MWANDISHI: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Mpendwa
msomaji tunaendelea na sehemu ya tatu kwa neema ya Mungu. Bila shaka Mungu ana
mengi bado ya kuongea na wewe kuhusu somo hili na kukufahamisha mambo
mbalimbali au hata kukukumbusha na kukutia moyo katika habari za zinaa. Kama
hujasoma sehemu mbili za kwanza zilizotangulia bonyeza HAPA ili kupata
mtiririko mzuri zaidi wa somo hili. Katika sehemu hii ya tatu tunaendelea
kujadili zile sababu zinazopelekea watu kuzini au kuwa wazinifu. Lengo hapa ni
kuwafanya watu waelewe wapo wapi na ni mambo gani wayafanye wanapokutana na moja
kati ya hali tunazozijadili hapa kwamba zinaweza kupelekea mtu kuzini au kuwa
mzinifu. Mungu amekuwa mwaminifu katika kulipa uhai neno lake na nakusihi
ulisome somo hili kwa kuomba na kutafakari kwa kina na usisahau kuwataarifu na
wenzako wengine ili nao wapate maarifa haya. Ubarikiwe sana.
Tamaduni za kigeni
Tamaduni za kigeni zinajumuisha mambo mengi, tunapoiga
mavazi, mienendo na tabia za kigeni tunakuta tunaambukizwa mifumo ya maisha
ambayo kwetu haipo. Mavazi yana mchango mkubwa sana katika tabia chafu za
zinaa. Haya yanawafanya watu wakumbuke zinaa na kuishikilia. Kwa mfano, mtu ukitaka
kusahau jambo, inabidi jambo hilo lisiongelewe na wala mtu asikukumbushe
kabisa. Vivyo hivyo ukitaka kusahau zinaa, inatakiwa mawazo yako yasikumbuke
kabisa habari hizo. Lakini akipita mbele yako mtu aliyeacha maumbile yake wazi,
moja kwa moja anakurudisha tena kwenye zinaa. Huwa nawaambia wanawake mara
nyingi sana moyoni mwangu, “why do you always keep reminding us of the things
we are struggling to forget?” yaani kwa nini siku zote mnatukumbusha mambo
ambayo tunatumia nguvu zote kuyasahau?
Basi tunapoongelea tamaduni za kigeni, tunajikita zaidi
katika tamaduni za kimagharibi, hawa watu wanafanya bidii kukifanya kizazi hiki
cha sasa kione kuwa zinaa ni jambo la kawaida sana kama kula ugali.
Wanaiaminisha jamii kuwa kuzini ni kama kupumua na kila mtu anaweza kuwa
anakifanya kitu hicho muda wowote, popote, na anaweza kufanya na yeyote. Mambo
haya wanayatangaza kupitia video zao, mziki wao na mambo mengine wanayoyaonesha
kwa namna mbalimbali.
Hii ni kazi ya shetani, kwani yeye siku zote anaigeuza
kweli kuwa uongo.
Yohana 8:44 Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo
mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika
kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake
mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.
Tamaduni zetu zinasaidia sana katika kujenga jamii zenye
maadili katika maisha. Ambapo suala la zinaa kwa watoto wadogo na vijana
linapigwa vita.
Kushindwa kuitawala na kuidhibiti akili
1Wakorintho
15:34
Tumieni akili kama ipasavyo, wala
msitende dhambi
Watu wengi hawajui kuwa ili uweze kuepuka dhambi yoyote ile lazima
uanze kwanza na akili. Kama akili yako itajikita katika kuwaza tamaa na
kutamani, wewe utataenda dhambi tu. Kama akili yako itajikita katika kuutafuta
wema na kuwaza mambo yenye maana, basi wewe hauwezi kufanya ujinga. Ndiyo maana
Mungu anasema katika
Luka 10:27
Akajibu akasema,
Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu
zako zote,na kwa akili zako zote;
Kama akili zako zitajikita katika kutafakari mambo ya Mungu tu,
huwezi kufanya dhambi hata siku moja. Kila baya mtu afanyalo, hulitafakari
kwanza na kulifanya akilini mwake kabla hajalifanya katika mwili, au katika
uhalisia, yale mambo tuyaonayo mtu anayafanya hadharani, ni matokeo tu ya
kinachoendelea akilini mwake. Bwana Yesu asifiwe.
Ikataze akili yako kuwaza zinaa na uzinzi nawe utafanikiwa
kujizuia na dhambi hiyo:
Mithali
13:14
Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.
