajui majira waliyopo bado walinufaika na neema iliyokuwepo.
Lakini kwa Misri wao walikuwa na ajenda ya ziada.
Walikuwa wamepewa hekima ya kuishi kwenye wakati huo wa neema. Wao waliutumia
wakati wa neema kujiwekea akiba ya kutosha kwa ajili ya wakati wa baadae. Baada
ya miaka saba – neema ikaondolewa!
Neema ilipoondolewa, iliondolewa kwa mataifa yote –
sio Misri tu! Sasa kila taifa ambalo halikupata hekima ya kuutumia wakati ule
wa neema likaanza kupata shida ya chakula. Mataifa yote yakaenda Misri kununua
chakula. Ila jambo la kushangaza ni kuwa hata wamisri wenyewe ambao nchi yao
ilipewa hekima ya kuweka akiba bado na wao hawakuweka akiba! Unasema nimejuaje?
Biblia inasema hata Wamisri wenyewe walienda kununua chakula kwa Yusufu! (Mwanzo 41:55).
Ninachotaka uone hapa ni kuwa neema ikiachiliwa
inaachiliwa kwa watu wote, lakini ni watu wachache sana wanaopata hekima ya
kuitumia hiyo neema kwa ajili ya maisha yao ya baadae pale ambapo neema
itaondolewa. Watu wengi wanafikiri kuwa neema itakuwepo siku zote! La hasha! Neema ni kipindi maalumu! Kuna wakati
lazima neema iondolewe na huo ndio wakati ambao watu wengi huwa wanaingia
katika shida kubwa – kwa sababu hawakutambua majira ya kujiliwa kwao.
Ndio maana watu wawili wanaweza kuokoka wote katika
siku moja – wakiwa kwenye (level) sawa ya kimaisha. Lakini baada ya muda mfupi
unaona mmoja wao amefanikiwa na anazidi kusonga mbele kwa mafanikio kuliko
mwenzake. Je, tatizo liko wapi? Tatizo liko kwenye namna wanavyotumia neema
waliyoipata walipookoka. Kuokoka kunakupa (access) ya kuingia kwenye bank
account ya neema iliyo ndani ya Kristo Yesu. Lakini kama huna hekima ya kutumia
fursa hiyo, bado kuokoka hakuwezi kubadili maisha yako – hata kama neema ipo.
Chukua hatua ya kuomba
hekima
Kila mtu kwenye dunia hii ana wakati wake wa neema.
Kuna kipindi ambacho Mungu amekubariki sana au atakubariki sana. Watu wengi
huwa wakiwa kwenye kipindi hiki cha mafanikio huwa wanasahau na kufikiri kuwa
kipindi kama hiki kitaendelea tu siku zote. Hapana! Biblia inasema pamoja na
kuwa na wakati wa kucheka na kufurahi lazima pia uje wakati wa kulia (Muhubiri 3:4).
Namna gani una hekima ya
kutumia wakati wako wa kucheka ndio itakusaidia namna utakavyoishi wakati wa
kulia. Omba hekima ya Mungu kukusaidia kutambua majira uliyopo sasa na
akusaidie kujiandaa kwa ajili ya nyakati ngumu zinazokuja.
Nataka kusisitiza jambo moja kabla sijahitimisha.
Yesu alipokuja duniani alituletea neema. Ndani ya neema ya Yesu kuna (package)
kubwa sana ya baraka za Mungu kwetu sisi. Lakini tunaweza kushindwa kunufaika
nazo kwa kukosa hekima na maarifa ya kuitumia hiyo neema. Kumbuka Mungu anasema
“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa
maarifa” (Hosea 4:6).
Kuna maarifa ya ki-Mungu ambayo inahitajika kuweza
kuishi wakati wa neema. Japokuwa wengi tunajua kuwa neema ya Yesu imeachiliwa
bado hatuna hekima ya kutusaidia kuitumia neema hiyo. Ndiyo maana bado shetani
anatuonea, magonjwa yanatusumbua, umaskini umetujaa, hatufanikiwi kwa lolote
tunalolifanya licha ya kwamba tumeokoka. Hapana! Neema ya Yesu imekuja ili
tufaidike wakati huu na kwa ajili ya wakati ujao. Watu wa Misri walijulishwa
wakati wa neema na wakati wa mabaya lakini bado hawakuweza kuitumia neema ile
kujiwekea akiba ya chakula kwa ajili ya wakati wa njaa.
Hapana! Tusiwe kama hao. Chukua hatua ya kupiga
magoti na kuomba Mungu akupe hekima ya kuitumia neema iliyofunuliwa ndani ya
Kristo Yesu. Kumbuka kuwa Mungu anafurahishwa na mafanikio ya watu wake (Zaburi 35:27); lakini pia yeye
anatuwazia mawazo mema wala si ya mabaya (Yeremia
29:11). Njia mojawapo ambayo Mungu anaitumia katika kutufikisha kwenye mema
aliyokukusudia, ni kwa kukupa hekima ya kuishi wakati ambao neema imefunuliwa.
Mungu akubariki sana!
Mwl. Lukiko
No comments:
Post a Comment