Ukitafakari na kuwaza mema siku zote, hauwezi kutenda yasiyoendana
na mawazo yako. Ina maana akili yako itakuwa imejaa uzima, huo uzima
utadhihirika katika matendo yako na utakuwa na matendo yenye tija kwako na kwa
jamii yako na kwa Mungu wako. Utakuwa na uwezo wa kupambanua mambo na kuelewa
maana ya kila tendo ulifanyalo au kuliwaza:
Mithali
14:8
Akili za
mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
Utatafakari
mambo yatakayokuondoa kwenye kawaida na desturi za kibinadamu ambazo
zinawaangamiza watu:
Proverbs
15:24
Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.
Tatizo moja kubwa la walokole ni kwamba wakishaokoka wanaacha
kutumia maumbile waliyopewa wanamuachia Mungu kila kitu. Anaomba kwa kila jambo
kwa sababu tu ameambiwa aombe bila kukoma. Miguu anayo anashindwa kukimbia
zinaa, anakemea, matokeo yake anajikuta anaangushwa na shetani.
Kitu cha msingi ni kutumia kila kitu ulichopewa kupigana na
shetani, kama unaona hapo ulipo hakuna usalama, kimbia utoke hapo, usianze
kukemea wakati unaona haitakusaidia.
Hiyo akili pia uliyopewa, itumie ipasavyo, siyo unategemea maombi
tu hata mahali ambapo ungetumia tu akili ungeokoa muda. Mungu alikupa akili ili
uitumie, Mungu hamaanishi kuwa ukiokoka usitumie kabisa akili, la sivyo basi
angekuwa anawaondolea akili watu pindi tu wanapoongozwa sala ya toba na
wanakuwa mapunguani.
Ifundishe akili yako kutenda na kuwaza mema, ikataze kuwaza maovu
nawe kamwe hautafanya ujinga. Akili ikiwa na nguvu nyingi utaweza kumtoroka mtu
aliyekubananisha chumbani kama alivyofanyiwa Yusufu.
Akili ikiwa na nguvu unaweza kuacha kuzini na mtu hata kama kwa
sababu zisizozuilika umelala naye. Akili yako ina nguvu kuliko unavyojua sema
tu ni wewe hujaamua kuitumia. Mungu akusaidie kuitumia akili na kuifuata badala
ya kufuata tamaa na hisia za mwili.
2Timothy
2:7
Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa
maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.
Dhana potofu
Kuna watu
wameaminishwa kuwa usipofanya mapenzi kwa muda fulani basi unapata matatizo ya
uzao au mengine. Jambo hili ni uongo tu unaotumiwa na shetani kuwapoteza watu.
Mungu ndiye muumbaji na angejua kuwa suala hili lina madhara asingekukataza.
Lakini
wapo pia walioaminishwa kuwa zinaa ndiyo ‘habari ya mjini’ na wanaaminishwa
kuwa kama kijana lazima uzini na haiwezekani kuishi bila kuwa na mwenzi ambaye
unakuwa unashiriki naye mapenzi. Hizi zote ni dhana potofu kuhusu maisha ya
mapenzi na hazifai kuzifuata. Kiuhalisia kitu chochote kile ambacho hakitokani
na neno la Mungu siyo cha kweli na haifai kukiamini au kukifuata.
Romans 14:23
Na kila tendo
lisilotoka katika imani ni dhambi.
Malezi
Biblia inasema mlee mtoto katika njia impasayo naye
hataiacha hata atakapokuwa mzee. Wazazi kutokuwaelekeza watoto njia njema
katika maisha yao hupelekea watoto kujaribu na kufanya kila kitu wanachojisikia
kufanya au wanachoombwa na wenzao kufanya.
Lakini pia wazazi wenyewe wanaposhindwa kutumika kama
mfano bora kwa watoto inapelekea watoto kuwaiga. Kwa mfano kama baba au mama
anajihusisha na vitendo vya ukahaba na kutokuwa mwaminifu katika ndoa, mtoto
anaweza kuiga.
Ikumbukwe kuwa mtoto kabla hata hajashawishiwa kufanya
uasherati, ipo nguvu ndani yake inayomsukuma kufanya vitu hivyo, sasa
wanaomzunguka ndio wanaotakiwa watumie nguvu kumzuia, wasipofanya hivyo ni
lazima tu mtoto ataangukia kwenye zinaa.
Usikose kufuatilia sehemu zinazofuata za somo hili.
Endelea kubarikiwa na Mungu akuzidishie nguvu za kutenda yale yakupasayo
sawasawa na maarifa aliyokupa katika neno lake. Ubarikiwe na Bwana.
No comments:
Post a Comment